Kipindi cha Majilio:Mungu ni mwaminifu kwa ahadi zake
Na Padre Paschal Ighondo – Vatican
Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya Kwanza ya Majilio Mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa. Tumemaliza mwaka B katika liturujia ya Kanisa na tunaanza mwaka mpya C wa kiliturujia kwa kipindi cha majilio. Awali ya yote ni vyema tujikumbushe mambo muhimu ya kiliturujia ili kujiandaa vyema kwa kipindi hiki. Kwanza kabisa ni kuchukua tahadhani. Kuna uwezekano wa kufikiri na kudhani kuwa hakuna jipya katika kipindi hiki na kipindi kilichopita cha mwaka wa kiliturujia. Tukumbuke kuwa kila adhimisho la tukio lolote la kiliturujia, linapoadhimishwa na Mama Kanisa lina hali mbili. Kwanza kabisa ni kutukumbusha yaliyotokea katika historia ya wokombovu wetu. Na pili ni kuhuisha na kupyaisha maisha yetu ya kiroho. Kumbe kila mwaka wa kiliturujia ni mpya na wa pekee na hakuna unaofanana na mwingine. Hii ni kwa sababu kila mwaka unapyaisha na kuhuisha maisha yetu ya kiroho na uhusiano wetu na Mungu Baba yetu.
Basi daima tukumbuke kuwa matukio yote ya kiliturujia tunayoadhimisha zaidi ya kutukumbusha yaliyotokea zamani, yanafanya sehemu ya maisha yetu na yanatufanya tuonje upendo wa Mungu katika mafumbo yanayoadhimishwa katika kila hatua ya maisha yetu hapa duniani tunapoelekea maisha ya umilele mbinguni. Kumbe kama maadhimisho ya kiliturujia hayachukui nafasi katika maisha yetu. Basi yatabaki kuwa ni kumbukumbu tu na hayawezi kutupatia wokovu. Sherehe na vigelegele vitabaki kuwa ni mambo ya nje yasiyogusa maisha yetu. Basi tusikianze kipindi hiki kwa mazoea, bali kwa unyenyekevu, tufungue macho na masikio ya mioyo yetu tuweze kujichotea neema na baraka zitokanazo na kipindi hiki.
Baada ya huo utangulizi, sasa tujikumbushe nini maana ya Majilio. Neno Majilio lina maana mbili. Kwanza kabisa zamani lilitumiwa na wapagani kumaanisha ujio wa miungu yao, katika siku maalumu ambapo walizitoa sanamu za miungu yao kutoka mahali zilipohifadhiwa ili kuzisujudia na kuziabudu, ziwapatie baraka na fanaka. Pili lilimaanisha mda wa maandalizi kwa “ziara rasmi ya mfalme”. Wakristo wa mwanzo walichukua maana hizi mbili kwanza kumaanisha ujio wa Mungu duniani aliyejifunua na kujidhihirisha katika nafsi ya Mwanae wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo. Na pili kumaanisha kipindi cha maandalizi ya ziara ya Mungu kwetu sisi wanadamu. Kwetu sisi kipindi hiki ni cha kufanya maandalizi ya kumpokea Mungu anayekuja kwetu katika nafsi yake ya pili, Mungu Mwana, Bwana wetu Yesu Kristo, akiwa katika umbo na hali ya kibinadamu kwa njia ya umwilisho mwilini mwa Mama Bikira Maria.
Kipindi hiki kimegawanywa katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza huanza kwa Dominika ya kwanza ya majilio na huishia tarehe 16 Disemba. Katika sehemu hii, masomo yanatuelekeza kutafakari ujio wa pili wa Kristo katika utukufu wake. Na sehemu ya pili ambayo huanza tarehe 17 hadi 24 Disemba, masomo yake yanatuongoza kutafakari juu ya ujio wa kwanza wa Yesu Kristo na kutukumbusha zile siku Waisraeli walipokuwa wakimsubiri aje. Ni wakati wa matayarisho ya sikukuu ya kuzaliwa kwake Kristo katika historia ya maisha.
Ujumbe wa masomo ya dominika hii ya kwanza ya majilio inayofungua sehemu ya kwanza ya kipindi hiki unahusu habari za ujio wa pili wa Yesu Kristo katika utukufu. Ndivyo unavyoashiria wimbo wa mwanzo ukisema; “Ee Bwana, nakuinulia nafsi yangu, ee Mungu wangu, nimekutumainia wewe, nisiaibike, adui zangu wasifurahie kwa kunishinda. Naam, wakungojao hawataaibika hata mmoja.” Naye mama Kanisa akiongozwa na tumaini hili katika sala ya mwanzo anatuombe kwa Mungu akisali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi, tunakuomba utujalie sisi watumishi wako neema hii, ya kwamba Kristo atakapokuja, tumlaki na matendo mema, atuweke kuume kwake, tustahili kuupata ufalme wa mbinguni.
Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Yeremia (Yer. 33:14-16). Somo hili linahusu uaminifu wa Mungu katika ahadi zake. Mungu kwa kinywa cha Nabii Yeremia anaahidi kuwaletea watu wake Mkombozi atakayewakomboa na kuwaletea amani na haki. Hiki kilikuwa ni kipindi ambapo mji wa Yerusalemu ulivamiwa, ukateketezwa na watu wake kuchukuliwa mateka na kupelekwa uhamishoni Babeli mnamo mwaka 587 KK, kwa sababu ya kuasi na kukengeuka kwao. Hivyo Yeremia anawaasa na kuwaita wamrudie Mungu, maana ni mwenye huruma atawasikiliza na kuwaokoa na taabu zao. Ni katika muktadha huu mzaburi katika wimbo wa katikati anasema hivi; “Ee Bwana, nakuinulia nafsi yangu. Ee Bwana, unijulishe njia zako, unifundishe mapito yako, uniongoze katika kweli yako, na kunifundisha. Bwana yu mwema na mwenye adili, kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia. Wenye upole atawaongoza katika hukumu, na kuwafundisha njia yake. Njia zote za Bwana ni fadhili na kweli, kwao walishikao Agano na shuhuda zake. Siri ya Bwana iko kwao wamchao, naye atawajulisha agano lake (Zab. 25: 1, 4-5, 8-9, 10, 14). Licha ya kuwa ahadi hii ilitimia kwa waisraeli kurudi kutoka utumwani Babeli. Uaminifu wa Mungu kwa ahadi yake ya wokovu kwa watu wote, ulitimia kwa ujio wa Yesu Kristo, katika historia ya maisha ya mwanadamu na unaendelea kila tunapofungua mioyo yetu kumpokea katika maadhimisho ya kisakramenti katika nyakati mbalimbali za maisha yetu.
Somo la pili ni la waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wathesalonike (1Tes. 3:12-13; 4:1-2). Somo hili ni pongezi za Mtume Paulo kwa Wathesalonike kwa bidii yao ya kuiishi imani kwa upendo. Mtume Paulo aliazisha hii jumuiya wakati wa safari yake ya pili ya kimisionari mnamo mwaka 50 BK (Mdo 17:1-11). Kihistoria, mji wa Thesalonike ulioko kaskazini-mashariki mwa Ugiriki, ulikuwa chini ya utawala wa Warumi kuanzia mwaka 140KK. Mji huu ulikuwa maarufu kwa kuwa makao makuu ya mkoa wa Makedonia, kwa sababu ulibahatika kuwa na bandari na barabara nzuri iliyounganisha nchi za Magharibi na Mashariki. Wakazi wake walijumuisha Wagiriki, Warumi na Wayahudi. Mataifa haya yote yaliingiza imani na madhehebu ya dini zao. Mtume Paulo alipofika, alihubiri katika Sinagogi la Wayahudi. Watu wengi walipokea ujumbe wake. Lakini viongozi Wayahudi katika Sinagogi waliona wivu na kufanya ghasia za kumwondoa katika mji huo. Paulo na wasaidizi wake waliondoka, wakaendelea na safari ya kutangaza habari njema ya wokovu, wakapitia mji wa Bera hadi mji wa Athene. Toka mjini Athene Paulo alimtuma Timotheo aende Thesalonike ili akaone na kutathimini maendeleo ya mbegu ya imani aliyoipanda.
Wakati Timoteo anaelekea Thesasonike, Paulo aliendelea na safari mpaka mji wa Korintho na kumsubiri mjumbe wake Timoteo arudi toka Thesalonike. Baada ya kujionea hali halisi ya mbegu ya imani huko Thesalonike, Timoteo alienda Korintho kwa Paulo na kumpa taarifa kuwa waamini waliendelea kushika imani aliyoipanda licha ya mateso wanayoyapata. Lakini pia baadhi yao walipata huzuni kuona wenzao wanakufa kabla ya kushuhudia ujio wa pili wa Yesu Kristo. Hali hii ilimsukuma Paulo awaandike barua hii: Kwanza, kuwashukuru na kuwapongeza kwa kuipokea na kuendelea kuizingatia imani hata katika mazingira magumu. Pili, kuwatuliza na kuwafariji waliofiwa na ndugu zao akiwaeleza habari za ujio wa pili wa Yesu Kristo ambapo waamini wote, wazima na wafu, watahukumiwa na kuurithi uzima wa milele. Na tatu, kuwaasa waamini waepukane na utovu wa maadili. Basi nasi tunapaswa kuishi kwa upendo na amani katika kipindi hiki cha majilio ili Kristo ahuishwe ndani mwetu kama anavyosisiza Mtume Paulo akisema; “Bwana na awaongoze na kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi na kwa watu wote, kama vile sisi nasi tulivyo kwenu; apate kuifanya imara mioyo yenu iwe bila lawama katika utakatifu mbele za Mungu Baba yetu, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo pamoja na watakatifu wake wote.”
Injili ni ilivyoandikwa na Luka (Lk. 21:25-28, 34-36). Sehemu hii ya Injili inatueleza mambo ya kutisha na kuogofya yatakayotokea wakati wa ujio wa pili wa Yesu Kristo. Mambo na matukio hayo ni pamoja na dhiki, uvumi wa bahari na msukosuko wake, kuvunjika mioyo kwa hofu ya kuona mambo yanayoupata ulimwengu. Ni wazi kuwa kunapokuwa na tafrani kama hizo watu hukimbia kujificha. Lakini Yesu anatuambia kuwa mambo hayo yanapoanza kutokea, tuchangamke, tuviinue vichwa vyetu. Kwanini? Kwa sababu ukombozi wetu umekaribia. Lakini ili tuwe katika hali hii ya kuchangamka na kuviinua vichwa vyetu, lazima mioyo yetu isiwe imeelemewe na ulafi, ulevi, na masumbufu ya maisha haya, kwa sababu “siku ile itakuja ghafula. Hivyo basi, tunapaswa kukesha, kuwa tayari wakati wote.
Basi kipindi hiki tujitahidi kutathimini matendo yetu ili siku ya kiyama itakapowadia, tusiiogope kwani siku hiyo ndio mwanzo wa maisha mapya ya huko mbinguni. Mwaliko huu unapotolewa kipindi hiki cha majilio, ni kutukumbusha kuwa maisha yetu yote ni kipindi cha majilio, mwendelezo wa kumsubiri Kristo hadi atakapokuja tena kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu kwa uzima wa milele. Ndiyo maana katika sala ya kuombea dhabihu mama Kanisa anasali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba uzipokee dhabihu tunazokutolea kutokana na mapaji yako. Umetujalia mapaji haya tuyatumie kwa ajili ya ibada hapa duniani, yatupatie tuzo la ukombozi wa milele”. Na katika sala baada ya komunyo anahitimisha maadhmisho ya dominika hii kwa kutuombea akisali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba mafumbo haya tuliyoadhimisha yatufae sisi tunaotembea katika malimwengu, nawe utufundishe kupenda mambo ya mbinguni na kuzingatia ya milele”. Nawatakia mwanzo mwema wa mwaka mpya wa kiliturujia na majilio mema tujiandae vyema kiroho ili Kristo aendelee kuzaliwa ndani ya mioyo yetu siku baada ya siku na kutuhuisha katika maisha ya kiroho kwa kutuweka karibu zaidi na Mungu Baba yetu.