Tafuta

Tafakari Dominika ya 30 ya Mwaka B wa Kanisa: Kristo Yesu ni Nuru ya Ulimwengu. Tafakari Dominika ya 30 ya Mwaka B wa Kanisa: Kristo Yesu ni Nuru ya Ulimwengu.  (AFP or licensors)

Tafakari Neno la Mungu Dominika ya 30 Mwaka B wa Kanisa: Yesu Nuru ya Mataifa

Masomo ya dominika hii yanatilia mkazo juu ya kutimia kwa utabiri wa manabii kwa njia ya Yesu Kristo, nuru na mwanga wa mataifa anayewaponya watu na kuwajaza furaha mioyoni mwao kwa kuwafunulia na kuwaonesha Uso wa Mungu Baba mwingi wa huruma na mapendo kwa waja wake. Ndiyo maana Mzaburi katika wimbo wa mwanzo anasema hivi; “Ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana. Mtakeni Bwana na nguvu zake, utafuteni uso wake siku zote” (Zab. 105:3-4).

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 30 ya mwaka B wa Kiliturujia Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatilia mkazo juu ya kutimia kwa utabiri wa manabii kwa njia ya Yesu Kristo, nuru na mwanga wa mataifa anayewaponya watu na kuwajaza furaha mioyoni mwao kwa kuwaonesha uso wa Mungu Baba. Ndiyo maana mzaburi katika wimbo wa mwanzo anasema hivi; “Ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana. Mtakeni Bwana na nguvu zake, utafuteni uso wake siku zote” (Zab. 105:3-4). Ni katika muktadha huu mama Kanisa katika sala ya mwanzo anatuombea sisi wanae akisali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, utuzidishie imani, matumaini na mapendo. Utuwezeshe kupenda unayoamuru, tustahili kupata na hayo unayoahidi.” Baba Mtakatifu Francisko mwanzoni kabisa mwa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu 2021-2024, Jumamosi tarehe 9 Oktoba 2021, alitoa hotuba elekezi, ambayo ni msingi wa maadhimisho ya Sinodi katika hatua mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Watu wa Mungu wakajitambua kuwa wao ni sehemu ya Kanisa la Kisinodi, tayari kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Mungu, kwa kushirikiana na binadamu wote, kwa kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini kile ambacho Roho Mtakatifu anataka kuyaambia Makanisa. Huu ni mwendelezo wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu iliyozinduliwa kunako mwaka 2021 na inafikia kilele chake Dominika tarehe 27 Oktoba 2024.

Kristo Yesu anamponya Bartimayo Mwana wa Timayo Kipofu
Kristo Yesu anamponya Bartimayo Mwana wa Timayo Kipofu

Somo la kwanza ni la Kitabu cha Nabii Yeremia (31:7-9). Somo hili ni utabiri/uaguzi wa Nabii Yeremia juu ya ujio wa Masiya ambaye kupitia yeye Mungu atawaponya wagonjwa na vipofu. Utabiri huu Yeremia anautoa kwa watu waliobaki Yerusalemu wakati wa uhamisho wa Babeli ndiyo maana anasema; “Mkampigie kelele mkuu wa mataifa, tangazeni, sifuni, mkaseme; Ee Bwana, uwaokoe watu wako, mabaki ya Israeli.” Kipindi cha uvamizi na kuchukuliwa mateka, watu wengine waliachwa na majeraha na mavunjiko mbalimbali. Yeremia anawafariji kwa kuwaahidi kuponywa kwako. Utabiri huu pia unawahusu wale walioko uhamishoni Babeli kuwa nao watarudishwa nyumbani salama. Ndiyo maana anasema kuwa; “Watakuja kwa kulia, na kwa maombi nitawaongoza; nitawaendesha penye mito ya maji, katika njia iliyonyooka; katika njia hiyo hawatajikwaa; maana mimi ni Baba wa Israeli, na Efraimu ni mzaliwa wangu wa kwanza.” Utabiri huu ulitimia kwa wana wa Israeli kurudi kutoka uhamishoni Babeli. Ndiyo maana mzaburi katika wimbo wa katikati anasema hivi; “Bwana alipowarejeza mateka wa Sayuni, tulikuwa kama waotao ndoto. Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko, na ulimi wetu kelele za furaha. Ndipo mataifa waliposema, Bwana amewatendea mambo makuu. Bwana alitutendea mambo makuu, tulikuwa tukifurahi. Ee, Bwana, uwarejeze watu wetu waliofungwa, kama vijito vya kusini. Wapandao kwa machozi, watavuna kwa kelele za furaha. Ingawa mtu anakwenda zake akilia, azichukuapo mbegu za kupanda. Hakika atarudi kwa kelele za furaha, aichukuapo miganda yake (Zab. 126). Lakini kutimia kwa utabiri huu ulikuwa ni mwangwi tu wa ujio wa Kristo Mwanga na Nuru ya mataifa aliyekuja kuwaponya na kuwaokoa watu kutoka giza la utumwa wa dhambi na mauti.

Kristo Yesu ni Nuru ya Uzima wa Milele
Kristo Yesu ni Nuru ya Uzima wa Milele

Somo la pili ni la Waraka kwa Waebrania (5:1-6). Somo hili linatoa ufafanuzi wa ukuhani wa Yesu katika Agano jipya na ule wa Agano la Kale. Kwanza kabisa Kuhani ambaye ni mpatanishi kati ya Mungu na watu, inampasa kuwa na hali ya ubinadamu, ili aonje udhaifu wa kibinadamu, aweze kuwachukulia kwa upole wale wasiojua na wenye kupotea, kwa kuwa yeye mwenyewe yu katika hali ya udhaifu. Ndiyo maana Yesu Kristo, Kuhani Mkuu alichukua mwili wa kibinadamu katika fumbo la umwilisho ili ashiriki hali yetu ya kibinadamu, aonje uhalisia wa mahangaiko yetu na kutupa uwezo nasi wa kushiriki katika ukuhani wake katika kuwafanya watu wamjue, wampende na wamtumie Mungu na mwisho kufika kwake mbinguni. Kumbe kuhani/Padre anatwaliwa kati ya wanadamu, anawekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ili atoe matoleo na dhabihu; kwanza kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za watu wake. Hadhi na heshima hii, hakuna anayeweza kujitwalia mwenyewe, ila yeye aitwaye na Mungu. Vivyo hivyo Kristo naye hakujifanya kuhani mwenyewe. Bali Mungu Baba alimfanya hivyo. Ndiyo maana maandiko matakatifu yanasema; “Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa na kukufanya kuhani milele, kwa mfano wa Melkisedeki.”

Dominika tarehe 27 Oktoba 2024 Kufunga Sinodi ya XVI ya Maaskofu
Dominika tarehe 27 Oktoba 2024 Kufunga Sinodi ya XVI ya Maaskofu

Injili ni kama ilivyoandikwa na Marko (10:46-52). Sehemu hii ya Injili inahusu simulizi la kumponywa kwa Bartimayo, mwana wa Timayo, kipofu wa Yeriko. Yeye aliposikia Yesu Mnazareti anapita, alipaza sauti akisema; “Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu”. Watu walimkemea ili anyamaze. Lakini yeye alizidi kupaza sauti; “Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu.” Yesu anasimama na kuamuru aitwe. Waliokuwa wanamkemea walimwambia; “Jipe moyo; inuka, anakuita.” Akatupa vazi lake, akaruka kwa shangwe, akamwendea Yesu. Yesu akamwambia; Wataka nikufanyie nini? Akasema; “Bwana, nataka nipate kuona.” Sala ya Bartimayo kipofu ni fupi mno; “Bwana nataka nipate kuona.” Ni sala itokayo ndani kabisa mwa mtima wa moyo wake. Yesu akamwambia; “Enenda zako, imani yako imekuponya.” Mara akapata kuona. Kumbe ni kwa imani, Bartimayo aliponywa upofu wake. Nguvu ya imani inashinda upeo wa macho yetu, huweza kuona yanakoshidwa kuona macho. Tukumbuke kuwa, ukiwa katika dhambi unakuwa kama kipofu; hauoni uzuri wa maisha. Saikolojia inatueleza kuwa mtu anapotenda dhambi kwa mara ya kwanza anakuwa na hofu, woga na wasiwasi mkubwa. Hivyo anaitenda kwa kujificha. Lakini akishaizoea, haoni haya tena. Amepoteza mizani ya maadili na kukatika mshipa wa aibu. Kumbe sisi nasi tunaweza kuwa vipofu wa kiroho, tukashindwa kuona udhaifu na kasoro zetu. Kama hatuoni uovu na dhambi zetu, hatuwezi kuomba msamaha kwa Mungu. Hali hii inatufanya tuishi maisha ya huzuni, mfadhaiko, msononeko na kukosa amani. Bartimayo anatualika tumlilie Yesu na kumwambia: “Bwana, nataka nipate kuona.” Kama kuna dhambi uliyoizoeana na huionei aibu tena; “Jipe moyo, inuka, Yesu anakuita utoke huko ulikozama na anakuuliza; “Wataka nikufanyie nini?” Sema bila kuogopa; “Bwana nipate kuona tena.” Kama ndoa na familia yako imejaa malumbano na matatizo hakuna furaha wala amani, mwambie Yesu; “Bwana nipate kuona.”

Kristo Yesu ni Nuru ya Mataifa
Kristo Yesu ni Nuru ya Mataifa

Ubinafsi umekufanya kipofu hata huoni matatizo ya wengine, sema; “Bwana nipate kuona.” Ufisadi umekufanya kipofu huoni wanaoteseka kwa ajili yako, sema; “Bwana nipate kuona.” Tamaa za dunia zimekufanya kipofu huoni mwelekeo wa maisha, sema; “Bwana nipate kuona.” Umeugua muda mrefu na umekosa matibabu, mwambie Yesu; “Bwana nipate kuona.” Tukiomba hivyo kwa imani; jibu la Yesu daima ni kuwa; “Imani yako imekuponya, nenda na amani”. Ili Yesu asikie kilio chetu, lazima sisi nasi tusikie na tusikilize vilio vya wengine. Kwa maana, kipimo kile kile tuwapimiacho wengine, ndicho tutakachopimiwa. Yawezekana kila siku tunasikia vilio vya wengine vya kuomba msaada, vilio vya kutaka kufarijiwa, vilio vya kuomba mwanga, lakini tunajifanya viziwi, hatusikii wala kugeuka kuwasaidia. Tutambue kuwa kufanya hivyo ni ujeuri na ukatili. Tujifunze kutoa faraja kwa wanaolia na kuwaambia: “Jipe moyo; inuka anakuita”. Tujifunze kufumbua macho yetu na mioyo yetu kwa wahitaji wanaopiga kelele kama Bartimayo, wakihitaji msaada na sio kuwafunga mdomo na kuwanyamazisha wasisikike, bali tuwatie moyo ili nao waweze kuishi kwa furaha. Tukumbuke daima kuwa tukiwasaidia wengine kwa sifa na utukufu wa Mungu Baba, tutafanikiwa zaidi. Ndiyo maana katika sala ya kuombea dhabihu mama Kanisa anasali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba upokee dhabihu tunazokutolea wewe mtukufu, ili ibada tunayofanya iwe hasa kwa ajili ya utukufu wako. Na katika sala baada ya Komunyo anahitimisha maadhimisho haya akisali hivi; “Ee Bwana, tunaomba neema ya sakramenti zako zitukamilishe, ili hayo tupokeayo katika maumbo, tufahamu ukweli wake”. Na hili ndilo tumaini letu, kuufahamu ukweli, yaani kumwona Mungu Baba huko mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari D 30
23 October 2024, 16:52