Watanzania Wakatoliki,Italia,Padre Lubuva:kama Kanisa la kisinodi tuwe mashuhuda wa kweli na sura halisi ya Kanisa!
Na Padre Victory B Tluway na Angella Rwezaula – Vatican.
Jumuiya ya Watanzania wakatoliki nchini Italia, kwa upande wa Umoja unaojumuisha Mapadre, Masista, Mabruda na mafrateli (wa mashirika) na waseminari ambao wako nchini Italia kwa ajili ya masomo na wengine katika utume mbalimbali walikutana pamoja katika Chuo cha Kipapa cha Mtakatifu Paulo jijini Roma, Jumamosi tarehe 9 Novemba 2024, kama sehemu ya matukio mbali mbali ya kawaida ya mwaka hasa awali ya yote misa kwa nia ya kumshukuru Mungu kwa mwaka uliopita na kuanza mwaka mpya wa masomo masomo 2024/2025. Misa pia ilikuwa kuwaombea ndugu zetu marehemu hasa wale wa wanajumuiya wenzetu waliokufa mwaka huu na marehemu wote katika mwezi huu wa Novemba wa kuwakumbuka waliotangulia mbele ya haki.
Misa hiyo iliongozwa na Padre Honest Lubuva kutoka Jimbo Kuu la Dodoma, Tanzania na ambaye ni Mwalimu na Mlezi katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Paulo Mtume, Tabora, kwa sasa yupo Roma kwa ajili ya shughuli za kitaaluma na aliweza kujumuika na watanzania wenzake. Katika Mahubiri yake kwa kuongoza na masomo ya Injili ya siku na vile vile kutazama jumuiya hii Padre Lubuva alijikita na mada ya UMOJA. Katika hilo alisisitiza kwa wanajumuiya hao kuwa Kanisa ni moja Takatifu katoliki la mitume. Kwamba “sisi sote tumetoka katika majimbo tofauti ya Tanzania lakini tukiwa huku ughaibuni tunatambulika kama watanzania, tuendelee kulinda na kutunza heshima ya Kanisa.” Padre huyo akiendelea alisema kuwa “tuwe Mitume wa kimisionari; akimnukuu Papa Francisko kuwa ‘sisi sote tunapaswa kuwa mitume wa kupeleka habari njema, ujumbe wa amani.’ Kwa njia hiyo “Tunaalikwa kujifunza kutoka kwa Yule anayetutuma yaani Yesu Kristo ili tuhubiri yaliyo ya Kristo kwa watu wake.”
Katika kuendelea na mada hiyo ya umoja, Padre Lubuva alisema kuwa “Kristo ni Kichwa na Kanisa ni Mwili wake; kichwa daima kinabeba maono na mwili unatekeleza maono,” kwa njia hiyo aliwataka “watanzania kubeba maono ya Kanisa kwa kumsikiliza Kristo ambaye ni Kichwa cha Kanisa. Nasi kama Kanisa la kisonodi tunaalikwa kuwa mashuhuda wa kweli na sura halisi ya Kanisa linaloishi na linaloendelea, likiwafundisha waamini wake mafundisho sahihi ya Imani.”
Kikao cha Umoja wa Watanzania
Kama ilivyo desturi ya kikao kwa kawaida wanajumuiya wanapokutana hujadili masuala yanayohusu umoja wao na kuweka mipango yao ya mwaka hasa katika kusaidiana kama wakristo na kujengana kwa masuala yanayohusu maisha ya kiroho na kiimani kama watanzania.
‘Mmekwenda kuchuma mrudi na mliyo chuma ugenini’
Wakati wa mkutano, vile vile Padre Honesti Lubuva alitoa neno la kuwashukuru sana Jumuiya ya watanzania na kueleza furaha yake ya bkukutana na wanafunzi wake ambao aliwafundisha Seminari Kuu ya Tanzania. Pia aliwataka kukumbuka kurudi kusaidia katika malezi na kufundisha katika seminari. Kwa kukazia alitumia maneno ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyependa sana kusema: “Mmekwenda kuchuma, na mje nayo mliyoyachuma huko ugenini” ili kusaidia jamii ya watanzania. Tukio hilo lilimalizika kwa chakula na sala na kurudi kila mmoja katika sehemu yake.