Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S. wa Jimbo Katoliki Morogoro, Tanzania amezindua Parokia mpya ya Mtakatifu Benedikto Mdaula, Jimbo Katoliki la Morogoro. Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S. wa Jimbo Katoliki Morogoro, Tanzania amezindua Parokia mpya ya Mtakatifu Benedikto Mdaula, Jimbo Katoliki la Morogoro.  

Askofu Msimbe: Parokia ya Mt. Benedikto Mdaula Kitovu Cha Uinjilishaji!

Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S. wa Jimbo Katoliki Morogoro amezindua Parokia mpya ya Mtakatifu Benedikto Mdaula, Jimbo Katoliki la Morogoro na kumtangaza Padre Patrick Kung’alo kuwa ni Paroko wa kwanza wa Parokia hii mpya na pamoja kutoa Sakramenti ya Kipaimara kwa waamini 80, tayari kulinda, kutetea, kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Parokia ni kitovu cha uinjilishaji, mahali pa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa! Ushuhuda.

Na Angela Kibwana, - Jimbo Katoliki la Morogoro

Parokia ni mahali ambapo, utamaduni wa watu kukutana unapaswa kujengwa na kudumishwa, ili kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene; mshikamano pamoja na kuendelea kuwa wazi kwa ajili ya watu wote, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Jumuiya ya Kiparokia inapaswa kuwa ni msanii wa utamaduni wa ujirani mwema, kama kielelezo na ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa kwa namna ya pekee katika Injili ya huduma. Pamoja na ukweli huu, Mama Kanisa anatambua kwamba, kuna uhaba mkubwa wa miito ya Kipadre katika baadhi ya maeneo, kiasi kwamba, mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache katika shamba la Bwana. Kumbe, kuna haja ya kuwa na mwelekeo na utambuzi mpya wa “dhana ya Parokia.” Parokia, ni mahali ambapo maisha ya Kisakramenti yanapewa uzito wa pekee sanjari na ushuhuda wa upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji, sehemu muhimu ya uinjilishaji wa Kanisa kwa ajili ya Kanisa linaloinjilisha. Parokia inapaswa kuwa ni Jumuiya ya waamini inayoinjilisha na kuinjilishwa. Hii ni Jumuiya inayotangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo makini cha imani tendaji! Parokia ni mahali muafaka pa waamini kujisikia kupenda na kupendwa; mahali pa kukutana, ili hatimaye, kuweza kuutafakari Uso wa huruma ya Mungu katika kina na mapana yake. Ni mahali muafaka pa kusimama kidete, kulinda, kutetea na kutunza mazingira bora nyumba ya wote.

Parokia ni mahali pa: Neno, Sakramenti na Ushuhuda wa imani.
Parokia ni mahali pa: Neno, Sakramenti na Ushuhuda wa imani.

Parokia ni mahali pa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na kurithisha imani, ili kuziwezesha familia kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara yaani wa kuwa ni: Kanisa dogo la nyumbani, mahali ambapo watoto kwa njia ya: Sala, Sakramenti za Kanisa, Tafakari ya Neno la Mungu na Matendo ya huruma, wanapewa malezi na makuzi yatakayowawezesha watoto hawa kuwa kweli ni mashuhuda wa maisha ambayo yamepigwa chapa ya fadhila za Kimungu yaani: Imani, Matumaini na Upendo. Parokia ni mahali ambapo wanafamilia wanapaswa kujisikia kuwa wako salama salimini. Kuna haja ya Parokia kuendelea kushirikiana na kushikamana, ili kujenga Jumuiya kubwa zaidi ya watu wanaoinjilisha na kuinjilishwa. Katika mchakato huu, Paroko anapaswa kuwa ni mfano bora wa kuigwa na watu wa Mungu katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha na utume wake. Watu wote wa Mungu wanaitwa, wanatumwa na wanahamasishwa kushiriki katika safari hii ya imani, chemchemi ya furaha, amani na utulivu wa ndani unaofumbatwa katika ari na mwamko mpya wa kimisionari. Haya ni mambo yanayobainishwa katika Waraka Kuhusu: Maagizo: “Wongofu wa Kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa” unaopania pamoja na mambo mengine, kupyaisha ari na mwamko wa wito na utume wa kimisionari katika maisha na utume wa Kanisa na umuhimu wa Parokia kama kitovu cha uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Kanisa ni nyumba ya Sala, Nyumba  ya Mungu, Nyumba ya Ibada
Kanisa ni nyumba ya Sala, Nyumba ya Mungu, Nyumba ya Ibada

Ni katika mukadha huu, hivi karibuni, Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S. wa Jimbo Katoliki Morogoro, Tanzania amezindua Parokia mpya ya Mtakatifu Benedikto Mdaula, Jimbo Katoliki la Morogoro na kumtangaza Padre Patrick Kung’alo kuwa ni Paroko wa kwanza wa Parokia hii mpya pamoja kutoa Sakramenti ya Kipaimara kwa waamini 80, tayari kulinda, kutetea, kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Hili ni tukio ambalo limehudhuriwa na waamini kutoka ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Morogoro. Ibada hii ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuzindua Parokia na kutabaruku Kanisa hili imeanza kwa sala na kubariki maji yaliyotumika kuwanyunyizia waamini na baadaye kuta za Kanisa. Hiki ni kielelezo kwamba, Kanisa hili sasa limewekwa wakfu kwa ajili ya kumtolea Mungu: sifa, shukrani na sala, ili waamini waweze kutakatifuzwa. Kanisa hili kwa sasa ni nyumba ya Sala, Nyumba ya Mungu na Nyumba ya Ibada. Ni mahali ambapo waamini wanalishwa kwa Neno la Mungu na kushibishwa kwa Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu. Altare imetabarukiwa na hivyo kuwekwa wakfu, inapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa kwa sababu Altare ni kielelezo cha Kristo Yesu, Mwanakondoo wa Mungu anayejisadaka kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Ni mahali ambapo waamini wanatolea sala na sadaka zao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa. Kanisa pawe ni mahali pa: amani, usalama na utulivu wa ndani. Waamini wajifunze kutumia vyema nyumba ya Mungu. Askofu Msimbe amefafanua maana ya Kanisa kama: Jumuiya ya watu wa Mungu inayoongozwa na nguvu ya Mungu. Ni watu wenye imani moja katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na Ubatizo mmoja kwa maondoleo ya dhambi. Wao wanaofungamanishwa na nguvu ya Kristo Yesu inayowatakasa na kuwaokomboa. Kanisa pia ni jengo maalum lililotengwa kwa ajili ya kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa. Ni mahali pa sala ya kumsifu, kumtukuza, kumwabudu na kumheshimu Mungu. Kimsingi Kanisa ni nyumba ya Mungu.

Waamini walei wanaitwa na kutumwa kuyatakatifuza malimwengu
Waamini walei wanaitwa na kutumwa kuyatakatifuza malimwengu

Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S. amewashukuru na kuwapongeza waamini wa Parokia mpya ya Mtakatifu Benedikto Mdaula, Jimbo Katoliki la Morogoro kwa umoja, mshikamano, upendo, majitoleo na sadaka yao, hadi kukamilisha Nyumba ya Mungu. Hapa pawe nio mahali pa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu, amani na maridhiano. Waamini wajenge utamaduni wa kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa na hasa ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho, ambazo kimsingi ni Sakramenti pacha. Ni mwaliko kwa waamini waliozama na kubobea kwenye uchumba sugu, kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kurekebisha maisha yao, kadiri ya Sakramenti za Kanisa. Waamini wanapaswa sasa kujitegemea na kuitegemeza Parokia yao, ili iweze kuendelea kukua na kupanuka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wake. Wajitahidi kutoa sadaka na kulipa zaka; daima wakumbuke kwamba, Msimamizi na Mwombezi wa Parokia yao alikazia sana “Sala na Kazi”: Ora et Labora” kwani kazi ni kipimo cha utu na ukamilifu wa mwanadamu na wala si katika miujiza! Mtakatifu Augustino Askofu na Mwalimu wa Kanisa anasema, “Sali kana kwamba, kila kitu kingemtegemea Mungu, lakini fanya kazi kana kwamba, kila kitu kingekutegemea wewe.” Ni matumaini ya Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S. kwamba, Parokia hii itasonga mbele: Kiroho, kimaadili, kiutu na kiuchumi. Tayari waamini wameanza kuchanga kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Mapadre.

Askofu Msimbe Parokia
14 October 2024, 14:24