Tafuta

Maaskofu Nchini Kenya. Maaskofu Nchini Kenya. 

Kenya Maaskofu:Watu wanapoteza imani na serikali;tunahitaji kurejesha matumaini kwa taifa!

"Tunajisikia kulazimishwa kuelezea wasiwasi wetu kuhusu hali mbaya ya kisiasa ambayo imeathiri nchi yetu."Walisema hayo Maaskofu wa Kenya katika taarifa yao yenye kichwa:"Turudishe matumaini Kenya",iliyowasilishwa katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika tarehe 14 Novemba 2024.“Maaskofu pia walizindua ombi kwa Wakenya wote kuiombea Kenya hasa waamini wakatoliki ambao wamealikwa kujiandaa na Jubilei 2025 kama 'Mahujaji wa matumaini.'

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baraza la Maaskofu katoliki nchini Kenya (KCCB) imeingilia kati kwa mara nyingine kuelezea wasiwasi mkubwa wa idadi ya watu katika kukabiliana na hali ya vurugu za kisiasa ambazo nchi imekuwa ikiishi kwa miezi kadhaa, kufuatia maandamano ya kupinga sheria ya fedha na gharama kubwa ya kuishi. "Migogoro ya kisiasa imezua mivutano isiyo na sababu na imezidisha migawanyiko kati ya watu wetu. Licha ya utulivu tulionao, kuna wasiwasi mwingi na watu wengi wanapoteza imani na Serikali. Walitoa maoni katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika tarehe 14 Novemba 2024 kwa kuongoza na  mada “Turudishe matumaini Kenya”, kwa sababu "Tunajisikia kulazimishwa kuelezea wasiwasi wetu kuhusu hali mbaya ya kisiasa ambayo imeathiri nchi yetu"walisema  maaskofu hao.

Visa vya mara kwa mara vya utekaji nyara na ufisadi

Baraza la Maaskofu Kenya (KCCB) kwa hiyo linakosoa “kutokujali na kutowajibika kunakooneshwa na tabaka la kisiasa la Kenya ambalo linajumuisha wabunge miongoni mwa wanaolipwa vizuri zaidi duniani, na hali ya uwongo na ufisadi ambayo inadhihirisha mfumo wa kisiasa wa kitaifa.” Maaskofu walitangaza kuwa "wameshtushwa na visa vya mara kwa mara vya utekaji nyara, kutoweka, kuteswa na mauaji ya Wakenya, wakikumbuka familia nyingi zilizoshtushwa na kifo, kujeruhiwa au kutoweka kwa watoto wao kwa kushiriki katika maandamano ya Kizazi Z."

Ni nani anayeteka watu nyara?

Kinachotisha zaidi walisisitiza ni “ukuaji wa mauaji ya wanawake. Hili limesababisha mshtuko mkubwa, hasira na chukizo.” Na wakirejea watu waliopotea,  Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Kenya (KCCB) linauliza: "Ni nani anayewateka nyara watu hawa? Je, serikali haina uwezo wa kukomesha utekaji nyara na mauaji haya?" Baraza la KCCB linatoa wito kwa serikali kuheshimu Katiba ambayo katika kifungu cha 26 inalazimu Serikali kutetea maisha ya kila binadamu. Katika ngazi ya kiuchumi, Maaskofu walikumbuka "maswala ambayo hayajatatuliwa ambayo tumezungumza na serikali hivi karibuni , ushuru wa kupindukia wa Wakenya, ongezeko la vibali vya kazi ya wamisionari, ukosefu wa ajira kwa vijana." Hatimaye Maaskfu hao  wanabainisha kuwa “Tunamshukuru Mungu kwa kuweka nchi katika umoja licha ya misukosuko ya kisiasa na kijamii" lakini wakati huo huo walizindua  ombi kwa Wakenya wote kuiombea Kenya, na hasa wamini wa Kikatoliki ambao wamealikwa kujiandalia Jubilei ya 2025 inayoongozwa na kauli mbiu ya "Mahujaji wa Matumaini."

16 November 2024, 12:37