Mwanzilishi wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, Bwana Riccardi. Mwanzilishi wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, Bwana Riccardi.  (ANSA)

Uganda:mkutano wa Jumuiya ya Mt.Egidio katika Roho ya Assisi,Chuo Kikuu cha Makerere

Jumamosi tarehe 2 Novemba 2024,mjini Kampala,katika Chuo Kikuu cha Makerere, ulifanyika mkutano kati ya wawakilishi wa imani na tamaduni tofauti,katika roho ya Assisi.Mkutano huo uliongozwa na mada ya“Kufikiria Amani,”mkutano ulifuata ule uliofanyika jijini Paris mnamo Septemba 2024.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Mkutano kati ya wawakilishi wa imani na tamaduni tofauti, kwa moyo wa Assisi, ulifanyika Jumamosi tarehe 2 Novemba 2024 jijini Kampala, katika Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda. Mpango huo ulihamasishwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kwa moyo wa Assisi na kwa kujikita na kauli mbiu: “Kufikiria Amani.” Kwa namna ya pekee, walisikiliza hata maneno ya Ujumbe wa Papa Francisko pamoja na “Wito kwa ajili ya amani” uliosomwa na kijana mmoja. Kama ilivyo desturi ya mikutano hiyp, wakati wa sherehe za mwisho viongozi wa kidini waliwasha mshumaa wa amani na kutia saini ya “Wito wa  Amani” na kuhitimisha kwa kukumbatiana kwa amani kati ya washiriki wote.

Wito wa papa Francisko kwa ajili ya amani

Hata hivyo tukumbuke wakati wa  hafla ya ufunguzi wa Mkutano huko Paris, walisoma ujumbe wa Papa Francisko wa nguvu uliokuwa na wito mkubwa wa uvumilivu na kujitolea kwa amani. Papa Francisko alikumbuka jinsi ambavyo “miaka 38 imepita tangu 1986, tarehe ya mkutano wa kwanza wa maombi ya amani. Tangu wakati huo, matukio mengi yameashiria historia ya ulimwengu: kuanguka kwa Ukuta wa Berlin, mwanzo wa milenia ya tatu, kuongezeka kwa misimamo mikali na migogoro mingi ambayo imeathiri sayari, pamoja na changamoto za ajabu za mabadiliko ya tabianchi. Ujio wa teknolojia, kuibuka na kubadilika, na magonjwa ya milipuko ambayo yameathiri ubinadamu. Tuko katikati ya mabadiliko ya enzi ambayo madhara yake bado hatuyajui,” aliandika  Papa  na kuhimiza kila mtu asijisalimishe “kwa mantiki ya vita na migawanyiko. Amani ni njia inayohitaji ujasiri, imani na mazungumzo.” Papa pia alisema kwamba kufanya kazi kwa ajili ya amani si kazi rahisi, lakini ni jambo la msingi katika kujenga jamii inayoheshimu utu wa binadamu na kuendeleza haki. “Tunaendelea kuwa wajenzi wa amani, bila kuchoka katika dhamira yetu ya upatanisho na udugu. Asanteni nyote kwa kuwaza amani pamoja!" alihitimisha ujumbe huo.

Viongozi wa dini mbali mbali walipokutanika Paris kwa ajili ya mkutano juu ya Amani
Viongozi wa dini mbali mbali walipokutanika Paris kwa ajili ya mkutano juu ya Amani

Walioshiriki pamoja na Monsinyo Gerevers Mukasa, anayewakilisha Jimbo Katoliki la Kampala, walikuwa Sheikh Salim wa Nakulabye kwa Jumuiya ya Kiislamu; mjumbe wa Sikh, N.H Singh; Mchungaji Mugabi Christopher wa Kanisa la Uganda. Pia alikuwepo balozi wa Italia Mauro Massoni. Kila mtu alionesha nia ya kuendeleza mazungumzo yaliyopendekezwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio “katika Roho ya Assisi.”

Mkutano wa Jumuiya ya Mt.Egidio huko Makerere
05 November 2024, 16:55