Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme:Ufalme wake si wa Dunia hii,bali ni wa Mbinguni!
Na Padre Paschal Ighondo – Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 34 ya mwaka B wa kiliturujia Kanisa kipindi cha kawaida. Hii ni Dominika ya mwisho wa mwaka wa kiliturujia na dominika ijayo tunaanza mwaka mpya wa kiliturujia, mwaka C kwa dominika ya kwanza ya majilio. Kadiri ya utaratibu wa Mama Kanisa, Jumapili hii tunaadhimisha Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme. Itakumbukwa kuwa katika Kanisa kuna baadhi ya sherehe, kadiri ya utaratibu wake zilipaswa ziadhimishwe ndani ya Juma Kuu. Lakini kwa sababu za kichungaji, sherehe hizo zinahamishiwa katika kipindi mara baada ya Pasaka au katika kipindi cha mwaka. Moja ya sherehe hizo ni Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme iliyopaswa kuadhimisha siku ya Dominika ya Matawi. Lakini kutokana na mazingira ya liturujia ya siku hiyo yalivyochanganyika kwa furaha na huzuni ambapo katika sehemu ya kwanza ni maandamano ya Yesu Kristo kuingia Yerusalemu kwa shangwe kama Mfalme, umati mkubwa wa watu ukimshangilia na kumlaki, wakishika matawi mikononi na kama walivyofanya nyakati zile kule Yerusalemu. Sehemu ya pili inahusu historia ya mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo inayoonesha jinsi alivyokamatwa na kutiwa nguvuni, mchakato mzima wa kesi yake ulivyoendeshwa hadi kuhukumiwa na kuteswa mpaka kufa kifo cha aibu msalabani. Na sehemu ya tatu ni liturjia ya kawaida kama Dominika ya Kwaresma.
Kutokana na mwingiliano huo wa furaha na huzuni katika siku ya Dominika ya Matawi, Kanisa limeihamishia sherehe hii kutoka Dominika ya Matawi na kuiweka katika Dominika ya 34 ya mwaka ili kupata wasaa mzuri wa kumtafakari Kristo kama Mfalme wetu wa kweli, Mfalme asiyeeleweka kwa watu wake, ndiyo maana alihukumiwa, akateswa, akasulubiwa na kuuawa kwa kifo cha aibu msalabani. Lakini kwa kifo chake kilivyokuwa cha ajabu watu walishuhudia na kukiri ukuu wa ufalme wake na kusema hakika huyu alikuwa mwana wa Mungu. Kihistoria sherehe hii iliidhinishwa na Baba Mtakatifu Pius wa XI mwaka 1925 akiuambia ulimwengu kwamba: “Dunia haiwezi kuuepa utawala wa Kristo kama inataka kubaki salama.” Kwa kuwa tangu mwanzo, wakristo waliogopa kumwita Kristo Yesu Mfalme, kwa kuhofia kumfananisha na wafalme wa dunia hii, Baba Mtakatifu Pius XI alisisitiza kuwa; “wakristo tusiogope wala tusione aibu juu ya kumkiri Kristo kuwa Mfalme, Bwana Mwokozi na Mkombozi wetu kwani Pilato alipomwambia; Wewe u Mfalme basi? Yesu alijibu; Wewe wasema, kwa kuwa mmi ni mfalme” (Yn.18:37).
Kwa mwaka mzima Kanisa limetukumbusha ya kwamba: Kristo ni Mfalme na Mchungaji mwema wa wanadamu wote kwa maisha ya sasa hapa duniani na maisha yajayo mbinguni baada ya kufa; kwani Yeye ndiye Mfalme, hakimu na Mwokozi wetu. Kumbe iwe tu hai au tumekufa, kama anavyotuambia Mtume Paulo tu mali yake Kristo maana yeye ni muweza wa yote kama wimbo wa mwanzo unavyosema; “Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima. Utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele” (Ufu. 5:12, 1:6). Hivyo tunapoadhimisha sherehe hii tunapaswa kujiuliza kama kweli maisha yetu yanaakisi utawala wa Yesu Kristo ndani mwetu, kama kweli tunamtumikia, na tuko chini ya utawala wake au tuko chini ya falme na tawala zingine ambazo kwazo kwa maisha yajayo zitatuangamiza milele yote. Sherehe hii inatuhimizwa kumfuata Kristo mfalme wetu, kusudi mwisho wa maisha yetu hapa duniani atukaribishe katika ufalme wa milele mbinguni. Ni katika tumaini hili mama kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, umependa kutengeneza upya mambo yote katika Mwanao mpenzi, Mfalme wa ulimwengu. Utujalie kwa wema wako, viumbe vyote vilivyokombolewa utumwani vikutumikie na kukusifu bila mwisho”.
Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Danieli (7:13-14). Somo hili ni tangazo la utukufu wa Masiha anayekuja mwisho wa nyakati. Danieli anasimulia alichokiona katika ndoto akisema; “Niliona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akawa pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribisha huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na mataifa yote, na lugha zote, wamtumikie, mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo haitapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa.”
Zaburi: Mzaburi katika wimbo wa katikati anatoa wasifu wa ufalme na utawala huu akisema; “Bwana ametamalaki, amejivika adhama, Bwana amejivika, na kujikaza kwa nguvu. Naam, ulimwengu umethibitisha usitikisike. Kiti chako kimekuwa thabiti tokea zamani. Wewe ndiwe uliye tangu milele. Shuhuda zako ni amini sana; Utakatifu ndio uifaao nyumba yako; Ee Bwana, milele na milele (Zab. 93:1-2, 5).
Somo la pili ni la kitabu cha Ufunuo (1:5-8). Somo hili linahusu kufunuliwa kwa yale yaliyofichika. Kitabu hiki kilichoandikwa na Mtume Yohani mwishoni mwa maisha yake, miaka 60 baada ya kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, kwa lengo la kutangaza ushindi wa mwisho wa Bwana wetu Yesu Kristo, na ushindi wa wafuasi wake. Hivyo linatuonyesha kuwa Kristo ni Mfalme mwenye nguvu na ukuu wake hauna mwisho. Ni “Mkuu wa Wafalme wa dunia” (Ufu 1:5), “Mfalme wa Wafalme na Bwana wa Mabwana” (Ufu 19:16). Yohani anapotumia cheo au jina hilo anawakumbuka Wakuu wa Warumi kuwa Yesu ndiye Bwana na Mfalme wa maisha yote.
Tukumbuke kuwa nyakati hizo sanamu ya mkuu wa Warumi iliwekwa kila mji na watu walilazimishwa kumwabudu. Cheo cha Bwana kilikuwa ni kwa ajili ya mfalme wa Kirumi tu. Wakristo wa kwanza walikataa kumwabudu mfalme wa Kirumi kadiri walivyoamriwa na sheria. Wengi walikubali kufa mashahidi kuliko kuabudu sanamu hiyo. Ni katika muktadha huu waliamwita Kristo “Bwana” wakikiri kuwa Yeye peke yake ndiye Bwana. Kwa maneno haya waliikiri imani yao kwa Yesu bila kuogopa mateso na kuuawa wakitumaini kuingia katika uzima wa milele pamoja na Kristo aliye “Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, aliyeko, aliyekuwako, na atakayekuja, Mwenyezi (Ufu 1:8).
Injili ni ilivyoandikwa na Yohani (18:33-37). Sehemu hii ya Injili inatuonesha jinsi Yesu alivyojidhihirisha kama Mfalme wakati wa mateso yake na katika mahojiano yake na Pilato. Hata hivyo utawala wake si wa dunia hii bali ni wa mbinguni. Utawala wake ni utawala wa Amani na upendo, mamlaka na uwezo wake ni mkuu kuliko mamlaka na uwezo wa wafalme wa dunia hii. Katika Prefasio ya sherehe ya hii mama kanisa anaukiri ukuu wa ufalme Kristo na kuupamba kwa sifa nyingi akisali hivi; “Wewe ulimpaka mafuta ya furaha Mwanao wa pekee, Mfalme wa ulimwengu wote. Alijitoa mwenyewe msalabani, awe sadaka safi iletayo amani, ili atimize mafumbo ya ukombozi wa watu. Kwa kuviweka viumbe vyote chini ya utawala wake amekutolea wewe Mungu mkuu ufalme wa milele na wa ulimwengu wote, ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na wa neema, ufalme wa haki, mapendo na amani”.
Basi na tumfanye Yesu Kristo awe mfalme wa maisha yetu ili tuweze kuwa na maisha ya neema, haki, upendo na amani. Ndiyo maana katika sala ya kuombea dhabihu mama kanisa anasali kwa matumaini haya akisema; “Ee Bwana, tunakutolea sadaka ya kuwapatanisha wanadamu nawe. Tunakusihi huyo Mwanao ayajalie mataifa yote umoja na amani”. Nayo antifona ya wimbo wa komunyo inasisitiza hivi; “Bwana Mfalme ameketi milele, Bwana atawabariki watu wake kwa amani” (Zab. 28:10, 11). Na ktika sala baada ya komunyo mama kanisa anahitimisha maadhimisho haya akisali hivi; “Ee Bwana, sisi tuliopokea chakula cha uzima wa milele tunaona fahari kuzitii amri za Kristu Mfalme wa ulimwengu. Tunakuomba utujalie tuishi milele pamoja naye katika ufalme wa mbingu”.