Tafuta

Watakatifu Cosmas na Damiani ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa wagonjwa, changamoto kwa madaktari kujisadaka kwa ajili ya wagonjwa na wale walioko kufani! Watakatifu Cosmas na Damiani ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa wagonjwa, changamoto kwa madaktari kujisadaka kwa ajili ya wagonjwa na wale walioko kufani!  (Vatican Media)

Watakatifu Cosmas na Damiani Wafiadini: Kielelezo cha Huruma na Upendo Kwa Wagonjwa

Kila ifikapo tarehe 26 Septemba ya kila mwaka Mama Kanisa anaadhimisha kumbukumbu ya Watakatifu Cosmas na Damiano, ndugu mapacha waliozaliwa huko Arabia mwanzoni mwa karne ya tatu na kuishi huko Cilicia mpakani mwa Uturuki na Siria. Kwa neema ya Mungu walisoma na kufudhu vizuri sana sayansi ya udaktari na kutumia taaluma yao kuwatibu watu magonjwa mbalimbali bila kudai malipo na wakajulikana kwa lugha ya Kilatini kama “Andriri.”

Na Damian Kongwa, Dar es Salaam, Tanzania

Kanisa Katoliki linasadiki katika ushirika pamoja na watakatifu “Communio Sanctorum” kwa kuheshimu kumbukumbu ya wakazi wa mbinguni kwa sababu ya mfano wao kwani kama ushirika kati ya wakristo duniani unavyotusogeza karibu zaidi na Kristo, ndivyo umoja pamoja na watakatifu unavyotuunganisha na Kristo, zinakotoka kama chemichemi neema zote na uzima wenyewe wa Taifa la Mungu (Rej. KKK 957). Katika ukatoliki wake “Catholicism” Kanisa la mbinguni na duniani linaunganika pamoja kama watoto wa Mungu kwa njia ya Yesu Kristo (Rej. Efe 3: 14-15). Mababa wa Kanisa katika Mtaguso wa Pili wa Vatican wanafundisha kuwa “ilimpendeza Mungu katika wema na hekima yake kujifunua mwenyewe na kulidhihirisha fumbo la mapenzi yake. Katika fumbo hilo kwa njia ya Kristo, Neno la Mungu aliyefanyika mwili, katika Roho Mtakatifu, wanadamu wanapata njia ya kumwendea Baba na kushirikishwa hali ya kimungu (Rej. Dei Verbum 2). Ukristo wetu unatudai kuishi maisha ya utakatifu na amani na watu wote kwa sababu hakuna mtu atakayemwona Mungu bila ya maisha kama hayo (Rej. Ebr 12:14). Kwa mifano ya maisha ya watakatifu tunakumbushwa siku zote asili, umuhimu, thamani na kusudi la Mungu kwetu huku tukijibidiisha katika tumaini la kurithishwa uzima wa milele mbinguni. Kusanyiko la watakatifu mbinguni linaunda kundi la mashahidi ambao hawachoki kuliombea kanisa linalosafiri hapa duniani ili liweze kufikia ile taji ya utukufu mbinguni. Wito wa Utakatifu unatudai kukesha siku zote huku tukingojea ujio wa pili wa Bwana Wetu Yesu Kristo (Rej. Mat 24:42).

Watakatifu Cosmas na Damian, Mtuombee
Watakatifu Cosmas na Damian, Mtuombee

Ni katika muktadha huo kila ifikapo tarehe 26 Septemba ya kila mwaka Mama Kanisa Mtakatifu anaadhimisha kumbukumbu ya Watakatifu Mashahidi Wafiadini Cosmas na Damian. Cosmas na Damian walikuwa ndugu mapacha waliozaliwa huko Arabia mwanzoni mwa karne ya tatu na kuishi huko Cilicia mpakani mwa Uturuki na Siria. Kwa neema ya Mungu walisoma na kufudhu vizuri sana sayansi ya Udaktari na kutumia taaluma yao kuwatibu watu magonjwa mbalimbali bila kudai malipo na wakajulikana kwa lugha ya Kilatini kama “Andriri.” Ni katika kutumia ujuzi na taaluma yao ya udaktari waliwaponya watu afya zao huku wakiwavuta kwa Kristo apate kuwaponya roho zao pia (Rej. Luka 5:31). Kwa ushuhuda wa maisha yao walidhihirisha imani yao kwa Bwana wetu Yesu Kristo wazi wazi bila hofu na woga wowote wakiamini kuwa Kristo atawalinda na kuwatetea mbele ya Mungu Baba Mwenyezi (Rej. Mat 10:32). Katika shughuli zao za udaktari walipata fursa za kuingia katika nyumba na makazi ya wapagani kutoa huduma na kuwahubiria Injili ya Kristo na kufanikiwa kuwaongoa watu wengi. Nguvu ya Kristo Yesu ilifanya kazi ndani ya mioyo yao siku zote (Rej. 2 Kor 13:3). Waliwatibu watu bure na kamwe hata mara moja hawakudai fedha kwa huduma walizotoa, hivyo walikuwa maarufu sana na watu waliwaita “watakatifu bila fedha”. Kwa njia ya uponyaji walifanya miujiza mingi na muujiza maarufu sana ni ule wa kumponya mtu aliyepata shida ya mguu.

Madaktari na wauguzi ni faraja kubwa kwa wagonjwa
Madaktari na wauguzi ni faraja kubwa kwa wagonjwa

Kwa pamoja walivumilia mateso, chuki na madhulumu yote wakitazamia tuzo waliyowekewa mbinguni (Rej. Luka 6:22) huku wakiamini kuwa baada ya mateso na kifo, kwa imani Mungu atawafufua katika hali ya neema (Rej. 1 Thes 4:14). Cosmas na Damian walisikia Neno la Mungu na kuvumilia mpaka mwisho wakazaa matunda bora (Rej. Luka 8:15b). Mungu alidumu kuwa tumaini lao milele (Rej. Zab 91:2) nao waliishi wakimfuata Roho Mtakatifu aliyemiminwa ndani yao kwa njia ya Yesu Kristo (Rej. Tito 3:4). Walipigana vita vya roho kwa imani huku wakijihadhari kujitenga na Mungu aliye hai (Rej. Ebr 3:12). Waliendelea kudumu wakiwa na furaha hata wakati walipopatwa na majaribu mbalimbali (Rej. Yak 1:2). Watakatifu madaktari hawa mapacha (Cosmas na Damian) ni kielelezo na mfano wa kuigwa kwa madaktari wa nyakati zetu za sasa hasa tunaposhuhudia vifo vya wagonjwa vinavyotokana na ukosefu wa huduma bora za afya na dawa na hata wakati mwingine watu kupoteza maisha kwa kukosa fedha za kugharamia matibabu. Cosmas na Damian walikamatwa na kuteswa sana wakati wa madhulumu ya Diokletiani na hatimaye kuuawa mashahidi tarehe 27 Septemba 287. Cosmas na Damiano ni wasimamizi na waombezi wa Wafamasia na Madaktari. Ibada yao ilianza kuenea kati ya Karne ya IV na Kanisa kuu likajengwa kwa heshima yao mjini Roma na Papa Felix IV (526-530.) Na hatimaye majina yao yakaandikwa kwenye Kanuni ya Kirumi na hivyo kuadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Septemba.

Cosma na Damian walijisadaka kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa
Cosma na Damian walijisadaka kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa

Sala kwa Watakatifu Cosmas na Damian: Enyi watakatifu Cosmas na Damian tunawaheshimu kwa unyenyekevu wote na mioyo yetu yote. Tunawaomba nyinyi mliokuwa wafuasi wa Yesu Kristo na kutumia neema ya uponyaji kwa upendo na dhabihu ya kupendeza kuponya na kuhudumia magonjwa hatari, si kwa msaada wa madawa na ujuzi, bali kwa kuomba jina lote la nguvu ya Yesu Kristo. Sasa kwa kuwa ninyi ni wenye nguvu zaidi mbinguni tunaomba msaada na huruma yenu juu ya mioyo yenye shida na magonjwa mengi ambayo yanatukandamiza, magonjwa mengi ya kiroho na kimwili yanayotuzunguka. Tunaomba mtusaidie katika kila shida. Hatuombi kwa ajili yetu tu bali kwa jamaa zetu wote, familia, marafiki na maadui ili kurejeshwa kwa afya ya nafsi na mwili tuweze kumtukuza na kumheshimu Mungu milele na milele. Amina. Watakatifu Cosmas na Damian Mtuombee!

25 September 2024, 17:06