Seminari Ndogo ya Limbo ilishambuliwa na Padre Thomas Oyode kutekwa nyara!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Jimbo Katoliki la Auchi nchini Nigeria, limetangaza kwamba "mnamo saa 1 jioni ya siku ya Dominika tarehe 27 Oktoba 2024, Mapadre na Waseminari wa Seminari Ndogo ya Mkingiwa Dhambi ya Asili huko Ivhianokpodi, Etsako Mashariki Halmashauri ya Jimbo la Edo, walishambuliwa na watu wenye silaha wakati wa sala zao za masifu na Baraka." Hayo yametolewa na taarifa kutoka kwa Padre Peter Egielewa, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Jimbo Katoliki la Auchi nchini Nigeria. Katika taarifa hiyo inaendelea: "Katika mchakato huo, Mkuu wa taasisi hiyo, Padre Thomas Oyode, alitekwa nyara na kupelekwa msituni. Hata hivyo, Makamu Gambera wa Seminari na Wanaseminari wote wamehesabiwa na wako salama na wamehamishwa kwa muda katika eneo salama hadi hatua za ulinzi wa kuzunguka Seminari hiyo zitakapoimarishwa.Kwa bahati mbaya, hakuna bado mawasiliano ambayo yamefanywa na watekaji nyara."
Waamini waungane kumwombea Padre aliyetekwa nyara
Kutokana na tukio hilo Mkurugenzi wa Mawasiliano Jimbo aidha anabainisha kuwa: "Taarifa rasmi ya tukio hilo imewasilishwa kwa Vyombo vya Utekelezaji wa Sheria na tunatarajia msaada wao katika kufanikisha kuachiliwa kwa padre wetu aliyetekwa nyara. Seminari ndogo ya Mkingiwa Dhambi ya Asili ilianzishwa na Askofu wa Kikatoliki wa Auchi, Askofu Gabriel Dunia, mnamo mwaka wa 2006 kwa ajili ya mafunzo ya mapadre wa baadaye. Zaidi ya wanafunzi 500 hadi sasa wamefaulu kufuzu kutoka katika taasisi ya Kanisa. Jimbo katoliki la Auchi linawaomba watu wote wenye mapenzi mema kuungana na waamini wa Jimbo hilo katika sala ili watekaji nyara wamwachie Padre Oyode bila kujeruhiwa."