Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 28 ya Mwaka B wa Kanisa: Hekima ya Mungu na matumizi ya malimwengu. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 28 ya Mwaka B wa Kanisa: Hekima ya Mungu na matumizi ya malimwengu.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika 28 Mwaka B wa Kanisa: Hekima na Malimwengu

Masomo ya dominika hii yanatukumbusha kuwa kupenda mno na kujihusisha kupita kiasi na mali ya dunia hii, ni pingamizi la kufika kwenye uzima wa milele. Hii ni kwa sababu mtu aliyejishikamanisha sana na mali anajaa kiburi na kuona kuwa hana haja na huruma ya Mungu kwa makosa yake, huruma anayoiimba Mzaburi katika wimbo akisema; “Bwana, kama wewe ungehesabu maovu, ee Bwana, nani angesimama? Lakini kwako kuna msamaha, ee Mungu wa Israeli”

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 28 ya Mwaka B wa Kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatukumbusha kuwa kupenda mno na kujihusisha kupita kiasi na mali ya dunia hii, ni pingamizi la kufika mbinguni kwenye uzima wa milele. Hii ni kwa sababu mtu aliyejishikamanisha sana na mali anajaa kiburi na kuona kuwa hana haja na huruma ya Mungu kwa makosa yake, huruma anayoiimba mzaburi katika wimbo akisema; “Bwana, kama wewe ungehesabu maovu, ee Bwana, nani angesimama? Lakini kwako kuna msamaha, ee Mungu wa Israeli” (Zab. 130:3-4). Tunahimizwa kuzitumia vyema mali za ulimwengu huu kadiri ya mpango wa Mungu ili mwisho wa yote tukaurithi uzima wa milele. Lakini kwa nguvu zetu hatuwezi lolote ndiyo maana mama kanisa katika sala ya mwanzo anatuombea neema na baraka za Mungu zitusaidie akisali hivi: “Ee Bwana, tunakuomba neema yako ituongoze daima na kutusindikiza, itutie siku zote moyo wa bidii wa kutenda mema.”

Hekima ya Roho Mtakatifu Ituongoze katika maisha
Hekima ya Roho Mtakatifu Ituongoze katika maisha

Somo la kwanza ni la Kitabu cha Hekima ya Sulemani (7:7-11). Katika somo hivi Sulemani anatufundisha kuwa “hekima” ni bora zaidi kuliko kitu chochote duniani. Thamani yake inashinda vyeo vyote, utajiri wote na uzuri wote. “Hekima” hii ndiyo inayomuwezesha mwanadamu kumjua Mungu na kutimiza mapenzi yake. Ndiyo maana Sulemani anasema; “Naliomba, nikapewa ufahamu; nalimwita Mungu, nikajiliwa na roho ya Hekima. Naliichagua kuliko fimbo za enzi na viti vya enzi, wala mali sikudhani kuwa ni kitu ikilinganishwa nayo; wala sikuifananisha na kitu cha thamani; mradi dhahabu yote ya nchi ni kama mchanga kidogo mbele yake, na fedha itahesabiwa kama udongo. Naliipenda kupita afya njema na uzuri wa sura, hata zaidi ya nuru nikataka kuwa nayo, kwa maana mwangaza wake haufifii kamwe. Na pamoja nayo nikajiliwa mema yote ya jamii, na mikononi mwake mali isiyoweza kuhesabika.” Kumbe hekima ndiyo inayotusaidia tumjue, tumpende na tumtumikie Mungu na kwa namna hiyo tunapata neema na baraka zake zinazotuwezesha kuvipata na kuvitumia vitu alivyoviumba yeye kwa ajili ya sifa na utukufu wake ili kwavyo tuweze kutakatifuzwa na kustahilisha kuurithi uzima wa milele. Katika wimbo wa katikati Mzaburi naye anatoa wasifu na umuhimu wa Hekima ya kimungu akisema; “Utujulishe kuzihesabu siku zetu, tujipatie moyo wa hekima. Ee, Bwana, urudi, hata lini? Uwahurumie watumishi wako. Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako, nasi, tutashangilia na kufurahi siku zetu zote. Utufurahishe kwa kadiri ya siku ulizotutesa, kama miaka ile tuliyoona mabaya. Matendo yako na yaonekane kwa watumishi wako, na adhama yako kwa watoto wao. Na uzuri wa Bwana Mungu wetu, uwe juu yetu. Naam, kazi ya mikono yetu uithibitishe” (Zab. 90: 12-17).

Hekima ya Kimungu ituongoze kutenda mema
Hekima ya Kimungu ituongoze kutenda mema

Somo la pili ni la Waraka kwa Waebrania (4:12-13). Somo hili linatufundisha kuwa Neno la Mungu ni ufunuo wa Mungu mwenyewe uliotufikia kwa njia ya Manabii wake na kwa namna ya pekee kwa njia ya Mwanae wa pekee, Bwana wetu Yesu Kristo. Neno hili lina nguvu ya wokovu, ni neno lenye uhai. Neno hili lina ukali wa kuangamiza kila aina ya ubaya na kutupatia uzima kwa kutujalia uwezo wa kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. Hivyo Neno la Mungu ni la thamani sana katika maisha yetu. Tujitahidi basi kulisoma, kulitafakari na kuliishi kwani ndilo chakula cha roho zetu, kwa ajili ya uzima wa milele. Injili ni ilivyoandikwa na Marko (10:17-30). Katika sehemu hii ya Injili, Yesu anatuelekeza namna ya kuutumia utajiri wa dunia hii kwa ajili ya uzima wa milele. Ifahamike kuwa fundisho la msingi hapa sio katazo la kuwa na mali. Bali ni kutoa angalizo kwa wale wanaoweka tumaini lao lote katika mali na kumuweka Mungu pembeni. Yeyote anayefanya hivyo anajifungia mlango wa kuingi katika ufalme wa Mungu. Yesu anatoa tahadhari hii baada ya mtu mmoja kumwuliza; “Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele?” Katika kujibu swali hili, Yesu kwanza kabisa anaweka wazi hali ya binadamu kuwa sio ya ukamilifu akisema; “Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu.” Kisha akatoa maelekezo ya namna ya kuurithi uzima wa milele. Hatua ya kwanza ni kuzijua, kuzishika na kuziishi amri za Mungu. Hatua ya pili ni kuwatumikia wengine hasa walio na uhitaji zaidi: wagonjwa, maskini, wenye njaa na kiu kwa kutumia mali tulizojaliwa zaidi yao. Ndiyo maana Yesu alimwambia muuliza swali kuwa; “Enenda, ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.”

Mali ya dunia itumike hekima ili kujenfa majadiliano katika ukweli na uwazi
Mali ya dunia itumike hekima ili kujenfa majadiliano katika ukweli na uwazi

Mwinjili Marko anasema; “Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.” Kumbe kujilimbikizia mali nyingi kupita unachohitaji sio tu kunakuletea mkunjo wa uso na kuenenda kwa huzuni. Bali pia kunakufanya uingie kwa shida na taabu katika ufalme wa Mungu na wakati mwingine kuukosa kabisa! Hii ni kwa sababu mali inaweza kumfanya mtu aitegemee na kuiona ndiyo impayo uzima na kumsahau Mungu, Baba wa uzima. Kumbe basi kilema cha kukumbatia mali za dunia hii ni kushindwa kuukumbatia ufalme wa Mungu. Kujilimbikizia mali zaidi ya unachohitaji ni kuwa na uchoyo wa hali ya juu sana. Mtu mchoyo anatumia karama zake zote, nguvu zake zote na uwezo wake wote ili kuufurahisha mwili wake na kuiacha roho itiayo uzima ikiangamia. Hali hii yaweza kumpata pia maskini kwa kuwa na tamaa ya mali, kiasi cha Mungu anakuwa hana nafasi kwake. Kumbe maskini na tajiri wote wanapaswa kupambana na kilema hiki. Kwanza kabisa kwa sala kwani bila sala hatuwezi kupiga hatua yoyote katika maisha ya kumpenda na kumtumikia Mungu na jirani. Pili tukumbuke kuwa chochote tunachokihangaikia hapa duniani hakidumu na wengine watavifurahia na pengine kuvifuja. Ndiyo maana Mtume Paulo anasema hivi: “Maana hatukuleta kitu chohocte hapa duniani, wala hatutachukua chochote.” Kumbe Mungu akikujalia mali, maana yake amekuweka uwe mgawaji kwa wengine na sio kuendelea kuzirundika halafu mwisho unakufa na kuziacha. Kumbuka hizo ndizo ushahidi wako siku ya hukumu ya mwisho.

Upendo na ukarimu huvuta neema ya Mungu
Upendo na ukarimu huvuta neema ya Mungu

Hivyo basi, mali tulizojaliwa na Mungu, tuzitumie kwa ukarimu kama anavyotuasa Mtume Paulo akisema: “Furahini na wenye kufurahi, na lieni na wenye kulia” (Rum 12:15). Ukarimu ni fadhila inayofukuza ndani ya roho ya mwanadamu ubinafsi. Ukarimu unahimiza kuwapenda wenzetu kwa kufanya matedo ya huruma ya kimwili na kiroho. Daima tukumbuke kuwa kadiri unavyoweka matumaini katika hazina za dunia, ndivyo matumaini kwa Mungu yanavyopungua. Na kadiri tunavyowahudumia wengine kwa upendo, ndivyo tunavyozidi kupata neema na baraka za Mungu. Basi, ewe uliyejaliwa zaidi, toa zaidi kwa moyo wa upendo ili maskini waweze kupata mahitaji yao msingi naye mwenyezi Mungu atakubariki zaidi. Mtakatifu Francisko wa Assisi anasema “Ni katika kutoa ndipo tunapokea. Ni katika kusamehe ndipo tunasamehewa. Ni katika kufa tunazaliwa katika uzima wa milele”. Ndicho alichofanya mjane wa Seprepta kwa kumhudumia Nabii Eliya, pipa lake la unga na chupa ya mafuta havikupungua (1Fal. 17:1–16). Nasi tukitoa kwa moyo wa upendo, hatutapungukiwa na kitu maana Mungu anapokujaza zaidi ya kile ulichotoa na uzima wa milele juu yake. Ndivyo inavyosisitiza sala ya kuombea dhabihu ikisema; “Ee Bwana, pokea sala za waamini pamoja na dhabihu tunayokutolea, ili kwa ibada hii takatifu tupate kuufikia utukufu wa mbinguni.” Naye “Bwana atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo” (1Yoh. 3:2). Ni katika tumaini hili mama Kanisa anapohitimisha maadhimisho ya dominika hii anatuombea kwa sala baada ya kumunio akisali hivi; “Ee Bwana mtukufu, sisi unaotulisha Sakramenti ya Mwili na Damu Azizi tunakusihi utushirikishe pia umungu wako.” Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari D 28
08 October 2024, 14:48