2024.11.15Ijili ya  Dominika ya XXXIII ya Mwaka B 2024.11.15Ijili ya Dominika ya XXXIII ya Mwaka B 

Daima tuwe tayari kwa hukumu ya mwisho

Tupo ukingoni mwa mwaka B katika liturujia.Jumapili ijayo ni tunafunga mwaka B,kwa sherehe ya Kristo Mfalme na kuwa tayari kuanza liturujia ya mwaka C,kwa Jumapili ya kwanza ya Majilio.Ndiyo maana Mama Kanisa ametuwekea masomo yanayotuelekeza kutafakari juu ya siku za mwisho za maisha yetu hapa duniani.Kumbe tunaalikwa kujitahidi kutenda mema na kuacha dhambi kila siku katika maisha yetu.

Na Padre Paschal Ighondo – Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 33, mwaka B wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Tupo ukingoni mwa mwaka B katika liturujia. Jumapili ijayo ni tunafunga mwaka B, kwa sherehe ya Kristo Mfalme na kuwa tayari kuanza liturujia ya mwaka C, kwa Jumapili ya kwanza ya Majilio. Ndiyo maana Mama Kanisa ametuwekea masomo yanayotuelekeza kutafakari juu ya siku za mwisho za maisha yetu hapa duniani. Ni wakati wa kujichunguza mienendo yetu, mahusiano yetu sisi wenyewe katika nafsi zetu, pamoja na ndugu na jamaa zetu. Lengo ni kujiandaa vema kwa ujio wa pili wa Yesu Kristo. Katika kujiandaa huko hatupaswi kuwa na mashaka wala wasiwasi maana mzaburi katika wimbo wa mwanzo anatuambia hivi; “Bwana asema: Mawazo ninayowawazia ninyi ni mawazo ya amani wala si ya mabaya. Nanyi mtaniita nami nitawasiliza, nami nitawarudisha kutoka mahali pote watu wenu waliofungwa” (Yer. 29:11, 12, 14). Ni katika tumaini hili mama kanisa katika sala ya mwanzo anatuombea akisali hivi; “Ee Bwana Mungu wetu, tunakuomba utujalie tufurahi daima katika kukutumikia, maana kama tunakutumikia daima wewe Mwumba wa mema yote, tunayo heri iliyo kamili siku zote”.

Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Danieli (12:1-3). Somo hili ni ufunuo wa Mungu kwa njia ya Nabii Danieli unaotujulisha kuwa baada ya kufa kuna ufufuko wa miili na katika ufufuko huo kila mmoja atahukumiwa ambapo walioishi vema watapata uzima wa milele na walioishi vibaya watapata aibu na madharau yao milele. Tunasoma hivi; “Tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele. Na walio na hekima watang’aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengine kutenda haki watang’aa kama nyota milele na milele.” Ni mwaliko kwetu sote wa kujichunguza na kujitafakari namna tunavyoishi; kama maneno na matendo yetu yana kibali machoni pa Mungu, ili siku hii ikifika, itukute tuko tayari, na tustahilishwe kuingia katika uzima wa milele.

Basi tuweke tumaini letu lote kwa Mungu kama la mzaburi katika wimbo wa katikati akisema hivi; “Mungu, unihifadhi mimi, kwa maana nakukimbilia Wewe. Bwana ndiye fungu la posho langu, Wewe unaishika kura yangu. Nimemweka Bwana mbele yangu daima, kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa. Kwa hiyo moyo wangu unafurahi, naam, mwili wangu nao utakaa kwa kutumaini. Maana hutaiacha nafsi yangu kuzimu, wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu. Utanijulisha njia ya uzima, mbele ya uso wako, ziko furaha tele. Na katika mkono wako wa kuume, mna mema ya tele” (Zab. 16:1, 5, 8-11).

Somo la pili ni la waraka kwa Waebrania (10:11-14, 18). Somo hili ni mwendelezo wa mafundisho yanayohusu ukuhani na sadaka za Agano la kale kuwa vimekamilishwa katika ukuhani wa Yesu Kristo kwa Sadaka yake msalabani. Tunaelezwa kuwa kurudiarudia kwa sadaka za makuhani wa Agano la kale kila mwaka ni kwa sababu sadaka hizo zilikuwa hafifu na hazikuweza kuondoa dhambi za watu. Lakini Sadaka ya Yesu ilitolewa mara moja tu na iliwatakasa watu wote kwa nyakati zote. Misa Takatifu ni Sadaka ile ile ya Yesu Kristo ambapo kila inapoadhimishwa vyema watu huondolewa dhambi zao na kutakaswa kama wakitimiza masharti na maagano ya sadaka hii ya Misa Takatifu.

Injili ni ilivyoandikwa na Marko (13:24-32). Sehemu hii ya Injili ni utabiri wa Yesu Kristo juu ya uangamizi wa Yerusalemu. Utabiri huu licha ya kuwa ulitimia, ujumbe wake ni kuwa kila mmoja atahukumiwa baada ya kufa kwa namna alivyoishi hapa duniani. Kwa walioishi kadiri ya mpango wa Mungu watapokea uzima wa milele na walioishi vibaya wataadhibiwa. Siku ya kifo cha kila mmoja inafananishwa na matukio ya ajabu na ya kutisha kama vile; jua kutiwa giza, mwezi kutotoa mwanga wake na nyota kuanguka chini. Katika hali hiyo, Yesu anawaambia wanafunzi wake kuwa watamwona Mwana wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu. Siku ya kifo cha kila mmoja inapotokea watu wanakuwa katika shughuli zao za kila siku na inatokea pasipo mtu kujua. Hivyo ili isitukute hatujajiandaa Yesu anatuambia tujiweke tayari mda wote kwa kutenda mema kila siku, “kwa kuwa katika saa tusiyoidhania “Mwana wa Adamu yuaja” (Mt 24:44). Anasisitiza kusema; Angalieni, kesheni (ombeni) kwa kuwa hamjui wakati ule utakapokuwapo” (Mk 13:33).

Lakini hukumu ni nini hasa? Hukumu ni kitendo cha kutoa haki kwa mtu kadiri ya matendo aliyoyafanya. Hukumu hii humpa mtu aidha zawadi au adhabu. Katika maisha ya kawaida hukumu yaweza kutolewa katika mahakama, baraza la wazee, wazazi katika familia, katika taasisi mbalimbali n.k. Kutenda na kutendeana mema ni haki ya kila mwanajamii; haki inapovunjwa kwa namna yoyote ile hukumu hutolewa kwa mvunjaji wa haki hiyo. Kwa mtazamo huu, Mungu aliye hakimu wa haki hutoa hukumu kwa mwanadamu kulingana na jinsi alivyoishi hapa duniani. Katika hukumu ya kwanza, Mungu anampa mtu haki yake kulingana na matendo yake na imani yake, mara baada ya kifo chake.

Katekisimu ya Kanisa Katoliki inasema hivi; “Kila mtu toka saa ya kufa kwake hupokea katika roho yake isiyokufa tuzo la milele katika hukumu ya pekee kuhusiana na maisha yake na Kristo au kwa kupitia utakaso au kwa kuingia moja kwa moja katika heri ya mbingu au kulaaniwa moja kwa moja kwa milele” (KKK1022.) Kumbe baada ya kifo roho ya mtu inahukumiwa kadiri ya matendo yake katika hali tatu. Kama iliishi vyema na kutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu huenda moja kwa moja mbinguni, kama iliishi vema, lakini kuna mapungufu machache, roho hiyo huhitaji kutakaswa na hivyo huenda toharani, na kama iliishi vibaya na haikutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu huhukumiwa na kwenda Jehanamu ambako moto wake na mateso yake ni ya milele. Ndiyo maana mababa wa Kanisa wanasema kuwa mara baada ya hukumu ya kwanza maisha ya paradiso au ya adhabu huanza. Na kuhusu hukumu ya mwisho, wanasema kuwa kitakachofanyika ni ukamilisho wa hukumu ya kwanza.  

Basi tujitahidi kuishi vyema huku tukijua ya kuwa ujio wa pili wa Kristo sio kwa ajili ya msamaha wa dhambi, bali ni kwa ajili ya kutoa hukumu. Hii ina maana kuwa hakutakuwa na nafasi ya kutubu wala kuomba msamaha. Ujumbe huu hauna lengo la kututisha na kutufanya tuishi kwa hofu na mashaka. Ndiyo maana Yesu mwenyewe anasema kuwa tukiona dalili za siku ya mwishom tuchangamke, tuviinue vichwa, “kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia” (Lk 21:28). Ndivyo Mtume Paulo katika waraka wake kwa waamini Watesalonike anavyotusihi tusiwe na wasiwasi kuhusu ujio wa pili wa Kristo akisema; “Mungu wa Amani, mwenyewe awatakase kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe muwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo” (1Thes 5:23).

Kumbe tunaalikwa kujitahidi kutenda mema na kuacha dhambi kila siku katika maisha yetu. Ndiyo maana mama Kanisa katika sala kuombea dhabihu anasali na kuomba hivi; “Ee Bwana, tunaomba sadaka tuliyotoa mbele ya macho yako wewe mtukufu, itupatie neema ya kukutumikia na kutuletea heri ya milele. Na katika sala baada ya komunyo anahitimisha maadhimisho ya dominika hii akisali hivi; “Ee Bwana, tumepokea mapaji ya fumbo hili takatifu; na sasa tunakuomba kwa unyenyekevu, hayo aliyotuamuru Mwanao tuyafanye kwa ukumbusho wake, yafae utuongezea mapendo”.

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika XXXIII mwaka B
15 November 2024, 17:24