Tafakari Neno la Mungu Dominika ya 31 Mwaka B: Upendo Kwa Mungu Na Jirani
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 31 ya Mwaka B wa Kiliturujia Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanasisitiza kuwa furaha ya kweli hupatikana katika kuzishika na kuziishi Amri za Mungu. Na kinyume chake ni kweli, tunapokengeuka na kutokuzishika amri hizi, tunakosa amani na furaha, tunakuwa watumwa wa maisha yetu na hisia zetu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, tafakari ya maisha katika mwanga wa Amri za Mungu unamwonesha mwamini kuwa ni mtu wa shukrani, huru, mkweli, anayebariki, mkomavu, mlinzi na mtunza Injili ya uhai; mwaminifu, mkarimu na mkweli; mambo ambayo ni sehemu ya vinasaba vya maisha yake ya kila siku na hivyo kujiona kuwa mbele ya Kristo Yesu, kila siku ya maisha! Amri za Mungu ni sura na chapa ya Kristo Yesu kama inavyojionesha katika Sanda Takatifu. Ni kwa njia hii, Roho Mtakatifu anawakirimia waamini Matunda ya Roho Mtakatifu, ili kuenenda katika Roho, ili hatimaye kuona: uzuri, wema na ukweli unaofumbatwa katika maisha ya Kristo Yesu. Kwa njia ya Roho Mtakatifu, waamini wanakirimiwa fadhila ya matumaini, imani na upendo! Ikumbukwe kwamba, ujio wa Kristo Yesu ni utimilifu wa Sheria na kwa njia ya Matunda ya Roho Mtakatifu, waamini wanapata Sheria mpya inayowaongoza katika Roho, kwani kwa njia ya Roho Mtakatifu wanakuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa! Kristo Yesu anawapenda watu wake, anajitaabisha kuwatafuta, kuwasamehe, kuwafariji pale wanapohuzunika na kupondeka moyo! Kristo Yesu anawaunganisha na upendo wa Baba wa milele!
Kumbe, hapa kinachopewa mkazo anasema Baba Mtakatifu ni upendo kwa Mungu na jirani na kuwaachia wengine nafasi ya kuonja upendo huu, kama kielelezo makini cha utimilifu wa Sheria ulioletwa na Kristo Yesu! Ni katika muktadha huu, Amri za Mungu zinakuwa ni ukweli mfunuliwa unaokita mizizi yake katika maisha ya mwamini yanayofumbatwa katika upendo, hamu ya kutenda mema, kiu ya kufurahia maisha; hamu ya kupata amani, wema, uzuri, unyenyekevu pamoja na kuwa na kiasi katika maisha! Na mtu anayezishika na kuziishi amri hizi atakapomlilia Mungu katika taabu zake kwa moyo wa Imani na matumaini, atamsikiliza na kumwokoa. Hili ndilo tumaini la mzaburi katika wimbo wa mwanzo akisema; “Wewe Bwana usiniache, Mungu wangu, usijitenge nami, ufanye haraka kunisaidia, ee Bwana, wokovu wangu” (Zab. 38:21-22). Na Mama Kanisa akilitambua hili, katika sala ya mwanzo anatuombea akisali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi na mwenye huruma, wawajalia waamini wako neema ya kukutumikia vema na kwa uchaji. Tunakuomba utuwezeshe kukimbilia ahadi zako pasipo kukwaa.”
Somo la Kwanza ni la Kitabu cha Kumbukumbu la Torati (6:2-6). Hiki ni kitabu cha mwisho kati ya vitabu 5 vya Sheria/Torati ya Musa. Vitabu hivi Wayahudi wanaviheshimu sana, kwa kuwa vinabeba maagizo ya Mungu hasa amri 10. Somo hili limebeba mausia ya Musa kwa Waisraeli namna wanavyopaswa kumcha Mungu na kuzishika Amri zake katika maisha yao. Katika kuzishika amri hizi kuna ahadi zinazoambata nazo; kuwa na maisha marefu na yenye heri, usitawi katika familia, pamoja na kuwa na watoto na vitukuu vingi. Mapokeo yanasimulia kuwa Waisraeli katika kuhakikisha wanazishika vyema amri za Mungu, walizigeuza kuwa sala inayoitwa “shema Israeli au sikiliza ee Israeli. Sala hii ilifundishwa kwa kila mtoto, mara tu alipoanza kuongea na ilipaswa kusaliwa mara mbili kwa siku. Sala hii inasema hivi; “Sikiliza Ee Israeli; Bwana Mungu wako, Bwana ndiye mmoja. Nawe mpende Bwana Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote”. Kufundishwa watoto sala hii ilikuwa ni amri. Tunasoma hivi; Na maneno haya ninayokuamuru, yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo na uondokapo. Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako. Tena uyaandike katika miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako” (Kumb 6:4-9).
Kumbe, kutokana na maagizo haya, Waisraeli waliindika sala hii “sikiliza ee Israeli” kwenye vitambaa wakayatengenezea vishada mfano wa “skapulari” au “hirizi” kama ishara ya sala iletayo usalama na kuviweka kwenye vikasha vidogo na kuvivaa mbele ya uso wao ili kuwakumbusha kila wakati wajibu wao kwa Mungu. Kadiri ya kitabu cha Hesabu (15:37-39), wanaume wa Kiyahudi ili kuzikumbuka amri hizi walivivaa vishada vyenye amri hizi katika ncha za nguo zao. Wapo waliofanya hivyo kinafiki kama mafarisayo, ndiyo maana Yesu aliwakemea kwa kupanua hirizi zao na kuongeza matamvua yao (Mt 23:5). Hivyo basi, tunakumbushwa kuwa kuzishika amri za Mungu ni kuzuri kwani ndio msingi wa kuishi kwa furaha na amani. Tukifanya hivyo tunakuwa karibu na Mungu na kila tunapomlilia katika shida zetu atatusikiliza na kutuokoa. Hili ndilo tumaini la mzaburi katika wimbo wa katikati akisema; “Wewe, Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana; Bwana ni jabali langu, na boma langu na mwokozi wangu, Mungu wangu, mwamba wangu ninaye mkimbilia. Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, na ngome yangu. Nitamwita Bwana anayestahili kusifiwa, hivyo nitaokoka na adui zangu. Bwana ndiye aliye hai, na atukuzwe Mungu wa wokovu wangu ampa Mfalme wake wokovu mkuu, amfanyia fadhili Masihi wake (Zab. 18:1-3,46, 50).
Somo la pili ni la Waraka kwa Waebrania (7:23-28). Nalo linatoa ufafanuzi uliopo kati ya ukuhani wa Agano la Kale na wa Agano jipya. Makuhani wa Agano la Kale walikuwa wengi na walikufa, na ukuhani wao ukaisha. Makuhani wa Agano Jipya wanashirikishwa ukuhani wa Kristo, Kuhani mkuu, na wa milele. Kristo Yesu ni kuhani mkuu, mtakatifu, hana uovu, wala waa lo lote, ametengwa na wakosaji. Kristo ndiye kuhani wetu Mkuu na wa milele na mapadre wanashirikishwa ukuhani huu wa Kristo ili kupitia kwao waamini wajichotea neema na baraka kila wakati inapoadhimishwa sadaka ya Misa Takatifu. Injili ni kama ilivyoandikwa na Marko (12:28-34). Sehemu hii ya Injili ni mafundisho ya Yesu juu ya amri iliyo kuu kuliko zote: Amri ya mapendo. “Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.” Amri hii ndiyo msingi wa maisha yetu hapa duniani kwa ajili ya uzima wa milele. Kwani kumpenda jirani ni kumpenda Mungu na kutokumpenda jirani ni kutokumpenda Mungu kwani twampenda Mungu kwa kumpenda jirani. Kuzishika amri hizi “kwafaa kuliko sadaka za kuteketezwa na dhabihu zote pia.” Yesu anatoa fundisho hili baada ya kuulizwa ipi ni amri kuu na muhimu kuliko zote. Itakumbukwa kuwa kipindi Yesu anazaliwa Viongozi wa Dini ya Kiyahudi walizinyumbulisha amri 10 za Mungu hdi kufikia idadi ya 613. Kutokana na wingi huu, kulikuwepo malumbano yasiyoisha juu ya amri ipi ilikuwa kuu na muhimu. Yesu katika kujibu swali hili alinukuu aya mbili za Maandiko Matakatifu. Kwanza ni; “Sikiliza Ee Israeli; Bwana Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. Nawe mpende Bwana Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote (Kumb 6:4-5). Na ya pili ni; “Umpende jirani yako kama nafsi yako” (Wal 19:18).
Yesu anaziweka Amri hizi mbili kuwa na usawa na ukuu uleule. Ndiyo kusema upendo kwa jirani ni maelezo yetu ya upendo kwa Mungu. Hii ndiyo amri mpya kama alivyosema Yesu mwenyewe; “Amri mpya nawapa mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo” (Yn 13:34). Tukumbuke kuwa, kumpenda jirani ni kutambua kuwa sisi sote tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, na tumekombolewa sote kwa Damu Azizi ya Kristo Msalabani kutoka utumwa wa dhambi na mauti. Hivyo tunapaswa kuwajali wote katika mahitaji ya kiroho na kimwili, kwa namna ya pekee, wagonjwa, maskini, wajane, yatima, wafungwa na wakimbizi, kufurahi na wenye kufurahi, kusikitika na wenye kusikitika, na kuwasamehe wanaotukosea. Hivi ndivyo tunavyopaswa kuuishi ukristo wetu ili tupate kustahilishwa kuurithi uzima wa milele. Ni katika tumaini hili Mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali na kuomba hivi; “Ee Bwana, sadaka hii tunayokutolea iwe dhabihu safi mbele yako, ituletee na sisi huruma yako”. Na katika sala baada ya komunyo anahitimisha maadhimisho haya akisali hivi; “Ee Bwana, tunaomba neema yako izidi kutenda kazi ndani yetu, na tena ituweke tayari kupokea ahadi za Sakramenti hizi zilizotuburudisha.” Tumsifu Yesu Kristo!