Vijakazi wa Mtoto Mtakatifu Yesu:kumtumikia Mungu kwa njia ya elimu
Sr Emmanuella Dakurah, HHCJ
Watawa wa Wajakazi (Ancelle) wa Mtoto Mtakatifu Yesu ni Shirika la Kimataifa lililoanzishwa na Mtumishi wa Mungu Mary Charles Magdalen Walker, wa Shirika la Masista wa Upendo wa Ireland. Kwa mwaliko wa Mwakilishi wa Kitume, Kusini mwa Nigeria na Afrika Magharibi, Askofu Mkuu Joseph Shanahan CSSp, mtawa mwanzilishi wa Shirika hilo aliwasili nchini Nigeria mnamo mwaka 1923 kwa nia ya kutoa huduma yake katika uwanja wa uinjilishaji na kuhamasisha wanawake kupitia elimu. Mama Maria Charles alishuhudia maisha yake kile alichohubiri, yaani, kuwa kila kitu kwa watu wote, kujishughulisha na huduma yoyote inayoweza kusaidia kuinua kiwango cha maisha cha watu aliowatumikia. Alifanya kazi bila kuchoka kwa miongo kadhaa kama mwalimu, katika uwanja wa usaidizi wa matibabu, kama katekista na hata kama mfanyakazi wa kijamii.
Shirika la Kitawa mahalia
Shauku ya Mama Mary Charles ya kuanzisha Shirika la kitawa la kiasili, liliwezekana kiutimia mnamo mwaka wa 1931, wakati wanafunzi wanne wa shule ya Konventi ya Mtakatifu Joseph's huko Calabar, nchini Nigeria walipoomba kujiunga kuwa watawa. Jina alilochagua kwa ajili ya Shirika hilo jipya, lililowekwa rasmi mnamo Aprili 1937, lilikuwa ni "Wajakazi wa Mtoto Mtakatifu Yesu,” ambapo mnamo mwaka 1971 likawa Shirika lenye haki za kipapa. Katika miongo iliyofuata Watawa hao wameendelea kubadilika katika asili yao hadi kufikia ya kimataifa na baina ya makabila. Kwa hakika, wataw wengi wanatoka nchini Nigeria, Cameroon, Togo, Ghana, Sierra Leone, kisha Uingereza na Kenya. Kwa sasa, shirika linajivunia kuwa na nyumba nchini Nigeria, Ghana, Cameroon, Togo, Sierra Leone, Kenya, Tanzania, Italia, Ujerumani, London, Marekani, Canada na Grenada.
Elimu ni dhamira
Watawa hasa, Wajakazi wa Mtoto Mtakatifu Yesu wamejitolea kwa ajili ya mageuzi ya maisha kwa njia ya ushuhuda wa kinabii wa maisha ya kuwekwa wakfu, maisha ya jumuiya, uongozi shirikishi na huduma ya kitume, yenye chaguo maalum kwa maskini, wanawake na watoto. Elimu ya watoto ni mojawapo ya utume hai zaidi wa watawa: kiukweli, Wajakazi kwa ujumla wanajulikana kama walimu wazuri na wasimamizi wa shule. “Katika hawa wadogo tunamwona Yesu na ni shangwe kuwaona wakikua katika ujuzi na upendo wa Mungu,” alisema mmoja wa watawa hao. Kusudi ni kumfundisha mtu kwa ujumla, kwa hivyo maadili, nidhamu, fadhila na masomo: njia hii, kiukweli, husaidia wanafunzi kuwa raia wanaowajibika.
Watawa ni walimu, makatekista, mitume
Katika baadhi ya shule wanazosimamia, watawa hawa, wanatumia shuleni Mbinu ya Montessori katika nyayo za mwanzilishi wao ambaye alikuwa ametumia mbinu hii katika Shule ya Wasichana ya Mtakatifu Joseph huko Calabar, Nigeria. Mama Mary Charles alisema bila shaka kwamba ikilinganishwa na chekechea ya kawaida, Njia ya Montessori husaidia kukuza sifa tofauti za watoto. "Mtoto wa asili ana uwezo wa kufaulu katika wema wowote: kinachohitajika ni wakati, subira na fursa," aliandika mama Mary. Siku zote aliwasihi watawa wake wakumbuke msemo huu: “Kila mwalimu ni katekista na mtume.” Katika kupitisha urithi wake, Watawa wanaendelea kusomesha watoto kwa kushiriki katika huduma ya Kristo ya kufundisha, kutunza, na katekesi katika shule zao nyingi.
Shule za Ancella nchini Ghana
Nchini Ghana, Wajakazi wa Mtoto Yesu wanajulikana kwa shule mbalimbali wanazoziendesha zinazokwenda kwa jina la “Ancilla Schools”: “Tumedhamiria kuwafundisha vijana wetu kiakili, kimwili na kiroho: kwa ufupi, elimu kamili. ”, wanasema watawa. Shule nyingi hutoa elimu katika viwango tofauti, kuanzia shule ya chekechea hadi chuo kikuu. Katika kila kipengele cha ufundishaji wao watawa hawa wanakusudia kuwatayarisha wanafunzi kukabiliana na changamoto za maisha badala ya kutamani tu kuhitimu. Shirika lao pia linatoa shule maalum kwa watoto wenye ulemavu, huduma inayowapa wazazi wao matumaini makubwa. “Hatuwasomeshi watoto tu; tunaomba fedha kutoka kwa mashirika na watu binafsi ili kununua vitu wanavyohitaji, kama vile magongo, viti vya magurudumu, sare na kulipia karo za chuo kikuu,” watawa hao wanaendelea kusema.
Katika baadhi ya vijiji vya Ghana watoto wengi hawana fursa ya kupata elimu bora: kwa sababu hii watawa walianzisha jumuiya katika maeneo ambayo wanaweza kupanua huduma yao kwa vijana hawa ili wapate mafunzo ya kukabiliana na maisha yao ya baadaye katika moyo, akili na katika mikono. Katika kila nyanja ya huduma yao ya elimu, akina dada wamejitolea kuweka akilini lengo la kutoa elimu ya hali ya juu, wakifuata nyayo za mwanzilishi wao. "Katika vijana tunaona mustakabali wa Kanisa na wa ulimwengu kwa ujumla".