Tafuta

Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC)wanahamasisha watu wote wakapige kura tarehe 27 Novemba 2024 za uchanguzi wa serikali za mitaa. Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC)wanahamasisha watu wote wakapige kura tarehe 27 Novemba 2024 za uchanguzi wa serikali za mitaa. 

Tanzania,TEC,uchaguzi wa Serikali za mitaa:Uchaguzi uhakikishe demokrasia na uhuru

Baraza la Maaskofu Tanzania(TEC)limetoa ujumbe kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika tarehe 27 Novemba 2024 na kutaka uchaguzi huo uwe huru na wa haki.Wanaiomba Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI)"kuhakikisha'demokrasia inatawala nchini na kutuma ujumbe kwa dunia nzima kuwa Tanzania bado ipo kisiwa cha amani."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Ijumaa tarehe 15 Novemba 2024, Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Tanzania (TEC), mara baada ya kumaliza mkutano wao wa siku mbili wametoa Ujumbe kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni tarehe 27 Novemba 2024. Ujumbe wao ulisomwa na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Wolfagang Pisa OFMCap wa Jimbo Katoliki la Lindi, ambapo mbele ya  waandishi wa vyombo vya habari mara baada ya sala na salamu, alisema "Maaskofu wa Kanisa Katoliki wanathamini mshikamano wa Watanzania na kutaka kujitawala wenyewe" kutokana na kifungu kibiblia ambacho kinasema: "kila mtu aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu(rej. Warumi 13:1-7)." Askofu Mkuu Wolfagang alisema kuwa: “Tunapokaribia uchaguzi sisi viongozi wenu wa kiroho wa Kanisa Katoliki tunaungana na Watanzania kupata viongozi wa serikali za mitaa kupitia uchaguzi huru na wa haki. Tunafahamu kuwa Serikali inaundwa kwa lengo kuu la kuwaletea wananchi maendeleo ili kuwa na maisha bora ambapo kila kundi limedhamiria kuona kwamba utu wa kila mtu unaheshimiwa, unalindwa na unaendelezwa,” alibainisha Askofu.

Kila raia haki na wajibu wa kishiriki shughuli za umma 

Akitaja kifungu cha Katiba ya nchi hiyo,  Rais wa TEC alisema: “Kwa mujibu wa Ibara ya 21 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, kila raia anayo haki na wajibu wa kushiriki katika shughuli za umma endapo kutakuwa na uchaguzi. Kwa mujibu wa Ibara ya 146 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lengo la Serikali za Mitaa ni kukabidhi madaraka kwa wananchi.” Kwa njia hiyo “Maendeleo ya kweli ni ya watu na yanaletwa na watu. Watu lazima wawe chanzo na lengo la maendeleo. Watu ndio wenye mamlaka na maamuzi ya maendeleo yao. Hili linawezekana pale tu unapokuwa na viongozi wazuri na waliochaguliwa kwa haki. Ili kufanikisha uchaguzi ni lazima kuwe na mfumo wa wazi, wa haki na uwajibikaji katika kusimamia uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa. Wameeleza kuwa, tangu mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mwaka huu 2024 uanze, wananchi wamekuwa wakilalamikia utaratibu wake kutotendewa haki.”

Uandikishaji wa wapiga kura uliendeshwa hovyo

Rais wa TEC kwa niaba ya Maaskofu wote akiendelea na Ujumbe huo kuhusiana hilo aliongeza: “Pia wameshuhudia jinsi zoezi zima la uandikishaji wapiga kura kwa mwaka huu 2024 lilivyoendeshwa hovyo, ikiwa ni pamoja na kutotoa vitambulisho vya wapiga kura, na kufuatiwa na upendeleo wa wazi na usiojificha wa watendaji kwa kuwatenga kwa wingi, kwa gharama za vyama vya upinzani. Hii imeacha doa kubwa katika taifa.” Kwa njia hiyo  Baraza la Maaskofu “TEC inasisitiza kuwa uchaguzi pekee unaoheshimika ni ule unaofanywa kwa misingi ya uhuru, haki, uwazi, kutoegemea upande wowote. Uchaguzi unaoheshimu ukuu wa mamlaka ya wananchi juu ya viongozi waliowachagua.”

Jukumu la TAMISEMI

Rais wa Baraza la Maaskofu alifafanua kuwa “TAMISEMI ihakikishe kuwa zoezi zima la upigaji kura linafuata misingi ya kidemokrasia na watatangazwa walioshinda kihalali pekee.” Maaskofu wamesisitiza “kuwa wasimamizi wa uchaguzi wanapaswa kuratibu uchaguzi kwa misingi ya haki na kutopendelea chama chochote. Ukiukwaji wa matakwa ya wananchi hupelekea kuwa na viongozi ambao si chaguo la wananchi. Kiongozi anayepatikana madarakani, kwa uongo husababisha kutoaminiana kwa kukiuka misingi ya demokrasia. “Tusijenge jamii ya matapeli, tujenge taifa ambalo linalelewa katika ukweli na kufanya kazi katika ukweli. Mungu wetu hadanganyi kamwe, ha adanganyiki na angependa sisi watu wake tuishi kwa misingi ya haki na ukweli. Tuendelee kuwajenga watu katika dhamiri safi na haki wanaoweza kusema huu ni uongo tuuache na huu ndiyo ukweli tuufuate,”Alisisitiza.

Kuiambia dunia nzima kuwa Tanzania ni kisiwa cha amani

 Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kwa njia hiyo  wanaiomba Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) ambayo ni taasisi ya serikali nchini Tanzania inayorahisisha shughuli za kiutawala katika serikali za mitaa “kuhakikisha demokrasia inatawala nchini na kutuma ujumbe kwa dunia nzima kuwa Tanzania bado ipo kisiwa cha amani.” Kwa hiyo Ujumbe wa Maaskofu pia unahitimishwa kwa kuwataka “wananchi kushiriki kwa wingi kupiga kura tarehe 27 Novemba 2024 kama ilivyotangazwa na serikali.” Askofu vile vile  alieleza kuwa naye "atashiriki kwenda kupiga kura. Mungu Ibariki nchini Yetu, Mungu atubariki Sisi tulio hapa na Mungu abariki Taifa letu la Tanzania. Maaskofu wenu Kanisa Katoliki Tanzania, Asanteni sana," alihitimisha.

Ufuatao ni Ujumbe kamili wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Tanzania kuhusiana na Uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa tarehe 27 Novemba 2024.

Ujumbe wa Baraza la Maaskofu wa Tanzania kuhusu Uchaguzi 2024
15 November 2024, 16:31