Tafuta

2023.11.24 Kristo Mfalme wa Wafalme. 2023.11.24 Kristo Mfalme wa Wafalme. 

Sherehe ya Bwana Yesu Kristo Mfalme:Hamu ya Kristo ni sote tuingie&tufurahie uzuri wa utawala wake!

Kristo ni Mfalme wa utukufu,ufalme wake unaanza ndani ya mioyo iliyonakshiwa kwa pendo na roho zilizotakatifuzwa kwa neema.Ni utawala unaodhihirishwa na wale ambao maisha yao yamegeuzwa kikamilifu kwa utii kwa mapenzi ya Mungu,duniani kama mbinguni,zaidi sana ni utawala unaojipatia ukamilifu wake kisha kumshinda Ibilisi na malaika wake.Kwa njia hiyo:Ufalme wangu si wa ulimwengu huu.”(Yh 18:36).

Na Padre Joseph H. Luwela – Vatican.

Mpendwa msikilizaji na msomaji wa Tafakari kutoka Radio Vatican, huwa wanasema kwamba 'hakuna lenye mwanzo likakosa mwisho'... kwa Neema ya Mungu kipindi cha liturujia cha Mwaka B kadiri ya mpango wa Mama Kanisa takatifu kinatamatika katika Juma hili la XXXIV, na kwa hiyo tunasema asante kwa kuwa nasi kwa mwaka mzima wa liturujia yaani MWAKA B. Ni mengi tumelishwa na kuboreshwa, pia yapo tuliyoshindwa kufanya kwa namna mbalimbali lakini leo tunayakabidhi kwa Kristo Mfalme wa Ulimwengu ili aendelee kutawala,  na bila kusahau,  napenda kukumbusha yale tunayofunzwa na Mama Kanisa katika Kanuni ya IMANI, kwamba "Kristo ni Mungu kweli na mtu kweli," kwamba: "Yumo mzima katika maumbo ya mkate na divai," kwamba "Roho Mtakatifu  anatoka kwa Baba na Mwana," kwamba "Bikira Maria Mtakatifu ni Mama wa Mungu, Bikira daima na ametwaliwa mbinguni mwili na roho" ni baadhi ya mafundisho ya imani yaliyopingwa na kupitia migogoro mikubwa… lakini hakujawa na ubishi uwao wote juu ya Kristo kama Mfalme na hivi makundi yote ya wakristo yanakiri kwamba "Kristo Yesu ni Mfalme wa Mbingu na Dunia.!

UFAFANUZI

Mungu Mwenyewe alikuwa Mfalme wa Israeli (Theocracy) hadi pale watu wake, kupitia nabii Samuel, walipodai mfalme wa kibinadamu wakapewa Sauli mwana wa Kishi (1 Sam 8 - 10) na kufikia kipeo chake nyakati za wafalme Daudi na Sulemani kwa kuunda dola imara ikiunganisha kabila 12 za Yakobo. Baadaye Ufalme huo ulipita misukosuko mingi na kugawanyika kuwa na ufalme wa Israel (kaskazini) na ufalme wa Yuda (kusini)... Utawala huu ulikuwa ni mfano wa utawala mkubwa zaidi wa baadaye chini ya Daudi mkubwa zaidi, Kristo Yesu Bwana wetu. Mbele ya Pilato Kristo hakuukana ufalme wake lakini alijibu utawala wake si sawa na wa Kaisari, utawala wa kujitwalia kwa nguvu, hila au dhuluma au kwa demokrasia bali ni ufalme ulio ndani mwake kwa asili, ufalme wa mbinguni ambao Yeye amekuja duniani ili kuupanda…

Kristo ni Mfalme wa utukufu, ufalme wake unaanza ndani ya mioyo iliyonakshiwa kwa pendo na roho zilizotakatifuzwa kwa neema… ni utawala unaodhihirishwa na wale ambao maisha yao yamegeuzwa kikamilifu kwa utii kwa mapenzi ya Mungu, duniani kama mbinguni… zaidi sana ni utawala unaojipatia ukamilifu wake kisha kumshinda Ibilisi na malaika wake. Ni hamu yake Kristo sote tuuingie, tuushiriki na tuufurahie uzuri wa utawala wake, “Baba hao ulionipa, nataka wawe pamoja nami popote nilipo, wapate kuutazama utukufu wangu ulionipa” (Yh 17:24). Sala hii imewanufaisha wengi, nao ni umati usiohesabika wakifurahia matunda yake mbinguni.

Kristo Mfalme
Kristo Mfalme

Watawala wa kidunia hupimwa kwa uwezo wao wa diplomasia, kudhibiti maasi, miundo mbinu, nguvu ya dola na wengine hutamani kuogopwa, kuhofiwa na kudumu madarakani kwa daima na hivi kuzungukwa na ulinzi usiomithilika... wapo waliojipatia madaraka kwa udanganyifu, ubabe, wizi na hata kwa vita na damu. Utawala wao hautazami sana haki na ukweli bali sifa na umaarufu wa kisiasa… hawa wana jambo la kujifunza kwa Kristo Mfalme ambaye ni Mfalme mwenye nguvu na amri juu ya majeshi yote ya malaika lakini ni mpole na mnyenyekevu, amepanda punda naam mwanapunda mtoto wa punda (Zek 9:9, Mt 21:5). Kwa kuviweka viumbe vyote chini ya utawala wake, Kristo amemtolea Mungu Mkuu ufalme wa milele na wa ulimwengu wote… ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na wa neema, ufalme wa haki, mapendo na amani (rej. Prefasio ya leo), ufalme wa usawa, upendo na msamaha… hakika anasadifu maono ya nabii Daniel

katika somo La kwanza kutoka (Dan 7:13-14) ajapo uwinguni kwa nguvu na utukufu na watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote watamtumikia na mamlaka yake ni ya milele, Yeye aliye Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi… utukufu una Yeye hata milele na milele, amina (Somo II – Ufu 1:5-8). Tumshukuru Mungu kwa kutushirikisha ufalme wake, kutufanya wana wa Mfalme na warithi pamoja naye. Kama vile tunavyowasikia na kuwatii wakuu wa kidunia basi tumtii na tumsikilize Yeye aliye juu yao wote. Neno lake ni amini, hekima yake haielezeki, busara yake ni kuu na mkononi mwake mna kuwawezesha wote. Moyo wa Mfalme huyu mtukufu unatamani mioyo ya watu wote ifanane na Moyo wake. Tujibidishe basi kutembea katika njia yake tukiyashika vema, bila kugeuka mkono wa kushoto au wa kuume, mausia yake tukienenda katika uwajibikaji upasao, uadilifu na upendo kamili naye Mungu Mkuu, katika Mwanaye Mfalme, atatubariki na kutuinua, mosi hapa duniani halafu katika furaha za mbinguni… amina!

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya XXXIV:Kristo Mfalme
23 November 2024, 09:22