Tafuta

2024.11.15 Injili ya Dominika ya  XXXIII Mwaka  B 2024.11.15 Injili ya Dominika ya XXXIII Mwaka B 

Kristo anapotupatia ishara za mwisho wa nyakati,sisi tusali ili mtikisiko usitutokee!

Wanadamu tunakabiliwa na hukumu ya kwanza(binafsi)na hukumu ya pili(ya mwisho).Ya ni tendo la Mungu kumpa mtu haki yake kulingana na matendo na imani yake mara baada ya kifo(Lk 23:43; KKK:1022),hapa ni roho ya mtu pekee ndiyo inayohukumiwa.Hukumu ya mwisho itatanguliwa na ufufuko wa wote,wenye haki na wasio haki (Mdo 24:15).Roho zitaungana na miili yake halisi,walio wema watatengwa kwa uzima wa milele,na waovu kwa hukumu ya milele.Ufalme wa Mungu utajipatia utimilifu.

Na Padre Joseph H. Luwela – Vatican.

Mpendwa msikilizaji na msomaji wetu wa tafakari kutoka hapa Radio vaticano, Katika Dominika za mwishoni mwa mwaka Mama Kanisa hutualika kutafakari ‘mwisho wa dunia’. Na leo Dominika ya 33 tunakumbusha tena ujumbe huu kuwa Ni wakati mzuri kuchunguza mienendo yetu na hivi kujiandaa vema kwa ujio wa pili wa Kristo. Kutoka kina cha upendo na huruma yake anatudokeza juu ya majira hayo na nini kitautangulia ujio huo ili isije kuwa shida ya ghafla kwa tulio wengi. Tujipange vema ili siku hiyo itakapowadia tustahili kuingia mbinguni.

Wanadamu tunakabiliwa na hukumu ya kwanza (binafsi) na hukumu ya pili (ya mwisho).Hiyo ya kwanza ni tendo la Mungu kumpa mtu haki yake kulingana na matendo na imani yake mara baada ya kifo (Lk 23:43; KKK: 1022), hapa ni roho ya mtu pekee ndiyo inayohukumiwa. Hukumu ya mwisho itatanguliwa na ufufuko wa wote, wenye haki na wasio haki (Mdo 24:15). Roho zitaungana na miili yake halisi, walio wema watatengwa kwa uzima wa milele, na waovu kwa hukumu ya milele (Yn 5:28-29). Ufalme wa Mungu utajipatia utimilifu wake, wenye haki watatawala na Kristo wakiwa wametukuzwa mwili na roho.

UFAFANUZI

Jambo hili halikuwa geni kwa waisraeli, tangu manabii wa kale hadi Yohane Mbatizaji waliihubiri hukumu hii (Dan 7:10, Mal 4:1-3, Mt 3:7-12). Katika somo I (Dan 12:1-3) tunachota dhana ya ufufuko wa miili ili ihukumiwe pamoja na roho. Kristo katika Injili pia anaeleza itakavyokuwa na matukio ya awali (Mk 13:24-32) kama vile jua kutiwa giza, mwezi kutotoa mwanga, nyota kuanguka na nguvu za mbinguni kutikisika. Jua, mwezi na nyota vilichukuliwa kama miungu, viliabudiwa na kufukiziwa uvumba. Vinawakilisha ulimwengu wa pepo, uovu na ubaya, nguvu za giza, uadui na upinzani, ulimwengu wa fujo, vurugu na ghasia. Lengo la Kristo sio kututisha bali kutufariji na kutupa matumaini kuwa katika Yeye vita imekwisha. Mwana wa Adamu atakuja katika mawingu kwa nguvu na utukufu mwingi, atausimika imara utawala wake na kuondoa kabisa hila za adui mwovu na kutupatia hali njema tena.

Mkristo hufurahi, inua uso wako… katika mashaka na dhiki, maumivu, sintofahamu na kukata tamaa, ujipe moyo, simama imara sababu nabii Daniel anatuambia yupo Mikaeli Jemadari Mkuu wa majeshi ya mbinguni kutupigania, mbele yake Ibilisi ni mnyonge kabisa… wana wa Mungu tutang’aa kama mwangaza wa anga na hao waongoao wengi kutenda haki watang’aa kama nyota milele na milele. Kristo anapotupatia ishara za mwisho wa nyakati, sisi tusali ili mtikisiko huo usitokee kwetu.  Jua lisitiwe giza nyumbani kwako baba, mwezi usizimike nyumbani mwako mama na nyota zisianguke kwako kijana. Ni giza baya pale ambapo Kanisa, Polisi, Serikali ya kijiji na majirani wanatingwa ili kutatua migogoro ya nyumbani kwangu ambako kila siku ni shida, kila wiki ni kilio. Jua linatiwa giza nyumbani kwetu pale ndoa zinapopimwa kwa mambo ya kimwili tu, kunapokuwa na uholela baina ya wanafamilia, ukatili na hata ushirikina.

Ndoa imebeba mafumbo matakatifu hivi kuihusianisha na ushirikina, talaka, ubaridi, kutosali, mawasiliano mabovu nk haitakiwi. Badala yake jua liangaze nyumbani kwetu kwa kuishi kitakatifu, utii kwa mapenzi ya Mungu, sala, unyenyekevu, upendo, huduma, kujali, usafi wa moyo, uvumilivu, kazi, ujasiri, huruma na msamaha, utulivu wa ndani na zaidi sana kuishi katika Mungu. Jua linakuwa giza na mwezi hautoi nuru pale wahudumu wa Neno tunaposisitiza vitisho na hofu ya hukumu, hofu ya shetani na kuwakatisha watu tamaa badala ya kuwafariji na kuwajengea ujasiri wa kuishi mustarehe katika Kristo Mfufuka. Hakuna giza hapa, jua halizimiki, mwezi haupotezi nuru na nyota hazianguki, jua linaangaza maisha yako mkristo jipige kifuani ukaenende katika amani ya Kristo.

Umewahi kutikiswa? ni nini kilichokutikisa? unatamani familia ya furaha lakini huipati? unapenda marafiki lakini huna rafiki wema? ungependa kusoma lakini huna nguvu? kusali lakini haujui sala ipi ndio bora? unapenda amani na utulivu lakini jirani wanakukosesha? unasingiziwa? unasengenywa? Hupandi daraja wala cheo? Biashara haiendi? umetikiswa na kuugua, kuuguliwa, kufiwa, kufilisika na kuishi katika familia isiyo na upendo? jipe moyo, Kristo anatangaza leo ushindi wake wa siku za mwisho. Wakati jua linatiwa giza huko mtaa wa pili wewe kwako unashaini tu, wakati mwezi unazimika mtaa wa pili kwako kunashaini tu, wakati nyota zinaanguka mtaa wa pili kwako zinang’aa na baraka ya Mungu inakufuata… mwamini Kristo utakuwa heri na baraka tele.

Hata hivyo ahadi hii na furaha ya ushindi inatudai kazi kidogo... kwamba tusilale usingizi, tupigane kufa na kupona kuhakikisha tunaingia katika kitabu cha uzima. Nabii Daniel anasema watakaookolewa ni wale tu watakaoonekana wameandikwa humo... tulio wengi tumeandikwa katika dubwana liitwalo mitandao ya kijamii kila mmoja wetu hapa hajaachwa salama yaani ni muhanga ndio kusema wachachesanaaaa wanaonusurika naweza kusema hapa kwa kimombo( there are natives and migrants in ) kizazi kinachokimbizana na teknolojia na wale wa waliozaliwa miak ya nyuma lakini nao sasa wanauthubutu kwenye whatsapp, insta na fb...  tukumbuke jamani ni muhimu kuwemo katika orodha ile ya wateule wa Mungu, ndio watakatifu wenye kuizunguka Altare ya Bwana… tutamani kuingia katika waliosajiliwa ndani  ya kitabu kile... haya na tujiangalie, tukeshe, tuombe kwa kuwa hatujui wakati ule utakapokuwapo, “na hilo niwaambialo ninyi nawaambia watu wote, kesheni.”

Tafakari ya Dominika 17 Novemba 2024
16 November 2024, 11:04