Tunapenda kuutambua na kuuthamini mchango wake hususan kwa kipindi cha takriban miaka 15 (2009 hadi 2024), ambacho amehudumu kwa nafasi ya Rais wa Tume ya Uinjilishaji ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Tunapenda kuutambua na kuuthamini mchango wake hususan kwa kipindi cha takriban miaka 15 (2009 hadi 2024), ambacho amehudumu kwa nafasi ya Rais wa Tume ya Uinjilishaji ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.  

Askofu Mkuu Damian Dallu Miaka 15 ya Huduma Kwa PMS: Hongera!

Askofu mkuu Damian Dennis Dallu aliteuliwa kuyaongoza Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari nchini Tanzania mwaka 2009 hadi mwaka 2024. Anakumbukwa sana kwa kuhimiza nafasi ya sala katika maisha ya waamini; Ukarimu kwa ajili ya Mfuko wa Kiulimwengu wa Uinjilishaji wa Khalifa wa Mtakatifu Petro; Umoja na Ushiriki wa matukio ya kimisionari. Askofu mkuu Dallu alihimiza maadhimisho ya kitaifa, kikanda, kijimbo na kiparokia pamoja na malezi endelevu ya waamini!

Na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., - Dar es Salaam.

Historia ya Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari inadhihirisha wazi kuwa Mashirika haya ni zawadi ya Mungu kwa Kanisa lake kwa njia ya Roho Mtakatifu, kadhalika ni zao la bidii ya kimisionari ya waasisi wake. Kwa nyakati mbalimbali, Mwenyezi Mungu ameendelea kuwatumia watu/wanadamu kwa ajili ya kuyastawisha Mashirika haya katika Kanisa. Kwa Kanisa Mahalia la Tanzania, tunakiri kuwa kati ya wale ambao Mwenyezi Mungu amependa kuwatumia katika kuyasimika na hata kuyaeneza Mashirika haya hapa kwetu, miongoni mwao ni Baba Askofu Mkuu Damian Denis Dallu. Tunapenda kuutambua na kuuthamini mchango wake hususan kwa kipindi cha takriban miaka 15 (2009 hadi 2024), ambacho amehudumu kwa nafasi ya Rais wa Tume ya Uinjilishaji ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Hakika tunayo kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa ajili yake na pamoja naye, kadhalika kuendelea kumuombea utumishi mwema wa umisionari anaoendelea nao kwa nafasi yake kama Askofu Jimbo na kupitia nafasi nyingine za kiutendaji katika Kanisa. Katika kudhihirisha mchango mkubwa wa Baba Askofu Mkuu Dallu, tunapenda kuainisha maeneo machache ambayo kwayo atakumbukwa daima: Nafasi ya Sala: Kwa kuzingatia kuwa SALA ndio moyo wa Umisionari, katika utumishi wake kwa nafasi ya Rais wa Tume ya Uinjilishaji (TEC), Baba Askofu Mkuu Dallu amehimiza sana juu ya nafasi ya sala. Daima amekuwa akikumbusha kuwa mafanikio katika kazi ya Umisionari yanategemea nguvu na maongozi ya Roho Mtakatifu.

Askofu mkuu Dallu: Alihimiza sana maisha ya sala binafsi za kijumuiya
Askofu mkuu Dallu: Alihimiza sana maisha ya sala binafsi za kijumuiya

Ni katika msingi huu, alihimiza nafasi ya Sala binafsi na za jumla katika kuombea kazi ya Umisionari; Rozari Takatifu hususan Mwezi wa Oktoba hali akionesha mfano hai kwa kushiriki nafasi mbalimbali za Sala ya pamoja: Mfano Mzuri hapa ukiwa ni ushiriki wake katika Sala ya Rozari ya Pamoja ya Watoto inayosaliwa kitaifa siku ya Jumamosi inayotangulia Dominika ya Misioni. Aidha, aliliunga mkono na hata kulipa msukumo wa pekee sana pendekezo la kuanzishwa kwa Wiki ya Miito kadhalika na Sala ya Novena kuelekea Maadhimisho ya Dominika ya Misioni ya kila mwaka. Ni katika muktadha huu, amehimiza daima uadhimishaji mzuri wa Siku Maalum zilizotengwa na Kanisa kuhimiza nafasi ya Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari, yaani Dominika ya Miito, Dominika ya Kimisionari na Sikukuu ya Watoto Mashahidi. Mwaliko wake daima umekuwa ni kutuhimiza kuzitazama siku hizi, kwanza kabisa, kama fursa ya Sala na makuzi ya kiroho kwa ujumla. Ukarimu kwa ajili ya Mfuko wa Kiulimwengu wa Uinjilishaji wa Baba Mtakatifu: Kwa kujisimika katika ukweli kwamba Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari yamejengwa juu ya msingi wa SALA na MAJITOLEO, Mhashamu Baba Askofu Mkuu Dallu aliweka msisitizo wa pekee katika nyanja hii ya majitoleo. Katika kuonesha thamani ya tendo hili alihimiza kuwa badala ya kutumia neno michango ni vema tutumie neno UKARIMU. Mchango ni kitu cha wakati tu na chaweza kuwa cha kupita na pengine chaweza kufanyika kwa malengo mbalimbali hata mengine ya binafsi tu, lakini Ukarimu hutoka ndani ya moyo wa mtu na huandamana na sadaka ya kweli tena inayouma. Tunamshukuru sana na kumpongeza Baba Dallu kwa kutufundisha kwa vitendo juu ya Ukarimu kwa kazi ya Umisionari, kama ilivyojidhihirisha kupitia majimbo aliyoyaongoza, yaani Jimbo la Geita na baadaye Jimbo Kuu la Songea analoliongoza hadi sasa.

Askofu mkuu Dallu: Mchango wa Mfuko wa Kiulimwengu wa Uinjilishaji
Askofu mkuu Dallu: Mchango wa Mfuko wa Kiulimwengu wa Uinjilishaji

Ushirika na Ushiriki (communion): Kwa kuzingatia ukweli kwamba Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari ni “mtandao wa kiulimwengu”, yaani unajisimika katika Ushirikiano wa Kimisionari (Missionary Cooperation); Baba Dallu amekuwa muumini kwa vitendo juu ya ukweli huu. Katika Uongozi wake kama Rais wa Tume ya Uinjilishaji, mara nyingi amehimiza ushiriki wa matukio mbalimbali ya pamoja na kwa namna ya pekee Vikao vya Kila Mwaka vya Mashirika ya Kipapa Kitaifa. Mara zote, Baba Dallu alihimiza juu ya umuhimu wa Vikao kwani ni fursa muhimu za kupanga, kutekeleza na hatimaye kujitathimini pamoja ili kuweka mikakati zaidi ya kusonga mbele. Kazi ya Kimisionari ina hulka ya kisinodi (synodality). Ndio maana kila mwaka alijibidisha kuhudhuria Vikao hivyo isipokuwa kwa mara zile chache sana ambapo alipatwa na dharura kubwa. Hakika tunayo kila sababu ya kumshukuru kwa ajili yake na kumpongeza. Aidha, katika msingi huo huo wa kutembea pamoja kama wamisionari, alihimiza sana juu ya umuhimu wa kuwa na maadhimisho mbalimbali ya kitaifa yanayotuleta pamoja. Matukio ya aina hiyo yamekuwapo mengi kwa kipindi chote cha Uongozi wake. Itoshe tu kutaja haya mawili makubwa: (1) Maadhimisho ya Mwezi wa Pekee wa Kimisionari yaliyofanyika kitaifa na pia kuhudhuriwa na washiriki maalum, yaani Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari Kiulimwengu wakati huo – Askofu Mkuu Giampietro Dal Toso na Wakurugenzi wa Mashirika ya Kipapa wa Nchi za Afrika zinazoongea Lugha ya Kiingereza (NDESA) yaliyofanyika tarehe 28 Juni, 2019 Msimbazi, Dar es Salaam na (2) Maadhimisho ya Jubilei za Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari yaliyofanyika tarehe 12-13 Novemba, 2022 hapa Kurasini, Dar es Salaam; yakijumuisha Miaka 400 tangu kuanzishwa kwa Dikasteri ya Uinjilishaji (wakati huo ikijulikana kama Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu), Miaka 200 tangu kuanzishwa Shirika la Kipapa la Uinjilishaji wa watu; Miaka 100 tangu kupandishwa hadhi kwa Mashirika Matatu ya Kwanza na Miaka 150 tangu kuzaliwa kwa Mwanzilishi wa Shirika la Kipapa la Umoja wa Kimisionari.

Askofu mkuu Dallu: Alikazia kuhusu Umoja na Ushiriki wa watu wa Mungu
Askofu mkuu Dallu: Alikazia kuhusu Umoja na Ushiriki wa watu wa Mungu

Malezi Endelevu juu ya Umisionari (Missionary Formation/Animation): Moja kati ya nguzo msingi za Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari ni Malezi Endelevu kuhusu Umisionari. Pamoja na kwamba kila mmoja kwa Ubatizo anafanyika kuwa Mmisionari, ila kuelewa vema matakwa ya umisionari huo ni muhimu kupata malezi stahiki. Kati ya yale mambo mengi ambayo wakati wa uongozi wake Baba Askofu Mkuu Dallu ameyapa kipaumbele ni kuhusu Malezi Endelevu juu ya Umisionari kwa kila kundi la wanakanisa. Ni katika mtazamo huu, amehimiza juu ya kufanya semina mbalimbali katika ngazi ya jimbo, kanda na hata taifa kwa makundi mbalimbali hususan kwa Walezi (Mapadre, Watawa na Walei). Katika mlengo huo huo wa kutoa Malezi Endelevu juu ya Wito wa Umisionari, amehimiza kwa namna ya pekee juu ya kutanua wigo wa fursa za kutolea malezi hayo. Miongoni mwa fursa hizo ni Makongamano ya Majimbo, Kanda na hata Taifa. Itoshe kutaja kwa uchache Makongamano ya Utoto Mtakatifu Kitaifa: Kongamano la Kitaifa lililofanyika katika Jimbo la Mahenge mwaka 2011 lililoongozwa na Kauli Mbiu isemayo: “Mtoto ni Malezi”; Kongamano la Kitaifa lililofanyika katika Jimbo la Tunduru-Masasi mwaka 2014 likiongozwa na Kauli Mbiu: “Nimtume nani? Unitume mimi Bwana” (Isaya 6:8); Kongamano la Kitaifa lililofanyika katika Jimbo la Kondoa mwaka 2023 likiongozwa na Kauli Mbiu: “Ushirika na Utunzaji wa Mazingira.”

Askofu mkuu Dallu: Ushirika na Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba ya wote
Askofu mkuu Dallu: Ushirika na Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba ya wote

Kwa kuzingatia ukweli kuwa Kanisa Katoliki limegawanyika katika ngazi mbili muhimu, yaani Kanisa la Kiulimwengu (Universal Church) na Kanisa Mahalia (Local Church), Baba Askofu Mkuu Dallu alihimiza pia juu ya umuhimu wa kuishi katika muungano na Kanisa la Kiulimwengu lenye makao yake makuu kule Roma. Hivyo basi, kila ilipojitokeza fursa ya kujifunza iliyoratibiwa na uongozi wa Roma, alihimiza ushiriki wa Kanisa Mahalia la Tanzania katika programu hizo kadiri uwezo ulivyoruhusu. Katika kulidhihirisha hili, itoshe tu hapa kuainisha mifano miwili: (1) Mwaka 2018 Ofisi yetu ya Mashirika ya Kipapa Taifa ilituma wawakilishi watatu kushiriki Semina Maalum huko Roma (wakiwemo Pd. Christopher Ndizeye – kwa sasa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Kahama; Sista Dolorosa Kissaka – wakati huo akihudumu kwa nafasi ya Katibu wa Shirika la Utoto Mtakatifu Taifa na Mama Renalda Killa – muamini Mlei kutoka Jimbo la Dar es Salaam anayehudumu kwa nafasi ya Mlezi) na (2) Mwaka 2023 Ofisi yetu ilituma Washiriki Watatu katika Semina Maalum iliyoratibiwa na Shirika la Kipapa la Umoja wa Kimisionari huko Roma (tukiwakilishwa na Pd. Nestory Bombo – Mkurugenzi wa Mashirika ya Kipapa Jimbo la Mbulu, Pd. Silverius Nziku – Mkurugenzi wa Mashirika ya Kipapa Jimbo Kuu la Songea na Sista Anagladness Mrumah – Katibu wa Utoto Mtakatifu Taifa). Mwisho, tunaendelea kumshukuru Mungu kwa namna ya pekee kwa zawadi ya Baba Askofu Mkuu Damian Dallu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea kwa mchango wake wa pekee sana katika Utume wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari kwa hapa Tanzania. Sote tunaalikwa kujifunza kutoka kwake Upendo wa Pekee kwa Utume, Uthabiti na Uwajibikaji (commitment). Aidha, tunatambua kuwa kumaliza utumishi wake kwa nafasi ya Rais wa Tume ya Uinjilishaji sio mwisho, anaendelea kubakia kuwa Mmisionari wa mfano kwetu kupitia utume anaoendelea nao sasa kwa nafasi yake kama Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Songea na majukumu mengine ya kiaskofu. Tunamshukuru Mungu na pia Maaskofu wenzake wote waliomwamini na kumpa dhamana ya kusimamia Utume huu muhimu sana katika Kanisa kwa niaba yao. Mungu atubariki sote!

Askofu mkuu Dallu
16 October 2024, 15:40