Tafuta

Familia ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Familia ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana.  

Askofu Msaidizi Kibozi: Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre na Utawa: Zawadi ya Maisha na Wito!

Askofu Msaidizi Wilbroad Henry Kibozi wa Jimbo Kuu la Dodoma, hivi karibuni amewaongoza waamini katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu Padre Albert Msafiri Lubuva alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre na Sr. Agatha Malusu Leo wa Shirika la Masista wa Mtakatifu Gemma Galgani, Jimbo kuu la Dodoma, alipowekwa wakfu. Imekuwa ni fursa pia kwa watu wa Mungu kumpongeza kwa kuteuliwa na kuwekwa wakfu kama Askofu msaidizi wa Jimbo kuu. la Dodoma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Bikira Maria ni Sanduku la Agano Jipya na la Milele. Ni Mama wa Mkombozi aliyekwenda kumtembelea binamu yake Elizabeti. Hapa wanawake wawili wanaohifadhi ndani mwao Injili ya uhai wanakutana. Bikira Maria ni mtumishi wa Bwana na Elizabeti ni kielelezo cha matumaini mapya kwa Waisraeli. Bikira Maria anakwenda kwa haraka kumsalimia Elizabeti, kielelezo makini cha huduma ya upendo kwa jirani na mfano bora wa kuigwa hasa katika ulimwengu mamboleo unaogubikwa na ubinafsi na uchoyo wa kutisha! Utenzi wa Bikira Maria unajikita katika fadhila ya kusikiliza kwa makini, kutafakari na kutenda kwa imani, mapendo na matumaini. Bikira Maria kumtembelea Elizabeth ni tukio la imani na upendo na ambalo linatangaza utimilifu wa nyakati, kwa kuzaliwa Mkombozi wa ulimwengu anayetanguliwa na Yohane Mbatizaji. Huu ni mwaliko wa kujifunza kujisadaka kwa ajili ya huduma ya mapendo kwa Mungu na kwa ajili ya jirani, jambo ambalo lingeweza kuleta mageuzi makubwa duniani. Bikira Maria kumtembelea Elizabeti ni tukio linalobubujika furaha inayoyajaza maisha ya watu kutokana na ujasiri wa mwanamke mwenye uwezo wa kuona, kusikia na kuguswa na mahitaji ya ndugu yake na hivyo kuwa ni chemchemi ya furaha inayowakutanisha ndugu hawa wawili. Haya ndiyo yanayosimuliwa na Mwinjili Luka; Injili inayobubujika furaha inayoijaza nyoyo za watu!

Shukrani kwa Jubilei ya Miaka 25, Maisha na Wito
Shukrani kwa Jubilei ya Miaka 25, Maisha na Wito

Ni katika muktadha huu, Askofu Msaidizi Wilbroad Henry Kibozi wa Jimbo Kuu la Dodoma, hivi karibuni amewaongoza waamini katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu Padre Albert Msafiri Lubuva alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre na Sr. Agatha Malusu Leo wa Shirika la Masista wa Mtakatifu Gemma Galgani, Jimbo kuu la Dodoma, alipowekwa wakfu. Hii pia ilikuwa ni nafasi kwa watu wa Mungu kutoka Jimbo kuu la Dodoma kumpongeza Askofu Msaidizi Wilbroad Henry Kibozi wa Jimbo Kuu la Dodoma, aliyezaliwa tarehe 30 Aprili 1973. Akapewa Daraja Takatifu ya Upadre 9 Julai 2010. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 12 Februari 2024 akamteuwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu la Dodoma na hatimaye, kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 12 Mei 2024, Jimboni Dodoma. Katika Ibada hii ya Misa Takatifu ameshiriki pia Askofu Emile Mushosho Matabaro wa Jimbo Katoliki la Dungu-Doruma kutoka DRC. Askofu Msaidizi Wilbroad Henry Kibozi katika mahubiri yake amegusia umuhimu wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre na maisha ya kitawa, lengo ni kumshukuru Mungu, na kuomba toba, msamaha wa mapungufu yote yaliyojitokeza katika safari hii ya maisha katika kipindi cha miaka 25, tayari kuomba tena baraka na neema za kuendelea na safari hii ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema kwa ari na moyo mkuu.

Zawadi ya maisha na wito wa kipadre na kitawa ni kwa ajili ya huduma
Zawadi ya maisha na wito wa kipadre na kitawa ni kwa ajili ya huduma

Hii imekuwa ni fursa pia ya kusali na kuombea miito mitakatifu kwa kutambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumba, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Huu ndio mwelekeo wa pekee uliotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, changamoto inayofanyiwa kazi na Mama Kanisa, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia, kielelezo cha ukomavu wa imani. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii. Lakini, familia katika ulimwengu mamboleo inakabiliwa na changamoto pevu kama zilivyoainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia.” Hii ilikuwa ni siku ya pekee kwa Maaskofu, mapadre, watawa na waamini walei kusherehekea kwa pamoja safari ya miaka 25 ya sadaka, majitoleo na huduma kwa watu wa Mungu. Shukrani na pongezi kwa Sr. Agatha Malusu Leo aliyezaliwa tarehe 2 Februari 1972, Kondoa, Parokia ya Goima na kuweka nadhiri zake za kwanza kunako mwaka 1999, Lumuma, Jimbo kuu la Dodoma na Nadhiri za daima mwaka 2006 Kondoa. Kwa sasa anafanya utume wake katika Parokia ya Castelcovati, Jimbo Katoliki la Brescia, nchini Italia. Padre Albert Msafiri Lubuva kwa muda wa miaka saba yuko kwenye Parokia ya Missaglia akitoa huduma yake kwenye Chama cha Mama Yetu wa Lourdes - San Luigi, Jimbo kuu la Milano. Padre Lubuva alipewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 15 Agosti 1999.

Shukrani kwa Mungu kwa Zawadi ya Uhai na Wito
Shukrani kwa Mungu kwa Zawadi ya Uhai na Wito

Kumbe, hii imekuwa ni Siku ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya: Imani, maisha na wito wa kipadre na kitawa pamoja na kuwaombea wazazi waliotangulia mbele za haki, wakiwa na tumaini la ufufuko, maisha na uzima wa milele. Imekuwa ni fursa ya kusali kwa ajili ya kuombea familia kwa kutambua kwamba, familia za kikristo ni chimbuko la miito mitakatifu ndani ya Kanisa, hili ndilo Kanisa la nyumbani, shule ya utakatifu, haki, amani, upendo na ukarimu na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Ni mahali ambapo mtu anajifunza kuonja upendo na hali ya kujitoa kwa ajili ya wengine, changamoto kwa wazazi kuwa kweli ni mashahidi wa tunu msingi za maisha ya kifamilia. Askofu Msaidizi Wilbroad Henry Kibozi wa Jimbo Kuu la Dodoma amewaomba wanafamilia kuonesha ukarimu na upendo, kwa kulea na kukuza miito mitakatifu ili hatimaye, Kanisa liweze kuwapata wahudumu na mashuhuda wa Injili walio wema, watakatifu, waadilifu, wachapakazi na wachamungu. Kwa upande wake, Askofu Emile Mushosho Matabaro wa Jimbo Katoliki la Dungu-Doruma kutoka DRC katika salam zake kwa waamini amegusia kuhusu: fursa, shida, changamoto na matatizo yanayowakumbuka watu wa Mungu Jimboni mwake na DRC katika ujumla wake! Huu ni mwaliko kwa watu wote wa Mungu kuguswa na matatizo ya Wakristo sehemu mbalimbali za dunia na zaidi wasali kwa ajili ya kuombea: haki, amani, utulivu na maridhiano. Anasema, yeye alipewa Daraja takatifu ya Upadre tarehe 17 Septemba 2000 na kuwekwa wakfu kuwa Askofu 8 Desemba 2022. Kumbe, panapo majaliwa ataadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre mwaka 2025.

Askofu Msaidizi Kibozi
02 October 2024, 13:42