Uchu wa mali na madaraka visiwe ni kikwazo cha kumfuasa Kristo Yesu ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia Uchu wa mali na madaraka visiwe ni kikwazo cha kumfuasa Kristo Yesu ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Tafakari Dominika 28 ya Mwaka B wa Kanisa: Mali Kisiwe ni Kikwazo Cha Ufuasi

Uhuru wa ndani unamtaka mwamini ajinasue kutoka katika mambo na tabia ambazo zinakwenda kinyume na nidhamu ya maisha ya kiroho. Ni changamoto ya kuwa ni mtu wa kiasi, mwenye matumizi sahihi ya fedha na mali na kwa namna ya pekee, kuwa na maadili kuhusu matumizi ya fedha. Kumbe, uchu wa mali na madaraka visiwe ni vikwazo vya kumfuasa Yesu ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Mali isaidie kukoleza huduma ya uinjilishaji wa kina!

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Mpendwa msikilizaji na msomaji ni wazo hofu ya kesho daima haiachi kumtesa mwanadamu hasa anapoona viashiraia vya kutopata matarajio yake kwa kitu anachokifanya kwa wakati huo daima huwa katika majadiliano ya nafsi na hatimaye hutoka nje na kuanza kujadiliana na wanaomzunguka ikiwa ni ishara ya kuomba ushauri au msaada ili kujihakikishia kesho yake. Njiani Kristo anaulizwa “Mwalimu mwema, nifanye nini niupate uzima wa milele?” nia ya muulizaji ilikuwa vile alikuwa mcha Mungu akitafuta ukamilifu. “Unazijua amri?” lilikuwa swali la Kristo, akasema “Amri zote nimezishika tangu utoto” Mwinjili Marko anasema Yesu alimkazia macho akampenda. Mali inayopatikana kihalali ni haki ya mtu, inayomwezesha kupata mahitaji yake msingi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, fedha ni kipimo cha amana, inaeleza thamani ya bidhaa au huduma inayotolewa kwa jamii. Inaonesha uwezo wa kununua bidhaa au huduma alio nayo mtu; inatunza na kuonesha uwezo wa kununulia bidhaa na huduma kwa siku za usoni. Kila mtu anahitaji fedha, lakini Mwenyezi Mungu anawaalika waja wake kutoa kipaumbele cha kwanza kwake. Uhuru wa ndani unamtaka mwamini ajinasue kutoka katika mambo na tabia ambazo zinakwenda kinyume na nidhamu ya maisha ya kiroho. Ni changamoto ya kuwa ni mtu wa kiasi, mwenye matumizi sahihi ya fedha na mali na kwa namna ya pekee, kuwa na maadili kuhusu matumizi ya faida ya fedha. Myumbo wa uchumi kitaifa na Kimataifa na madhara yake ni matokeo ya kukosa nidhamu katika matumizi ya sera za fedha duniani. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, fedha ni thamani inayowekwa katika kitu chochote ambacho unahitaji, fedha badala ya kutumika kama chombo, inaweza kukugeuza na kuwa ni mtumwa. Yule kijana alikuwa ni tajiri, lakini utajiri wake, ukawa ni kikwazo cha kumfuasa Kristo Yesu ili hatimaye kupata uzima wa milele!

Uchu wa mali na madaraka visiwe vikwazo vya kumafuasa Kristo Yesu
Uchu wa mali na madaraka visiwe vikwazo vya kumafuasa Kristo Yesu

UFAFANUZI: Kwa nini alimpenda? Kwanza ni kwa sababu kijana huyu alikuwa jasiri wa kumkaribia Kristo ili kujiuliza, hakwenda kwa mwingine... Huwa nafurahi vijana wanaponiuliza ‘Padre nataka kuwa kama wewe, nifanyeje?’ Nawe ufurahi na uwapende wanaojiuliza jambo kwako, kwamba mimi nataka nikikua niwe kama huyu mama, au kama huyu baba.  Ukiona watu hawajiulizi kwako, huwavutii hata wadogo zako tu, ‘you are not an inspiration to anyone’ kidogo unakuwa unakwama. Pengine wanakujia kujiuliza nawe kwa vile umeishakata tamaa na kila kitu ni kigumu kwako basi unawapa ushauri wa kuwavunja moyo, ‘hilo jambo gumu sana huliwezi, kwenye ukoo wenu hakuna mwenye hicho kipaji’ nk. Huenda hatuna jambo la kuwashauri wenzetu lakini ndio ushindwe hata kumwambia tu ‘katika maisha yako muogope Mungu na uwajali na kuwapenda watu wote? Wakati mwingine tunawajibu wenzetu vizuri, ila tunakosa vifua vya kuwasitiri na kuwaambia wengine, tunatoa siri zao, wanasononeka na hawatarudi tena kwetu. Yesu anampenda huyu kwa uthubutu wake. Pili, anampenda kwa sababu amejitahidi kushika amri za Mungu tofauti na akina siye, unakuta ndani ya saa 6 tu tumeishakurupusha amri kama tano hivi za Mungu… kijana huyu anakaziwa macho na Kristo na anapendwa. Hii ilikuwa bahati tunayotamani wote, kukaziwa macho na Kristo, macho yale ya kibuluu, mapole yenye wema na upendo tungejisikia raha nafsini mwetu, changamoto zingejibiwa, tungejipatia wepesi wa nafsi na amani ya moyo. Akamwambia ‘Umefanya vema, upo vizuri dogo, unatishaje! Sasa kamilisha neno moja tu, unanisikia! moja tu, kauze ulivyo navyo uwape masikini utakuwa na hazina mbinguni kisha unifuate…’ oh! Neno hili lilikuwa mkuki moyoni mwa kijana yule tajiri… akamtazama Yesu kwa uchungu, akatikisa kichwa na huku akiinamia chini akaondoka kwa huzuni kuu.

Vijana tumieni mali na utajiri wenu kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu
Vijana tumieni mali na utajiri wenu kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu

Neno hili lilimuhuzunisha pia Kristo, akaanza kufundisha hatari za kuzingatia mambo ya dunia yenye kutupatia mashaka katika maisha yetu ya kiroho. Kwamba sio rahisi tajiri kuingia mbinguni, hamaanishi tupende ufukara usio na maana, tusifanye kazi na kuboresha hali zetu. Kristo hamaanishi tushabikie uvivu na umasikini sababu tu ni rahisi ngamia kupenya tundu la sindano kuliko tajiri kuingia mbinguni… uvivu ni kilema, mojawapo ya mizizi 7 ya dhambi. Wavivu ni kama tushetani tusaidizi, “sio utu” (aliwahi sema Baba wa taifa la Tanzania hayati Mwalimu J.K. Nyerere). Inaumiza vijana wenye nguvu kushinda bila kufanya chochote leo kuan msamiatai vijana wanaitana kuwa machawa katika dhana ya kuwasifia watu badala ya kyafanya kazi hii ni hatari sana nao akina dada utakuta katika mambo ya urembo na kujipamba Kusukana siku nzima huku wakiwazungumza watu, Hapa ni kumkaribisha shetani anayetafuta sana pa kukaaa kwani “mwili mlegevu ni karakana ya ibilisi” Kazi ni agizo la Mungu kwa Adam, kuilima na kuitunza nchi (Mwz 2:15). Tufanye kazi tuboreshe maisha. Kristo anatukumbusha iwapo tutaweka nafsi zetu nzima, mioyo, roho na akili zetu katika mali, fedha na vitu tutaikosa mbingu. Lakini utajiri wa hatari sio tu wa mali. tupo matajiri wenye store kubwa za tabia mbaya, matajiri wa maneno yasiyo na stara, matajiri wa visa na mikasa, hila, chuki na visasi, matajiri wa roho za kwa nini… sisi pia itakuwa ngumu kuuingia mbinguni. Baada ya fundisho hilo Petro akaguswa sana, ni kama aliona Yesu analalamika mno au analaumu mno au labda anasisitiza mno, akamwambia “Mwalimu hayo sisi hayatuhusu Bwana, tazama sisi tumeacha vyote tukakufuata wewe…” Yesu anampa moyo na kwa upole anamwambia “aliyeacha yote kwa ajili yangu atapokea mara mia sasa, na katika ulimwengu ujao uzima wa milele.”

Vijana amueni kutumia mali na utajiri  wenu kama ushuhuda wa maisha adili
Vijana amueni kutumia mali na utajiri wenu kama ushuhuda wa maisha adili

Mkristo jiamini, jipige kifua useme na Petro “Tazama mimi nimeacha vyote nimekufuata Kristo”. Kwa ubatizo tumemkataa shetani, mambo na fahari zake tukaahidi kumsadiki Mungu, tumeacha yote ili kumfuata Kristo, naye amesema tutapokea hayo tuliyoacha na mengine mengi mara mia. Ndugu unadhani umeacha nini kwa ajili ya Kristo? kipi kinakukwamisha? kauze ulivyo navyo, wape masikini uwe mwepesi, kisha mfuate Kristo. Pamoja na kuacha yote, tunapaswa kujitambua na kuiishi hekima ya kimungu kadiri ya somo I (Hek 7:7-11). Suleiman anafundisha kwamba hekima ndio kila kitu, ni nzuri kuliko mali, ya thamani kuliko dhahabu, nuru yake haififii, tuipende kupita afya njema na uzuri wa sura. Hekima hiyo kadiri ya somo II (Ebr 4:12-13) ipo katika maandiko yenye pumzi ya Mungu, “Maandiko Matakatifu yameandikwa kwa uongozi wa Mungu (kwa ajili ya wenye mapenzi mema na dhamiri safi) yanafaa kufundisha ukweli, kuonya, kusahihisha makosa, kuwaongoza watu waishi maisha ya adili, ili anayemtumikia Mungu awe mkamilifu na tayari kufanya kila tendo jema” (2Tim 3:16-17), tujibidishe kulisoma, kulitafakari na kuliishi Neno la Mungu. ‘Tazama, sisi tumeacha yote tukakufuata wewe...’ tuache mila na desturi zisizofaa, imani potofu, ushirikina, uganga na uganguzi, kuagua/ramli/bao/chale/ na hirizi, tumfuate Kristo… tuyaache yanayotugawa tushike yanayotuunganisha. Hekima ya Mungu inadai umoja na mshikamano. Jumuiya Ndogondogo za Kikristo pawe mahali pa msaada tunaposali, kutafakari na maendeleo, zisaidie kuwarudisha kwa Kristo walioondoka kwa huzuni kama kijana wa Injili. Ziwahamasishe warudi, waishi sakramenti na sala, waepuke ukristo wa kitandani... hili ni muhimu sababu huwezi kujua kama neema ya dakika ya mwisho itakuangukia. Watamtafuta Paroko akuhudumie watamkosa, atakuwa kwenye semina. Paroko Msaidizi, katika saa yako ngumu ya mwisho, atakuwa mjini kwenye shughuli zake, nawe utamaliza maisha yako bila upatanisho… dini ni leo, amua sasa, mgeukie Mungu, hapa na wakati huu! Tunapoendelea na ratiba zetu tumuombe Mungu Baba yetu, kwa maombezi ya Mama Maria na ya watakatifu wote atusaidie tuache yote na kumfuata Kristo na hivi kupokea thawabu yetu mara mia, tunie kuambiwa neno lile zuri ‘vema mtumwa mwema, ingia katika furaha ya Bwana wako’, kwa sifa na utukufu wa Mungu.

Liturujia D 28 Mwaka B
11 October 2024, 16:31