Papua New Guinea,Kard.Ribat:Papa ni Nuru ya matumaini iletayo amani!
Na Kardinali John Ribat.
Ziara ya Papa Francisko huko Port Moresby itakuwa tukio kubwa. Jimbo hilo limegawanywa katika parokia 22 na Parokia 19 ziko mjini, na zingine ziko vijijini. Kuna jumla ya wakazi 500,000. Wamisionari wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, ambapo mimi ni mshirika wao, walifika Papua New Guinea mnamo mwaka wa 1882. Walianzisha parokia ya kwanza huko Rabaul mwaka huo. Kisha, miaka mitatu baadaye, katika mwaka 1885, wamisionari walifika kwenye Kisiwa cha Yule. Wengi wao walitoka Ufaransa, lakini pia kulikuwa na wamisionari wa Ujerumani, Marekani, Italia, Hispania na Uswisi. Walifanya kazi kubwa, na tangu wakati huo, Kanisa la mahali hapo limekua. Tutakuwa na idadi kubwa ya watu wanaokuja hapa kwa ziara ya Papa kutoka sehemu nyingine za nchi.
Kwa mfano, takriban watu 100 watawasili kutoka Jimbo kuu la Mount Hagen katika Milima ya Juu. Watatembea hadi Kerema na kutoka hapo watachukua barabara ya Port Moresby. Itachukua kama siku tano. Hivi sasa majimbo mawili pekee yanayofikiwa na Port Moresby kwa barabara ya Kerema na Bereina. Kwa wengine, unaweza kuruka kwa ndege au kusafiri kwa mitumbwi, baharini. Kwa vyovyote itakavyokuwa, waamini watafanya kila juhudi kukutana na Papa. Ndiyo maana tunajaribu kupanga kuwapokea watu wanaoingia. Tutatumia shule na parokia zetu kuwakaribisha. Kama Maaskofu wa Papua New Guinea na Visiwa vya Solomon, tutakuwa na Mkutano na Baba Mtakatifu Jumamosi, tarehe 7 Septemba 2024, pamoja na mapadre, mashemasi, wanaume na wanawake waliowekwa wakfu, waseminari na makatekista. Siku hiyo hiyo, Papa atakutana na watoto waliotengwa, watoto wa mitaani, wale wanaoteseka, wale ambao wameathiriwa na ulemavu, viziwi na upofu. Hasa, Papa atatembelea watoto wanaosaidiwa na Huduma ya Mtaa, ofisi ya kichungaji niliyoanzisha mwaka wa 2010, na “Callan Services”, ambayo ilianzishwa na Shirika la Ndugu Wakristo. Kwa njia hiyo, sote tunafanya kazi pamoja kuwatunza watoto hawa wote katika hali hizo walizomo. Katika Jimbo letu kuna mazungumzo ya kiekumene na ya kidini, ikijumuisha na Waislamu, Wahindu na Wabaha’i. Tunapoingia katika mazungumzo haya, kuna hali ya kujuana, kuheshimiana, kukubaliana. Hii hutuleta pamoja kwa amani na huturuhusu kufanya kazi pamoja, na ni nzuri.
Hivi karibumi tulikuwa na mkutano na wote, na mada ya mkutano wetu ilikuwa: “Wafanyie ndugu zako kile unachotaka wakufanyie. Tulitafakari kuhusu Kanuni Bora, yaani, “kuwatendea wengine mema, nao wataweza kukufanyia vivyo hivyo”. Ilikuwa ya kututajirisha sana, ikituunganisha, na kutusaidia kuweza kuendelea kujenga uhusiano ambao msingi wake ni kutenda mema, na huyu mwema kwetu ni Kristo. Hiyo ilikuwa nzuri sana. Kuna shida: mnamo Mei mwaka huu, kulikuwa na maporomoko makubwa ya ardhi, na mali nyingi ziliharibiwa. Huko Port Moresby, kuna vurugu, uporaji na mauaji. Changamoto yetu kuu ni kujaribu kuishi kwa amani. Ndiyo maana tunatazamia jambo hili, tunapoona kwamba hii itakuwa ziara inayoleta nuru, inayoleta tumaini, inayoleta baraka, na hivyo, inayoleta upya. Upya kwa maana inatutia moyo kuweza kuanza upya ili kuweza kufanya jambo chanya na jema kwa taifa letu.
Tulikuwa tunatafuta fursa na ujio wa Baba Mtakatifu ni fursai. Kama Padre wa Kristo, zaidi ya hayo, Papa ni kwa ajili yetu tumaini kubwa, njia ya kutuletea nguvu na amani, kwa sababu tumepitia magumu haya yote, na si rahisi. Lakini hili ndilo tumaini letu sasa. Tunatumaini kwamba uwepo wa Baba Mtakatifu utaleta kitu ambacho ni kizuri, kitu chanya, kitu cha amani, kitu ambacho kinatuunganisha sisi sote, na pia kinachotufanya upya kuanza kufanya kazi pamoja tena, kujenga Papua New Guinea katika roho mpya: roho ya amani, roho ya msamaha na roho ya upendo.