Ask.Niwemugizi,Rulenge-Ngara:Ndoa ya Familia katika Mpango wa Mungu!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika ibada ya Misa Takatifu, tarehe 6 Oktoba 2024 katika fursa ya Hija ya Jimbo huko Rusenyi, Parokia ya Bikira Maria wa Lourdes, Katoke, kama sehemu ya Maadhimisho ya Somo wa Jimbo, Mtakatifu Francis wa Assisi ambayo huadhimishwa kila tarehe 4 Oktoba ya kila mwaka, Askofu Severine Niwemuguzi, wa Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara, Tanzania aliongoza Ibada ya Misa Takatifu. Dominika hiyo ilikuwa tayari ni kesha la Siku Kuu ya Bikira Maria wa Rozari, ambapo misa iliyudhuriwa na idadi kubwa ya mapadre, watawa, waaamini watu wa Mungu, viongozi mbali mbali wa dini na serikali. Katika mahubiri ya Askofu Niwemuguzi, yalijikita na mada ya Ndoa ya Familia katika Mpango wa Mungu, kama Mpango madhbuti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kuhusiana na Ulinzi wa Watoto, ambapo Askofu huyo ni Rais wa Kamati ya Kichungaji kwa ajili ya Ulinzi wa Watoto, Wahamiaji na Wakimbizi ya Baraza hilo, la Maaskofu Katoliki sanjari na Mpango kabambe wa Mabaraza ya Maaskofu ya Nchi zote za (AMECEA) yaani, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki ya Afrika Mashariki. Yafuatayo ni sehemu fupi tu ya mahubiri yake mara baada ya masomo ya Domika tarehe 6 Oktoba 2024 kutoka:(Mwa 2:18:24; Zab: 128, Ebr 2:9-11; Mk 10:2-16).
Mti mzuri hauzai matunda mabaya,wala mti mbaya kuzaa matunda mazuri
Askofu Niwemugizi akianza mahubiri yake alisema: “Ndugu zangu wapendwa, Kristo katika mafundisho yake, wakati fulani alitoa msemo huu: “Mti mzuri hauzai matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri,(Mt 7,17-20) na ukitoa, basi itakuwa ni jambo lisilotegemewa. Walau inategemewa mti mzuri kutoa matunda mazuri. Ndugu zangu wapendwa, tutafakari leo juu ya Ndoa na Familia katika Mpango wa Mungu. Tunaweza tukasema: “familia ni tunda la ndoa nzuri.” Na tumesikia Kristo mwenyewe alisema tangu mwanzo wa Ulimwengu, tangu kuumbwa kwa Ulimwengu alimfanya mtu mwanaume na mtu mwanamke. Na hao akawaunganisha kama tulivyosikia katika somo la Kwanza kutoka katika kitabu cha Mwanzo(Mwa 2:18:24). Baada ya kuumba Adamu, akaumba na viumbe wengine, lakini tunaambiwa kuwa, hakuona anayefanana na Adamu wa kusaidiana naye, ndipo akamuumba Mwamamke, kutoka katika ubavu wake Adamu. Na alipomleta mwamke mbele ya Adamu, Adamu akasema: “sasa huyu atakuwa mwanamke, kwa sababu katoka ndani ya ubavu wangu na huyo ndiye anafanana naye, anayeweza kusaidiana naye. Na tunakumbuka katika kitabu cha Mwanzao huko huko baada ya kumuumba Adamu na Eva akawapa kazi: Sasa zaeni mkaongezeke na kuijaza dunia na muitale.” Ndugu zangu wapenda, ndoa nzuri itazaa familia nzuri, familia nzuri itazaa jamii nzuri, la sivyo ndiyo maana italeta matunda mabaya na familia mbaya italeta matunda mabaya, au itazaa jamii mbaya.
Rais wa Kamati ya Ulinzi wa Watoto,Wahamiaji na Wakimbizi ya TEC
Ndugu zangu wapendwa mimi katika Baraza la Maaskofu Katoliki, Tanzania (TEC) nimepewa Kamati ya Ulinzi wa Watoto kuisimamia, lakini pia wakimbizi na wahamaji au wahamahamaji. Ni vitengo ninavyosimamia katika Baraza la Maaskofu. Na Juma lililopita, nilikwenda Nairobi (Kenya). Huko niliitwa kushiriki katika Mkutano wa kujifunza juu ya namna ya kutunza na kulea watoto katika Nchi za AMECEA. Nchi 9 za Maaskofu katika Eneo hili la Nchi 9 kutoka Ethiopia, Eritrea, Sudan, Sudan Kusini, Kenya, Uganda, Tanzania, Malawi, na Zambia. Tulikutanika pale kujifunza: “tunawatunaje kulea watoto katika mazoea yetu tuliyo kuwa nayo? Sawa watoto wanazaliwa katika mazingira ya aina mbali mbali, wengine wana baba, wana mama, lakini wengine wanazaliwa hawajuhi mama ni nani, na wengine hawajuhi baba ni nani, na wengine wameokotwa. Wanaokotwa kwa sababu mama amemzaa na amemtupa polini, au amempeleka mahaliambapo anaona kwamba, hapa labda mtoto wangu anaweza kuokotwa na kutunzwa mahali fulani, kwa sababu ya kitu fulani ambacho kimo ndani ya mama huyo. Mama na Mtoto wana mshikamano wa kipekee. Kwa njia hiyo unapokutana na mtoto anazaliwa alafu anatupwa, na anakulia katika mazingira ya kutatanisha, inaumiza sana!
Vituo vya kulelea na kutunza watoto
Kwa hiyo ndiyo ikafikia mahali, tukajikuta tunaanzisha vituo vya kulelea watoto na kutunza watoto. Tunavyo vituo vyetu kwa mfano, kijimbo: kimoja kinaitwa “Nyumba ya Malaika-Rulenge,” inayosimamiwa na Masisita wetu, Masisita wa Mtakatifu Bernadetta, lakini pia wapo Masisita wa Mama Theresa wa Kalkutta pale “Goyagoya,” wanacho kituo pia kinachopokea watoto wa aina mbali mbali. Lakini pia kipo kituo kingine cha “Nazareth” pale Ngara mjini, kinachopokea na kuwatunza watoto wanaoitwa wa ‘mitaani.’ Jina baya kabisa lisilostahili. Hakuna mtoto wa mitaani. Wote tumezaliwa na baba na mama, lakini vituo viko hivyo vya aina hiyo. Sasa tumezoea watoto ambao wamekulia katika mazingira magumu magumu kwa sababu mbali mbali, tunawapeleka pale. Wengine wanatunzwa kwa muda na baadaye wanarudi kwenye familia, lakini wengine ambao hawajulikani baba ni nani, na mama ni nani, inakuwa ngumu hata kuwafutatilia wazazi wake, basi wanatunzwa kwenye vituo hivyo mpaka wanapokua na kuwa watu wazima na wakaanzisha miji yao.
Mpango mpya wa pamoja wa utunzaji wa watoto katika Nchi za AMECEA
Sasa nchi za AMECEA zimefika mahali fulani zikasema lazima sasa tutazame upya jinsi tunavyowatunza na kuwalea watoto. Mazingira yao ya kuwalea vizuri kabisa ni katika mazingira ya familia na si vinginevyo. Kwa njia hiyo tulikuwa na siku tatu za kujifunza pale na kufanya maazimio. Changamoto inayokuwepo sasa hivi ni familia kushambuliwa na nguvu za uovu, za aina mbali mbali. Familia inashambuliwa kutoka pande zote na shetani mwovu. Tumesikia hapa wanasimuuliza Bwana wetu Yesu Kristo kuwa: “Je ni halali mwanamme kumwacha mke wake kwa sababu yoyote? Na kuwauliza: “je mlielekezwa nini? Wanamjibu kwamba: “Musa aliwambia kwamba, wamwandikie talaka.” Kwa hiyo adui mmojawapo wa familia ni talaka. Adui mkubwa wa familia ni wazazi kuachana kwa sababu yoyote. Ninasema yupo shetani anayeshambulia familia kwa namna mbali mbali. Siku hizi tunasikia habari za Single mother, Single father, yaani baba mmoja anajifanya naye ana familia. Je anakuaje na familia bila mke. Anakwenda kama kobokobo anayegonga huko anazalisha watu, alafu analeta watoto nyumbani au anamkuta mama na kumwambia mama ninaomba unitunzie watoto wangu. Mama wa mtu hana ujanja, anasema ni wajukuu nimepata! Anajaribu kutunza watoto hao, hivyo hivyo mabinti na (wengine mko hapa) mnagongwa gongwa huko, bila mpango na mnazaa au mnawaleta kwa mama yako, hapo nyumbani, una shughuli zako huko na kumwachia hapo ili mama alee mjukuu. Na wengine wanawatunza wenyewe. Kwa hiyo tuna mazingira hayo.
Shetani mwingine ndani ya jamii mamboleo
Mtoto anazaliwa lakini analelewa katika mazingira yasiyo ya kikwelikweli, hasa kuna shetani mwingine ameingia, ambaye tunamsikia anasambaa, tena kwa kasi: ushoga na usagaji. Mwanaume kuoana na mwanaume mwenzake; mwanamke kuoana na mwanamke mwenzake. Hebu tufikirie hao je wanatengeneza familia ipi? Hiyo ni ndoa inaweza kuleta familia bora? Lazima kujiuliza masuala haya. Na wanafika mahali mme na mme wanaoana na wanasema kuwa, sisi tutakuwa na watoto. Kwa namna gani? Tutakwenda kwenye vituo vya watoto Yatima,“tutaasili.” Upo utaratibu wa “kuasili.” Yaani mtoto yupo kwenye kituo pale, unakwenda na kufuata taratibu za kisheria na unapewa mtoto huyo, anakuwa kama mtoto wako(kuasili.) Unajiuliza je huyo mume na mme watamtuzaje mtoto huyo na kupatia malezi mazuri na salama?
Lengo ni Mtoto alelewe katika mfumo wa joto la familia
Lengo, ndugu zangu tunataka mtoto azaliwe na alelewe katika mazingira ya mfumo wa familia ambayo itampatia mazingira bora ya kukua na kulelewa na kupata haki zake kama mtoto. Mazingira ya upendo na salama. Kiukweli utunzaji wa mtoto, utunzaji salama kabisa unapaswa kuwa katika mazingira ya kifamilia. Changamoto iliyopo: je familia hii inazo sifa za kutoa malezi na matunzo ya mtoto? Kwa sababu siyo familia zote zina uwezo wa kufanya hivyo. Kwa hiyo lengo tunalo lenga sasa ni kuangalia kuimarisha familia ili iweze kutoa malezi au kutoa mazingira ya upendo na usalama kwa watoto. Kwa sababu hiyo nilikwenda Da Es Salaamu, kwa sababu ilinipasa kuudhuria kikao cha Idara ya Kichungaji ya Baraza la Maaskofu(TEC) nitoe ripoti ya yale yote niliyojifunza huko Nairobi, ili sisi tuanza mkakati. Kwa sababu tumejifunza huko Kenya. Nchini Kenya imekuwa kama ndiyo nchi ya Mfano katika kueleza mpango huu,kwamba “tutoke sasa katika malezi ya mtoto kwenye vituo na kumtafutia malezi mtoto katika mfumo wa familia.” Sisi tunayo familia kwa mfano inayoitwa familia ya asili, baba, mama na watoto, lakini, pia tuna familia pana, mtoto ana shangazi, bibi, mjomba, nk. Hii yote ni familia pana, ambamo sote kama hiyo familia imetayarishwa vizuri inaweza kutoa malezi bora ya upendo na salama kwa watoto. Ni kazi kubwa!
Ndugu msomaji wa Makala hii; hii ni sehemu ndogo tu iliyoahaririwa kuhusu maelezo ya Askofu wa Rulenge-Ngara akifafanua juu ya Mpango mzuri wa baadaye wa Nchi za AMECEA unaotarajia kuondoa vituo vya kulelea watoto/kutunza watoto wenye uhitaji iliwaweze kulelewa na kukua katika mfumo wa mazingira ya familia. Siyo kazi rahisi kama alivyofafanua Askofu NiweMuguzi, lakini itafanikiwa tu, kadiri suala hili likavyotolewa ushirikiano wa kina na wote katika jamii, hasa baada ya kujua maana ya nini "Mtoto kukaribishwa ndani ya joto la familia!" Sehemu ya mwisho ya maandishi itafuata, lakini kwa sasa unaweza kusikiliza Audio nzima ya mahubiri yake hapa chini: