Tafuta

Ujumbe wa Neno la Mungu leo ni juu ya kanuni za Maisha mintarafu kuzingatia amri na maagizo ya Mungu Ujumbe wa Neno la Mungu leo ni juu ya kanuni za Maisha mintarafu kuzingatia amri na maagizo ya Mungu   (SVasco)

Tafakari Dominika 22 ya Mwaka B wa Kanisa: Kanuni Bora za Maisha: Amri za Mungu

Ujumbe wa Neno la Mungu leo ni juu ya kanuni za Maisha mintarafu kuzingatia amri na maagizo ya Mungu na kwa kuzingatia taratibu njema na kanuni na sherea tulizojiwekea kwa maongozi ya Mungu lili kupata furaha timilifu katika Maisha haya na yajayo. Somo I (Kumb 4:1-2, 6-8) ladokeza umuhimu wa kushika amri na hukumu zake tutaonekana watu wenye hekima na akili machoni pa ulimwengu wote, tutaishi vizuri tukipendwa na wote, naye BWANA atatusikiliza.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wetu wa Radio Vatican, katika dominika hii ya 22 ya mwaka B wa Kanisa, ujumbe wa Neno la Mungu leo ni juu ya kanuni za Maisha mintarafu kuzingatia amri na maagizo ya Mungu lakini pia inatukumbusha sisi kuishi kwa kuzingatia taratibu njema na kanuni na sherea tulizojiwekea kwa maongozi ya Mungu lili kupata furaha timilifu katika Maisha haya na yajayo. Somo I (Kumb 4:1-2, 6-8) ladokeza umuhimu wa kuzishika amri. BWANA asema tukishika amri na hukumu zake tutaonekana watu wenye hekima na akili machoni pa ulimwengu wote, tutaishi vizuri tukipendwa na wote, naye BWANA atakuwa karibu nasi akituitikia tumwitapo. Amri za Mungu ndio “TORATI” aliyomkabidhi mtumishi wake Musa Mlimani Sinai (Kut 20:1-17, Kumb 5:7-21). Pamoja na sala ya Shema/sikia Israel (Kumb 6:4-7) amri hizi 10 ndiyo Kanuni ya imani ya dini ya Kiyahudi. Ni amri za kimamlaka, zimekamilika, hazina maelezo, zina nguvu. Amri 8/10 ni “HASI” maana yake zinakataza zikitumia nafsi ya pili umoja rejea “Usi…”, 2/10 ni “CHANYA” yaani zinaagiza “shika kitakatifu… waheshimu baba na mama…” 1-3 zazungumzia uhusiano wetu na Mungu: Ukuu wake, ibada kwa miungu, heshima kwa Jina lake na ibada Kwake… 4-10 zazungumzia mambo ya kijamii: umoja wa familia, heshima kwa uhai, heshima kwa viapo vya ndoa, kwa mali, ukweli katika maneno na mwon chanya wa wenzetu na mali zao.

Amri za Mungu ni dira na mwongozo wa maisha
Amri za Mungu ni dira na mwongozo wa maisha

UFAFANUZI: Amri hizi zilifafanuliwa na walimu hadi kufikia 613. Walipaswa kuzikariri kwa kuzitamka mara kwa mara na kuzivaa mikononi na usoni zikawa mzigo na mara nyingi walishindwa kuzifuata. Mfano wa mapokeo hayo upo katika Injili ya leo (Mk 7:1-8, 14-15). Mafarisayo na waandishi wanamnung’unikia Yesu sababu wanafunzi wake wanakula bila kunawa. Hii ilikuwa amri mojawapo ya kimapokeo ambapo mmoja anapotoka kwenye mikusanyiko alipasika kutoa unajisi kwa kunawa hadi viwiko (kipepsi). Kristo anamnukuu nabii Isaya katika 29:13 akiwaona wanafiki wanaomuheshimu Mungu kwa midomo, wanamuabudu bure wakifundisha mafundisho ya wanadamu mioyo yao ikiwa mbali na BWANA.  Zaidi ya kunawa mikono walichagua pia vyakula. Nguruwe, wanyama wanaotambaa na wanaokula nyama ilikuwa haramu kwao kwa sababu za kiusafi, mshikamano wa kidini (kuepa wanyama walioliwa na wasio wayahudi/wapagani, kuepa wanyama wala nyama sababu hula nyama na damu kitu kilichokatazwa na Musa, badala yake walihimizana kula wanyama wala majani sababu hucheua iliyo ishara ya kutafakari Neno la Mungu. Kristo anatakasa vyakula vyote (Mk 7:19) akitoa shule ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula, kwamba kinachoingia hakina unajisi vile kinapita tu njia ila kinachotoka ndani huweza kumnajisi mtu.

Umuhimu wa kuzingatia kanuni na taratibu za maisha.
Umuhimu wa kuzingatia kanuni na taratibu za maisha.

Mwisho anatutaka tushikilie amri za Mungu na sio maagizo ya wanadamu. Namna gani? Ndipo somo II (Yak 1:17-18, 21-22, 27) linapoingia… kuweka mbali uchafu wote na ubaya uzidio na kupokea kwa upole neno lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu, kuwa watendaji wa neno na sio wasikilizaji tu. Amri safi ya Mungu na dini ya kweli kadiri ya Mt. Yakobo ni kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao na kujilinda na dunia pasipo mawaa. Hii ndio amri muhimu kuliko kunawa mikono na kubagua nyama za kula (miiko), upendo kwa Mungu na jirani. Upendo halisi u katika huduma kwa wenye shida mfano wajane na yatima. Hii ni changamoto, kujali watu ambao hawatatulipa kitu. Ni rahisi kuwahudumia wenye uwezo sababu nao watatusaidia, amri kuu ya upendo imekosa kabisa mashabiki. Licha ya kuwa na mahitaji muhimu tunashambuliwa na msongo, vidonda vya tumbo, shinikizo la damu nk kutokana na upweke, kutopendwa na kutothaminiwa. Wajane na yatima wapo wengi, tunafanya nini juu yao? Ni muhimu kuachana na amri za kimapokeo na kushika amri za Mungu kwa kutunza vema familia, hizo ziakisi upendo wa Kristo. Wanetu wanahitaji malezi bora na maonyo makali sababu wanaye mwalimu wao dunia asiye na mtaala mwema akiwafundisha mengi kuliko hata umri wao, wakubwa wao. BWANA ni mwema anatutazama kwa upendo, tushike amri zake, tupokee sakramenti na tusali. Tuchuchumie ya muhimu badala ya mapokeo ya mila na desturi zisizofaa zenye kututesa. Kufanya yapasayo si rahisi sababu ya udhaifu wetu wa kibinadamu. Tuombe neema ya Mungu kwa maombezi ya Maria Mtakatifu Mama wa Mungu na ya watakatifu wote ili tufanye yote vema kwa sifa na utukufu wa Mungu na kwa wokovu wetu sisi sote, amina!

Liturujia D 22 Mwaka B
31 August 2024, 08:57