Tafuta

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika 27 ya Mwaka B wa Kanisa: Ndoa na maisha ya familia mintarafu mpango wa Mungu. Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika 27 ya Mwaka B wa Kanisa: Ndoa na maisha ya familia mintarafu mpango wa Mungu.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika 27 ya Mwaka B wa Kanisa: Ndoa na Familia Katika Mpango wa Mungu

Masomo ya dominika ya 27 ya Mwaka B wa Kanisa ni Katekesi inayohusu asili yetu sisi wanadamu, asili ya maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu. Ndivyo unavyoashiria wimbo wa mwanzo ukisema; “Ee Bwana, ulimwengu wote u katika uwezo wako, wala hakuna awezaye kukupinga ukipenda. Wewe umeumba yote, mbingu na nchi, na vitu vyote vya ajabu vilivyomo chini ya mbingu; ndiwe Bwana wa yote” (Est. 13:9, 10-11). Umuhimu wa Ndoa na Familia!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 27 ya mwaka B wa Kiliturujia Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii ni Katekesi inayohusu asili yetu sisi wanadamu, asili ya maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu. Ndivyo unavyoashiria wimbo wa mwanzo ukisema; “Ee Bwana, ulimwengu wote u katika uwezo wako, wala hakuna awezaye kukupinga ukipenda. Wewe umeumba yote, mbingu na nchi, na vitu vyote vya ajabu vilivyomo chini ya mbingu; ndiwe Bwana wa yote” (Est. 13:9, 10-11). Huu ndio wema wa Mungu kwetu sisi wanadamu ambao mama Kanisa anaukiri katika sala ya mwanzo akisali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, unatujalia kwa wema wako mkuu mema mengi kupita yale tunayoomba na kutamani. Utushushie huruma yako, utusamehe makosa yanayotuletea hofu moyoni, utuongezee na hayo tusiyothubutu kuomba.” Somo la kwanza ni la kitabu cha Mwanzo (2:18-24). Somo hili ni simulizi la kuumbwa kwa mwanadamu kulivyo tofauti na uumbaji wa viumbe vingine. Katika simulizi hili tunaona kuwa mwanamke ana hadhi na utu sawa na mwanaume, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kadiri ya mpango wa Mungu Mwanamke ni msaidizi wa mwanaume, sio mtumwa kwake. Maana Mungu alisema hivi; “Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanya msaidizi wa kufanana naye.” Maana ni katika ubavu wa mwanamume akiwa usingizini, mwanamke amepatika. Tunasoma hivi; “Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha, akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, na ule ubavu alioutwaa katika Adamu, Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu.”

Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea familia.
Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea familia.

Naye Adamu alipomwona alisema; “Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume. Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.” Hapa tunaona asili ya ndoa kuwa ni ya mume mmoja na mke mmoja kadiri ya mpango wa Mungu. Kinyume na hapo, tofauti zingine zinazojitokeza katika maisha ya ndoa ni ya ibilisi na lengo ni kupinga mpango wa Mungu, na matokeo yake yako wazi kuteseka kwa mwanadamu kwa kuishi na kufanya yaliyo kinyume na mpango wa Mungu. Lakini kwa wanaishi kadiri ya mpango wa Mungu, watafurahi milele. Ndivyo unavyosisitiza wimbo wa katikati ukisema; “Bwana atubariki siku zote za maisha yetu. Heri kila mtu amchaye Bwana, aendaye katika njia yake. Taabu ya mikono yako hakika utaila, utakuwa mwenye heri na baraka tele. Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao, vyumbani mwa nyumba yako; wanao kama miche ya mizeituni, wakizunguka meza yako. Hakika, atabarikiwa hivyo, yule amchaye Bwana. Bwana akubariki toka Sayuni, uone uheri ya Yerusalemu siku zote za maisha yako; naam, ukawaone wana wa wanao. Amani ikae na Israeli” (Zab. 128).

Familia ni msingi bora wa malezi na makuzi ya Kikristo
Familia ni msingi bora wa malezi na makuzi ya Kikristo

Somo la pili ni la Waraka kwa Waebrania (2:9-11). Somo hili linatufundisha kuwa Yesu Kristo nafsi ya pili ya Mungu alipochukua umbo la mwanadmu katika fumbo la umwilisho na kuwa Mungu-Mtu, alizaliwa, akakua na kuishi katika familia ya kawaida kabisa. Katika utu wake, alionekana kuwa mdogo kuliko malaika, akaonja mateso na kifo kwa kumtii Mungu Baba yake. Tunasoma hivi; “Ndugu, twamwona yeye aliyefanywa mdogo punde kuliko malaika, yaani, Yesu, kwa sababu ya maumivu ya mauti, amevikwa taji ya utukufu na heshima, ili kwa neema ya Mungu aionje mauti kwa ajili ya kila mtu.” Kwa sababu hiyo alipata utukufu na heshima za pekee hivi hata wanadamu wanaweza kukombolewa kwa njia yake; “Kwa ajili yake na kwa njia yake vitu vyote vimekuwapo, akileta wana wengi waufikilie utukufu, kumkamilisha kiongozi mkuu wa wokovu wao kwa njia ya mateso. Maana yeye atakasaye na hao wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii haoni haya kuwaita ndugu zake.” Hapa tunaona dhamani na umuhimu wa familia katika maisha ya mwanadamu hata Mungu alipokuja kutukomboa kutoka utumwa wa dhambi na mauti, alikuja kwa kupitia katika familia ili kutuonyesha umuhimu na dhamani ya ndoa na maisha ya familia.

Watoto ni baraka kwa familia
Watoto ni baraka kwa familia

Injili ni ilivyoandikwa na Marko (10:2-16). Sehemu hii ya Injili imegawanyika katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza inatufundisha kuwa katika ndoa ya kweli mume na mke ni mwili mmoja. Hivi hawawezi kutengana. Hili ni fundisho la Yesu mwenyewe akijibu swali hili la mafarisayo; “Je, ni halali kwa mwanamume kumwacha mkewe?”. Katika kutoa jibu, Yesu alirejea sheria ambazo Musa aliwapa akiwauliza; “Je, Musa aliwaauru nini?” Nao walijibu kuwa; “Musa alitoa ruhusa kuandika hati ya talaka na kumwacha”. Yesu anatoa sababu ya Musa kutoa ruhusa hiyo kuwa ni “ugumu wa mioyo yao”. “Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, Mungu aliwafanya mume na mke. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja, hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.” Wanafunzi wake nao hawakuelewa fundisho hilo, ndio maana wakiwa nyumbani wanamuuliza habari ya neno hilo. Yesu anawaambia kuwa; “Kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine azini juu yake; na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine azini.” Sehemu ya pili ya Injili hii inatueleza kuwa tukitaka kuingia katika ufalme wa Mungu lazima tuwe watulivu, waongofu na wanyenyekevu. Yesu anatoa fundisho hili baada ya wanafunzi wake kuwakataza watoto wadogo walioletwa kwake ili awaguse. Kitendo cha wanafunzi kuwakemea waliowaleta watoto kwake kilimfanya achukizwe sana na kuwaambia; “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambieni, Yeyote asiyekubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa. Akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabarikia.”

Watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu walindwe na kuendelezwa
Watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu walindwe na kuendelezwa

Kumbe tunaona wazi kuwa ndoa ya mume mmoja na mke mmoja na mwanadamu kuishi katika familia ni mpango wa Mungu. Lakini hali ya maisha ya ndoa na familia nyakati zetu imegubikwa na changamoto nyingi. Wapo waliofunga ndoa na wanaishi vizuri. Tuwapongeze na kumshukuru Mungu. Ni ukweli kuwa mafanikio yao si kwamba hawana matatizo bali wanayavumilia kwa moyo wa sadaka na imani. Wapo waliofunga ndoa lakini ndoa zao zimegubikwa na matatizo mbalimbali na wengine wameachana. Tuwaombee. Wapo wale wanaoishi pamoja bila kufunga ndoa. Lakini pia wapo wanaoishi peke yao hawajaolewa wala kuoa, labda kwa kupenda au kutokupenda. Hili nalo ni tatizo na changamoto katika jamii zetu. Tufanye nini basi katika hali hii. Tukubali kuwa ndoa na familia ni tunu kwa maisha ya mtu. Ndiyo maana Mungu anasema; “Si vema huyu mtu awe peke yake.” Kwa vijana; tuwasihi, tuwashauri, tuwafundishe na kuwaelimisha wajue uzuri na furaha ya ndoa na familia na ubaya wa kuishi kiholela. Ni wajibu wa wazazi kuwasaidia kujiandaa vyema kuingia katika maisha ya ndoa na familia. Wazazi muwajibike kuwafundisha watoto madhara ya ngono kabla ya ndoa. Tabia hii sio tu ni dhambi bali pia inaleta ubaridi katika ndoa pindi mtu anapoolewa au kuoa maana hana chochote kipya anachotarajia katika ndoa. Zaidi sana anayefanya ngono kabla ya ndoa hana zawadi yoyote ya dhamani anayoitunza kwa ajili ya mwenzake wa ndoa na hivyo hana cha kujivumia kwa mume au mke wake maana atamwona yuko sawa tu na wengine aliowahi kuwa nao.

Maisha ya ndoa na familia yana mazuri na changamoto zake.
Maisha ya ndoa na familia yana mazuri na changamoto zake.

Wazazi wafundisheni na dumisheni usawa, haki, heshima na ushirikiano kwa watoto. Pasiwepo Bwana na mtumwa katika maisha ya ndoa. Lakini pia mnapopigania usawa na haki mkumbuke kuwa “mke asiache kuwa mke na mme asiache kuwa mme” na kila mtu atimeze wajibu wake katika familia. Hili linapaswa kuambatana na sala na uaminifu. Kukosa uaminifu katika ndoa ni chanzo cha matatizo ambako kunaendana na uongo katika maisha. Moyo wa sadaka unahitajika katika maisha ya ndoa na familia. Hii inaambatana na kuamua kuachana na wengine. Wazazi mjifunze na muwafundishe watoto webu “kuacha”, na kusema “inatosha.” Hapo atakuwa na ujasiri wa kumwacha baba na mama na kuambatana na mwenzake. Tujifunze kutoka kwa Tobia ambaye ni mfano wa upendo wa dhati na wa kweli katika ndoa. Kabla ya kuoa Tobia alisali akisema: “Utukuzwe ee Mungu wa wazee wetu…ndiwe uliyesema: Si vizuri mwanamume kuwa peke yake; tumuumbe mtu wa kumsaidia aliye kama yeye. Kwa hiyo namchukua dada yangu Sara, si kwa sababu ya tamaa ya mwili, ila nafanya hivyo kwa dhamiri safi” (Tobiti 8: 5-7). Tobia alimchukua Sara kuwa mke wake si tamaa ya mwili bali kwa upendo wa dhati. Ni kwa neema na baraka za Mungu wana ndoa wanaweza kuishi pamoja kwa umoja na upendo wakizifuata amri na maagizo ya Mungu. Ndiyo maana mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, tunaomba uzipokee sadaka zilizowekwa kwa amri yako. Upende kutujaza neema za ukombozi wako kwa mafumbo haya matakatifu tunayoadhimisha kwa mujibu wa utumishi wetu”. Na chemichemi ya neema na baraka zote ni Ekaristi Takatifu, mkate wa uzima wa milele. Ndivyo inavyosisitiza antifona ya komunyo ikisema; “Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja: kwa maana sisi sote twashiriki mkate mmoja na kikombe kimoja” (1Kor. 10:17). Na sala baada ya komunyo inahitimisha ikisema; “Ee Mungu Mwenyezi, utujalie sakramenti hizi tulizopokea zizidi kutuburudisha na kutusitawisha tupate kuwa na uzima wake yeye tuliyempokea.” Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari Dominika 27
01 October 2024, 14:51