Zambia:Kituo cha Radio Katoliki-Kabangabanga kutimiza miaka kumi ya utangazaji
Padre Wilbroad Musonda – Solwezi na Angella Rwezaula – Vatican.
Akihutubia waamini wa Jimbo la Kaskazini Magharibi katika matangazo ya moja kwa moja Jumamosi, tarehe 12 Oktoba 2024, katika kuadhimisha miaka kumi ya kituo cha radio ya Kanisa, Askofu Kasonde wa Jimbo Katoliki la Solwezi aliwapongeza Wakristo wakatoliki na watu wenye mapenzi mema kwa uaminifu wao kwa mpango wa Kanisa.
Radio kwa ajili ya maendeleo fungamani ya binadamu
Askofu Kasonde alielezea kuridhishwa na kuthaminiwa na kiwango cha msaada ambacho kituo cha radio kimepokea kutoka kwa watu wa Jimbo la Kaskazini Magharibi katika miaka kumi iliyopita. “Kwa kweli, nataka kusema pongezi kwa Jimbo Katoliki, kwenu nyote Wakristo Wakatoliki, kaka na dada zetu wa Jimbo la Kaskazini Magharibi, na watu wenye mapenzi mema ambao wamekuwa wakitumia kituo hiki cha radio,” alisema Askofu Kasonde. Kiongozi wa Solwezi alisema miongoni mwa malengo ya kituo hicho cha radio ni kueneza Habari Njema ya Injili, kuhimiza maendeleo fungamani ya binadamu, kutoa taarifa na elimu juu ya masuala mbali mbali yanayowahusu watu wa Jimbo la Solwezi na Kaskazini Magharibi mwa mkoa.
Kukuza mahusiano mazuri katika jamii
Kabangabanga, "nyota" katika lugha ya kienyeji ya Kikonde inayozungumzwa sana katika eneo hilo, ilichaguliwa kama jina la radio na "iliyoundwa kuifanya kuwa nyota ya jimbo," alisema Askofu Kasonde. Askofu aliwahimiza watayarishaji wa vituo vya radio kuendelea na vipindi vya radio vyenye mwelekeo wa kijamii vinavyosaidia kujenga na kukuza uhusiano mwema miongoni mwa wanajamii na makabila ya mkoa huo. "Tunapoadhimisha miaka kumi ya kuwepo kwa kituo hiki cha radio, pia tunaangalia nyuma katika historia yetu - tunakotoka tunapokabili siku zijazo - tunakokwenda," alisema. Hata hivyo mapema katika mahubiri yake wakati wa Misa ya Shukrani, Askofu Kasonde aliwataka Wakristo wote kuiombea radio hiyo ili kweli iwe sauti na nyota inayoonekana kwa Kanisa mahalia na jamii kwa ujumla.
Padre Samasumo:Changamoto na ushindi wa Jimbo la Solwezi
Akizungumzia kuhusu miaka kumi ya matangazo ya Radio Kabangabanga, Mfanyakazi wa Radio Vatican, Padre Paul Samasumo wa Idhaa ya Kiingereza Afrika alikazia radio na ukuzaji wa mahusiano mazuri katika jamii huko akiipongeza radio hiyo kwa hatua hiyo muhimu. Hayo yaliriji wakati wa mahojiano mafupi ya Radio Kabangabanga na Radio Vatican ambapo, Padre Samasumo, ambaye aliwahi pia kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Sekretarieti ya Kanisa Katoliki ya Zambia, alikumbusha baadhi ya changamoto na ushindi wa Jimbo la Solwezi katika kuanzisha kituo hicho cha radio.
Padre Samasumo, pia kama Makamu wa Rais wa sasa wa SIGNIS Ulimwenguni - chama cha Kikatoliki cha wataaluma wa vyombo vya habari, aliakisi umuhimu wa radio hata katika ulimwengu ambao umeenda kidijitali na bila kujali ukuaji wa mitandao ya kijamii. Alisema “watu wengi hasa barani Afrika bado wanategemea radio kama chanzo muhimu cha habari na burudani. “Padre Samasumo “aliitambua na kuishukuru Radio Kabangabanga kwa kutangaza tena kipindi cha habari za kila siku za Kiingereza Afrika cha Radio Vatican.” “Ushirikiano unaoendelea, alisema, “unahakikisha kwamba sauti za Baba Mtakatifu, Papa Francisko, Kanisa la Afrika, pamoja na zile za Kanisa zima ulimweguni linasikika na kufika katika nyumba za wasikilizaji wa Kabangabanga kila siku.”
Shukrani kutoka kwa Padre Christopher Sawila Meneja wa Kituo cha matangazo
Katika maoni ya shukrani wakati wa kusherehekea kumbukumbu ya miaka na Siku ya Wazi ya Radio Kabangabanga, Meneja wa Kituo Padre Christopher Sawila alimshukuru Askofu Kasonde kwa msaada anaoendelea kuutoa kwa kituo hicho cha radio. “Baba wangu Askofu, kwa niaba ya wasimamizi na wafanyakazi, tunakushukuru kwa kuadhimisha Misa kwa ajili ya kuadhimisha miaka kumi ya Radio Kabangabanga. Hii inaonesha jinsi unavyothamini Radio kama chombo cha Uinjilishaji Kikamilifu wa watu wa Mungu katika Kanisa na jumuiya ya Jimbo la Kaskazini Magharibi,” alisema Padre Sawila. Tarehe 28 Juni 2014, Radio Kabangabanga ilibarikiwa rasmi na Askofu wa Kawaida wa mahalia Charles Kasonde. Baadaye ilizinduliwa rasmi na aliyekuwa Waziri wa Mkoa wa Kaskazini Magharibi, Bwana Nathaniel Mubukwanu, mbele ya aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Zambia na Malawi Askofu Mkuu Julio Murat.