Tafakari Dominika ya 24 ya Mwaka B wa Kanisa: Wewe Ndiwe Kristo Yesu!
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Mpendwa msikilizaji na msomaji wetu dominika hii ya 24 tunaulizwa swali la utambulisho wetu na jinsi tunavyojifahamu wenyewe, “Je watu husema ya kuwa mimi ni nani”? Hili ni swali ambalo Yesu aliwauliza wanafunzi wake ( Mathayo 16:13-28; Luka 9:18- 21 na Marko 8:27-38), Wao waimjibu kuwa watu wanamtambua kwa njia mbalimbali, ila wao walimtambua yeye ni Kristo wa Bwana... jibu lililokuwa sahihi. Naye Yesu aliwakatazia wasimwambie mtu ukweli ule kwa wakati huo ... Habari hii ina tupa maswali mengi; Hivi Yesu hataki ajulikane yeye ni nani? Au Je,Alikuwa na wasiwasi wa ni jinsi gani watu waivyokuwa wana mtambua? .....Mara nyingi sisi tunakuwa na wasiwasi sana kuhusu ni jinsi gani watu wanavyo tuchukulia. Tunapotimiza amri “shika kitakatifu siku ya Bwana”, siku aliyoitakatifuza Mwenyewe, tunapomtafakari Yeye na makuu yake tunaongozwa na swali la Kristo “watu huninena mimi kuwa ni nani? Na ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani?”
UFAFANUZI: Injili leo (Mk 8:27-35) inasimulia kuwa Kristo Yesu akiwa safarini kuelekea Yerusalemu anapita Kaesaria Filipi. Kijiji hiki kinasadikika alizaliwa mungu wa kigiriki PAN aliyekuwa mungu wa asili na maumbile (nature), ndipo penye chanzo cha mto Yordani na kulikuwa na sanamu kubwa ya Kaisari wa Roma aliyeabudiwa kama mungu. Sanamu hiyo iling’aa ilipomulikwa jua la asubuhi na kuwakumbusha watu kuwa Kaisari ni bwana, mtawala na mungu wao. Inashangaza kuwa ni katika eneo kama hili la kipagani kabisa ndipo Mt. Petro alipoweza kumtambua Masiha/Kristo wa Bwana. Aliweza kuona utofauti mkubwa ndani ya Seremala huyu wa Nazareti na kumtaja kuwa Masiha/Mpakwa wa Bwana. Kwa nini Kristo aliuliza swali hili? Tazama, alikuwa anaelekea kuteswa, kufa na kufufuka ili aukomboe ulimwengu, aanzishe Kanisa halafu aondoke zake kimwili. Kwa swali hili alitaka kujua mafundisho yake ya miaka 3 yamezaa matunda yoyote katika watu? au ndio alikuwa anapoteza muda na nguvu zake somo halikueleweka tunaweza sema ni swali la kupima uelewa mwa mwanafunzi.
Swali la 1, “watu…” linaonesha wengi walikuwa bado kumuelewa Yeye ni nani, lakini majibu tofautitofauti yanayotoka yanaonesha walimuona siyo mtu wa kawaida, yupo tofauti na wao, ana kitu cha pekee. Anapowauliza “Na ninyi…” ndipo Petro anatoa jibu sahihi na hapo Kristo anafurahi kwamba walau KAZI YAKE HAIJAENDA BURE. Hata hivyo anawakataza wasiseme Yeye ni Masiha, kwa nini? Mosi alitaka kuwafundisha Petro na wenzake ni nini maana ya Masiha, na pili kuwafanya kwanza waelewe amekuja kufanya nini duniani, kazi gani aliyokuwa nayo mkononi na umuhimu wake ambayo bado ilikuwa haijaeleweka kabisa ndio maana Petro anamkemea Yesu kuhusu kuteswa na anaonekana “shetani…” mpingaji wa mpango wa ukombozi. Masiha ni nani, wao walimtazamia Masiha yupi? Yesu ni Masiha wa namna gani? na yafahamike haya kwanza ndipo isemwe wazi Yeye ndiye Masiha.
Swali la Kristo linatuhusu pia. Swali la 1, “Watu…” linaonesha Mitume walipaswa kujua huko nje watu wanasemaje juu ya Yesu, ndio maana walijibu vizuri hivi yatupasa kuelewa huko nje Kristo anaonekanaje, kutambua watu wa dini nyingine wanamchukuliaje: waislamu, wabudha, wahindu, wayahudi, dini ya asili nk. Ni swali linalohamasisha ushiriki wetu kwenye mambo ya jamii, tamu na chungu zake. Swali la 2 “Na ninyi…” linatuhusu sisi mitume, yaani wakristo, tunamchukuliaje Kristo? ni nani? na kwa vile tupo katika madhehebu mbalimbali Je, tunamuelewa Kristo katika namna moja? Katika mazingira hayo tutaweza kweli kumjibu Kristo kuwa Yeye ni nani? Sisemi tubadili madhehebu yetu hapana, hilo ni jambo baya, ni mahangaiko tu, ishara wazi kuwa mwenzetu huyu hana msimamo, hana imani ya kutosha, anam-beep tu Mungu, ndio maana leo yupo Kanisa hili kesho lile na keshokutwa lile kule. Kila dini ina sadaka zake, ina magumu yake, YESU NDIYE MASIHA/KRISTO tujitulize kwake. Tusihamehame madhehebu, muda wa maisha yetu duniani ukiisha kwisha na sisi kuitwa na Baba tutawapa shida wenzetu, kugombea marehemu, “Hapana huyu ni mkatoliki…” “No no no ni mlutheri huyu tena ni mzee wa Kanisa” “Siwaelewi, huyu alikuwa msabato safi kabisa, ni lazima azikwe kisabato”... Msimamo wako na ujulikane, tena msimamo thabiti.
“Na ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani…” Je, tunalo jawabu kama Mt. Petro? tunaelewa kweli Yeye ni nani na anataka nini kwetu? Mbona tunamkosea kwa uzito wetu? hatutimizi wajibu zetu kama wakreli, watawa, wanandoa, wafanyakazi, wakulima, wanafunzi, vijana na watoto? Haitoshi kusema ‘Yesu ni Bwana, ni Masiha, Mwana Wa Mungu’. Hilo anaweza sema yeyote hata asiyeamini, muhimu ni kumuishi huyo tunayemkiri... namna gani? Mosi kwa kuwa wafuasi kamili tukichukua misalaba nyuma Yake. Kituo II Njia ya Msalaba namba 2 chaeleza msalaba waweza kuwa jirani, jamaa, wazazi, kazi, joto, baridi, njaa, kiu, vishawishi, magonjwa, wajibu kwa Mungu kwa uma na kwa Kanisa, tupokee yote kwa ukarimu bila kunung’unika tukiyabeba vema. Halafu tuzingatie mausia ya Masomo la Kwanza (Isa 50:5-9) na Somo la Pili (Yak 2:14-18). Nabii Isaya anasema tukaze nyuso kama gumegume kuelekea Yerusalemu yaani kufuata njia ya Mungu sio ya wanadamu, ya mbingu siyo ya ulimwengu wenye udanganyifu, ushawishi na kupoteza. Mt. Yakobo anatufundisha kumkiri Yesu kuwa ni Masiha kwa uthabiti wa imani, kusadiki bila kuona ili kuelewa ‘credo ut intelligam’(Mt. Anselimo). Imani hiyo sharti iambatane na matendo kwani pasipo na hayo imani huwa mfu. Matendo yasindikizayo imani ni “kuwalisha wenye njaa, kuwanywesha wenye kiu, kukaribisha wageni, kuwavika walio uchi, kuwaona wagonjwa na walio kifungoni” (Mt 25:35-36). Kwa ajili ya matendo haya Kristo anasema tutabarikiwa na kuurithi ufalme tuliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu (Mt 25:34). Shime watu wa Mungu, tutende mema.