Tafuta

Mtakatifu Paulo wa Msalaba: Furaha katika mateso na maumivu ya ndani chemchemi ya matumaini mapya! Mtakatifu Paulo wa Msalaba: Furaha katika mateso na maumivu ya ndani chemchemi ya matumaini mapya! 

Mtakatifu Paulo wa Msalaba: Furaha Katika Mateso na Maumivu Ya Ndani!

Kwa kuyapokea mateso na magumu katika hija ya maisha tunaungana na Kristo mwenyewe aliyeiendea njia ngumu ya msalaba, iliyojaa uchungu na maumivu makali ili kuweza kuukomboa utu wetu ulioharibiwa na dhambi. Ni katika mtazamo huo tunamuona mtumishi wa Mungu Mtakatifu Paulo wa Msalaba aliye kuwa tayari wakati wote kuyapokea mateso akiamini kwamba ni katika mateso kuna saburi, furaha tele na matumaini katika maisha mapya! MATESO!

Na Padre Octavian Onesmo Hinju, CP – Morogoro, Tanzania.

Ndani ya moyo na maisha ya Mt. Paulo wa Msalaba tunapata mwaliko wa pekee wa kurejea tena maneno ya Mt. Ignatio wa Antiokia anaye fundisha katika barua yake kwa kanisa la Roma akisema kwamba “Mimi ni ngano ya Mungu na nisagwe sagwe na meno ya wanyama wa kali, ili niweze kumpatia Kristo mkate safi”, yaani utayari na msukumo wa ndani wa kuyavumilia na kuyakabili magumu na mahangaiko yetu ya maisha tukiamini kwamba tuzo lake ni kubwa mbinguni. Tema ya mateso ingawa haizoeleki wala kufurahisha katika maisha ya wanadamu lakini ni ufunguo wa kujitumbukiza katika Moyo Mtakatifu wa Yesu ili kuweza kuchota nguvu na kuonja ukuu wa huruma ya Mungu iliyo kitovu cha upendo wake; kama anavyo kaza kusema Mtakatifu Paulo wa Msalaba kwamba “mateso ya Kristu ni bahari pana yenye kina kirefu, mwombe Bwana akuwezeshe kuzama na kuogelea katika bahari ya mateso.” Tema ya mateso inapaswa kushughulikiwa katika namna ambayo haipelekei watu kukata tamaa ya maisha na kuhisi wametengwa sio tu na ulimwengu lakini na Mungu Muumba wao. Kwa kuyapokea mateso na magumu katika hija ya maisha tunaungana na Kristo mwenyewe aliyeiendea njia ngumu ya msalaba, iliyojaa uchungu na maumivu makali ili kuweza kuukomboa utu wetu ulioharibiwa na dhambi. Ni katika mtazamo huo tunamwona Mtumishi wa Mungu Mtakatifu Paulo wa Msalaba aliye kuwa tayari wakati wote kuyapokea mateso akiamini kwamba ni katika mateso kuna saburi na furaha tele. Mpendwa Msikilizaji na Msomaji wa Vatican News, kila mwaka tarehe ifikapo tarehe 19 Oktoba Mama Kanisa ulimwenguni kote anafanya kumbukumbu ya Mtakatifu Paulo wa Msalaba Padre na Baba Mwanzilishi wa Shirika la Kimisionari la Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo. Paulo Francesco Danei alizaliwa huko Ovada, Piedmont katika miji ya Torino na Genoa nchini Italia mnamo tarehe 3 Januari mwaka1694 kwa baba Luca Danei na mama Anna Maria Massari. Ni mtoto wa pili kuzaliwa kati ya watoto 16 wa baba na mama yake ambapo miongoni mwao ni 6 tu ndio walio salia kufuatia vifo wakati wa utoto, hii ilimfanya Paulo kuwa mkubwa kati ya watoto walio bakia. Katika hali ya namna hii, Paulo alijifunza tangu akiwa mdogo ukweli juu ya kifo na ugumu wa maisha. Hivyo kufanya maisha yake mwenyewe kuwa tafakari ya kwanza juu ya Mateso na Msalaba wa Kristo.

Angalieni furaha inayobubujika katika Moyo Mtakatifu wa Yesu
Angalieni furaha inayobubujika katika Moyo Mtakatifu wa Yesu

Mwaka huu tunaadhimisha Sikukuu yake tukiwa bado na kumbukumbu njema za Jubilee ya takribani miaka 300 tangu yeye mwenyewe alipo anzisha Shirika letu. Ingawa sherehe za Jubilee ziligubikwa na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona-Uviko-19 kiasi cha kushindwa kuziadhimisha kwa shamrashamra na bashasha kubwa, pengine ilikuwa kwetu fundisho kuu la kuiona furaha itokayo kwa Kristu katika magumu na yale yanayo tuumiza katika maisha yetu ya kila siku. Ni changamoto ya kumwiga Kristo aliyeteseka kwa upendo bila manung’uniko nafsi mwake. Kristu kama alivyo fanya Yeye mwenyewe anatutaka kuyaacha yote mikononi mwa Mungu Baba mwenye huruma, ‘Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu (Lk. 23:46). Hili linajidhihirisha pia katika hatua za mwanzo na harakati za Paulo katika kuanzisha shirika. Licha ya kukataliwa na kunyimwa idhini ya kukutana na Baba Mtakatifu, hakusikitika ama kukata tamaa bali alishuka chini kwa magoti alisali ili kuomba msaada ya Mungu. Anatufundisha sio tu kusamehe lakini pia kuwaombea wale wote wanaotumia nafasi na mamlaka walizo nazo kunyanyasa nakuwasukumiza wengine pembeni, ‘Baba, wasamehe, kwa maana hawajui walitendalo, (Lk. 23:34). Aliyachukua yote moyoni mwake (Lk. 2:19) na kuyaunganisha yale ya Kristu msalabani. Huu ni mwaliko pia kwa waamini wote kuhakikisha kwamba, wanaunganisha mahangaiko yao pamoja na mateso ya Kristo Yesu. Kristo Yesu katika maisha na utume wake alikuwa na huruma sana kwa watu kwa sababu kwake walikuwa kama Kondoo wasiokuwa na mchungaji (Mt. 9:36). Aliwaonea huruma watu zaidi ya elfu, akawalisha kwa mikate saba na samaki wawili (Yoh. 6; Mt 14:13-21; Mk 6:30-44; Lk 9:10-17). Aliwahudumia wagonjwa bila kuchoka; akasimama na kusikiliza kilio chao kama ilivyotokea kwa wale vipofu wawili wa Yeriko (Mt. 20:29-34). Kwa hakika kulikuwa na umati mkubwa sana wa wagonjwa walioomba huruma yake, kama ilivyotokea kwa wakoma kumi na kama alivyomfufua kijana wa Naini, Mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane. Huruma hii ilimwezesha Kristo Yesu kuwa karibu na wagonjwa hata kiasi cha kujitambulisha nao akisema, “nilikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama.” Kristo Yesu aliguswa na ugonjwa na mateso ya watu wengi, kiasi cha kuwashughulikia kikamilifu, ili kuwaokoa na kuwashirikisha upendo wake usiokuwa na kikomo; upendo uliomfanya hata akatundikwa Msalabani na hivyo kutoa maana mpya ya mateso katika maisha ya mwanadamu.

Mtakatifu Paulo wa Msalaba Muasisi wa Shirika la Mateso ya Kristo
Mtakatifu Paulo wa Msalaba Muasisi wa Shirika la Mateso ya Kristo

Katika kuyapokea mateso kwa mtazamo chanya ni mwanzo wa mapendo ya dhati na kweli ambayo Mtakatifu Paulo wa Msalaba anayaona katika mti wa msalaba na bustani ya Gethsemane. Kwa wengi mti wa msalaba ni aibu na adhabu lakini kwetu sisi ni mti wa wokovu kama tunavyo alikwa siku ya Ijumaa kuu kwa wimbo wa kilatino unaosema “Ecce lignum crucis, in quo salus mundi pependit: venite, adoremus” yaani Huu ndiyo mti wa msalaba ambao wokovu wa ulimwengu umetundikwa juu yake, njoni tuabudu. Kumbe tema ya mateso kama chanzo cha furaha ni fundisho zuri kulirithisha kwa kila kizazi ili vizazi vijavyo viweze kuiga tena mfano wa mtumishi wa Mungu Ayubu aliye ona bado nafasi ya kujipatia utakatifu katika mateso. Ndugu msomaji na msikilizaji wa Vatican News, katika tafakari yao juu ya wimbo huu ndiyo mti wa msalaba ambao ni wokovu wa ulimwengu, njoni tuabudu. Mababa wa Kanisa: Mtakatifu Ambrosi na Augostino walilinganisha mti wa Msalaba na mti wa Edeni. Mahali ambapo pana uzuri wa ajabu ambao unatufanya tumtafakari na kumfurahia Mungu Mkuu. Ulinganisho wao ulikuwa ukitofautisha kati ya mti wa Edeni ulioning’iniza tunda lililosababisha hukumu yetu, yaani dhambi na mauti viliingia ulimwenguni kwa tendo la tunda la mwanzo wakati Mti wa Msalaba ulining’iniza tunda ambalo lilituongoza kufikia wokovu wetu kama anavyo tanabaisha Mt. Anselm wa Kantabari katika kitabu chake “Cur Deus Homo” yaani kwanini Mungu alifanyika mwanadamu: Tafakari juu ya Fumbo la Umwilisho. Kuwa dhambi iliyo ingia ulimwenguni kwa njia ya mwanadamu ilitakiwa mwanadamu mwingine mkamilifu katika ukamilifu wote yaani Kristu ilikuukomboa utu wa kale kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake wa ajabu. Asili ya mti wa Msalaba na kwa sababu hiyo tunda ambalo hutegemea kutoka kwake ni kiini tofauti kabisa na kile kilichoashiria mwanzoni mwa historia yetu ya kutotii na umbali wetu kutoka kwa Mungu; umbali ambao hutuletea mateso na mahangaiko ya ndani. Kwa sababu hiyo, ikiwa kwa kutotii kwa Adamu wa kwanza, tunda la hukumu yetu lilinyang’anywa kutoka katika mti wa Edeni, na kwa utii wa Adamu mpya tunda la wokovu wetu liling’olewa kutoka mti wa Msalaba, ambalo katika hali ambayo hatuelewi zaidi lakini ya kupendeza na kushangaza inafanana na Adamu mpya huyo huyo, ambaye ni Kristo na ni hilo tunda ambalo tunataka kulichuma kwa njia ya uvumilivu katika mateso tukiongozwa na tafakari ya maisha aya Mt. Paulo wa Msalaba. Ni yule ambaye kwa kutii anachukua wokovu ambao unatoka kwa Mungu na kwa hali halisi ni mtu yule yule, yaani Bwana mmoja Yesu Kristu, mwana wa pekee wa Mungu. Aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote. Mungu aliyetoka kwa Mungu, mwanga kwa mwanga, Mungu kweli kwa Mungu kweli. Aliyezaliwa bila kuumbwa, mwenye umungu mmoja na Baba, kama tunavyo sali katika kiri kuu ya Imani yetu katika Kanuni ya Imani ya Nicea.

Fumbo la Pasaka ni chemchemi ya imani, matumani na mapendo
Fumbo la Pasaka ni chemchemi ya imani, matumani na mapendo

Mpenzi msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tunapo yatafakari hayo yanayo muhusu Mtakatifu Paulo wa Msalaba tunajipima nasi katika maisha yetu ya kawaida ya kila siku. Upi ni mtazamo wetu juu ya magumu, shida na mahangaiko yetu ya maisha? Wakati mwingi tumekuwa watu wa kulalamika na kuhudhunika tukilaani na kujikatia tamaa. Kumbe, Ndani ya moyo na maisha ya Mtakatifu Paulo wa Msalaba tunapata mwaliko wa pekee wa kurejea tena maneno ya Mt. Ignatio wa Antiokia anaye fundisha katika barua yake kwa kanisa la Roma akisema kwamba “Mimi ni ngano ya Mungu na nisagwe sagwe na meno ya wanyama wa kali, ili niweze kumpatia Kristo mkate safi”, yaani utayari na msukumo wa ndani wa kuyavumilia na kuyakabili magumu na mahangaiko yetu ya maisha tukiamini kwamba tuzo lake ni kubwa mbinguni. Maisha yetu ni mfano tunda, ni kuwaza utamu wa kuonja na wakati huo hapa tuwaze tunda linazungumzia maisha si uchungu na kifo tu bali furaha ya kuupata uzima wa milele. Pamoja na ukweli kwamba mateso ni tema na fumbo lilisiloeleweka kwa mwandamu la mapenzi ya Mungu kwetu wanadamu lakini linatoa uhakika wa umilele katika Kristo Bwana wetu. Maisha yetu yawe daima ni Injili ya msalaba inayo jitanabaisha katika ukweli kwamba msalaba huleta saburi na wokovu. Katika magumu ya ndoa za kikristu, uchungu wa kufiwa na wapendwa wetu, magumu ya utume wetu na kazi za uinjilishaji wa kina, tujiandae kukabiliana na mateso kwa furaha kubwa ili ukuu wa Kristo ujifunue kwa watu wote kupitia sisi.  Tukumbuke kwamba mateso ni lazima kwa kila anayekubali kumfuasa Kristu aliye yakabili mateso kwa Imani kuu. Katika Waraka wake wa Kiitume wa Salvifici Doloris wa Mtakatifu Yohane Paulo II, 1984 Mtakatifu Yohane Paulo II anasema kuwa: “Wale wanaoshiriki katika mateso ya Kristo huwekwa katika mateso yao chembe maalum sana ya hazina isiyo na kikomo ya ukombozi wa ulimwengu, na wanaweza kushirikishana hazina hii na wengine. Kadiri mwanadamu anavyotishiwa na dhambi, ndivyo miundo ya dhambi ilivyo nzito ambayo ulimwengu wa leo umebeba ndani yake, na ndivyo unavyozidi kuwa ufasaha ambao mateso ya wanadamu wanayo wenyewe. Na ni kadri Kanisa linavyohisi zaidi hitaji la kukimbilia thamani ya mateso ya wanadamu kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu na tunawaomba ninyi nyote mnaoteseka, kutuunga mkono. Na zaidi ninyi nyote ambao ni wadhaifu, muwe chanzo cha nguvu ya Kanisa na kwa ajili ya wanadamu. Katika vita ya kutisha kati ya nguvu za mema na mabaya, ambayo ulimwengu wetu wa kisasa unatupatia, mateso yenu yashinde kwa muungano na Msalaba wa Kristo.”

Shirika la Wamisionari wa Mateso ya Bwana
Shirika la Wamisionari wa Mateso ya Bwana

Ingawa zipo nyakati Ni kama vile hatupendezwi na mapenzi ya Mungu yaani Yeye anaye ruhusu tupitie mateso ni kama vile hatuna tena tofauti na Mtakatifu Petro baada ya Yesu kuwatangazia kifo na mateso yake, Petro alikataa kwamba jambo hilo halitatokea. (Mt. 16: 21-23). Hata sisi tumejiuliza mara nyingi swali kwamba ‘kwanini mimi? Kwanini nayapitia haya? Kumbe, tunapaswa kuyapokea yote kwa maana ni kama mbegu iliyopandwa, ambayo isipokufa haiwezi kutoa matunda. Naye Baba Mtakatifu Francisko anatufunda akisema kwamba “yapo mengi yenye kuumiza yanayo waka ndani mwetu. Haya ni mateso na mahangaiko yenye kutunyong’onyeza.  ambayo yanawaka ndani mwetu, kiasi cha kusumbua moyo; wakati huo huo, hata hivyo, ikiwa tutatoka, kama wanavyofanya wengine kwa ujasiri mwingi na hata kwa shida, ni maswali haya ya uchungu ambayo hufungua cheche za mwanga, ambayo hutoa nguvu ya kusonga mbele. Kiukweli, hakuna kitu kibaya zaidi kuliko kunyamazisha maumivu, kuweka ukimya juu ya mateso, kuondoa kiwewe bila kushughulika nacho, kama ulimwengu wetu mara nyingi hutuongoza katika kukimbia matatizo kwa namna usingizi wetu. Ikiwa inatulazimisha kuzama katika kumbukumbu chungu na kuomboleza hasara, inakuwa wakati huo huo hatua ya kwanza ya sala na inatufungua sisi kupokea faraja na amani ya ndani ambayo Mungu hakosi kamwe kutoa. Injili inatuambia juu yake, katika kifungu hicho ambacho walivuviwa kutoa jina la safari yao (Mk. 5: 22-43). Inatuambia juu ya mkuu wa sinagogi, pamoja na binti mgonjwa sana; mtu huyo habaki kufungwa katika maumivu yake, akiwa na hatari ya kukata tamaa, bali alimkimbilia Yesu na kumsihi aende nyumbani kwake. Kwa mfano wa Mt. Paulo wa Msalaba, tusafiri na Yesu katika uchungu na maumivu ili aweze kutupa faraja ya kweli na ahueni ya kudumu. Nawatakia sherehe njema ya Mt. Paulo wa Msalabana Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristu yawe daima mioyoni mwetu. AMINA.  Tumsifu Yesu Kristo.

19 October 2024, 10:48