2024.11.08 Dominika ya  XXXII ya mwaka B wa kawaida. Yesu anatazama rohoni mwa kila mtu anavyotoa sadaka. 2024.11.08 Dominika ya XXXII ya mwaka B wa kawaida. Yesu anatazama rohoni mwa kila mtu anavyotoa sadaka. 

Baraka za Mungu haziishi kwa walio wakarimu

Somo la kwanza ni la kitabu cha kwanza cha Wafalme linadhihirisha ukarimu wa Mungu kwa walio wakarimu na wanaomtumainia Yeye.Somo la pili ni la waraka kwa Waebrania hili linatueleza jinsi Yesu alivyojitoa sadaka kwa ajili yetu mara moja tu katika utimilifu wa nyakati, kwa maondoleo ya dhambi.Injili ilivyoandikwa na Marko,inatupatia fundisho la moyo wa ukarimu kupitia kwa mama mjane kama mjane wa sarepta katika somo la kwanza.

Na Padre Paschal Ighondo – Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 32 ya mwaka B wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe wa masomo ya domenika hii ni huu: Neema na baraka za Mungu haziishi kamwe kwa walio na moyo wa ukarimu kwa wengine. Maana maombi yao daima yanasikilizwa na Mungu kwa wema wao. Ndiyo maana mzaburi katika wimbo wa mwanzo anasali hivi; “Maombi yangu yafike mbele zako, uutegee ukulele wangu sikio lako, ee Bwana” (Zab. 88:2). Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi Rahimu, utuepushe kwa wema wako na yote yawezayo kutudhuru, tuwe tayari rohoni na mwilini kutimiza mapenzi yako pasipo kizuio.”

Somo la kwanza ni la kitabu cha kwanza cha Wafalme (17:10-16). Somo hili linadhihirisha ukarimu wa Mungu kwa walio wakarimu na wanaomtumainia Yeye. Ndivyo alivyofanya kwa mjane wa Serepta aliyeweka matumaini yake yote kwake hata akatoa kilichokuwa chakula chake yeye na mwanae akampa nabii Eliya. Maandiko yanasimulia hivi: ilikuwa kipindi cha njaa katika Israeli. Mvua haikunyesha kwa miaka 7 kama alivyotabiri Nabii Eliya kwa sababu za dhambi ya kuabudu miungu mingine wakati wa mfalme Ahabu. Mke wa mfalme Ahabu, Yezebeli aliamuru Nabii Eliya auawe kwa utabiri huo. Basi Eliya akakimbilia Sarepta. Huko alikutana na mwanamke mjane akamwambia; “Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa na kipande cha mkate mkononi mwako.” Huyu mama alimjibu Elia; “Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tule tukafe.” Eliya akamwambia; “Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema. Lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. Kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema; “Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitakauka, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi.”

Basi yule mama mjane kwa kuamini maneno ya Eliya na kwa moyo wake wa ukarimu, alienda, akafanya kama alivyoagizwa nao wakala siku nyingi. Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawa sawa na neno la Bwana alilolinena kwa kinywa cha Eliya.” Huu ndio ukarimu wa Mungu kwa walio wakarimu. Ndivyo anavyosema mzaburi katika wimbo wa katikati kuwa; “Ee nafsi yangu, umsifu Bwana. Bwana huishika kweli milele, huwafanyia hukumu walioonewa. Huwapa wenye njaa chakula; naye huwafungua waliofungwa. Bwana huwafumbua macho waliopofuka, naye huwainua walioinama. Bwana huwapenda wenye haki, naam, huwahifadhi wageni. Bwana huwategemeza yatima na wajane, bali njia ya wasio haki huipotosha. Bwana atamiliki milele, Mungu wako, ee Sayuni, kizazi hata kizazi (Zab. 146:1, 6-10).

Somo la pili ni la waraka kwa Waebrania (9:24-28). Somo hili linatueleza jinsi Yesu alivyojitoa sadaka kwa ajili yetu mara moja tu katika utimilifu wa nyakati, kwa maondoleo ya dhambi zetu tofauti na vile kuhani mkuu wa Agano la Kale alivyoingia katika patakatifu kila mwaka kwa damu isiyo yake. “Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu; kadhalika Kristo naye, alitolewa sadaka mara moja akazichukua dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu. Kwa maana yeye hakuingia katika patakatifu palipofanyika kwa mikono ya wanadamu, bali alingia mbinguni hasa, usoni pa Mungu kwa ajili yetu.” Huu ni ujumbe wa matumaini na faraja kwetu, kwamba tukimtumaini Yesu Kristo kuhani wetu mkuu tutaokolewa kutoka utumwa wa dhambi na kushirikishwa uzima wa milele, na tusipomtumaini, hukumu ya milele inatuhusu.

Injili ni ilivyoandikwa na Marko (12:38-44). Sehemu hii ya Injili inatupa fundisho la moyo wa ukarimu kupitia kwa mama mjane kama mjane wa sarepta katika somo la kwanza. Katika simulizi hili tunaambiwa kuwa mama huyu mjane, maskini alitoa senti mbili, kiasi cha nusu pesa kama sadaka. Naye Yesu akausifia ukarimu wake. Hili ni fundisho kuwa ukarimu hautegemee wingi wa vitu tunavyotoa. Bali utayari wa moyo kutoa kile tulichonacho kwa upendo kwa ajili ya wengine. Ndiyo maana Yesu anasema; “Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina. Maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu mjane katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote.”

Kumbe ukarimu unahitaji moyo wa sadaka na kuwa tayari kujiachia kwa ajili ya wengine. Ndiyo maana kila mara Mama Kanisa anatufundisha umuhimu wa kutoa sadaka kwa kuwa hili ni tendo la kiliturujia. Na kwa kuwa liturujia ni kazi ya ukombozi, kila anayetoa sadaka anashiriki kazi ya ukombozi. Moyo wa sadaka na ukarimu unahitaji moyo wa Imani na Matumaini ili kukishinda kishawishi cha woga kuwa nikitoa nitabakia na nini? Zaidi sana maandiko Matakatifu yanatufundisha kuwa; “Apandaye kidogo huvuna kidogo; apandaye kwa wingi huvuna kwa wingi…” (2 Kor 9:6, 12). Ndivyo ilivyokuwa kwa Mjane wa Sarepta, kwa kumpatia Eliya mkate, pipa la unga halikupungua wala chupa ya mafuta haikuisha. Hata Waswahili katika methali husema; “Mkono utoao ndio upokeao”.

Na katika kutoa usijilinganishe na wengine. Kama una vichache usiogope kutoa kidogo ulichonacho ukijilinganisha na wenye vingi. Kama una vingi usitoe vichache ukijilinganisha na wengine ambao wanatoa kidogo au hawatoa kabisa. Usitoe sadaka yako kwa kulalamika. Mtume Paulo anatuasa akisema; “Kila mmoja na atoe kadiri alivyoamua, kwa moyo na wala si kwa huzuni au kwa kulazimishwa, maana Mungu humpenda yule mwenye kutoa kwa furaha” (2Kor 9:7).  Maandiko matakatifu yanaendelea kusisitiza; “Usicheleweshe sadaka yako kwa maskini mwombaji. Usikatae kumsaidia mwombaji aliye na taabu, wala usimpe kisogo masikini. Usiepe kumwangalia mtu fukara, usimpe nafasi ya kukulaani. Maana akikulaani katika uchungu alionao, Muumba wake ataisikia sala yake” (Sira 4: 3-6).

Basi tumwombe Mungu Roho Mtakatifu atujalie moyo wa ukarimu ili utusaidie kujipatia neema na baraka zitakazotustahilisha kuingia katika ufalme wa Mungu Mbinguni. Ndivyo inavyosisitiza sala ya kuombea dhabihu ikisema; “Ee Bwana tunaomba upende kuzitazama dhabihu hizi, ili tujipatie kwa huruma yako neema za fumbo hili la mateso ya Mwanao tunaloadhimisha. Na katika sala baada ya komunyo mama Kanisa anahitimisha maadhimisho ya dominika hii akituombea hivi; “Ee Bwana, sisi tulioburudishwa kwa neema takatifu tunakushukuru na kukuomba sana rehema yako. Nayo neema ya uchaji idumu ndani yetu sisi, tuliopata nguvu ya mbinguni kwa Roho wako”.

Dominika ya 32 ya mwaka B
08 November 2024, 14:26