Maaskofu wa Kenya. Maaskofu wa Kenya. 

Kenya:Askofu Mkuu wa Nairobi alitangaza:"Tunarudisha pesa zilizochangwa na Rais"!

Katika kanuni zilizoainishwa na Muswada wa Sheria ya Rufaa ya Kuchangisha Fedha za Umma wa 2024,inakataza kuomba au kukubali michango yoyote kutoka kwa watu mashuhuri wa kisiasa ili kuhakikisha kwamba makanisa yanasalia bila ushawishi wa kisiasa.Ni katika muktadha huo,Askofu Mkuu Anyolo wa Jimbo Kuu Katoliki la Nairobi,alitangaza kukataa michango iliyotolewa na Rais wa Kenya Bwana William Ruto na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja,kwa Jimbo Kuu la Nairobi.

Na Angella Rwezzula – Vatican.

Ilikuwa ni wakati wa ibada iliyofanyika Dominika tarehe 18 Novemba 2024 ambapo Rais  wa jamhuri ya Kenya, Bwana William Ruto alipotoa shilingi za Kenya 600,000 zenye thamani ya (euro 4,384.85) kwa kwaya ya parokia ya Kikatoliki ya Soweto na kuahidi shilingi milioni 2 nyingine zenye thamani ya (euro 14,628.39) kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya mapadre. Kwa mujibu wa "Fedha hizi zitarejeshwa kwa wafadhili husika"alisema Askofu Mkuu Philip Arnold Subira Anyolo, wa Jimbo Kuu Katoliki la Nairobi, alipotangaza kuwa amekataa michango iliyotolewa na Rais wa Kenya, Bwana William Ruto, na gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, kwa Jimbo Kuu la Nairobi. Rais pia aliahidi shilingi milioni 3 nyingine (euro 21,942.59)kununua basi la parokia hiyo, huku gavana Sakaja akitoa shilingi 200,000 (zenye thamani ya euro 1,459.76).

Kuendana na kanuni za kisheria za nchi na za Kanisa

Kwa njia hiyo sambamba na msimamo mkali wa hivi karibuni  wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya (KCCB) kuelekea sera ya Askofu Mkuu Anyolo aliamua tarehe 19 Novemba 2024 kukataa michango hiyo, akieleza kuwa "Kanisa Katoliki linafungwa na kanuni zilizoainishwa katika Muswada wa Sheria ya Rufaa ya Kuchangisha Fedha za Umma wa 2024, unaokataza michango hiyo ambayo inaweza kufifisha mipaka kati ya siasa na dini.

Sheria inakataza kuomba au kukubali michango kutoka watu mashuhuri wa kisiasa

Sheria hii inakataza kuomba au kukubali michango yoyote kutoka kwa watu mashuhuri wa kisiasa ili kuhakikisha kwamba makanisa yanasalia bila ushawishi wa kisiasa. “Fedha hizi zitarejeshwa kwa wafadhili wao. Zaidi ya hayo, Sh 3 milioni zilizoahidiwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Mapadre pamoja na mchango wa Bus la Parokia na Rais, zinakataliwa,” Askofu Anyolo alisema. "Kanisa linaitwa kudumisha uadilifu kwa kukataa michango ambayo inaweza kuhatarisha uhuru wake bila kukusudia au kuwezesha utajiri usio wa haki," akaongeza na kisha akamalizia kwa kusema kwamba "Kanisa lazima libaki kuwa shirika lisiloegemea upande wowote ili kutumikia kusudi lake la kweli katika jamii".

21 November 2024, 09:30