Papua New Guinea:Imani changamfu iliyoboreshwa na Wamisionari wa Moyo Mtakatifu
Na Claudia Torres – Port Moresby na Angella Rwezaula – Vatican.
Wamisionari wa Moyo Mtakatifu (MSC) wamedumisha uwepo wa kudumu nchini Papua New Guinea tangu kuwasili kwao tarehe 29 Septemba 1882, na kuwafanya kuwa sehemu muhimu ya historia na utume wa Kanisa Katoliki nchini humo na kuwa msingi rejea wa siku, ikiwa ni pamojakatika sekta ya elimu na afya. Hivyo ndivyo Askofu Mkuu Rochus Joseph Tatamai, MSC, Askofu Mkuu wa Rabaul, alivyothibitisha katika mahojiano kabla ya ziara ya Papa Francisko huko Papua New Guinea, kuanzia 6 hadi 9 Septemba 2024.
Katika karne ya 19, Wamisionari wa Moyo Mtakatifu walifika kutoka sehemu mbalimbali za dunia, na wakagawanya kazi yao ya uchungaji, kila kikundi kikisimamia eneo tofauti la Papua New Guinea. “Wafaransa na Waswiss walitunza maeneo yote kutoka Kisiwa cha Yule, ni Jimbo la Bereina leo hii - hadi Kerema na kurudi Daru-Kiunga na Mendi,” alielezea Askofu Mkuu. Wamisionari kutoka Australia waliangalia Port Moresby na Alotau-Sidea, wakati Wajerumani walitunza Rabaul na Kimbe.” Wamisionari wa Marekani na Ireland walifika baadaye.
Hata hivyo, Wamisionari wa Moyo Mtakatifu hawakuwa vichocheo pekee vya uinjilishaji katika siku za kwanza. Kwa sababu kuna Wamarist, Taasisi ya Kipapa ya Tume za Kigeni,(PIME) na baadaye, Wamisionari wa Neno la Mungu, pia walitekeleza majukumu muhimu. Muundo huu wa wamisionari kutoka nchi mbalimbali ulikutana na eneo kubwa tajiri tayari la nchi yenye tamaduni nyingi ya lugha zaidi ya 800, ambapo kueneza ujumbe wa Injili wa umoja kwa kila mtu halikuwa jambo rahisi. Askofu Mkuu alieleza kwamba “changamoto kuu tangu mwanzo ilikuwa changamoto ya ufahamu, kwa sababu wamisionari walipokuja, hakuna hata mmoja wao aliyezungumza lugha ya kienyeji.” Kutengwa kwa kijiografia kwa makabila mengi kulizidisha shida hii. Watu walioishi kwenye mipaka walikuwa na faida ya kuzungumza lugha kadhaa kwa sababu ya uhusiano wao na mipaka na makabila tofauti,” alieleza, wakati wale walio katika maeneo ya mbali zaidi hawakufanya hivyo."
Hata hivyo "Ili kushinda changamoto hiyo, wamisionari waliishi kati ya watu na kujifunza lugha yao. Kwa kufanya hivyo, alieleza Askofu Mkuu, wamisionari waliweza “kuelewa ulimwengu wa ndani, mtazamo wa ulimwengu wa Melanesia wa watu, na hivyo kubadilisha kizuizi kuwa fursa ya uinjilishaji. “Kwangu mimi, ni jambo la maana sana hivi kwamba wamisionari wa kwanza, ingawa Mtaguso wa Vatican ulizungumza juu ya kueneza kiutamaduni mwishoni mwa miaka ya 1960, Wamisionari wa kwanza wa Moyo Mtakatifu waliokuja kwenye ufukwe wetu, ingawa inawabidi kushinda kizuizi cha kujaribu kuelewa lugha, wao walitumia mara moja lugha na desturi, maadili ya kiutamaduni, ili waweze kujaribu kuona muungano na hasa kujaribu kutangaza Habari Njema kwa watu.”
Mahojiano yaligeukia hata sura ya Mwenyeheri Peter To Rot, ambaye alitangazwa mwenye heri na Papa Yohane Paulo wa Pili tarehe 17 Januari 1995. Wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, Katekista mlei, ambaye wazazi wake walikuwa miongoni mwa watu wa kwanza katika Papua New Guinea kubatizwa na Wamisionari wa Moyo Mtakatifu, alifundisha imani ya Kikatoliki kwa jumuiya mahalia na kukaidi amri kutoka kwa majeshi ya Japan. Kwa hiyo alikamatwa na hatimaye akauawa kishahidi na polisi wa Japan. “Mwenyeheri Peter To Rot,” alisema Askofu Mkuu Tatamai, ambaye babu yake alikuwa kaka yake Peter To Rot, “kwangu anawakilisha ushirikiano mkubwa kati ya wamisionari na makatekista. Na katekista ni mtu wa kati anayeelewa utamaduni wa mahali hapo na watu.
Na mmisionari huzungumza kila mara na katekista. Na katekista ndiye anayewasiliana na kurahisisha mambo haya kwa wenyeji na utamaduni wa mahali hapo.” Papa Francisko ametoa idhini ya kutangazwa kwa Mwenyeheri kuwa mtakatifu, ingawa tarehe bado haijapangwa. "Watu wamefurahi sana na wana uhakika sana kwamba kile Peter To Rot anawakilisha kwa ajili yetu, kiukweli, ni Kanisa la Papua New Guinea na Melanesia, na hasa Mkutano wa Visiwa vya Solomon vya Papua New Guinea," alisema Askofu Mkuu. Anaangazia waamini na mchango wao katika kazi ya ubinadamu. Na chochote ambacho Kanisa la Papua New Guinea linaweza kutoa wakati huu kwa hakika ni msisitizo wa hali ya kiroho ya walei na ushiriki hai katika kazi ya uinjilishaji”.
Kadhali Askofu Mkuu alibainisha kwamba Papa Francisko mwenyewe amewaambia wamisionari kwamba “Peter To Rot anawakilisha aina ya mtakatifu tunayemhitaji leo hii kwa ajili hasa ya changamoto zinazoiba uzuri wa sakramenti ya ndoa na msingi wa jamii zote na maisha ya familia. Askofu Mkuu alihitimisha kwa kueleza matumaini yake kuhusu ziara ya Papa Francisko ,kwamba anaona "uamsho mkubwa zaidi na ufufuo wa imani kati ya wazee, na watu wazima, lakini pia kati ya kizazi chetu cha vijana," hata kama tunaweza kuwa mbali na pembezoni, tuna Kanisa zuri, tuna imani thabiti na vijana wetu bado wanajaa makanisani.