Tafuta

Ujumbe wa masomo ya dominika hii huu: uongozi ni utumishi. Sifa kuu ya kiongozi ni kutumikia. Ujumbe wa masomo ya dominika hii huu: uongozi ni utumishi. Sifa kuu ya kiongozi ni kutumikia.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Tafakari Neno la Mungu Dominika ya 29 Mwaka B wa Kanisa: Uongozi Ni Huduma!

Ujumbe wa masomo ya dominika ya 29 ya Mwaka B wa Kanisa ni huu: uongozi ni utumishi. Sifa kuu ya kiongozi ni kutumikia. Na Mungu ndiye mfano wa uongozi wenyewe, anatulinda na kutuongoza katika kila hali na hatua ya maisha yetu. Tukiwa katika taabu yoyote, tukamwita daima anatusikiliza. Kiongozi mzuri ni mwenye uwezo wa kusikiliza kwa makini, anayejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa watu wake; kwa kusimamia: utu, heshima na haki msingi.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 29 ya mwaka B wa Kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe wa masomo ya dominika ya 29 ya Mwaka B wa Kanisa ni huu: uongozi ni utumishi. Sifa kuu ya kiongozi ni kutumikia. Na Mungu ndiye mfano wa uongozi wenyewe, anatulinda na kutuongoza katika kila hali na hatua ya maisha yetu. Tukiwa katika taabu yoyote, tukamwita daima anatusikiliza. Ndiyo maana mzaburi katika wimbo wa mwanzo anasema hivi; “Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika, utege sikio lako ulisikie neno langu. Ee Bwana, unilinde kama mboni ya jicho, unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako (Zab. 17: 6,8). Naye Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anatuombea akisali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, utuwezeshe kufuata daima mapenzi yako matakatifu na kuitumikia fahari yako kwa moyo mnyofu”. Somo la kwanza ni la Kitabu cha Nabii Isaya (53:10-11). Somo hili ni utabiri wa ujio wa “mtumishi wa Bwana” atakayetolea nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi za watu. Mtumishi huyu ataona uzao wake, ataishi siku nyingi na mapenzi ya Bwana yatafanyika kwa mkono wake. Kwa kuwa ni mwenye haki, atawafanya wengi kuwa wenye haki. Mababa wa imani wameona katika utabiri huu nafsi ya Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu, nafsi ya pili ya Mungu aliyechukua mwili kwa Bikira Maria kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Yeye kwa mateso, kifo na ufufuko na wake, amewafanya wengi kuwa wenye haki, watoto wateule wa Mungu. Nasi kwa njia ya ubatizo tumezaliwa upya na kuwa watu wa haki mbele za Mungu. Hivyo nasi tuna wajibu wetu kutenda haki kwa watu wengine.

Uongozi ndani ya Kanisa ni kielelezo cha huduma ya upendo
Uongozi ndani ya Kanisa ni kielelezo cha huduma ya upendo

Ili tuweze kuishi vyema na kutenda yote kwa haki lazima tuongozwe na Neno la Mungu. Ndivyo anavyosisitiza mzaburi katika wimbo wa katikati akisema; “Neno la Bwana lina adili, na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu. Huzipenda haki na hukumu, nchi imejaa fadhili za Bwana. Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao, wazingojeao fadhili zake. Yeye huwaponya nafsi zao na mauti, na kuwahuisha wakati wa njaa. Nafsi zetu zinamngoja Bwana, Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu. Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi, kama vile tulivyokungoja Wewe” (Zab. 33: 4-5, 18-20, 22). Somo la pili ni kutoka katika Waraka kwa Waebrania (4:14-16). Somo hili linatueleza matunda yaliyoletwa na mtumishi wa Bwana, Yesu Kristo, Kuhani Mkuu, ambaye kwa mateso, kifo na ufufuko wake ametuwezesha kukisogelea kiti cha enzi ch Mungu Baba. Yesu Kristo Kuhani mkuu yuko mbinguni, ili nasi tuweze kufika aliko yeye, sharti tuyashike maagano ya ubatizo wetu. Yeye anayajua madhaifu yetu, maana hata yeye alijaribiwa sawa sawa na sisi katika mambo yote, isipokuwa hakutenda dhambi. Hivyo mtume Paulo anatutia moyo na kutihimiza kuwa; “Tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji,” ili mwisho wa yote tuufikie uzima wa milele mbinguni aliko Mwokozi wetu Yesu Kristo. Injili ni kama ilivyoandikwa na Marko (10:35-45). Sehemu hii ya Injili ni mawaidha na mafundisho ya Yesu ya namna tunavyopaswa kuishi ili tuweze kuurithi uzima wa milele. Kwanza kabisa lazima tuwatumikie wengine kwa upendo. Huu ndio wajibu wetu. Pili ni Mungu Baba peke yake ndiye mwenye mamlaka na uwezo wa kumketisha yeyote yule mkono wa kuume au kushoto kwa Yesu. Mafundisho haya Yesu anayatoa baada ya mitume Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, kumwomba kuketi, mmoja mkono wake wa kuume, na mmoja mkono wake wa kushoto, katika utukufu wake. Hawa ndugu walitamani kuwekwa katika mamlaka ya juu. Yesu anawaambia kuwa hawajui wanaloliomba, kwa sababu ombi lao lilisukumwa na moyo wa tamaa na ubinafsi. Tamaa hii walikuwa nayo hata mitume wengine. Ndiyo maana waliwakasirikia Yakobo na Yohane kwa ombi lao.

Kiongozi bora ni yule anajitahidi kuwasikiliza watu wake
Kiongozi bora ni yule anajitahidi kuwasikiliza watu wake

Ni katika muktadha huu Yesu anatoa fundisho kuwa kiongozi ni mtu mkubwa na mwenye mamlaka. Lakini katika ukubwa wake na mamlaka yake, anapaswa na anawajibika kuwatumikia wengine. Kumbe uongozi ni utumishi. Yakobo na Yohane walitamani kukaa na sio kutumikia. Ndiyo maana walisema; “utujalie tukae mmoja mkono wako wa kulia na mmoja mkono wako wa kushoto katika utukufu wako.” Wanataka wakae. Haja yao ni kukaa na kustarehe katika utukufu. Uongozi sio kukaa ni kutumikia. Mwinjili Luka anaposimulia tukio hili anasema kuwa kulikuwa na majadiliano na kati ya wanafunzi wa Yesu kuhusu nani kati yao aliyekuwa mkuu zaidi (Lk. (9:46).  Bila shaka Yakobo na Yohane baada ya kushindwa katika mjadala huo waliamua kwenda moja kwa moja kwa Yesu ili awafanyie upendeleo. Tabia hii inaendelea hata leo. Wapo wanaotumia kila mbinu hata kutoa rushwa ili wapendelewe na wapewe nafasi za juu za uongozi, wakae, wastarehe. Yawezekana hawa ndugu walikuwa na mali wakajiona kuwa maarufu na wanaostahili kuwa viongozi hata kwa rushwa. Ndiyo maana wanasema; “Tunataka utufanyie lolote tutakalokuomba.” Ni kama vile kunasema utufanyie lolote tunalotaka kama ni pesa tutakupatia. Kumbe, tunafundishwa kuwa uongozi sio swala la upendeleo. Mtu kuwa kiongozi ni maamuzi ya Mungu. Na kinachomfanya mtu kuwa kiongozi ni moyo wake wa kujitoa na kuwa tayari kutoa maisha yake kwa ajili ya wale atakaowaongoza.

Kiongozi awe na kipaji cha kusikiliza kwa makini
Kiongozi awe na kipaji cha kusikiliza kwa makini

Kiongozi bora lazima awe tayari kuutoa uhai wake kwa ajili ya wale anaowaongoza. Kiongozi bora yuko tayari kuteseka kwa ajili ya watu wake. Kiongozi bora yuko tayari kuchubuliwa, anakubali kuhuzunishwa na kutukanwa kwa kutetea haki za watu wake na kuzisimamia. Kiongozi bora yuko tayari kukinywea kikombe cha kupambana na maovu katika jamii yake. Kumbe basi katika maisha tusitafute vitu vya kupendelewa. Maana tukifanya hivyo tunapoteza uhuru kwa yule anayetupendelea. Tutafute maendeleo katika maisha kwa kupambana kwa njia halali. Zaidi sana kiongozi bora ana huruma, anachukuliana na watu wake katika unyonge na kuwasaidia waweze kuondokana na unyonge huo. Kiongozi bora yuko tayari mapenzi ya Mungu yatafanyika kwa mikono yake. Kiongozi bora ni mcha Mungu, anatambua kuwa Mungu anamtumia katika kutimiza mapenzi yake. Sifa hizi ni kwa kila kiongozi kuanzia ngazi ya familia, jumuiya, Kanisa, na taifa kwa ujumla wake. Basi kila mmoja katika nafasi yake ajitahidi kutumikia na sio kutumikiwa, kwani ni katika kutumika tunastahilishwa kuurithi uzima wa milele. Ndiyo maana mama Kanisa katika sala ya kuombea Dhabihu anatuombea akisali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba utuwezeshe kukutumikia kwa uhuru kwa vipaji vyako. Ututakase kwa neema yako na kwa sadaka hii tunayokutolea”. Na katika sala baada ya Komunyo anahitimisha maadhimisho haya akisali hivi; “Ee Bwana, utuwezeshe kupata maendeleo ya roho tunaposhiriki mara nyingi mambo haya matakatifu. Tujaliwe riziki za hapa duniani na hekima katika mambo ya mbingun.” Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari D 29
15 October 2024, 14:03