Hitimisho la Kongamano la Ekaristi Kitaifa,Tanzania:Hii ni sakramenti ya upendo na tusibaguane kwa itikadi
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika hitimisho la Kongamano la V la Ekaristi Takatifu kitaifa nchini Tanzania, kwa ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika katika Uwanja wa Taifa mjini Dar Es Salaam, Dominika tarehe 15 Septemba 2024, na ambalo liiwawaona maelfu ya waamini wa Kanisa Katoliki kutoka maeneno mbalimbali nchi nzima, lakini pia kwa kuudhuriwa na maaskofu, mapadre na watawa viongozi wa dini nyingine na wa serikali ya nchi kwa Ujumla. Shamra shamra zilianza tangu alfajiri kwa kuona wimbi la watoto wa Utoto Mtakatifu na mavazi yao, waamini wote wazee kwa vijana.
Katika mahubiri ya Misa Takatifu wakati wa Kongamano hilo, Askofu Wolfgang Pisa (OFMCap,) Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Tanzania (TEC) na pia Askofu wa Jimbo Katoliki Lindi, alianza kufafanua maana ya siku hiyo hasa kwa kuwakumbusha kwamba pia ilikuwa ni kuhitimisha Jubilei ya miaka 50 ya Jumuiya Ndogondogo za Kikiristo katika majimbo yote nchini, “hata kama hiyo haikusikika sana, lakini ilikuwa muhimu ambayo ilianza mnamo 2023 katika Nchi zote za AMECEA.” Kwa njia hiyo alisisisitiza kuwa kwa miaka mingi nchini Jumuiya Ndogo Ndogo zimetumika kama chombo cha kuwafikia waamini wote na kuwa Ekaristi Takatifu tu ndio kiunganisho cha wakristo. Askofu aliendelea na mahubiri yaliyojikita zaidi katika kauli mbiu iliyoongoza Kongamano hilo isemayo: Udugu katika kuuponya ulimwengu: Ninyi nyote ni ndugu (Mt 23:8), ambayo ilichaguliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuongoza Maadhimisho ya Kongamano la 53 la Ekaristi Kimataifa, huko, Quito nchini Ecuador hadi tarehe 15 Septemba 2024, na ambalo limekwenda sambamba na la Tanzania.
Askofu Pisa alikazia kusema kwamba: “Hii ni sakramenti ya upendo hivyo tusibaguane kwa itikadi, rangi wala sababu zingine kwa kuwa sote tuna Mungu mmoja. Ndugu zangu twende katika sakramenti hii katika hali isiyo na dhambi, tumuombe Mungu sakramenti hii itubadilishe tuwe wapya.” Kwa kufafanua aliongoza “Ili imani na matendo viweze kuwafikia watu wengine kwa haraka inahitajika Jumuiya Ndogondogo, ambacho ni Chombo mahususi cha uinjilishaji cha kuwafikia watu wote na kwa ukaribu.” Kiongozi huyo wa TEC alisema kila mmoja anapaswa kuwa na moyo wa Ibada wa kumsifu Mungu ili kuendelea kupokea makuu yake hasa yanayopatikana kupitia Ekaristi Takatifu ambaye ni Mungu kweli na Mtu kweli.
Kwa kukazia zaidi alisema: "Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya upendo, Sisi tuwe mashuhuda wa huruma na upendo kwa kuwajali majirani wenzetu'. Sakramenti ya Ekaristi ndimo kila mtu anakutana na Mungu, hivyo amewataka Wakristo wasameheane na kushirikishana upendo kama Sakramenti ya Ekaristi inavyowataka na sio vinginevyo. Aidha aliongeza kusema “ni katika adhimisho watu wote wanakuwa sawa na hakuna ubaguzi wowote kwenye Ekaristi Takatifu na katika Ekaristi ndipo mtu anajisikia hawezi kuachwa na Mungu.
'Sakramenti tunayoiadhisha itufanye tuwe ndugu na tusibaguane kwa namna yoyote kwa sababu tuna Mungu mmoja'. Ukimpokea Yesu wa Ekaristi na ukabaki kama ulivyo bila kuhisi utofauti wowote ule, basi kuna kitu hakiko sawa ndani mwako. Kwa njia hiyo Sakramenti itufanye wapya, ili tumtangaze, tumshukuru Yesu wa Ekaristi na tuitukuze kila mara Sakramenti hii Kuu!” Askofu Pisa, alitoa mifano kadhaa, hasa kuhusiana na ukuu wa Bwana Yesu, kwa kuzingatia maandamano ya Ekaristi kutoka Chang’ombe hadi Msimbazi, ambapo watu wa kila sehemu walisimama kutazama Yesu akipita.
Ni Bwana wa wote na ndiyo maana wengi walichungulia au kupiga picha. Kuhusiana na kuaminiana pia alikazia kutoa mfano wa kukaribishana kama ndugu na hata kuamini kwa mfano: “unaweza kumwachia mtu simu, unaweza kumwachia mtu pochi yako” hii yote ilikuwa ni kutaka kusisitizia, udugu ambao tunapaswa kuwa nao kwa kizingatia Kauli mbiu iliyoongoza Kongamano hilo. Askofu Pisa alisisitiza huku akiwashukuru waamini kutoka majimbo mbalimbali nchini kwa kushiriki Kongamano hilo la Ekaristi Takatifu na kwamba hatimaye baada ya kulihitimisha Kongamano hilo la V lilifofanyika kwa siku nne watakutana tena miaka minne ijayo katika Jimbo Kuu la Arusha ambalo litakuwa Kongamano la VI 2028.
Balozi wa Vatican nchini Tanzania alitoa salamu zake
Akitoa salamu za Baba Mtakatifu, Balozi wa Vatican nchini Tanzania Askofu Mkuu Angelo Accattino alisema kuwa Kongamano hilo limeeleza umuhimu wa Ekaristi Takatifu kama kiini cha imani yao. Ekaristi inatuunganisha na kristo na ndugu zetu katika imani Ekaristi inaimarisha upendo wetu kwa Mungu. Balozi wa Vatican pia aliipongeza Serikali kwa kufanya matukio kama haya kwa uhuru na amani.
Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko
Kwa upande wa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko aliwaalika Watanzania kuishi kwa kuvumiliana, kuheshimiana na kupendana kama ilivyoagizwa na vitabu vya Mungu, wakati wa kupewa fursa ya kusalimia mara baada ya Misa Takatifu hiyo, katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaaam. “Wote tuliokuja hapa tumesikia mahubiri mazuri, tumehubiriwa kuwa wamoja zaidi tukavimiliane zaidi na kuheshimiana kama Watanzania wamoja. Kuwa na mawazo tofauti kusitufanye tugawanyike. Ekaristi Takatifu hii itufanye tuwe wamoja. Tuwafundishe jamii tuliyonayo kuwa na huruma kwa watu wote wanaohitaji na muhimu zaidi kuwa na huruma na taifa letu la Tanzania,” alisema Dk. Biteko. Kwa kutazama kaulimbiu ya Kongamano hilo kuhusu “Udugu Kuponya Ulimwengu, Ninyi Nyote ni Ndugu,” Mjumbe huyo wa Serikali katika Kongamano alisema kuwa kauli mbiu ni muhimu na inawaunganisha watu pamoja. “Tunapotoka hapa tuwafundishe watu, tuwe wapya Ekaristi Takatifu imetuagiza tuishi upya.” Hakuishia hapo bali pia alitumia fursa ya kuwahimiza Watanzania kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Serikali za Mitaa utakofanyika tarehe 27 Novemba 2024 kwa kuchagua viongozi kulingana na sifa zao watakaosaidia kuleta maendeleo nchini.
Viongozi wa vyama mbali mbali Tanzania wahamasishwa kuwa na upatanisho badala ya marumbano. Katika Kongamano hilo hawakukosa vingozi wa serikali wakiwa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhs William Lukuvi, Waziri wa Ujenzi, Mhs Innocent Bashungwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Msh Albert Chalamila. Viongozi wengine ni Spika wa Bunge Mstaafu, Bi Anne Makinda, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhs Emannuel Nchimbi na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), MhsTundu Lissu, Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mhs John Mnyika. Ni katika Muktadha huo ambapo Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Padre Charles Kitima aliwaita mbele viongozi wa vyama, ili kuonesha ukweli wa udugu huo wa wawe wamoja, wafurahi pamoja na mshikamano, wasamehane licha ya tofauti zao za vyama na zaidi udugu kama kauli mbiu ilivyokuwa ikisisitiza.
Baraza la Maaskofu Tanzania TEC, hatimaye walitoa Tamko lao na kubainisha “kuwa Tanzania imekuwa inasifika kama kisiwa cha amani” na kwa njia hiyo “lililaani vikali matukio ya utekaji na mauaji yanayoendelea nchini na kutaka vyombo vya dola kutimiza wajibu wake ipasavyo ili kurudisha heshima ya Tanzania kama kisiwa cha amani.” Ujumbe Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ulisomwa na Askofu Eusebius Alfred Nzigilwa, Makamu Rais wa TEC na Askofu wa Jimbo la Mpanda Tanzania. Katika matukio hayo aidha, maaskofu hao walibainisha kuwa “viongozi waliopo kwenye nafasi za kusimamia matukio hayo yasitendeke kama “Hawakuwajibika kwa kadri ya nafasi zao wawajibishwe.” Ifuatayo ni Tamko kamili hilo:
SALAMU ZA BARAZA LA MAASKOFU (TEC) KWENYE HITIMISHO LA KONGAMANO LA TANO LA EKARISTI TAKATIFU KITAIFA, DAR ES SALAAM, 15 SEPTEMBA 2024
“UDUGU KUPONYA ULIMWENGU, NINYI NYOTE NI NDUGU”
Wapendwa Taifa Takatifu la Mungu
1. Tunapohitimisha Kongamano letu la tano la Ekaristi Takatifu kitaifa, tunapenda kwanza kabisa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka zake nyingi alizotujalia katika Kongamano letu hili. Tumekuwa na siku nne za neema zilizojaa vipindi vya sala, ibada, mada na tafakari mbalimbali za kiroho. Pia tumepata nafasi ya kujenga na kustawisha umoja na urafiki kati ya waamini wa majimbo mbalimbali walioshiriki kwenye kongamano hili.
2. Kauli mbiu ya Kongamano inasema: “Udugu Kuponya Ulimwengu; Ninyi Nyote ni Ndugu”. Kupitia mada na tafakari mbalimbali tumeweza kuona jinsi Ekaristi Takatifu ambayo ndiyo chemchemi na kilele cha maisha ya kikristo, inavyoweza kuwa chumbuko la uhakika la umoja, udugu na mshikamano wa kweli wa jamii ya wanadamu. Udugu wetu wa ki-Ekaristi uendelee kuuponya ulimwengu na kulijenga Kanisa na Taifa letu. Tumealikwa kwenda kuishi maisha ya ki-Ekaristi yanayojengwa katika misingi ya upendo, huruma, mapatano, msamaha na majitoleo kwa ajili ya ustawi wa wote. Tunapomwabudu na kumpokea Yesu wa Ekaristi tunapaswa kugeuzwa na kufanana naye zaidi na zaidi katika mwenendo, mahusiano na utendaji wetu wa kila siku katika nyanja zote za maisha.
3. Tunapoliangalia Taifa letu, tunatambua kuwa Taifa letu la Tanzania kwa miaka mingi limejulikana kama kisiwa cha amani, udugu na mahali pekee Afrika ambapo raia wake licha ya tofauti zao za kikabila, kiimani, kiitikadi na kiuchumi tumeweza kuishi kwa umoja, amani, na kindugu. Kila mtu alihakikisha anaimiliki tunu hii na kuilinda.
4. Lakini tukiangalia hali ya sasa ya nchi yetu, tunaona tunu yetu ya undugu na amani imeshambuliwa. Hii inatokana na matukio yaliyotokea nyakati za karibuni, za watu kutekwa, kuumizwa na hata kuuawa. Tunajiuliza nini kimepotea kwenye tunu yetuhii? Taifa letu limekosea wapi? Je, uongozi na mamlaka husika pamoja na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimezidiwa nguvu na maarifa hata kushindwa kudhibiti hali hii? Sisi Maaskofu hatuamini kuwa makundi haya ya kihalifu yana nguvu kuliko vyombo vyetu vya ulinzi na usalama; hivyo tunaviomba vyombo vyetu hivi vitimizemajukumu yao ili kurudisha heshima ya Taifa letu ya kuwa kisiwa cha udugu na amani.
5. Tunatoa pole kwa ndugu na familia za wale waliouawa, na tunawaombea marehemu wote pumziko la amani mbinguni. Aidha, tunatoa pole kwa wale walioumizwa na kujeruhiwa katika matukio haya ya kihalifu.
6. Tunaungana na watu, taasisi na jumuiya za kimataifa kulaani na kukemea vitendo hivi vya kihalifu vya utekaji na mauaji. Pia tunaunga mkono wito wa viongozi na watu mbalimbali wa kufanyika uchunguzi wa kina na wa haraka ili wale wote waliohusika na matukio hayo wafikishwe mbele ya sheria. Pia na wale wote ambao hawakuwajibika kwa kadiri ya nafasi zao wawajibishwe.
7. Uhai ni zawadi kutoka kwa Mungu. Mtu ameumbwa kwa sura na mfano wake Mungu mwenyewe (Mwanzo 1:27). Hivyo maisha na utu wa mtu ni lazima viheshimiwe, na kulindwa kwa nguvu zote.
Udugu Kuponya Ulimwengu; Ninyi Nyote ni Ndugu