2024.10.08:Misa ya Jubilei miaka 25 ya Upadre kwa Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo la Geita, Tanzania. 2024.10.08:Misa ya Jubilei miaka 25 ya Upadre kwa Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo la Geita, Tanzania. 

Miaka 25 ya Upadre wa Ask.Kassala na mapokezi ya Watanzania,Parokia ya Mtakatifu Maria wa Mateso

Mhashamu Askofu Kassala aliadhimisha kwa mara nyingine Misa ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa makuu mengi anayojaliwa ya kutimiza miaka 25 ya Upadre,katika Parokia ya Mtakatifu Maria wa Mateso huko Monte San Giovani Campano,Frosinone,Italia,Oktoba 5,2024.“Tunabaki wadogo kwa kuwa tumefanywa wana wa Mungu.”

Na Padre Angelo Shikombe na Angella Rwezaula – Vatican.

Jumamosi tarehe 5 Oktoba 2024, Mhashamu Askofu Flavian Matindi Kassala, Askofu wa Jimbo la Geita nchini Tanzania, aliitikia mwaliko wa Paroko Padre Stefano di Mario, wa Parokia ya Bikira Maria wa Mateso, Monte San Giovanni Campano katika Jimbo la  Frosinone,  Mkoani Lazio, kilomita chache kutoka Mji Mkuu Roma, Italia, ili kuongoza Misa ya Shukrani kwa mara nyingine ya kutimiza miaka 25 ya upadre. Misa hiyo ilifanyika ndani ya  muktadha wa maadhimisho ya sherehe za Mtakatifu Francisko wa Assisi yaliyohitimishwa Dominika tarehe 6 Octoba 2024 kwa maandamano na Misa Takatifu yaliyoudhuriwa na waamini wengi kutoka ndani na nje ya Parokia hiyo pamoja na watanzania waishio Italia na wanafunzi wanaosoma nchini Italia.

Askofu Kassala akiongoza misa takatifu
Askofu Kassala akiongoza misa takatifu

Mhashamu Askofu Kassala alipokelewa kwa shangwe na nderemo na watanzania mapadre, watawa na walei waliounganika na wanaparokia ambapo aliongoza Misa Takatifu. Kabla ya kuanza Misa, Padre Stefano alitoa utangulizi wa kumshukuru Mwashamu, na kuelezea hali halisi ya Parokia hiyo katika suala zima la Kichungaji na kwa ufupi kukaribisha Jimbo la Geita ili kutenda pamoja utume wa kichungaji akitoa mifano kadhaa ya Jimbo lake ambalo tayari limefungua milango kwa majimbo mengine kadhaa ya Afrika kama Burundi na kwingineko.

Misa ya Jubilei miaka 25 ya Upadre wa Askofu Kassala
Misa ya Jubilei miaka 25 ya Upadre wa Askofu Kassala

Ilifuatiwa liturujia ya Neno na baadaye  mahubiri ya Askofu Kassala  kwa Lugha ya Kiitaliano yalikijikita juu ya maandiko matakatifu ya siku yaliyosomwa hasa katika Injili ya kurudi kwa wafuasi 72 waliotumwa na Yesu ambao walirudi kwa furaha kutoka katika utume wao. Askofu kassala alisisitiza mafanikio ya kimisionari yenye furaha, kwa sababu ndani ya utume wa kimungu kuna furaha kubwa inayoibua pia mapungufu ya kibinadamu yanayokamilishwa katika fumbo la neema za Mungu zinazotenda ndani yetu. Askofu Kassala akiendelea na mahubiri yake alikazia kusema kuwa “kama Mungu ametuchagua hatatuacha kamwe kama sisi tutabaki waaminifu kwake. Hakuna kuchaguliwa kunakozidi kuchaguliwa na Mungu katika sakramenti ya Ubatizo ambao ndani yake sisi sote ni wadogo mbele ya Mungu. Tunabaki wadogo kwa kuwa tunafanywa wana wa Mungu na kufanyika huko kuwa wana wa Mungu, kunatuwezesha kuyatambua mafumbo ya Mungu," alisema.  Katika Kuhitimisha mahubiri yake aliungana na wanaparokia ya Bikiria Maria wa Mateso kuwaombea marehemu waliotangulia mbele ya mungu, akiwemo kijana aitwaye Mikaeli Marino aliyefriki akiwa na umri wa  miaka 29.

Padre Stefano di Mario pamoja na Askofu na mapadre kutoka Tanzania
Padre Stefano di Mario pamoja na Askofu na mapadre kutoka Tanzania

Na katika kutoa neno lake la shukrani alimshukuru sana, Paroko wa Parokia hiyo, Padre Stefano kwa jitihada zake kubwa za kufungua milango ya mahusiano na mawasiliano katika harakati za kuwasaidia wahitaji. Mwisho aliomba kudumisha mahusiano hayo kati ya Kanisa la Italia na Kanisa la Tanzania ili kuweza kujibu changamoto zinazolikabiliwa kwa pamoja. Neno pia lilimwendea  Padre Angelo Shikombe akimpongeza kwa kuishi vizuri na Jumuiya hiyo mahali ambapo anatumia muda wake katika huduma ya kichungaji wakati akiendelea na masomo yake.  

Picha ya pamoja na Askofu Kassala
Picha ya pamoja na Askofu Kassala

Pamoja na hayo pia Padre Shikombe aliwashukuru wote kuanzia na Askofu wake aliyemwezesha fursa hii ya kuja masomoni, lakini pia hata Paroko na Jumuiya nzima kwa ujumla iliyompokea na kuweza kuishi udugu. Baada ya Misa hiyo, kulifuatiwa na shamrashamra za kumpongeza Baba Askofu, nyimbo na nderemo zilizowashangaza wananchi wa Italia, zikiambatana na kutembelea maeneo ya kihistoria ya familia ya Mtakatifu Thomaso wa Acquino, hata katika chumba ambacho Mtakatifu Thomas mwenyewe alitunga wimbo wa kuabudu unaojulikana sana(Adoro te devote - Ninakuabudu Mungu wangu...),moja ya nyimbo tano za Ekaristi alizotunga katika fursa ya utangulizi wa Sikukuu ya Mwili na Damu ya Yesu kwa utashi wa Papa Urbano IV(1264).

Mbele ya Kikanisa cha Mtakatifu Familia ya Mtakatifu Thomas wa Aquino
Mbele ya Kikanisa cha Mtakatifu Familia ya Mtakatifu Thomas wa Aquino

Ikumbukwe kwamba Askofu Flavian Matindi Kassala alipadirishwa mnamo tarehe 11 Julai 1999 katika Parokia ya Bikira Maria wa Fatima huko Geita nchini Tanzania na kwa njia hiyo mnamo tarehe 11 Agost 2024 aliadhimisha Jubilei ya fedha ya miaka 25 ya upadre iliyohudhuriwa na Makardinali, Maskofu wakuu, maaskofu, mapadre, watawa na waamini weng, viongozi wa serikali na vyama na pia kutoka madheheu mengine ya kidini. Maadhimisho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Jimboni Geita kwa kuakisi hakika umoja wa Kanisa la Tanzania.


Askofu Kassala baada ya upadirisho wake alihudumu kama Paroko Msaidizi, Mwalimu na Mlezi wa Seminari ndogo, Mkurugenzi wa Mashirika ya Kipapa, na baadaye alikwenda masomoni nchini Italia ambako alihitimu masomo ya uzamivu(doctorate) katika Utume wa Vijana na Katekesi kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Salesian, Roma.  Wakati akiwa masomoni, pia alitumia muda  wake kuwa katika viunga vya Radio Vatican, kwa  kutoa  vipindi mbalimbali  vya mafunzo kwa vijana. Baada ya kutoka masomoni alihudumu kama Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha SAUT, Mwanza, Msimamizi wa uhasibu katika Chuo kikuu cha Maria Stella Mtwara. Mnamo tarehe 28 Aprili 2016, Baba Mtakatifu Francisko alimteua kuwa Askofu wa Jimbo la Geita na kupewa daraja la Uaskofu na kusimikwa kakiwa askofu wa tatu wa Jimbo hilo, mnamo tarehe 12 Juni 2016.

Askofu Kassala akiwa Ukumbi wa Mkutano wa Sinodi ya Kisinodi
Askofu Kassala akiwa Ukumbi wa Mkutano wa Sinodi ya Kisinodi

Akiwa Askofu, amehudumu nyadhifa mbalimbali katika Kanisa mahalia akiwa kama Makamu Rais  wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC). Mhashamu Baba Askofu Kassala na Askofu Mkuu wa Jimbo la Dar es Salaam, Askofu Thadeus Rwaichi aidha waliteuliwa kuwa wawakilishi wa Tanzania katika Sinodi ya XVI ya Maaskofu kwa mwaka 2023 -2024, inayoongozwa na kauli mbiu: Kanisa la Kisinodi: Ushiriki, Ushirika na Umisionari. Kwa njia hiyo kuanzia tarehe 29 Septemba 2024 wako mjini Vatican kwa mara nyingine tena katika mwendelezo wa Sinodi hiyo iliyofunguliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 2 Oktoba na itahimishwa  tarehe 27 Oktoba 2024. Tunawatakia mema yote wajubilei wote kwa mwaka 2024.

Jubilei ya miaka 25 ya Upadre wa Askofu Flavian Kassala
07 October 2024, 16:46