Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu: Mwaliko ni kuishi vema kwa upendo katika jumuiya, kuepuka wivu, kutokuwa na tamaa mbaya, kujibidisha zaidi katika kuwasaidia na kuwahudumia wengine kwa yale tuliyojaliwa na Mungu Tafakari ya Neno la Mungu: Mwaliko ni kuishi vema kwa upendo katika jumuiya, kuepuka wivu, kutokuwa na tamaa mbaya, kujibidisha zaidi katika kuwasaidia na kuwahudumia wengine kwa yale tuliyojaliwa na Mungu  (Vatican Media)

Tafakari Dominika ya 26 ya Mwaka B wa Kanisa: Wivu na Unabii!

Masomo ya dominika ya 26 Mwaka B ni mwendelezo wa fundisho la masomo ya dominika ya 25ya mwaka B kuhusu kuishi vema kwa upendo katika jumuiya, kuepuka wivu, kutokuwa na tamaa mbaya, kujibidisha zaidi katika kuwasaidia na kuwahudumia wengine kwa yale tuliyojaliwa na Mungu, kuishi maisha vyema ahadi zetu za ubatizo kwa ajili ya uzima wa milele mbinguni. Ikitokea tumekosea basi tuombe msamaha. Mungu Baba yetu ni mwenye huruma atatusamehe.

Na Pascha Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 26 ya mwaka B wa Kiliturujia Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii ni mwendelezo wa fundisho la masomo ya dominika ya 25ya mwaka B kuhusu kuishi vema kwa upendo katika jumuiya, kuepuka wivu, kutokuwa na tamaa mbaya, kujibidisha zaidi katika kuwasaidia na kuwahudumia wengine kwa yale tuliyojaliwa na Mungu, kuishi maisha vyema ahadi zetu za ubatizo kwa ajili ya uzima wa milele mbinguni. Ikitokea tumekosea basi tuombe msamaha. Mungu Baba yetu ni mwenye huruma atatusamehe. Ndivyo wimbo wa mwanzo unavyosisitiza kusema; “Ee Bwana, yote uliyotutendea, umeyatenda kwa haki, kwa kuwa sisi tumetenda dhambi, wala hatukuzitii amri zako. Ulitukuze jina lako na kututendea sawasawa na wingi wa huruma zako (Dan. 3:31, 29, 30, 43, 42). Naye Mama Kanisa katika sala ya mwanzo akiitambua huruma ya Mungu anasali hivi; “Ee Mungu, wewe unaonyesha enzi yako kuu hasa kwa kusamehe na kuhurumia. Utumwagilie daima neema yako, tupate kuzishiriki baraka za mbinguni sisi tunaokimbilia ahadi zako.”

Waamini wote wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili
Waamini wote wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili

Somo la kwanza ni la kitabu cha Hesabu (11:25-29). Somo hili linatueleza jinsi Musa na wasaidizi wake walivyowaongoza Waisraeli toka utumwani kwa nguvu ya Roho wa Mungu. Mwanzoni roho wa Mungu ilikuwa juu ya Musa peke yake. Baadae Mungu alitwaa sehemu ya roho iliyokuwa juu Musa na kuiweka juu ya wazee sabini waliokuwa katika hema ya kukutana nao wakapokea kipaji cha unabii, wakaweza kutabiri, lakini mara moja tu. Eldadi na Medadi waliosalia kambini roho ile iliwashukia nao wakatabiri kambini. Musa alipoona hivyo alifurahi. Lakini Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa tangu ujani wake, aliposikia habari za Eldadi na Medadi kutoa unabii, alimwambia Musa; “Ee bwana wangu Musa, uwakataze.” Musa alimjibu; “Je! Umekuwa na wivu kwa ajili yangu; ingekuwa heri kama watu wote wa Bwana wangekuwa manabii, na kama Bwana angewatia roho yake.” Kumbe nasi tusiwaonee wivu wanaojaliwa na kushukiwa na neema na baraka za Mungu. Tukumbuke kuwa hakuna anayestahili kuzipokea neema na baraka zitokazo kwa Mungu. Bali tunazipokea kwa upendo na fadhili za Mungu pasipo mastahili yetu. Neema na baraka za Mungu anazipokea kila anazishika na kuziishi amri na maagizo yake kama mzaburi anavyoziimba katika wimbo wa katikati akisema hivi; “Maagizo ya Bwana ni ya adili, huufurahisha moyo. Sheria ya Bwana ni kamilifu, huiburudisha nafsi. Ushuhuda wa Bwana ni amini, humtia mjinga hekima. Kichwa cha Bwana ni kitakatifu, kinadumu milele. Hukumu za Bwana ni kweli, zina haki kabisa. Tena mtumishi wako huonywa kwazo, katika kuzishika kuna thawabu nyingi. Ni nani awezaye kuyatambua makosa yake? Unitakase na mambo ya siri. Umzuie mtumishi wako asitende mambo ya kiburi, yasinitawale mimi. Ndipo nitakapokuwa kamili, nami nitakuwa safi, bila kosa lililo kubwa” (Zab. 19: 8,7, 9, 11-13).

Epuka wivu, jibidiieshe kuwatumikia watu wa Mungu kwa ari na moyo mkuu
Epuka wivu, jibidiieshe kuwatumikia watu wa Mungu kwa ari na moyo mkuu

Somo la pili ni la Waraka wa Yakobo kwa watu wote (5:1-6). Somo hili linatoa maonyo juu ya utajiri wa dhuluma. Matajiri kwa kuwanyonya watu wengine, wanakosa haki mbele ya Mungu na wataadhibiwa sana. Yakobo anasema hivi; “Haya basi, enyi matajiri! Lieni, mkapige yowe kwa sababu ya mashaka yenu yanayowajia. Mali zenu zimeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo. Dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto. Mmejiwekea akiba katika siku za mwisho. Angalieni, ujira wa wakulima waliovuna mashamba yenu, ninyi mliouzuia kwa hila, unapiga kelele, na vilio vyao waliovuna vimeingia masikioni mwa Bwana wa majeshi. Mmefanya anasa katika dunia, na kujifurahisha kwa tamaa; mmejilisha mioyo yenu kama siku ya machinjo. Mmemhukumu mwenye haki mkamwua; wala hashindani nanyi.” Maonyo haya yanatutahadharisha na mali zitokanazo na dhuluma. Basi tujiepushe nazo, tusije nasi tukalia na kupiga yowe kwa maumivu makali, siku mwenyezi Mungu atakapotuita kutoa hesabu za matendo yetu mbele zake.

Umuhimu wa kuishi vyema kwa upendo na mshikamano
Umuhimu wa kuishi vyema kwa upendo na mshikamano

Injili ni ilivyoandikwa na Marko (9:38-43, 45, 47-48). Sehemu hii ya Injili imebeba mawazo makuu mawili: Wazo la kwanza ni maonyo ya Yesu kwanza kwa Mitume kwa kumkataza mtu aliyetoa pepo kwa jina lake Yesu kwa sababu hakufuatana nao. Ndivyo anavyosema Yohane akisema; “Mwalimu tulimwona mtu akitoa pepo kwa jina lako, ambaye hafuatani nasi; tukamkataza, kwa sababu hafuatani nasi.” Yesu akamjibu: “Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya mwujiza kwa jina langu akaweza mara kuninenea mabaya; kwa sababu asiye kinyume chetu, yu upande wetu.” Pili ni maonyo kwa wanaowapotosha na kuwaingiza wengine katika dhambi. Yesu anasema ni afadhali wafungiwe jiwe la kusagia shingoni na kutupwa baharini. Maana dhambi ya makwazo ni kubwa mno. Sehemu ya pili ni mafundisho ya Yesu kuhusu mawazo maovu yaliyo ndani ya nafsi ya mtu, yanayoweza kusababisha makwazo kwa wengine, sharti yang’olewe. Anasema hivi; “Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili na kwenda zako jehanumu, kwenye moto usiozimika. Na mguu wako ukikukosesha, ukate, ni afadhali kuingia katika uzima, u kiwete, kuliko kutupwa katika jehanumu ukiwa na miguu miwili. Na jicho lako likikukosesha, ling’oe ulitupe, ni afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu, una chongo, kuliko kutupwa katika jehanumu ambamo humo funza wao hawafi, wala moto hauzimiki ukiwa na macho mawili.”

Ondoeni wivu, dhambi na makwazo ili kutangaza vyema Injili ya upendo
Ondoeni wivu, dhambi na makwazo ili kutangaza vyema Injili ya upendo

Makemeo haya ni kuonesha ubaya wa wivu na dhambi za makwazo. Wivu unakwamisha maendeleo, unaleta uhasama na chuki. Maana wivu ni hasira itokanayo kwa kuona wema na maendeleo ya mwingine. Mtu mwenye wivu anakasirika akiona mwingine anaendelea zaidi yake, anaumia akiona wema wa Mungu kwa wengine. Yoshua alikasirika kuona Eldadi na Medadi wakitabiri kama Musa, akaumia moyoni. Yohane alikasirika kuona asiyeambatana na Yesu anaponya na kukemea pepo. Nasi tunaweza kuwa na mawazo kama ya Yoshua na Yohane. Tutambue na kukumbuka daima kuwa; wema wa Mungu hauna mipaka. Tusichukie tukiona wengine wakijaliwa karama ambazo sisi hatuna. Tusichukie tukiona wengine ni wema pengine zaidi yetu. Maana wema wao na mafanikio yao havituzuii sisi kuwa wema na kufanikia. Daima tujiepushe na wivu na tamaa mbaya kwa sababu tabia za namna hizo husababisha vita, chuki na mafarakano katika jumuiya na jamii zetu. Kwa upande mwingine, kwa mliojaliwa neema ya kuwa na mali. Mjihadhari, msiwanyanyase wengine kwa mali mlizo jaliwa na Mungu. Msiwafanyishe wengine kazi bila kuwalipa wanachostahili mkaenda kujistarehesha kwa anasa kwa kutumia jasho lao. Hakika hukumu iko mbele yenu. Tujifunze kuwa watu wa haki. Tuwalipe kwa haki wale wanaofanya kazi yoyote ile kwa niaba yetu. Tukumbuke kuwa yeyote usiyemlipa haki yake, akimlilia Mungu atasikia kilio chake, naye atakulipa sawa sawa na uovu huo. Watoto yatima na wajane, ukiwaibia urithi wao, wakamlilia Mungu, atasikia kilio chao na kukulipa kwa uovu huo. Mnaokula rasilimali za umma kwa ufisadi, watu wakakosa huduma za kijamii, mahakimu na mashahidi, mkitoa ushuhuda wa uongo mahakamani ili kumnyima haki mnyonge, kumbukeni kuwa wakimlilia Mungu, atawasikiliza na kuwalipa kwa uovu huo.

Huduma bora kwa watu wa Mungu ni ushuhuda wa imani tendaji
Huduma bora kwa watu wa Mungu ni ushuhuda wa imani tendaji

Kwa mliofanya hayo nawasihi, ililieni huruma ya Mungu, fanyeni toba ili mpone na hasira na hukumu ya Mungu. Tendeni haki, msiwadharau wengine, iweni wakarimu. Daima tukumbuke kuwa wema tunaoutenda kwa wengine, una thawabu yake. Maneno ya Yesu; “Lolote jema mlilowatendea hawa wadogo, mlinitendea mimi” ni ukweli wa nyakati zote. Yesu anatudai jambo dogo sana; “tuwape watu kikombe cha maji”. Wasaidie chakula walio na njaa, wafariji wanaoteseka. Tumia nafasi uliyonayo katika jamii kuboresha maisha ya watu hutakosa thawabu yako. Tukifanikiwa kuyaisha haya njia ya kwenda mbinguni i wazi. Lakini kwa nguvu zetu hatuwezi lolote. Ndiyo maana Mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anatuombea neema na baraka za Mungu akisali hivi; “Ee Mungu mwenye huruma, ukubali dhabihu yetu hii ikupendeze, nayo itufungulie chemchemi ya baraka zote”. Na katika sala baada ya komunyo anatuombea kwa matumaini haya; “Ee Bwana, fumbo hili la mbinguni lituponye mwili na roho, tupate kurithi utukufu pamoja na Mkombozi, ambaye tunamsikitikia tunapohubiri kufa kwake”. Hili ndilo tumaini letu, uzima wa milele. Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari Dominika 26
01 October 2024, 14:14