Maaskofu nchini Ghana. Maaskofu nchini Ghana. 

Maaskofu:Tume lazima ihakikishe mchakato mchakato unafanyika bila upendeleo&kwa mujibu wa sheria.

Mahakama na tume ya uchaguzi lazima wafanye sehemu yao ili uchaguzi ujao ufanyike kwa amani.Ndivyo Maaskofu wa Ghana wanabainisha katika ujumbe wao kwenye matazamioa ya Uchaguzi Mkuu ujao tarehe 7 Desemba 2024.Vyombo vya habari,kwa mujibu wa maaskofu,lazima navyo vitekeleze wajibu wao kwa kutoa habari sahihi,zisizopendelea upande wowote.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika ujumbe uliotiwa saini na Rais wa Baraza la Maaskofu nchini Ghana, Askofu Mathayo Kwasi Gyamfi wa Jimbo la Sunyani, unasisitiza umuhimu wa uchaguzi mkuu ujao tarehe 7 Desemba 2024 kwamba ufanyike katika hali ya amani na kwamba ni mategemeo yao hautakuwa na hali migogoro. "Mahakama ihakikishe kuwa kura ni ya haki na kamili. Inapotokea migogoro ya uchaguzi, tunaamini kwamba mahakama itashughulikia kwa uadilifu wa hali ya juu na kuzingatia utawala wa sheria," wanabainisha maaskofu.

Ghana inachukuliwa kuwa nchi ya Utulivu lakini...

Ghana inachukuliwa kuwa nchi yenye utulivu zaidi katika Afrika Magharibi, lakini matokeo ya kura ya urais yamepingwa angalau mara mbili. Mara ya kwanza ilikuwa mnamo mwaka 2012, wakati kiongozi wa upinzani Nana Addo Dankwa Akufo-Addo wa Chama cha New Patriotic Party(NPP) alipopinga ushindi wa Rais aliye madarakani John Dramani Mahama. Mahakama ya Juu ya Ghana ilipewa jukumu la kusikiliza kesi hiyo na hatimaye ikatoa uamuzi kwa upande wa Bwana Mahama baada ya mashauri ya miezi kadhaa.

Tume ihakikishe mchakato mzuri bila upendeleo

Mnamo 2020, hali ilibadilika wakati Rais wa zamani John Dramani Mahama, ambaye sasa ni kiongozi wa upinzani, alipinga kuchaguliwa tena kwa Nana Addo Dankwa Akufo-Addo. Kama ilivyokuwa katika kesi ya mwaka 2012, mahakama iliitwa kutatua mzozo huo. Baraza la Maaskofu pia limehamasisha Tume ya Uchaguzi na kusema kwamba: "ni lazima Tume kuhakikisha kuwa mchakato wa uchaguzi unafanyika bila upendeleo na kwa mujibu wa sheria."

Onyo kwa vyombo vya habari

Vyombo vya habari, kwa mujibu wa Maaskofu, "lazima navyo vitekeleze wajibu wao kwa kutoa habari sahihi, zisizopendelea upande wowote na zenye uwiano, kuepuka mihemko inayohatarisha kuchochea migawanyiko au migogoro."  Vyombo vya habari, wanasema maaskofu, "visaidie kukuza mazingira ya uchaguzi yenye ufahamu na amani."

Wito kwa vijana kuepuka mtego wa uchochezi,chuki na vurugu

Ujumbe huo unaendelea kutoa wito kwa vijana hasa wa kutoingia katika "mtego wa uchochezi wa chuki na vurugu," na hatimaye hata "viongozi wa kimila na dini waendeleze umoja wa kitaifa na kusaidia kupunguza mivutano." Uchaguzi wa 2024 utafanyika katika mazingira magumu ya kiuchumi kwa nchi; kutokana na janga la Uviko, kukatika kwa usambazaji wa nafaka kutokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, na ukosefu wa nidhamu ya fedha na fedha, wananchi wa Ghana wanakabiliwa na mfumuko wa bei. Hatimaye, makundi ya kijihadi yanayofanya kazi katika nchi jirani sasa yanatishia kuendeleza operesheni zao hatari hadi Ghana.

12 September 2024, 14:52