Kongamano la Tano la Ekaristi Takatifu Kitaifa, Tanzania: 11 Hadi 16 Sept. 2024
Na Padre Stefano Kaombe, Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania.
Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kitaifa na Kimataifa katika maisha na utume wa Kanisa ni katekesi angavu na endelevu inayogusa: Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji: kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo makini cha imani tendaji. Lina hitaji usikivu wa kiibada na ukimya wa kitafakari uwezeshao Neno la Mungu kugusa akili na nyoyo za watu. Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho na kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake. Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti na ni zawadi; na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani; kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha moto wa mapendo kwa Mungu na jirani. Ekaristi Takatifu ni chachu ya kukuza na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu kati ya waamini, kwa kuwa na jicho la upendo kwa maskini ndani ya jamii. Ekaristi Takatifu ni chachu makini ya Injili ya familia inayokumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini. Ekaristi Takatifu, inalisukuma Kanisa kutembea bega kwa bega na vijana wa kizazi kipya kwa njia ya utume kwa vijana, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Kimsingi, maadhimisho ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu ni kipindi cha katekesi ya kina kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu, Sala na Tafakari ya kina ya Neno la Mungu inayofanywa na Jumuiya ya waamini wa Kanisa mahalia mintarafu Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kama njia ya kuendelea kuzungumza na Kristo katika safari ya maisha ya waamini. Ni muda wa kuimarisha katekesi kuhusu Sakramenti ya Upatanisho, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.
Kanisa Katoliki nchini Tanzania limeandaa Kongamano la 5 la Ekaristi Takatifu Kitaifa kuanzia tarehe 11hadi tarehe 16 Septemba 2024 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Udugu wa kuponya Ulimwengu: “Nanyi nyote ni ndugu.” Mt 23: 8. Ujumbe wa udugu wa kibinadamu unagusa masuala mbalimbali ya kijamii, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kukimbilia Moyo Mtakatifu wa Yesu ili apate kuwaganga na kuwaponya. Kongamano hili litaadhimishwa katika metropolitani ya Dar es Salaam, kituo kikuu kikiwa ni Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Majimbo mengine yanayounda metropolitani hii ni Jimbo la Zanzibar, Tanga, Morogoro, Mahenge, Ifakara. Hili litakuwa Kongamano la tano la kitaifa mengine yakiwa Dodoma (2008), Iringa (2012). Mwanza 2016) na Tabora (2021). Kongamano hili litawajumuisha wawakilishi toka majimbo yote ya Tanzania: watoto, walei Vijana na watu wazima, watawa wa kike na wa kiume na waklero. Kituo kikuu cha Kongamano hili kitakuwa ni Msimbazi Senta, kwani watoto wao kituo chao kitakuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Msimbazi Senta ndipo mambo mengi yatakapofanyika, isipokuwa Misa ya Kilele ambayo “Statio Orbis” yake itakuwa Uwanja wa Uhuru, ulioko wilayani Temeke. Mambo mbalimbali yatafanyika kukuza uelewa, uchaji, ibada, utume na uwajibikaji wa kiekaristi wa kijamii na kimazingira. Lengo hili la Kongamano litafikiwa kwa kushiriki katika Misa, Saa Takatifu, Maungamo, Katekesi itakayotolewa juu ya mada mbalimbali zilizoandaliwa na kwa watoto kupokea Komunyo ya kwanza. Ukweli kwamba Kanisa la Tanzania litakusanyika pahala pamoja kutokana na uwepo wa Ekaristi Takatifu, ni chemchemi kubwa ya kuimarika kwa imani na kujenga hamasa ya umoja, kwani Ekaristi Takatifu ni chemchemi na kilele cha Ukristo. Washiriki wanaanza kuwasili Jumatano tarehe 11 Septemba na kurudi makwao Jumatatu tarehe 16 Septemba 2024.
Waamini wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, ambao wameshawahi kuandaa makongamano ya Ekaristi Takatifu, ngazi ya Jimbo mwaka 1998 na la kanda la Mashariki 2017, wamejiandaa vilivyo kuwa wenyeji wa tukio hili la kitaifa: waliutumia mwezi Julai kujiivisha katika kutafakari nafasi ya Ekaristi katika maisha yao binafsi na ya familia na jumuiya zao. Wameandaa wimbo na sala rasmi za Kongamano, aidha kuna vitenge, fulana, vipeperushi na mabango yanayochochea ushiriki wa tukio hili. Kwa hakika Jimbo zima kwa sasa macho na mioyo inaitazama, inaitafakari na kuwa na hamu kubwa ya kuiishi Ekaristi Takatifu na hasa kutimiza mwaliko wa dhamira yake: Udugu katika kuuponya ulimwengu: Ninyi nyote ni ndugu (Mt 23:8). Mada zitakazotolewa katika Kongamano hili ni: Ukuu wa Adhimisho la Misa, itatolewa na Askofu Simon Masondole wa Jimbo la Bunda, Udugu wa Kikristo kama nyenzo muhimu ya kuutukuza utu wa mwanadamu, itatolewa na Padre Joseph Mosha wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Ekaristi Takatifu na Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo itatolewa na Padre Benno Kikudo toka Baraza la Maaskofu Tanzania, Ekaristi Takatifu na Maadili, itakayotolewa na Askofu Christopher Ndizeye wa Jimbo Katoliki la Kahama, Ekaristi Takatifu na uponyaji katika familia, itatolewa na Padre Rogasian Msafiri, wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Changamoto za Upetentekoste itatolewa na Pd. Leonard Maliva wa Jimbo Katoliki la Iringa.
Historia ya Uinjilishaji Kanda ya Mashariki, itatolewa na Askofu Msaidizi Mstaafu wa Jimbo la Bukoba Methodius Kilaini. Mada hizi pia zitatolewa kwa upande wa watoto. Siku ya Jumamosi tarehe 14 Septemba 2024 kutakuwa na maandamano ya Ekaristi Takatifu toka viwanja vya Chuo Kikuu cha DUCE Chang'ombe mpaka viwanja vya Msimbazi Senta, yatakayopokelewa na Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora na ndiye atakayeadhimisha Misa ya siku hiyo. Misa ya ufunguzi itaadhimishwa na Askofu mkuu Jude-Thadeus Ruwa'ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam na Misa ya kilele itaadhimishwa na Askofu Wolgang Pisa wa Jimbo la Lindi, ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC. Misa hiyo ya kilele pia itashuhudia kufungwa kwa Mwaka wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka hamsini ya Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo nchini Tanzania.