Cameroon:Padre Badjougou wa Togo auawa huko Yaoundé
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Padre Christophe Komla Badjougou, Mtawa wa Shirika la Fidei Donum wa Togo aliuawa huko Yaoundé, mji mkuu wa Cameroon, jioni ya tarehe 7 Oktoba 2024. Padre huyo aliuawa kwa kupigwa risasi mbele ya lango la Wamisionari wa Moyo Safi wa Maria (CICM) huko Mvolyé, kitongoji cha mji mkuu. Askofu Mkuu Jean Mbarga, wa Jimbo Kuu la Yaoundé, alielezea huzuni yake kubwa na kutuma salamu za rambirambi kwa familia ya padre, marafiki zake na jumuiya nzima ya Kikristo. “Katika hali hii ya kusikitisha, Jimbo kuu la Yaoundé linatoa rambirambi zake za dhati kwa familia ya Padre Christophe, marafiki zake na waamini wa Jimbo la ya Yagoua. Jumuiya ya Kikristo inaalikwa kusali ili iweze kupata neema na Mungu” alisema Askofu Mkuu wa Yaoundé.
Kuhusu kifo chake
Kulingana na mamlaka ya Cameroon, Padre huyo aliuawa wakati wa wizi wa barabarani. Picha zilizopigwa na Camera za uchunguzi zilizopo kwenye eneo la uhalifu zilifanya iwezekane kuunda upya mienendo ya mauaji. Kulingana na kile ambacho kamishna wa polisi alitangaza kwa vyombo vya habari vya Togo kwamba: “Camera za uchunguzi zilizo kwenye eneo la uhalifu zinaonesha kwamba Padre huyo alitoka sehemu inayoitwa “Dakar en bas” kwa pikipiki iliyomwacha mbele ya lango la Wamisionari wa Moyo Safi wa Maria(CICM.) Sekunde chache baadaye, watu wawili walionekana wakiwasili kwa pikipiki kutoka upande wa Mvolyé. Baada ya kumpita yule Mtawa, waligeuka nyuma kurejea getini aliko Padri Christopher. Picha hizo zinaonesha ugomvi kati ya mwathiriwa na mmoja wa wauaji ambaye alifanikiwa kumiliki begi la Padre huyo. Kisha mhalifu huyo alimpiga risasi mbili hewani kisha akampiga risasi tatu Padre ambaye alianguka chini.”
Nyadhifa alizokuwa nazo
Padre Christophe alikuwa wakili wa parokia ya Watakatifu Petro na Paulo wa Zouzoui katika jimbo la Yagoua, eneo la Kaskazini ya Mbali nchini Togo. Alikuwa akipitia Yaoundé ambapo alikuwa karibu kuondoka kuja Italia kufanya mafunzo ya mwaka mmoja. Padre Christophe alikuwa sehemu ya chama cha Wafanyakazi Wakimya wa Msalaba akiongozwa na Mwenyeheri Luigi Novarese ambaye nyumba yake mama iko Ariano Irpino katika Madhabahu ya Valleluogo. Asili yaje kutoka Togo, alipewa daraja la upadre mnamo 2013 katika Kanisa Kuu la Mama Yetu wa Utatu, huko Atakpamé. Akiwa mwanashirika wa CICM tangu mwaka 2014 alianza utume wake katika jumuiya ya Mouda na alitumia muda wake katika huduma kama mkufunzi na kama paroko wa parokia ya Zouzoui.