Tafakari Dominika ya 25 ya Mwaka B wa Kanisa: Uongozi ni Huduma ya Upendo
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Mpendwa msikilizaji na masomaji karibu tena kwa neema ya Mungu leo ni dominika ya 25 tunapata muda wa kuutafakari upendo wa Mungu kupitia ujumbe wake kwa njia ya Maandiko Matakatifu. Wazo kuu linalojitokeza katika Liturujia ya Neno la Mungu ni: Haki kama kielelezo cha uchaji wa Mungu; Hekima inayofumbatwa katika unyenyekevu na kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma ya mapendo kwa watu wa Mungu. Haki ni fadhila adilifu iliyo na utashi wa kudumu na thabiti wa kumpa Mwenyezi Mungu na jirani haki yao. Mababa wa Kanisa wanasema, haki kwa Mwenyezi Mungu huitwa fadhila ya Kimungu. Haki kwa binadamu inakita mizizi yake katika amani, utu, heshima, usawa na maridhiano. Mtu mwenye haki atastawi kama mtende wa Lebanon, kwa sababu mawazo yake ni sahihi na anaonesha na kushuhudia kwa matendo yake unyofu wa moyo. Rej. KKK 1808. Kristo Yesu ni mfano kamili wa mtu mwenye haki, kwani aliteswa, akafa na hatimaye akafufuka kwa wafu. Hivyo tunapaswa kutunza heshima na sifa njema ya jirani, kwani kumwondolea mtu sifa njema ni kosa dhidi ya fadhila ya haki na mapendo. Kristo Yesu katika Maandiko Matakatifu anatuambia kwamba, Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa. Rej. KKK 1716. Matunda ya haki ni: heshima, ustawi, maendeleo, mafao ya wengi, amani na utulivu. Mababa wa Kanisa wanasema amani si kutokuwako na vita wala shinikizo la usawa wa nguvu kati ya wapinzani. Amani ni msingi wa wema, heshima na maendeleo endelevu ya binadamu; ni paji na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshirikisha na kumwajibisha binadamu. Amani ni tunda la upendo linalopaswa kuboreshwa kwa njia ya malezi ya dhamiri nyofu; ukweli na uhuru; usalama wa raia na mali zao; kwa kulinda na kuheshimu utu wa binadamu, ustawi na maendeleo ya wengi. Kwa ufupi, amani ni kazi ya haki na matunda ya upendo. Rej. KKK 2304.
Tutamsikia Yesu akiendelea kudadisi uelewa wa wafuasi wake. Kisha kuvuka bahari ya Sham Israel aliimba ‘Nitamwimbia Bwana kwa maana ametukuka sana… (Kut 15), ni wimbo wa ushindi, ilikuwa wauawe bahari ikafunguka wakavuka salama. Tunafurahi tunaposhinda mitihani ya maisha na changamoto zake. Kadiri ya Kamusi ‘kushindana ni hali ya kupimana nguvu, uwezo, uhodari, usogora nk. kupambana au kuchuana. Tabia ya kushindana, ukinzani, ukaidi, ubishi au ushupavu huitwa ushindani’. Ushindi ni jambo zuri na la furaha hasa mapambano yakiwa mazito na magumu. Leo Kristo anawauliza wanafunzi wake, ‘Mlishindania nini njiani?’ nao wananyamaza. Huenda aliwatazama tena mmoja baada ya mwingine na kurudia kwa msisitizo ‘Petro...Tomaso mlishindania nini njiani? Wee Yohane, Andrea!’ jamaa wanajipotezapoteza lakini bado jibu halikutoka, kwa nini? Ni kwa sababu waliona aibu kutokana na shindano lenyewe. Wanaume hawa, njia nzima wanashindana ‘mimi’ labda Petro ‘ndio mkubwa wenu hapa! Oneni mvi hizi kichwani?’ Yohane anajibu ‘mimi ndio bosi sababu hata kama mdogo kiumri nimesoma kuliko wote ninyi na Mzee ananipenda zaidi’. Yuda Iskariote anawashangaa na kusema kwa sauti ‘mkubwa wenu ni mimi kwa sababu hata mzee amenipa uhasibu, ameniamini kuliko wote’... wanatamani vyeo, madaraka na sifa.
UFAFANUZI: Dominika iliyopita tulisikia Kristo akitabiri kwa mara ya kwanza juu ya kuteswa kwake. Leo anapita Galilaya na anatabiri tena kwa mara ya pili. Mitume bado wazito, labda walielewa ila hakuweka akilini sababu moyo wa mwanadamu una maelekeo ya kukataa kuelewa kile ambacho haupendi kukisikia. Kwa kushindania ukubwa, ni dhahiri Mitume bado hawakumwelewa Kristo na hivi analazimika kuanza upya kufundisha maana ya utumishi wao. Kwamba kuwa MKUBWA MAANA YAKE NINI? Anazipindua fikra zao na kugeuza maelekeo yao ya kibinadamu na kuwafunulia ukweli wote. Kinyume na matarajio yao anasema wa kwanza awe wa mwisho, mkubwa awe mtumishi, kiongozi awe MNYENYEKEVU kama mtoto, wakazidi kuchanganyikiwa... Mtoto hawezi kujimudu, ni dhaifu, anahitaji uangalizi, kunyonya, kupakatwa, kubebwa, kufundishwa, kupendwa. Hana ushawishi, hawezi kutoa chochote zaidi ya kupokea, anachojua ni kulia akijichafua, njaa, usingizi, homa. Kristo anasema mkubwa awe mnyenyekevu kama kiumbe huyu mdogo na dhaifu, na kwamba ukimpokea mtu dhaifu unampokea Kristo, si Kristo tu bali Yule aliyempeleka, na kwa vile BABA, MWANA NA ROHO MT ni wamoja basi ukimpokea mtoto (mtu mdogo/dhaifu) unaupokea UTATU MTAKATIFU, raha sana! (Mt 25:40).
Mlishindania nini njiani? mwanadamu ana hali ya kushindana, katika Somo la Kwanza (Hek 2:12,17-20) waovu wanashindana na mwenye haki ili kumuangamiza. Naye Mt. Yakobo katika somo II (3:16-4:3) anasema mashindano yanayotokana na wivu na ugomvi huleta machafuko na ubaya... Tupo tunaoshindania madaraka/ukubwa, tukumbuke uongozi ni utumishi, utumwa, kujitoa, sio jambo la kukimbilia kwani una maumivu na sadaka kubwa. Mlishindania nini njiani? upo ushindani mwema, mfano wanafunzi wakishindana kufanya hesabu ubaoni wakati wa kipindi, wafanyabiashara wakishindana kuuza bidhaa origino, walimu wakishindana kufaulisha wanafunzi, madereva wakishindana kushika sheria za barabarani na hivi kupunguza ajali zinazochukua uhai wetu kila siku, serikali ikiwa na maono ya kuwaingiza wananchi katika ushindani wa kiuchumi, kuondoa umasikini, kuwa na uhakika wa mahitaji muhimu, sote tukishindana kupendana, kusameheana na kuvumiliana... ushindani wa hivi ni baraka ya Mungu.
Walakini tukishindania yasiyofaa mfano kupigania watu ambao hatujafunga nao hata ndoa, au mali kwa njia zisizo halali na fedha zisizo safi hali yetu itakuwa mbaya, tupo tunaoshindania nyumba, shamba na fedha za urithi, wengine tunashindana kudharauliana na mambo ambayo mwishoni hutuumiza wenyewe. Mlishindania nini njiani? tunabishana ni nani mkubwa? tukitaka ukubwa tushindane kuwa watakatifu, tushindane kusaidia wahitaji, kupendana na kulijenga Kanisa… msaidie mwenye shida utakuwa mkubwa wa kutisha. Tukizingatia hayo na kuacha kushindania yasiyo na faida, na badala yake tukishindana vita ya kiroho, isiyohusu damu na nyama (Efe 6:12), tukimkabili ibilisi na mamlaka zake kwa ujasiri na imani hakika yake tutavikwa taji. Hii ni kwa sababu shetani akiisha kuanguka hainuki tena, jehunumu ikiishakuanguka haiinuki tena, ubaya ukiisha kutiishwa hauinuki tena, ushindi ni dhahiri. Tutajipiga vifua kwa kiburi tukishangilia na Mt. Paulo wa Tarsus (2Tim4:7) ‘nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda…’ Mkristo mwenzangu kazi yetu ni moja kuilinda imani na kufa ikiwa lazima imani iwe salama, kwa wokovu wa ulimwengu.