Uganda:Kanisa la Mapeera Kigungu nchini Uganda limechomwa moto
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kanisa Katoliki la kihistoria la Mapeera Kigungu nchini Uganda lilipata uharibifu mkubwa baada ya watu wasiojulikana kuchoma moto ndani. Ukweli huu ni wa tarehe 7 Novemba 2024, wakati baadhi ya watu wasiojulikana waliingia ndani ya Kanisa saa 4 usiku na kuchoma moto upande wa kushoto wa Kanisa hilo. Moto huo uliharibu vitu vya thamani vya kidini ikiwa ni pamoja na mavazi ya kikuhani, vikombe vya madhabahuni, vitambaa vya meza na chupa za divai kubwa. Uharibifu unaokadiriwa ni zaidi ya milioni 10 hivi. Cheche za moto ziligunduliwa na waamini wengine ambao waliinuka na kupiga kengele, na kuruhusu kuzimwa kabla moto haujasababisha uharibifu mkubwa wa jengo hilo.
Polisi wanaendelea na uchunguzi
Polisi pia wanachunguza kwa usaidizi wa picha kutoka kwa kamera za usalama katika eneo hilo na vitengo vya uchunguzi. Wachunguzi wanashuku kuwa aliyeanzisha moto huo aliingia kanisani kupitia dirisha la nyuma. Aidha taarifa nyinginge kuhusiana na kitendo cha uharibifu na kufuru wanaweza kuhusishwa na mzozo juu ya ardhi karibu na parokia inayomilikiwa na Kanisa, ambayo kwa sasa inamilikiwa na shughuli za kibiashara. Mamlaka za kikanisa zingependa kuunda miundo mipya kwenye eneo hilo kwa kuwaondoa wale ambao hadi sasa wamekaa bila kulipa kodi.
Wamisionari wa kwanza 1879
Kanisa la Mapeera Kigungu limejengwa kwenye ncha ya Ziwa Victoria ambapo mnamo mwaka 1879 wamisionari wa kwanza wa Kikatoliki waliokuwa wakieneza Injili nchini, Padre Siméon Lourdel na Ndugu Amans Delmas wa Shirika la Wamisionari wa Afrika (White Fathers), walitua. Kwa sababu hiyo, Wakatoliki wa Uganda wanashikamana sana na Kanisa hilo, ambapo kila mwaka ifikapo tarehe 17 Februari wamini wengi huenda kuhiji kukumbuka kutua kwa wamisionari hao wawili na kuanza kwa uinjilishaji katika nchi. Kanisa limebadilika kwa wakati, kutoka muundo wa udongo na mwanzi uliojengwa na Askofu Mkuu Joseph Georges Edouard Michaud (Msimamizi wa Kitume wa Uganda kuanzia 1933 hadi 1945) hadi jengo la matofali na vigae vilivyochomwa moto. Hata hivyo Kanisa hilo linakabiliwa na hatari ya kuzamishwa na maji kutokana na kupanda kwa kina cha maji katika Ziwa Victoria. Na hii ni katika kuona jins gani mabadiliko ya Tabianchi yanaongezeka siku baada ya siku.