Tafuta

Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC Kuhusiana na Mgogoro wa Kuhamishwa Kwa Wamasai kutoka Katika Hifadhi ya Taifa, Ngorongoro. Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC Kuhusiana na Mgogoro wa Kuhamishwa Kwa Wamasai kutoka Katika Hifadhi ya Taifa, Ngorongoro.  

Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Wamasai Ngorongoro

Askofu Wolfgang Pisa, OFM Cap., amekazia sana umuhimu wa: Utawala bora; vyombo vya ulinzi na usalama kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa kuzingatia: maadili, kanuni na miiko ya taasisi. Amewataka watanzania kujenga na kudumisha dhamiri nyofu, sauti ya Mungu ndani mwao. Amempongeza Askofu Antoni Gasper Lagwen wa Jimbo Katoliki la Mbulu kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya zawadi ya maisha na wito wa Daraja Takatifu ya Upadre!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Utawala ni matumizi ya mamlaka ya kisiasa, kiuchumi au vinginevyo katika kusimamia masuala ya nchi kwenye ngazi zote. Utawala bora ni matumizi ya mamlaka ambayo yanakuwa na uwazi, uwajibikaji, ushirikishaji wa watu, ufanisi, tija, uadilifu usawa na unafuata utawala wa sheria. Ili kutekeleza dhana ya utawala bora mambo yafuatayo lazima yazingatiwe: Matumizi sahihi ya dola, matumizi mazuri ya rasilimali kwa faida ya wananchi, matumizi mazuri ya madaraka yao, kujua na kutambua madaraka waliyonayo na matumizi yake. Madaraka yanatumika kulingana na mipaka iliyowekwa na katiba na sheria za nchi. Utawala bora unasaidia kuwa na mambo yafuatayo: Matumizi mazuri ya rasilimali za nchi; Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu; Kupungua kwa umaskini, ujinga na maradhi maadui wakuu watatu wa nchi; Kutokomea kwa rushwa adui wa haki; Huduma bora za jamii; Amani na utulivu; Kuheshimiwa kwa haki msingi za binadamu; Utatuzi wa migogoro kwa mujibu wa sheria na taratibu na hatimaye kuleta ustawi wa wananchi.

Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki: Maasai Ngorongor0
Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki: Maasai Ngorongor0

Askofu Wolfgang Pisa, OFM Cap. Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki Lindi, katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre wa Askofu Antoni Gasper Lagwen wa Jimbo Katoliki la Mbulu, tarehe 22 Agosti 2024 ametoa Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC Kuhusiana na Mgogoro wa Kuhamishwa Kwa Wamasai kutoka Katika Hifadhi ya Taifa, Ngorongoro. Katika tamko hili, Askofu Wolfgang Pisa, OFM Cap., amekazia sana umuhimu wa utawala bora; vyombo vya ulinzi na usalama kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa kuzingatia: maadili, kanuni na miiko ya taasisi husika. Amewataka watanzania kujenga na kudumisha dhamiri nyofu, sauti ya Mungu ndani mwao katika kuamua mema ya kufuata na mabaya ya kuepukika. Amempongeza Askofu Antoni Gasper Lagwen wa Jimbo Katoliki la Mbulu kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya zawadi ya maisha na wito wa Daraja Takatifu ya Upadre.

Maaskofu wanawashukuru na kuwapongeza waamini wa Mbulu
Maaskofu wanawashukuru na kuwapongeza waamini wa Mbulu

Askofu Wolfgang Pisa, OFM Cap. Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC anasema, anapenda kutoa msisitizo wa pekee katika kujenga na kudumisha utawala bora ambayo ni njia halali na ya haki, inayowajibisha katika kuwaongoza watu. Uhalali wa uongozi katika dhana ya utawala bora unapata chimbuko lake kutoka kwa watu wenyewe na kumbe, viongozi wanawajibika kwa wananchi kwa jinsi wanavyotumia madaraka yao. Madaraka na rasilimali za nchi zinamilikiwa na wananchi, viongozi ni walinzi na wasimamizi wa mali ya umma na wala si wamiliki wake. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa kukazia dhana ya utawala bora imeiomba Serikali irudi kwenye meza moja na watu wa Ngorongoro. Serikali iwasikilize na wala isiwalazimishe kuhama, wala kuwakosesha huduma muhimu za jamii au kuzuia chakula kisiwafikie. Wananchi wa Ngorongoro wapewe haki ya kupiga kura mahali walipo, hii iwe ni haki ya kweli. Leo hii Wamasai wanalia na kulalama kwamba, wamepokwa haki yao! Maaskofu Katoliki wanakaza kusema, Utawala bora uendelee kukita mizizi yake katika utawala wa sheria, ili kulinda haki, kuwajibika; kwa kukazia ukweli na uwazi na hivyo kuzuia aina yoyote ile ya uvunjifu wa amani, hawa wakati huu, Tanzania inapoelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa hapo tarehe 27 Novemba 2024 na baadaye kwenye Uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge utakao fanyika kunako mwaka 2025.

Umuhimu wa kukuza na kudumisha utawala bora
Umuhimu wa kukuza na kudumisha utawala bora

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC limetoa shukrani na pongezi kubwa kwa vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa ulinzi wa mali na usalama wa raia, pamoja na kuendelea kuwadhibiti wavunjifu wa haki na amani. Huu si wakati wa kupiga watu. Binadamu mwenye: heshima, utu na haki zake msingi anapaswa kuheshimiwa na wala si kupigwa. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania inavitaka vyombo vya Ulinzi na Usalama kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa kuzingatia: kanuni maadili, miiko ya taasisi husika, kwani kwa kutozingatia mambo haya msingi unaweza kuzalisha “genge” la wahuni. Hata wale wanaopigwa wanaweza kujihami na “hapo, panaweza kuchimbika sana.” Mtuhumiwa anapokamatwa ahakikishe kwamba, anatii sheria bila shuruti, ili aweze kupata haki zake mbele ya vyombo vinavyohusika. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC imevishukuru na kuvipongeza vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama kwa kazi kubwa wanazotenda. Maaskofu wanavitaka vyombo hivi viendelee kulinda: Sheria, haki na amani; vijenge umoja na mshikamano wa Kitaifa miongoni mwa watanzania katika ujumla wao.

Dumisheni na kukuza utawala bora
Dumisheni na kukuza utawala bora

Mwanadamu anayo sheria moyoni mwake iliyoandikwa na Mwenyezi Mungu. Dhamiri yake ndio kiini cha ndani sana na siri kubwa ya mwanadamu, ndipo patakatifu ambamo yumo peke yake pamoja na Mwenyezi Mungu; ambamo sauti yake yasikika. Dhamiri adilifu iliyo moyoni mwa mtu yaamuru, wakati ufaao, kutenda mema na kuepuka mabaya. Yahukumu pia uchaguzi mmoja mmoja, ikithibitisha ulio mzuri na kulaumu ule mbaya. Hushuhudia mamlaka ya kweli kuhusu uzuri wa juu kabisa ambako mwanadamu avutiwa; na huzipokea amri. Anaposikiliza dhamiri yake, mtu mwenye busara aweza kumsikia Mungu anaposema. Mama Kanisa anatafsiri dhamiri kuwa ni hukumu ya akili ambamo mwanadamu hutambua sifa adilifu ya tendo halisi analoelekea kulitenda, angali akilifanya au amekwisha kulitekeleza. Katika yote asemayo na atendayo, mwanadamu hana budi kufuata kiaminifu anachojua kuwa ni haki na sahihi. Mwanadamu hufahamu na kutambua maagizo ya sheria ya Mungu kwa hukumu ya dhamiri yake. Hadhi ya binadamu yadokeza na kudai unyofu wa dhamiri adilifu. Dhamiri yamwezesha mtu kuchukua madaraka ya matendo yaliyotekelezwa. Mtu ana haki ya kutenda katika dhamiri na uhuru ili afanye mwenyewe maamuzi adilifu. Mtu asishurutishwe kutenda kinyume cha dhamiri yake. Wala asizuiwe kutenda kadiri ya dhamiri yake, hususan katika mambo ya kidini. Rej. KKK. 1776 – 1802.

Serikali iwasikilize na kuwalinda Wamasai
Serikali iwasikilize na kuwalinda Wamasai

Askofu Wolfgang Pisa, OFM Cap. Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC mwanzo kabisa mwa salama na matashi mema kutoka kwa Maaskofu Katoliki Tanzania wamempongeza Askofu Antoni Gasper Lagwen wa Jimbo Katoliki la Mbulu kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya zawadi ya maisha na wito wa Daraja Takatifu ya Upadre. Katika kipindi cha maisha na utume wake, ameendelea kumpatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza; kwa kujisadaka na kujitoa kikamilifu katika kulihudumia Kanisa. Shukrani kwa zawadi ya maisha na wito wa Kipadre na sasa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbulu. Ameendelea kutumikia bila ya kurudi nyuma; ametenda kwa moyo wake wote; kwa upole, upendo na unyenyekevu mkubwa. Kwa hakika ametekeleza dhamana na utume huu kwa ari na moyo mkuu. Jubilei ya Askofu kimsingi ni Jubilei ya Jimbo. Kumbe, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC linawashukuru na kuwapongeza watu waaminifu wa Mungu Jimbo Katoliki la Mbulu kwa kufanikisha maadhimisho haya kwa kiwango kikubwa. Askofu Antoni Gasper Lagwen wa Jimbo Katoliki la Mbulu ni Mwenyekiti wa Idara ya Fedha ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, utume ambao ameutekeleza katika kipindi cha miaka mitatu na sasa tena amechaguliwa kutumikia kwa miaka mingine mitatu, ili kuhakikisha kwamba, fedha, lakini hasa sadaka ya waamini wa Kanisa Katoliki Tanzania inatunzwa na kutumika vyema kwa ajili ya mafao ya Baraza la Maaskofu; ustawi na maendeleo ya Kanisa la Tanzania. Maaskofu Katoliki Tanzania wanawashukuru na kuwapongeza wazazi kwa malezi na makuzi yoa kwa Mapadre na Maaskofu.

Maaskofu Tanzania: Tamko
23 August 2024, 14:32