Maadhimisho ya Siku ya 98 ya Kimisionari Ulimwenguni Dominika tarehe 20 Oktoba 2024 unanogeshwa na kauli mbiu “Enendeni na alikeni kila mtu kwenye Karamu” (Rej. Mt. 22:9) Maadhimisho ya Siku ya 98 ya Kimisionari Ulimwenguni Dominika tarehe 20 Oktoba 2024 unanogeshwa na kauli mbiu “Enendeni na alikeni kila mtu kwenye Karamu” (Rej. Mt. 22:9)   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Tafakari Dominika ya 29 ya Mwaka B wa Kanisa: Unyenyekevu!

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 98 ya Kimisionari Ulimwenguni Dominika tarehe 20 Oktoba 2024 unanogeshwa na kauli mbiu “Enendeni na alikeni kila mtu kwenye Karamu” (Rej. Mt. 22:9) Baba Mtakatifu anakazia: Umuhimu wa kutoka na kualika na kwamba, kila Mkristo anawajibika. Kwenda arusini ni mwelekeo wa kieskatolijia na kiekaristi wa utume wa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Karibu msikilizaji na msomaji wetu katika tafakari ya Dominika ya 29 ya mwaka B wa Kanisa. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 98 ya Kimisionari Ulimwenguni Dominika tarehe 20 Oktoba 2024 unanogeshwa na kauli mbiu “Enendeni na alikeni kila mtu kwenye Karamu” (Rej. Mt. 22:9) Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anakazia: Umuhimu wa kutoka na kualika na kwamba, kila Mkristo anawajibika. Kwenda arusini ni mwelekeo wa kieskatolijia na kiekaristi wa utume wa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kila mtu anaitwa kushiriki katika utume wa Kiulimwengu wa wafuasi wa Kristo Yesu katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari katika utimilifu wake na uwajibikaji wake wote katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kama wafuasi wamisionari wa Kristo Yesu wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia sanjari na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi kama inavyobainishwa kwenye kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Tukiwa tumetembea tayari kilometa za kutosha, leo tunapata nafasi ya kutafakari fadhila msingi na mama wa fadhila zote yaani unyenyekevu, Mwanadamu anatamani furaha hivi huitafuta kwa nguvu wakati mwingine kwa njia zisizo sahihi. Unyenyekevu ni hali ya moyo na akili inayomfanya mtu ajikubali alivyo na awakubali wengine walivyo. Kwa njia ya unyenyekevu mtu anatambua analopaswa kutenda na analitenda na pia asilopaswa kulitenda na halitendi. Kwa njia ya unyenyekevu, mtu anawapa wengine nafasi ya kuwa wanavyotakiwa kuwa katika haki. Kwa njia ya unyenyekevu, tunakomesha vilema vyetu vyote vya majivuno, kiburi, maringo, kujionaona na kujikweza. Fadhila ya unyenyekevu inachukuliwa kuwa ya msingi na kiongozi wa fadhila nyingine zote. Mtakatifu Augustino anaendelea kusema kuwa “Kimsingi ni katika unyenyekevu mtu anafanywa kuwa mfuasi wa Kristo, na kwa hilo roho inaandaliwa kuungana na Mungu.” Mambo yote ni lazima yapate msingi wake katika unyenyekevu.

Waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu
Waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu

Unyenyekevu unachukua nafasi ya kwanza kwa vile, unafukuza majivuno. Fadhila ya unyenyekevu inatudai kujishusha ili tuinuliwe. Inatufanya tujione si kitu ili tuonekane kuwa ni kitu. Inatufanya tuwajali zaidi watu kuliko kujijali na kujipendelea sisi wenyewe. Inatufanya tuoneshe upendo wetu zaidi kuliko kutaka kupendwa. Inatufanya tuwaheshimu zaidi wenzetu kuliko kutaka kuheshimiwa. Kwa njia ya unyenyekevu, tunaweza kufundishwa, kuelekezwa, kuongozwa, kuonywa, kulindwa, kutetewa na kukuzwa kwa ujumla. Ni fadhila ya msingi sana katika maisha ya mahusiano ya kila siku katika familia na katika jumuiya yoyote ile ya watu. Hata marafiki wa kawaida tu, au wachumba wakikosa unyenyekevu basi mahusiano yao daima hayatakosa malumbano, matusi, dharau, ukandamizaji na kila aina ya mateso. Mitume Yakobo na Yohane wanaomba madaraka, enzi na fahari ya kuketi kuume na kushoto kwa Kristo ili wapate furaha. Mitume wengine 10 wanajenga chuki dhidi yao wakidhihirisha wao pia hamu yao ilikuwa hiyohiyo. Tujifunze jambo kwa ndugu hawa wawili… mosi, walikuwa watu wa malengo, kwamba Kristo akiisha kuurudisha ufalme wa Israel wangechukua nafasi za juu serikalini. Pili, hawakuuelewa utume wa Kristo, wanatamani madaraka wakati ambapo Kristo amezama katika mawazo ya anakoenda Yerusalem, na amewaambia mara 3 anakwenda kuteswa lakini hilo haliwaingii, wanataka ukubwa. Tatu, pamoja na yote, walikuwa na imani na Yesu kama Mtawala, hawana shaka na uweza wake na hivi wanaendelea kumfuata… Ombi lao ni sala ya wazi na ya moja kwa moja, hata hivyo ni sala isiyo na unyenyekevu ndani yake “twataka utufanyie lolote tutakalokuomba…” sala njema hububujika toka moyo mkunjufu, mnyenyekevu uliovunjika na kupondeka… Sala ya Yesu, “Baba ikiwezekana, kikombe hiki… lakini si kama nitakavyo mimi bali mapenzi yako yatimizwe…” (Mt 26:39) ni mfano mzuri.

Fadhila ya unyenyekevu ni Mama ya fadhila zote
Fadhila ya unyenyekevu ni Mama ya fadhila zote

UFAFANUZI: Tuzoee kusema “samahani, tafadhali, pole, inawezekana? ninaomba…”, badala ya “nataka! nipe! lete! njoo! nenda! ondoka! Kwa unyenyekevu wetu tutaziponya nafsi zetu... Kristo anawauliza “mwaweza kunywea kikombe ninyweacho na ubatizo nibatizwao?” Kunywea kikombe: Kikombe ni chombo cha kauri, chuma, madini nk kitumikacho kunywea kahawa, chai na maji… Vipo vikombe vya washindi michezoni, vya umeme (kutunza joto lisipotee) na baiskeli (gololi-kinu). Kibiblia kikombe ni mateso na madhulumu, tabu, shida, dhiki na maangamizi (Isa 51:17, Yer 25:15). Yakobo na Yohane kwa kujiamini wanajibu ‘tunaweza!’ na kweli walikinywea: Yakobo aliuawa na Herode mapemaa huku Yohane akiteswa na kufungwa kisiwani Patmo alikokufa mwaka 100. Na ubatizo anaobatizwa Yesu Je? neno ‘baptizein’ = zamisha, didimiza = kuzama katika hali fulani mf. madeni, huzuni, mawazo, pombe, kusoma, kazi nk. Ubatizo anaozungumzia Kristo hapa sio ule wa sakramenti, ni kama anahoji “Je, mnaweza kuzama katika hali ngumu ya uonevu, mateso na madhulumu kama nitakayopitia mimi? Mpo tayari kuzamishwa katika bahari ya chuki, maumivu, ugomvi na hata kifo kama itakavyonitokea mimi?” akimaanisha hakuna hakuna ushindi bila msalaba, mateso kwanza kisha utukufu. Swali hili linatuhusu pia “Je, mwaweza…” tunapaswa kujibu na wana wa Zebedayo “twaweza”. Kikombe hicho anasema nabii Isaya katika somo I (53:10-11) ni kuchubuliwa na kuhuzunishwa, kuwafanya wengi wawe wenye haki na kujitwisha maovu yao. Kutamani madaraka si dhambi, uongozi si kosa na hasa ukiwa na kipaji. Kristo anatufundisha nia ya uongozi sio kuwa mahali pa juu palipoinuka, kuwa na amri, sauti na nguvu… si lengo la uongozi kutufanya maarufu, tutambulike mbali, tutetemekewe na kuhofiwa… uongozi haupi mtu fursa ya kuwaweka chini ya miguu yake wenye mawazo/muono tofauti, kufanya unachotaka!

Sisi sote ni wamisionari, tunaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili
Sisi sote ni wamisionari, tunaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili

Uongozi ni kanuni, sheria, taratibu, haki na amani kwani hata Kristo aliye Kiongozi Mkuu amesema leo (Mk 10:35-45) hakuja kutumikiwa bali kutumika na kutoa nafsi yake kuwa fidia ya wengi… Nabii anasema “kwa maarifa yangu mtumishi wangu mwenye haki atawafanya wengi kuwa wenye haki, naye atayachukua maovu yao” hivi kiongozi abebe maovu ya watu wake, baba abebe maovu ya familia yake, Padre abebe maovu ya waamini wake, rais abebe maovu ya wananchi wake, mwenyekiti abebe maovu ya waliomchagua. Kwamba, uongozi ni utumishi na kuchubuka, halafu uongozi si jambo la kuomba/kukimbilia/kung’ang’ania bali ni wito kutoka kwa Mungu. Unyenyekevu wa uongozi unagusa wabatizwa wote. Mtu aliyebatizwa anashiriki ukuhani, unabii na ufalme wa jumla wa Kristo Mchungaji mwema. Kuongoza ni kuonesha njia na kuwa mfano hivi wabatizwa wadhihirishe madaraka yao kwa mifano ya maisha yao... namna gani? Mosi waonyeshe ukubwa na madaraka yao kwa kuishi fadhila za Kikristo… waketi kuume na kushoto kwa Kristo wakitoa amri juu ya tabia na maelekeo yenye kupofusha akili na macho ya wanadamu. Wakristo wawe viongozi wenye madaraka ya kufukuza giza ya dhambi na kutia nuru maisha yao wenyewe na ya wale wanaowazunguka... Wakristo wawe viongozi wenye madaraka ya kuzima cheche za usengenyi, uzushi, usingiziaji na uhasama wa kila aina. Wakristo wawe viongozi, wakae kuume na kushoto kwa Yesu wakitoa amri zenye kubatilisha ushawishi wote wa uvivu, uzembe, utepetevu na ubaridi katika kutoa huduma, kuwasaidia wahitaji, kusali na upatanisho. Wakristo waketi kuume na kushoto kwa Yesu na wawe viongozi wenye madaraka ya kuhamasisha umoja katika Jumuiya ndogondogo za Kikristo badala ya visa na mikasa, umoja wa Kanisa, umoja wa kijiji, umoja wa wakristo, umoja wa waafrika wa waamerka wa ulaya, nk ‘kwa unyenyekevu wetu, tutaziponya nafsi zetu.’

Dominika ya Kimisionari kwa Mwaka 2024
Dominika ya Kimisionari kwa Mwaka 2024

Unyenyekevu wa uongozi kwa mujibu wa ubatizo wetu, uonekane katika kushauri, kuelekeza na kusamehe. Mwanadamu ana shida na hofu nyingi (Zab 116:3). Wengi wana taabu na huzuni na hivi wanahitaji ushauri na maelekezo, bado hawajatambua njia njema ya maisha, bado hawajaujua wito wao, bado hawajatulia, bado hawajaona hata maana yenyewe ya maisha, wanatamani kufunga ndoa lakini hawajajua ni nani mke/mume mwema, wanatamani kusali lakini hawajui sala bora ni ipi, wanatamani kuwa watu wa dini lakini hawajajua dini ya kweli ni dini gani, wanapenda kufanya kazi lakini hawajapata mwanga ni kazi ipi, wanatamani wanyanyue vipato vyao lakini hawajui watokee mlango gani… wengine wamezama katika starehe kiasi hata maendeleo yao yamerudi nyuma… kwa busara yako utamuokoa mtu huyu nawe utakuwa mkubwa katika ufalme wa Kristo naye Mungu atakuweka mkono wa kuume na wa kushoto wa Kristo Mwanawe, ndio, kwa unyenyekevu wetu, tutaziponya nafsi zetu.

Liturujia D 29
18 October 2024, 10:57