Bukoba,Tanzania:Watawa waishi na kuzifuata amri za Mungu hasa Upendo!
Na Patrick P. Tibanga- Radio Mbiu - Bukoba.
Watawa wametakiwa kuzishika amri za Mungu na kuishi amri kuu ya mapendo kwa kutoa ushuhuda wa Kristu katika maisha yao na kuishi kadiri ya katiba ya shirika inavyowaagiza na kuwa tayari kuondoa vizingiti. Rai hiyo ilitolewa Mhashamu Jovitus F. Mwijage, Askofu wa Jimbo Katoliki Bukoba nchini Tanzania, wakati wa Homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu iliyokuwa na matukio yaliyogawanyika katika makundi: manovisi kufunga nadhiri za Kwanza, wengine za Daima na Wanajubilei ya fedha (Miaka 25) wa Shirika la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, tarehe 6 Desemba 2024. Adhimisho hilo lilifanyika katika nyumba Mama ya Shirika hilo huko Nyaigando, iliyoko katika Parokia ya Bikira Maria wa Mateso Saba Kashozi, Jimbo Katoliki Bukoba.
Katika homilia yake Askofu Mwijage alisema kuwa “Watawa wanatakiwa kuishi na kuzifuata amri za Mungu ikiwemo amri kuu ya mapendo na kuwa watu wa amani popote watakapoishi na kutoa ushuhuda wa Kristu kwa maisha yao ya kitawa. “Wapendwa wana nadhiri ili mfikie Utakatifu muombeni Mungu awasaidie kuishi viapo vyenu na kumuomba yeye awasaidie kuondoa vizingiti vitakavyo wafunga kutimiza mapenzi ya Mungu na kuishi Nadhiri zenu kadiri ya Katiba ya Shirika inavyowaagiza, toeni talanta zenu, akili yenu, moyo wenu, nguvu zenu zote kwaajili ya Kristu naye atawalipa mara mia,” alisema Askofu Mwijage.
Askofu wa Bukoba akiendelea na mahubiri hayo aliwashukuru na kuwapongeza Wanajubilei wa miaka 25 ya Utawa kwa kudumu vyema katika Wito wao na kukuza utajiri wao kwa kutumia talanta walizojaliwa na Mungu kwaajili ya Ufalme wa Mungu. “Nipende kuwashukuru Wanajubilei kwa miaka 25 ya Utawa, kwa miaka yote hiyo mmekubali kuuza utajiri wenu, kutumia talanta zenu na akili zenu kwaajili ya Ufalme wa Mungu, asante sana kwa Utume wenu nawaambia safari bado haijaisha, jitahidi kuishi ahadi zenu za nadhiri pia yachuchumilie yaliyo juu kumuiga ngamia kupita katika tundu la sindano au kupitia mlango mwembamba mkitoa sadaka na majitoleo mbali mbali” Alisisitiza Askofu Mwijage katika homilia yake.
Askofu Mwijage aidha aliwataka watawa hao kuishi ahadi zao za Nadhiri na kutoa sadaka kwa majitoleo mbali mbali wakiiga fadhila za Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu. Katika hilo alitaja fadhila za Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu zikiwemo zile za kujiamini na hivyo wanatakiwa kutambua kwamba wapo katika njia sahihi kwa kutembea kifua mbele, wakiishi fadhila ya upendo hasa kwa kutanguliza mahitaji ya wengine kuliko wao binafsi, kuwa wavumilivu, kuwa na fadhila ya Wema kwa kujinyenyekeza mbele ya Mungu na wengine, kuwa na fadhila ya ukarimu kwa kuwasaidia wengine pamoja na kuwa na fadhila ya kiasi kwa kujitawala na kujishinda ikiwemo kuzuia mihemko ya tamaa za mwili na roho.
Askofu Mwijage kadhalika aliwataka waamini kujifunza na kumsikiliza Kristo pamoja na kuwa na fadhiila ya utii na kutafuta utakatifu na kutamani kuwa karibu na Mungu kwa njia ya Sakramenti zake ikiwemo Sakramenti ya Kitubio na Ekaristi Takatifu kwa lengo la kuutafuta Utakatifu na kuzungumza na Mungu kwa njia ya sala na kupambana na shetani kwa sala na kueleza kuwa sala ni ngao bora na kimbilio kwa wenye wasiwasi na hofu.
Masista wa Shirika la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu ambao wanafanya Jubilei ya Miaka 25 ya Utawa ni Sr Maria Hellena Rhobi Petro, mzaliwa Parokia Nyamwanga Musoma, Sr Maria Florida Batujune Deogratias, mzaliwa Parokia ya Bushangaro Kayanga, Sr Maria Emilia Kokuleba Faustin, mzaliwa Parokia Katoke Bukoba, Sr Maria Symphorosa Nabuso Barthazar, mzaliwa Parokia Mwangika Geita, Sr Maria Clementina Tibezuka Benedikto, mzaliwa Parokia Kome Geita, Sr Maria Patricia Kagemulo Pastory, mzaliwa wa Rwambaizi Kayanga, Sr Maria Editha Mukahingika Gosbert, mzaliwa wa Rukindo Bukoba na Sr Maria Philipina Kilaya Burchard, mzaliwa wa Kimiza Kayanga.
Masista wa Shirika la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu ambao wameweka Nadhiri za daima ni Sr Maria Adriana Neema Richard, mzaliwa wa Maruku Bukoba, Sr Maria Jane Eudes Longino, mzaliwa wa Rutabo Bukoba na Sr Maria Goreth Kokushubira Paschal, mzaliwa Parokia Kilimilire Bukoba.
Na wakati huo huo Masista walioweka Nadhiri za Kwanza alikuwa ni Sr Lucia Komutonzi wa Parokia Sengerema Geita, Sr Plaxeda Mkesafari wa Parokia Busota Rulenge Ngara, Sr Alodia Kokusiima wa Parokia Rutete Bukoba, Sr Remina Chohairwe wa Parokia Busota Rulenge Ngara, Sr Veronica Ndaisavye wa Parokia Kakonko Kigoma, Sr Editha Imani wa Parokia Katoke Rulenge Ngara na Sr Judith Kokuberwa wa Parokia Kagondo Bukoba.
Katika Misa hiyo takatifu ilihudhuriwa na Askofu Almachius Rweyongeza wa Kayanga, Askofu Method Kilaini , Askofu Msaidizi mstaafu Jimboni Bukoba, Mapadre na Watawa kutoka majimbo na mashirika mbali mbali nchini Tanzania na ndugu zao.