Tafuta

Kiini cha ujumbe wa masomo ya dominika hii ni kukwepa vishwishi, kutowakwaza wengine na umuhimu wa kuyakubali, kuyapokea na kuyabeba magumu katika maisha. Kiini cha ujumbe wa masomo ya dominika hii ni kukwepa vishwishi, kutowakwaza wengine na umuhimu wa kuyakubali, kuyapokea na kuyabeba magumu katika maisha.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika 24 ya Mwaka B wa Kanisa: Kuubeba Vyema Msalaba Wako!

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 24 ya mwaka B wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Kiini cha ujumbe wa masomo ya dominika hii ni kukwepa vishwishi, kutowakwaza wengine na umuhimu wa kuyakubali, kuyapokea na kuyabeba magumu tunayokumbana nayo katika kuishuhudia imani yetu ndiyo kujikana na kujitwika msalaba kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu na sisi kutakatifuza ili tuweze kustahilishwa kuurithi uzima wa milele. Msalaba wa maisha!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 24 ya mwaka B wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Kiini cha ujumbe wa masomo ya dominika hii ni kukwepa vishwishi, kutowakwaza wengine na umuhimu wa kuyakubali, kuyapokea na kuyabeba magumu tunayokumbana nayo katika kuishuhudia imani yetu ndiyo kujikana na kujitwika msalaba kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu na sisi kutakatifuza ili tuweze kustahilishwa kuurithi uzima wa milele. Ni katika tumaini hili mzaburi katika wimbo wa mwanzo anasema hivi; “Ee Bwana, uwape amani wakungojao, ili watu wawasadiki manabii wako; usikilize sala ya mtumwa wako, na ya taifa lako Israeli” (27:30-28: 1-7). Naye Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali na kuomba akisema; “Ee Mungu uliye mwumba na mwongozi wa vitu vyote ututazame. Utuwezeshe kukutumikia kwa moyo wote, ili tupate baraka ya huruma yako.” Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Isaya (50:5-9). Somo hili ni utabiri wa wasifu wa mtumishi wa Mungu. Mtumishi huyu ni mwema, aliye tayari kutega sikio lake ili asikie na kufahamu vema mapenzi ya Mungu, ili aweze kumtumikia vyema. Lakini huko kumtumikia Mungu kunamletea mateso na madhulumu na mwisho kifo, tena kifo cha aibu kabisa. Katika mateso yake atabaki imara na mwaminifu kwa Mungu. Ndiyo maana aliwatolea wapigao mgongo wake, na wang’oao ndevu mashavu yake; hakuficha uso wake usipate fedheha na kutemewa mate, akitumaini kuwa Mungu atamsaidia, ndiyo maana anasema hivi; “Maana Bwana Mungu atanisaidia,” hivyo ana uhakika kabisa kuwa Bwana atamsimamia kwa sababu hiyo hakutahayari, bali aliukaza uso wake kama gumegume, wala hakuona haya maana aliamini kuwa; Mungu yuko upande wake, na hakuna atakayeshindana naye?

Kuwa Mfuasi wa Kristo: Kujikana na Kujitwika Vyema Msalaba
Kuwa Mfuasi wa Kristo: Kujikana na Kujitwika Vyema Msalaba

Mababa wa Kanisa waliona tangu mwanzo katika utabiri huu sura ya Yesu Kristo Bwana na Mwokozi wa maisha yetu, aliyeteswa na akafa kwa ajili yetu sisi ili tupate kukombolewa kutoka utumwa wa dhambi na mauti. Kama Kristo Mwokozi wetu, hatupaswi kuwa na mashaka wala kuogopa maana Mungu daima yuko upande wetu kama anavyosisitiza mzaburi katika wimbo wa katikati akisema; “Nitaenenda mbele za Bwana katika nchi za walio hai. Nampenda Bwana kwa kuwa ananisikiliza, sauti yangu na dua zangu. Kwa maana amenitegea sikio lake, kwa hiyo nitamwita siku zangu zote! Kamba za mauti zilinizunguka, shida za kuzimu zilinipata. Niliona taabu na huzuni, nikaliitia jina la Bwana; Ee Bwana, Mungu wangu, uniokoe. Bwana mwenye neema na haki. Naam, Mungu wetu ni mwenye rehema, Bwana huwalinda wasio na hila, nilikuwa taabuni, akaniokoa. Maana ameniponya nafsi yangu na mauti, macho yangu na machozi, na miguu yangu na kuanguka. Nitaenenda mbele za Bwana, katika nchi za walio hai” (Zab. 116: 1-6, 8-9). Somo la pili ni la Waraka wa Yakobo kwa watu wote (2:14-18). Katika somo hili mtume Yakobo anatufundisha kuwa imani lazima iendane na matendo ili iweze kutuletea wokovu. Imani isiyoendana na matendo haiwezi kumwokoa mtu. Matendo ya huruma ya kimwili na kiroho ndiyo yanayodhihirisha imani yetu. Na imani bila matendo, imekufa nafsini mwake. Ili imani yetu iwe hai na ituokoe ni lazima matendo yetu yamtangaze Kristo na kumpeleka kwa watu. Sisi wenyewe tuwe vyombo vya kumtangaza Kristo kwa wenzetu. Matendo yetu yatutambulishe kwa watu kuwa tunamfuata Kristo.

Msalaba wa Kristo Yesu ni chemchemi ya uadilifu na utakatifu wa maisha
Msalaba wa Kristo Yesu ni chemchemi ya uadilifu na utakatifu wa maisha

Injili kama ilivyoandikwa na Mwinjili Marko (8:27-35). Katika sehemu hii ya Injili Yesu anafafanua Umasiha wake kuwa amekuja kuwakomboa watu kwa mateso na kifo. Hivyo yeyote anayetaka kuwa mfuasi wake lazima awe tayari kuteswa pamoja naye. Fundisho hili Yesu analitoa akiwa njiani kuelekea katika vijiji vya Kaisara Filipi baada ya kuwauliza swali hili mitume; “Watu huninena mimi kuwa ni nani?” Nao wakatoa majibu kadiri walivyosikia watu wakisema yaweza kuwa ni; Yohana Mbatizaji, Eliya au mmojawapo wa manabii. Baada ya majibu kutoka kwa watu, Yesu aliwauliza mitume wake; “Na ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani?” Ndipo Petro alipojibu kuwa; “Wewe ndiwe Kristo Mwana wa Mungu aliye hai.” Baada ya hapo akaanza kuwafundisha kwamba imempasa kuteswa mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka. Mitume hawakuelewa fundisho hilo. Hapa yakaanza makemeo kati ya Yesu na Petro. Petro alimtoa Yesu pembeni na kumkemea kuwa haiwezekeani hilo limtokee. Yesu naye akamkemea Petro mbele ya wanafunzi wengine akimwambia; “Nenda nyuma yangu, Shetani; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu”. Kisha akatoa masharti na mwongozo wa yeyote anayetaka kuwa mfuasi wake kuwa ni lazima; “Ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, amfuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili ya Kristo na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha.”

Kristo Yesu ndiye yule Mtumishi mwaminifu
Kristo Yesu ndiye yule Mtumishi mwaminifu

Swali na fundisho la Yesu ni la nyakati zote. Nasi kila mmoja katika nafsi yake anapaswa kutoa jibu la “Yesu ni nani katika maisha yake?” Je, ni Kristo mwana wa Mungu, Bwana na mwokozi wa maisha yangu? Je, niko tayari kujikana, kujitwika msalaba wangu na kumfuata ili kuiponya nafsi yako? Yesu alimwambia Petro rudi nyuma yangu shetani kwa kuwa alitaka kumshawishi asitekeleze mapenzi ya Mungu. Ni fundisho kwetu tusifanye mzaha na vishawishi vinavyotufanya tushindwa kuyafanya mapenzi ya Mungu. Vikemee vishawishi kwa sauti ya ukali ili viweze kuondoka nawe ubaki imara katika njia ya Bwana. Daima shetani anakuja kwa sura na namna mbalimbali. Anaweza kuja kwa sura ya mwanamke, mwanaume, pombe, pesa, rushwa, madaraka, uchovu, mali au njaa. Lengo ni kukufanya usitimize mapenzi ya Mungu. Vikemee kwa ukali na umtegemee Mungu, naye atakuokoa. Tukumbuke kuwa Msalaba waweza kuwa ni maumivu ya kuacha vionjo vibaya, tamaa mbaya, fikra mbaya na maamuzi mabaya na kujikita katika kuyaishi mashauri ya Injili kwa ajili ya uzima wa milele. Tunaalikwa kuachana na uroho wa kujilimbikizia chakula na mali wakati wengine wanakufa kwa njaa. Kuachana na uroho na uchu wa madaraka, heshima na umaarufu unaowafanya wengine wateseke. Tusisahau kuwa tumekombolewa kwa fumbo la msalaba; mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo.

Msalaba wa Kristo Yesu ni chemchemi ya uadilifu na utakatifu wa maisha
Msalaba wa Kristo Yesu ni chemchemi ya uadilifu na utakatifu wa maisha

Ndiyo maana masharti ya kunufaika na Fumbo la Msalaba ni kujikana mwenyewe, kujitwika msalaba, na kumfuata Kristo Yesu. Hali yetu ya kibinadamu haipendi kusikia na kuuona Msalaba na hivyo tunauonea aibu. Tumwombe Mungu Roho Mtakatifu atuondolee aibu juu ya Msalaba. Tumwombe aijaze mioyo yetu nguvu na ujasiri ya kuitwaa misalaba yetu, kuichukua kwa ushujaa na kuibeba kwa hiari ikiwa katika umbo la ugonjwa, shida na taabu za kila namna, tupate nguvu za kuuchukua ili tuweze kuwa wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo na mwisho tuurithi uzima wa milele. Ndivyo anavyotuombea Mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu akisali hivi: “Ee Bwana, uridhike na dua zetu; uipokee kwa wema dhabihu yetu sisi watumishi wako, ili kitu alichokutolea kila mmoja wetu kwa heshima ya jina lako, kitufae sote kwa wokovu”. Hii ni kwa sababu kwa nguvu zetu wenyewe hatuwezi chochote. Ndiyo maana katika sala baada ya Komunyo mama Kanisa anatuombe neema za Mungu akisali hivi kwa matumaini makubwa; “Ee Bwana, tunakuomba nguvu ya neema zako za mbinguni itujaze mwili na roho, ili tusitawaliwe na tamaa zetu, ila tu na nguvu hiyo.” Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari D 24
13 September 2024, 15:59