2024.09.10 Ziara ya Kitume huko Timor-Leste. 2024.09.10 Ziara ya Kitume huko Timor-Leste.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa ahimiza Wakatoliki huko Timor ya Mashariki kuiishi imani yao kila siku

Baba Mtakatifu Francisko katika awamu ya tatu ya Ziara yake ya 45 ya Kitume Barani Asia na Oceania,Vatican News ilizungumza na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu la Timor ya Mashariki na Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dili kuhusu matarajio ya ziara ya Papa na changamoto zinazokabiliwa na taifa dogo la Kikatoliki huko Asia.

Na Padre  Bernardo Suate  na Lisa Zengarini - Dili

Wingi wa umati wa watu waliokusanyika katika barabara za Dili kumkaribisha Papa Francisko siku ya Jumatatu tarehe 9 Septemba 2024 aliposafiri kutoka uwanja wa ndege hadi Ubalozi wa Vatican nchini humo kwa hakika umethibitisha furaha kubwa na matarajio ya watu wa Timore ya Mashariki kwa ziara ya Papa. Baba Mtakatifu Francisko alipokuwa akijiandaa kwenda katika taifa la nusu kisiwa cha Kikatoliki linalopakana na Indonesia, Askofu Leonardo Maria Alves wa Bacau, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu la Timor ya Mashariki (CETL), aliviambia vyombo vya Vatican News, kupitia Padre Bernardo Suate kwamba waamini wa Kikatoliki nchini wamekuwa wakimngojea Baba Mtakatifu kwa hamu na wanatarajia baraka nyingi kutoka kwa Mungu, kupitia kwake. "Huu ni wakati muhimu na wa ajabu kwa watu wa Timor ya Mashariki, na hasa kwa Wakristo wa Timor," alisema, huku akisisitiza kwamba "ziara ya papa itathibitisha imani yetu katika Kristo na pia uaminifu wetu kwa Kanisa na, hasa, kwa Papa Francisko.” Askofu Alves alibainisha zaidi kwamba vijana, ambao ndio wengi zaidi wa watu na katika Kanisa, wameonesha shauku kubwa wakati wa maandalizi.

Wakati wa Misa huko Timor ya Mashariki
Wakati wa Misa huko Timor ya Mashariki

Pade  Jovito Rego: Matarajio makali kwa ziara hiyo

Naye Padre Jovito Rego alikumbuka vile vile kuwa Papa Francisko alitarajiwa kufika mnamo 2019 na wakati ziara hiyo ilipokatishwa kwa sababu ya janga la UVIKO-19,  watu wa Timore ya Mashariki walikatishwa tamaa sana. Hii ndiyo sababu, shauku yao ni kubwa zaidi sasa hasa: "Kutokana na masuala ya kiafya ya Papa wakati huu, ambapo ilikuwa vigumu kufikiria kwamba angekuja kututembelea.” Padre  Kisha Jovito alieleza jinsi walivyojitayarisha kwa ajili ya ziara hiyo, kwa njia ya vifaa kwa kushirikiana na serikali, na kiroho. Katika ngazi ya kiroho, Majimbo matatu ya nchi (Dili, Bacau na Maliana) zimeandaa mafunzo maalum ya katekisimu kuhusu wasifu wa Papa, waraka wake, utume wake kama Mrithi wa Petro na umuhimu wa ziara yake huko Timor ya Mashariki. Maaskofu pia waliandaa mafungo ya kiroho ya kitaifa juu ya mada kuu ya ziara hiyo, "Imani yako na iwe utamaduni wako," wakiakisi umuhimu wa kuunganisha imani na tamaduni kwa njia ya utamadunisho.

Wakati wa Misa huko Taci Tolu, Timor ya Mashariki
Wakati wa Misa huko Taci Tolu, Timor ya Mashariki

Changamoto katika jamii ya Timor ya Mashariki

Katika mahojiano hayo Padre wa Jimbo Kuu la Dili pia alitaja changamoto kadhaa "zisizoonekana" ambazo bado zinaikabili Timor ya Mashariki,  baada ya miongo miwili ya uhuru, ikiwa ni pamoja na "mivutano ya kisiasa, maridhiano, masuala ya maadili na ufisadi" unaoendelea. Padre huyo alisema anatumaini kuwa Papa Francisko atajifunza kuhusu hali hii na kutia moyoni mwake daima watu wa Timor  ya mashariki.

Papa akibariki mtoto
Papa akibariki mtoto

Ziara hii itahimiza Kanisa zaidi la kisinodi la Timor ya Mashariki

Hatimaye Padre  Jovito alionesha matumaini yake kwamba mada ya ziara hiyo ya Papa inaweza kuwatia moyo Wakatoliki wa Timor kuishi imani yao “si kwa maneno tu bali kwa vitendo”, wakitembea pamoja kama Kanisa la Sinodi kwa ushirika na Papa na kushiriki kikamilifu katika utume wake.

Ushuhuda Timor ya Mashariki
10 September 2024, 09:55