Tanzania;Ask.Mwijage:fungua macho ya Imani na achana na utapeli wa madhehebu wa kutafuta miujiza
Na Patrick P.Tibanga- Radio Mbiu na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika Mwezi wa kumi ambao kwa Kanisa Katoliki ni mwezi wa Mama Maria, Mama Kanisa anatukumbusha kumwelekea Yeye kama Mama wa Mbinguni, kumpatia heshima yake na kumuomba kwa maombezi yake kwa mwanae Yesu kristo, kupitia kusali Rozari. Ni mwezi ambao daima umekuwa na matukio mengi hasa kusali katika vituo mbali mbali, kama vile Madhabahu za kitaifa na kimataifa, katika vituo rasimi vya kijimbo, katika makanisa na nyumbani. Ni katika mukatadha huo hasa tunapoelekea kufunga Mwezi wa Maria na mwezi wa Kimisionari, Jimbo katoliki la Bukoba lilifanya matembezi ya miguu kutoka sehemu mbali mbali kufikia kituo cha Hija kiitwacho Nyakijoga kwa heshima ya Bikira Maria wa Lourdes katika Parokia ya Mugana Jimbo Katoliki Bukoba, nchini Tanzania Jumamosi tarehe 26 Oktoba, na Dominika tarehe 27 Oktoba 2024, ikahitimishwa kwa Adhimisho la Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Jovitus F. Mwijage wa Jimbo hilo akishirikiana na Askofu Almachius Vincent Rweyongeza, Askofu wa Jimbo Katoliki la Kayanga, na Askofu Methodius Kilain, Askofu Mstaafu wa Jimbo katoliki la Bukoba, Tanzania.
Askofu Mwijage katika homelia yake alisema kuwa kupitia Mama Bikira Maria kila Mkristo anatakiwa kumkimbilia mama Maria ambaye ataondoa hofu na mashaka kwa kuwa wanadamu ni watu wenye wasiwasi na kumkimbilia Mama Bikira Maria ili awaombee mahitaji yao.
“Katika harusi ya Kana, Mama Bikira Maria hakuombwa, kwamba watu wanahitaji divai bali aliona mahitaji ya watu akawaombea, hivyo ndugu zangu tumekuja hapa kumuomba mama Bikira Maria huenda mengine tukasahau lakini yeye anatuona kama watoto wake kama nyie wakina mama mnavyoona huko nyumbani unamuangalia mtoto unaona amepungukiwa hili na lile, ukiomba hapa ukasahau Mama Bikira Maria ataona mahitaji yako katika familia, watoto wako biashara na mahitaji yako na mahangaiko yako uliyo nayo wewe na familia yako, katika kazi na yeye atakuombea kwa mwenyezi Mungu,’’ Alisisitiza Askofu Mwijage.
Akiendelea na homelia yake Askofu Mwijage aidha alikemea tabia ya baadhi ya waamini kuomba miujiza kwa waganga wa kienyeji na watu wengine kwani alisema “Mama Maria hajawahi kumkatalia mtu” na kuwasishi waamini “kufungua macho ya Imani ili kuepuka matapeli kwa njia ya dini.” Askofu alisema “Hivyo waamini ninawaomba tuje kwa mama Bikira Maria tusiende kuomba miujiza kwa waganga wa kienyeji tuje kwake mama Bikira Maria atatusaidia kama tulivyosikia hajawahi kumkatalia mtu, kwani yeye atatutimizia mahitaji yetu ikiwa nyakati zetu hatuna budi kufungua macho ya Imani na kuachana na utapeli wa madhehebu unaoendelea kwani Yesu hakutaka miujiza yake ijulikane kwa sababu hakutaka umaarufu wa aina yoyote kwa wakati huu watu wanaojiita wanatenda miujiza wanataka umaarufu,’’ Alisisitiza Askofu Mwijage.
Akizungumzia juu ya kutoa ushuhuda kwa wale wanaotendewa miujiza, Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba alisema Kanisa Katoliki linachukua muda mrefu ili kujiridhisha na miujiza kwa kuwashirikisha madaktari ili wathibitishe juu ya Mgonjwa huyo ukiona mtu anatoa ushuhuda wa kupata gari au pikipiki ndani ya siku moja, shituka mkristo hao ni wezi na matapeli wa imani. “Mtu akisema ameponywa Kanisa letu halipokei kirahisi hivyo ni lazima lipitie mchakato, kama ana kansa lazima kutumia madaktari wanaothibitisha kuwa mtu huyo alikuwa na kansa au hatungi mimba, lakini kwa madhehebu haya yanayochipuka utasikia mtu anasema amepona kirahisi tu, nani anayethibitisha uponyaji huo? Ni udanganyifu mkubwa” Alihoji Askofu Mwijage katika homilia yake.
Askofu Mwija aidha amewataka wanandoa kukimbilia kwa Bikira Maria ili awaombee kwa Yesu aongeze divai kama alivyofanya huko Kana, aondoe magumu yote na huku aliwafundisha vijana kuwa ndoa takatifu ni ya mume na mke mmoja, siyo ya mashoga wala wasagaji na kuwashauri wanadoa wasitumie vidonge wala chanjo za kuua uzazi kwa kuwa kuna viashiria vya kupunguza uzao.
“Kwa hiyo ndugu zangu hatuna budi kuendelea kuitukuza Sakramenti ya ndoa na kuwafundisha hasa vijana waliopo shuleni na vyuo mbali mbali kwamba ndoa ni takatifu ya mme na mke na si vinginevyo kwani zaidi ya hapo hiyo sio ndoa na tuendelee pamoja kuhimiza watu wasitumie vidhibiti mimba au chanjo mbali mbali za kumaliza uzazi, tusije tukapata majanga kama tunavyoona shemu mbali mbali.” Kwa kutoa mfano dhahiri Askofu alisema “Mwaka jana alikuja Askofu kutoka Peoria amefunga zaidi ya makanisa 100, kwa sababu hakuna watu wa kusali na kutuma kwenye miito hivyo tulinde vizazi na uzao wetu tusipunguze uzao.’’
Askofu Mwijage alihitimisha homilia yake kwa kuwashukuru mahujaji waliotembea pamoja katika kumuunga mkono kwenye matembezi ya kuwezesha ujenzi wa hostel ya Nyakijoga unaotarajiwa kuanza Januari 2025 pamoja na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake wa shilling millioni 50 kufanikisha Ujenzi huo.
Katika matembezi hayo ya hisani yaliyofanyika Jumamosi tarehe 26 Oktoba 2024, yaliongozwa na Askofu mwenyewe Jovitus Mwijage wa Bukoba, akiwa pamoja na Askofu Almachius Rweyongeza wa Jimbo Katoliki la Kayanga na Askofu Method Kilaini, Askofu Mstaafu wa Jimbo Katoliki Bukoba ambapo matemezi ya hayo yalianzia kutoka Kanisa Kuu la Bukoba kuanzia saa 3. 48 asuhuhi na kuwasili saa 10. 04 jioni, katika Parokia ya Mugana Jimbo la Bukoba ambapo ni zaidi ya 26.8 Km.
Hija na Misa ilidhuliwa na Mapadre wengi kutoka jimbo loto la Bukba na majimbo ya karibu, watawa kike na kiume na waamini watu wa Mungu na wenye watu wa mapenzi mema ambao walijaza eneo lote la kituo cha hija kwa heshima ya Bikira Maria.