Tafuta

Sherehe ya Watakatifu Wote: “Tazameni ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu, na ndivyo tulivyo” (1Yn 3:1) Sherehe ya Watakatifu Wote: “Tazameni ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu, na ndivyo tulivyo” (1Yn 3:1)  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Sherehe ya Watakatifu Wote: Wote Wanaitwa Kuwa ni Watakatifu

Katika Sherehe hii ya Watakatifu Wote, Mama Kanisa anataka kumsifu na kumtukuza Mungu kwa njia ya watakatifu wake ambao wametambuliwa rasmi na Mama Kanisa: “Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-Kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao.” Ufu 7:9.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Mama Kanisa kila mwaka tarehe Mosi, Novemba, anaadhimisha Sherehe ya Watakatifu wote: “Sollemnitas Omnium Sanctorum” iliyoanzishwa na Papa Gregori IV (827-844). Katika Sherehe hii, Mama Kanisa anataka kumsifu na kumtukuza Mungu kwa njia ya watakatifu wake ambao wametambuliwa rasmi na Mama Kanisa: “Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-Kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao.” Ufu 7:9. Pamoja nao ni kundi lote la wabatizwa si kadiri ya matendo yao bali ni kadiri ya neema, kuhesabiwa haki na imani inayowafanya kuwa watakatifu na hivyo wanaonywa kuishi iwastahilivyo watakatifu. LG 40. Utakatifu wa maisha ni changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo, kwani utakatifu kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko ni chemchemi ya furaha ya kweli inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu! Utakatifu ni hija ya mapambano dhidi ya dhambi kwa kuendelea kupyaisha ile neema ya utakaso ambayo waamini wameipokea katika Sakramenti ya Ubatizo! Utakatifu unawawezesha waamini kuguswa na mahangaiko ya jirani zao, kwa kutambua na kuthamini utu na heshima yao kama watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Waamini wanaitwa kuwa watakatifu kwa sababu Mwenyezi Mungu ni Mtakatifu na ni kiini na utimilifu wa utakatifu wenyewe.

Sherehe ya Watakatifu Wote: Changamoto ya Utakatifu wa maisha
Sherehe ya Watakatifu Wote: Changamoto ya Utakatifu wa maisha

Utakatifu ni changamoto inayopaswa kupaliliwa kila kukicha na kamwe haitoshi kuwa Mkristo na mwamini kuanza kubweteka, bali daima ajitahidi kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, amani, upendo na mshikamano unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Kadiri ya Somo la Pili (1Yoh 3:1-3) pendo la Baba limetufanya wana wa Mungu.. kwa pendo la Baba tumefanyika waamini wa Kanisa kubwa, Yerusalemu ya Mbinguni aliye mama yetu.. kwa pendo la Baba tumekuwa ndugu: kaka na dada katika ukoo bora, raia katika ufalme wa ajabu na askari katika jeshi kubwa. Ni kwa pendo la Baba tumekuwa wanafunzi katika chuo kisifika tena, kwa njia ya pendo hilo la Baba sote tu wanafamilia wateule wa Mungu, tumejumuishwa kati ya umati ule, mkutano mkubwa usiohesabika kadiri ya somo I (Ufu 7:2-4, 9-14) ‘watu kutoka kila taifa, na kabila, na lugha na jamaa’.. ni watakatifu hawa, wana wa Mungu ambao kwa ubatizo wetu tumejumuishwa miongoni mwao kwa njia ya pendo hilo kuu la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu.

Utakatifu wa Mashuhuda wa Imani
Utakatifu wa Mashuhuda wa Imani

UFAFANUZI: Tunaadhimisha upendo wa Mungu anapomshirikisha mwanadamu uzima, makao na utukufu wa kimbingu, ni sherehe inayodhihirisha huruma ya Mungu anayefungua milango ya Paradisi kwa ajili ya wanawe wateule. Ni Sherehe ya watakatifu wote, watumishi wa Mungu ‘waliotoka katika dhiki ile iliyo kuu nao wamefua mavazi yao na kuyafanya meupe katika damu ya Mwanakondoo’ (Ufu 7:9). Watakatifu waliishi na kujaribiwa kama sisi, wapo waliotenda dhambi kama sisi na kuzidi, lakini walijitahidi kwa neema ya Mungu na kwa unyofu wao wa maisha.  Kama vile wao walivyojikongoja kwa uthabiti wa imani na uhodari katika majaribu sisi nasi tufanye vivyo hivyo.. vile wao walivyojitahidi kumpenda Mungu kwa dhati yote, kutambua thamani yake na kumpa nafasi ya kwanza kwetu iwe hivyo… vile walivyodharau fahari za kidunia nasi tuzingatie ya milele ‘tukiyatafuta yaliyo ya juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Baba’ (Kol 3:1) Tunapowatafakari watakatifu tujione tuna bahati. Kwamba kumbe inawezekana. Yote yanayohitajika ili mwanadamu awe mtakatifu tunayo, muhimu ni kuhakikisha ukaribu na Mungu aliye asili na chemchemi ya utakatifu wote.  Katika Injili (Mt 5:1-12) Yesu ametupatia heri 8 ziwe mwongozo kuifikia mbingu… masikini wa rohoni lakini matajiri katika Mungu, watu wenye huzuni lakini wenye furaha katika Bwana, wapole kama njiwa wenye busara kama nyoka, wenye njaa na kiu ya haki, wenye moyo safi na wapatanishi. Utakatifu unakuja kwa njia ya uadilifu, haki na amani, kusali, sakramenti, kushika amri, kuuishi upendo na kutimiza wajibu za dini na za maisha. ‘...kwamba tuitwe wana wa Mungu’ hao wana wanaheshimiana, wanapendana, wanajengana, wanasaidiana, wanafarijiana. Je, kuna yeyote msiyeheshimiana? Hilo linapunguza uwezekano wa kuwa mtakatifu... kuna mmoja unayechukiana naye? Hili pia linakuweka mbali na utakatifu. kuna mmoja una kinyongo naye, uliyemdhulumu/kumkandamiza? Hili nalo litakuondolea uwezekano wa kuwa mtakatifu.

Waamini wawe ni wajenzi wa Ufalme wa Mungu katika haki, amani na utu
Waamini wawe ni wajenzi wa Ufalme wa Mungu katika haki, amani na utu

Sherehe ya leo iamshe ndani yetu matumaini makubwa ya ushindi hata nyakati tunapojiona hatuwezi kujitoa katika makucha ya Ibilisi. Tusikate tamaa kwani neema ya Mungu ingalipo kutuwezesha. Safari ya kumwendea Mungu daima sio nyepesi, shida zipo lakini zinavumilika.  Ukiona unaonewa sana na watu mtazame Mt. Josefina Bakhita au Mwenyeheri Isidore Bakanja jinsi walivyoonewa, walivyovumilia na kushinda. Ukiona watoto wako wanakusumbua unao mfano wa Mt. Monika alivyosimama imara katika maombi hadi kuongoka kwa mwanaye Mt. Augustino Ukiona ndugu, jamaa na marafiki hawakuelewi usihofu, inua macho mtazame Mt. Francisko wa Assisi. Ukiona unataka kuongoka unababaika unao mfano wa Mt. Augustino Askofu na Mwalimu. Ukitaka kuwa baba mwema wa familia una mfano wa Mt. Yosefu. Kwenu wanafunzi kuhusu elimu na maarifa mnao mfano wa Mt. Thomas wa Aquino. Katika mapambano ya kiroho tunaye Mt. Mikaeli Mkuu wa majeshi. kwa mambo yaliyoshindikana sali kwa Mt. Rita wa Kashia, Mt. Yuda Thadei Mtume, Mt. Filomena, Mt. Padre Pio nk... unaposafiri mlinzi wa safari ni Mt. Kristofa. Udumifu wa imani ikibidi kuteseka kwa ajili hiyo wapo mitume wa Kristo na wanafunzi wao akina Mt. Ignas wa Antiokia, Polycarp wa Smyrna na mashahidi wa imani. Kwa maombezi ya Bikira Maria na ya watakatifu wote tunaweza kuushinda ulimwengu na kujipatia heri ya milele mbinguni. Watakatifu wote ndugu zetu wa mbinguni… mtuombee!

Sherehe Watakatifu Wote
30 October 2024, 10:58