Masomo ya dominika ya 23 ya Mwaka B wa Kanisa yanatukumbusha wajibu wa kuiishi imani yetu kwa maneno na mtendo, kuwafariji kwa kuwahudumia wahitaji kwa moyo wa upendo na ukarimu Masomo ya dominika ya 23 ya Mwaka B wa Kanisa yanatukumbusha wajibu wa kuiishi imani yetu kwa maneno na mtendo, kuwafariji kwa kuwahudumia wahitaji kwa moyo wa upendo na ukarimu   (ANSA)

Tafakari Dominika ya 23 ya Mwaka B wa Kanisa: Jipeni Moyo Msiogope!

Masomo ya dominika hii yanatukumbusha wajibu wa kuiishi imani yetu kwa maneno na mtendo, kuwafariji kwa kuwahudumia wahitaji kwa moyo wa upendo na ukarimu na kufanya juhudi ya kuwasaidia waondokane na hali ya unyonge, umasikini, hofu na mashaka ili nao waweze kuendelea na kusonga mbele kimaisha, waishi kwa furaha na amani. Ujumbe huu umejikita katika maneno haya; “Jipeni moyo, msiogope.” Mwenyezi Mungu ni Mwenye haki, atatukirimia mema!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 23 Mwaka B wa Kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatukumbusha wajibu wa kuiishi imani yetu kwa maneno na mtendo, kuwafariji kwa kuwahudumia wahitaji kwa moyo wa upendo na ukarimu na kufanya juhudi ya kuwasaidia waondokane na hali ya unyonge, umasikini, hofu na mashaka ili nao waweze kuendelea na kusonga mbele kimaisha, waishi kwa furaha na amani. Ujumbe huu umejikita katika maneno haya; “Jipeni moyo, msiogope.” Tukifanya hivyo Mungu atatukirimia zaidi maana yeye ni mwenye haki kama zaburi ya wimbo wa mwanzo inavyosema; “Ee Bwana, wewe ndiwe mwenye haki, na hukumu zako ni za adili. Kama zilivyo rehema zako umtendee mtumishi wako” (Zab. 119:137, 124). Hivyo hatuna budi kusaidiana maana sisi sote ni ndugu, sisi sote ni watoto wa Mungu. Ni kwa tumaini hili mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali na kuomba hivi; “Ee Mungu, umetuletea ukombozi na kutufanya watoto wako. Ututazame kwa wema sisi wanao wapenzi, utujalie uhuru wa kweli na urithi wa milele sote tunaomwamini Kristu”. Somo la kwanza ni la Kitabu cha Nabii Isaya (35:4-7a). Katika somo hili Nabii Isaya anawafariji watu wake kuwa mda umewadi Mungu atawaaokoa na kurudisha katika nchi yao kutoka uhamishoni Babeli. Maneno ya Nabii Isaya ni mazito na ya faraja kubwa ni vyema kuyasikiliza. Anasema hivi; “Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi. Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa. Ndipo mtu aliye kilema ataruka-ruka kama kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba; maana katika nyika maji yatabubujika; na vijito jangwani. Na mchanga ung’aao mfano wa maji utakuwa ziwa la maji, na nchi yenye kiu itakuwa chemchem za maji.”

Dominika ya 23 Mwaka B: Huruma, Ukaribu na Mshkamano
Dominika ya 23 Mwaka B: Huruma, Ukaribu na Mshkamano

Huko kukombolewa kwa Israeli toka utumwani Babeli ni mfano wa kukombolewa kwetu toka utumwa wa dhambi na mauti. Ni katika muktadha huu Mzaburi katika wimbo wa katikati anapaza sauti akisema; “Ee nafsi yangu umsifu Bwana. Bwana ndiye ashikaye kweli milele, huwafanyia hukumu walioonewa. Huwapa wenye njaa chakula, Bwana hufungua waliofungwa. Bwana huwafumbua macho waliopofuka, huwainua walioinama. Bwana huwapenda wenye haki, huwahifadhi wageni. Bwana huwategemeza yatima na mjane, bali njia ya wasio haki huipotosha. Bwana atamiliki milele, Mungu wako Ee Sayuni, kizazi hata kizazi” (Zab 146:1, 7-10). Somo la Pili ni la Waraka wa Yakobo kwa Watu Wote (2:1-5). Katika somo hili ujumbe Mtume Yakobo ni huu kuwa mbele ya Mungu binadamu wote, tajiri na maskini, wote ni sawa. Hivyo kusiwe kamwe na upendeleo wowote katika maswala ya imani miongoni mwa waamini. Mbele za Mungu, mtu tajiri na mwenye mavazi mazuri hana tofauti na mtu maskini, mwenye mavazi mabovu, wote ni sawa, wote wanamuhitaji Mungu kwa ajili ya uzima wao. Hivyo sio sahihi kumstahi aliyevaa mavazi mazuri na kumketisha mahali pazuri na maskini asimame, au aketi miguuni pa wengine. Yakobo anatukumbusha kuwa Mungu huwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao. Hivyo matajiri wasipendelewe kwa vyovyote vile kwa gharama za maskini.

Jipeni moyo msiogope
Jipeni moyo msiogope

Injili ni kama ilivyoandikwa na Marko (7:31-37). Sehemu hii ya Injili inahusu simuliza la Yesu kumponya kiziwi mwenye utasi. Uponyaji huu ni ashirio la kuanza kutimia kwa utabiri wa nabii Isaya kuwa; “Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa” (Isaya 35: 4-7). Kutoka katika tukio hili la uponyaji, mama Kanisa amechota humo tendo la mbatizwa kuguswa masikio na midomo yake kwa kidole gumba na mhudumu wa Sakramenti ya ubatizo huku akisali na kumwombea kwa sala hii akisema; “Bwana Yesu, aliyewafanya viziwi wasikie, na bubu waseme, akujalie uweze kusikia kwa masikio neno lake, na kuungama kwa mdomo imani ya kikristo, kwa sifa na utukufu wa Mungu Baba.”  Kumbe tunaona masomo yote katika dominika hii yana ujumbe wa matumaini kwa binadamu anayeteseka kwa matatizo na mahangaiko ya mateso. Matatizo ya kimaisha: uchumi mbaya, uhaba wa chakula, kukosa ajira au kazi zenye tija, manyanyaso kazini, matatizo ya kiafya, kufiwa, kubaki yatima, kubambikiziwa kesi, kutotendewa haki mahakamani, matatizo ya ndoa na familia, kukosa watoto; haya yote yanayotutia hofu, mashaka na wasiwasi. Tunahitaji kuisikia tena sauti ya Nabii Isaya; “Jipeni moyo, msiogope”. Lakini sauti tu haitoshi. Lazima ifuatane na matendo ya kusaidiana kuondokana na shida na matatizo haya. Lazima kuwe na mipango mikakati ya kimatendo kuwasaidia wenye hofu na mashaka kwa moyo wa upendo na ukarimu, sio tu kuwapatia misaada bali kuondoa mazingira na hali zinazowafanya wawe na hofu, mashaka na wasiwasi.

Injili ya huruma na upendo
Injili ya huruma na upendo

Zipo sababu nyingi zinazosababisha hofu, mashaka na wasiwasi kama vile: uwepo wa mila, tamaduni, sheria na taratibu kandamizi na za kujipendelea. Tufanye nini? Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika Waraka wake wa Kitume “Caritatis in Veritate” yaani “Ukweli katika Upendo” anatutaka sote tuwe na ukarimu katika ukweli. Inawezekana wengine wamekuwa maskini kwa sababu ya kukosekana ukweli katika ukarimu. Ukarimu unatolewa usipohitajika au pale panapokuwa na mwanya wa faida binafsi. Huwezi kujifanya mkarimu kwa kutoa nafasi za kazi kwa wasiostahili kwa kupokea rushwa, ukiwanyima wengine haki yao ya kupata kazi. Wengine wamekuwa ombaomba kwa sababu haki yao imechukuliwa na walionacho zaidi. Inawezekana watu wamekuwa maskini, wanakosa huduma za kijamii kwa sababu viongozi wamekula na wanaendela kula rasilimali za umma na kujinufaisha wao wenyewe, mbaya zaidi kwa kumwaga damu za waliopaswa kunufaika nazo. Kumbe, tunapswa kutenda kaki kabla ya ukarimu. Hakuna ukarimu kama hakuna haki. Kama tukiwanyima watu fursa na nafasi za kujiendeleza kimaisha na hivyo tukawa sababu ya wao kuwa maskini hatuwezi kujifanya wakarimu kwao kwa kuwapatia misaada. Ndiyo maana Mtakatifu Ambrose aliwahi kusema hivi; “Chochote unachompatia maskini kama msaada kutoka katika ziada uliyonayo, hilo sio tendo la huruma na ukarimu, bali unamrudishia haki yake uliyomwibia”. Jamii inapaswa kuondoa utegemezi kwa kuweka mipango mikakati yenye tija kwa wote kwa haki. Jambo la msingi sio kujifanya sauti za bubu na masikio ya viziwi.

Jipeni Moyo Msiogope
Jipeni Moyo Msiogope

Tusijifanye kuongea kwa niaba yao, au kusikia kwa niaba yao “tuwafanye waongee, tuwafanye wasikie” kwa kuwapatia haki zao na fursa katika ajira ili wajiendeleze na kujitegemea. Haya yatawezekana kama tukiwa na viongozi wanaodhubutu kujitoa kwa moyo wote katika kweli na haki kwa ajili ya kuwatumikia na kuwahudumia watu. Tunahitaji viongozi wanaoweza kuwaaambia watu kwa vitendo; “Jipeni moyo, msiogope”. Viongozi wanaobeba maisha ya watu katika mioyo yao. Viongozi wanaotambua haki za kila mtu. Viongozi wanaotunga sheria za haki zisizowakandamiza wengine kwa maslahi yao binafsi. Viongozi wasio na upendeleo, wanaotoa fursa sawa kwa wote na kugawana pato la taifa kwa usawa bila kujali jinsia, ukabila, udini au uchama. Basi tumwombe Mungu atupatie moyo wa ukarimu, haki, na upendo, kwa maana kutoka ndani ya mioyo yetu ndimo yanaweza kutoka mema au mabaya yategemea tumeijaza nini mioyo yetu (Mk 7: 15-23). Tuishi kwa umoja anaouomba mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu akisali hivi; “Ee Mungu, uliye asili ya ibada ya kweli na amani, tunakuomba utuwezeshe kukuheshimu vema kwa sadaka hii na kwa kulishiriki fumbo hili takatifu tuunganike kabisa tuwe moyo mmoja”. Ili tusienende katika giza tumfuate Kristo maana yeye anatuahidi hivi katika antifona ya Komunyo: “Mimi ndimi nuru ya ulimwengu; yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima” (Yn 8:12). Daima tutambue kuwa bila neema na baraka za Yesu wa Ekaristi sisi hatuwezi chochote. Ndiyo maana mama Kanisa katika sala baada ya komunio anasali hivi kwa matumaini; “Ee Bwana, sisi waamini wako umetulisha neno lako na kututia uzima kwa chakula cha sakramenti hii takatifu. Utuwezeshe kuendelea kwa msaada wa neema nyingi za Mwanao mpenzi, hata tustahili kushirikishwa daima uzima wake.” Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari D 23 Mwaka B

 

04 September 2024, 11:17