Domenika IV,Majilio mwaka C:Fumbo la Umwilisho,Mungu pamoja nasi
Na Padre Paschal Ighondo -Vatican
Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya nne ya majilio mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa. Hii ni Dominika ya mwisho ya kipindi cha majilio. Masomo ya dominika hii yanasisitiza juu ya ujio wa Yesu Kristo, Emanueli, Mungu pamoja nasi, Mwokozi Bwana wetu. Mwaliko huu unaashiriwa kwa maneno ya wimbo wa mwanzo yanayosema: “Dondokeni, enyi mbingu toka juu, mawingu na yammwage mwenye haki; nchi ifunuke, na kumtoa Mwokozi” (Isa. 45:8). Ni maneno ya faraja na matumaini kwetu sisi wanadamu, kwani yanatuonesha kuwa Mwokozi wetu alivyo karibu nasi. Ni mwaliko wa kukaa mkao wa kusheherekea kuzaliwa kwa Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Tunakuomba, ee Bwana, utie neema yako mioyoni mwetu, ili sisi tuliojua kwa maelezo ya Malaika kwamba Kristo Mwanao amejifanya mtu: kwa mateso na msalaba wake, tufikishwe kwenye utukufu wa ufufuko”.
Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Mika (Mik. 5:2-4). Ili kulielewa vizuri somo hili yatupasa kuifahamu japo kwa kifupi historia yake. Jina Mika linatokana na neno la Kiebrania “Mikayah” likimaanisha; “Ni nani aliye kama Bwana?” Mika alizaliwa huko Morashethi-Gathi (1:1,14), kusini magharibi mwa Yerusalemu, katika ufalme wa Yuda, upande wa kusini, wakati wa utawala wa Yothamu (751-736 K.K.), akaishi mpaka kipindi cha utawala wa Ahazi (736-716K.K.) na Hezekia (716-687K.K). Mika aliishi wakati mmoja na manabii Isaya na Hosea. Hivyo aliona na kushuhudia kuanguka kwa ufalme wa Isreali na kuwa jimbo la Ashuru (722-721 K.K). Kama nabii Amosi alivyotabiri kuangamizwa kwa miji ya Samaria na Yerusalemu kwa sababu ya wafalme, manabii na makuhani wake kuwa waovu, wakifanya biashara za udaghanyifu na mahakimu wao kupokea rushwa kwa kukosa uchaji na hofu ya Mungu. Matokeo yake kulikosekana kwa haki katika jamii, maskini kuonewa kwa kukosekana kwa uadilifu na utakatifu katika maisha ya kila siku. Ni katika hali hii, Mika aliwaonya watu juu ya dhambi zao za udhalimu, uroho, uchoyo, ufisadi na ibada za sanamu, akiwaambia kuwa hali hii itapelekea hukumu iwapo hawatatubu na kuziacha njia zao mbaya. Hali halisi ilivyokuwa inaelezwa vizuri katika kitabu cha 2Wafalme 15-20 na 2Nyakati 26-30.
Kitabu hiki cha Mika kimegawanyika katika sehemu kuu nne. Sehemu ya kwanza inahusu hukumu dhidi ya miji ya Samaria na Yerusalemu (1:1-16). Kwanza kabisa nabii Mika anaonya juu ya hukumu ya Mungu dhidi ya ufalme wa Yuda ambao mji wake mkuu ulikuwa Yerusalemu na Ufalme wa Israeli ambao mji wake mkuu ulikuwa Samaria. Sehemu ya pili inaongelea uonevu wa viongozi wake (2:1-3:12); sehemu ya tatu inahusu utabiri wa marejesho ya ki-Mungu (4:1-5:15) na sehemu ya mwisho inahusu hukumu na huruma ya Mungu (6:1-7:20). Sehemu tunayosomwa katika domenika hii ya nne ya majilio ni sehemu ya tatu ya marejesho ya ki-Mungu. Sehemu hii inatujulisha ahadi ya Mungu ya kumleta Mkombozi wa pekee kutoka Bethlehemu mji wa mfalme Daudi. Ni ahadi ya kufanywa upya kwa Sayuni na kurejeshwa kwa utawala wa amani kwa wale wanaomwamini na kumtumaini Mungu. Sayuni itakayofanywa upya itakuwa ndiyo kitovu cha utawala wa ulimwengu wote, mahali ambapo amani halisi na haki vitatawala na kudumu milele. Yesu Kristo, ndiye mfalme wa amani na haki tukimruhusu akae mioyoni mwetu daima haki na amani vitatawala katika maisha yetu.
Ni katika muktadha huu katika wimbo wa katikati tunasali na mzaburi tukisema hivi; “Ee Mungu, uturudishe, uangazishe uso wako nasi tutaokoka. Wewe uchungaye Israeli usikie, Wewe uketiye juu ya makerubi, utoe nuru. Uziamshe nguvu zako, uje, utuokoe. Ee Mungu wa majeshi, tunakusihi, urudi, utazame toka juu uone, uujilie mzabibu huu, na mche ule ulioupanda, na tawi lile ulilolifanya kuwa imara kwa nafsi yako. Mkono wako na uwe juu yake, mtu wa mkono wa kuume; juu ya mwanadamu uliyemfanya kuwa imara kwa nafsi yako. Basi hatutakuacha kwa kurudi nyuma, utuhuishe nasi tutaliitia jina lako takatifu (Zab. 80: 3, 1-2, 14-15, 17-18).
Somo la pili ni la waraka kwa Waebrania (Ebr. 10:5-10). Somo hili ni mhutasari wa lengo la fumbo la umwilisho kuwa Yesu Kristo nafsi ya pili ya Mungu amekuja kuyafanya mapenzi ya Mungu kuwapatia uzima wa milele watu wote wanaomwamini. Kwa sababu hiyo, Mungu Baba alimpa mwili ili ajitoe sadaka kwa ajili ya utakaso wa dhambi zetu. Na Yesu mwenyewe aliutoa mwili wake kwa hiari kama sadaka pekee na kamilifu akitimiza matakwa ya Mungu Mwenyezi. Na Sadaka ya Yesu Msalabani ni sadaka kamili na timilifu iliyofunga Agano jipya na la milele na kukomesha lile la zamani ambalo halikuwa timilifu, maana lilifanywa kwa dhabihu, matoleo na sadaka za kuteketeza wanyama ambazo hazikuwa na uwezo wa kumwondolea mwanadamu dhambi zake na kumpatanisha na Mungu.
Injili ni ilivyoandikwa na Luka (Lk. 1:39-45). Sehemu hii ya Injili ni simulizi la kukutana kwa Bikira Maria na Elisabeti. Katika kukutana kwao, Yohani Mbatizaji akiwa tumboni mwa mama yake Elizabeti anashangilia kwa kufuraha kukutana na Yesu Kristo naye akiwa tumboni mwa mamaye Bikira Maria. Hivyo, kabla ya kuzaliwa kwake, Yohane anaanza kazi ya kumdokeza Mkombozi anayekaribia. Elisabeti alipotambua ishara hiyo iliyodokezwa na mwanawe, kwa furaha na uchaji alimpokea Bikira Maria, sio kama binamu yake, bali kama mama wa Mkombozi, na mama wa Mungu. Ndivyo Mwinjili Luka anavyosimulia kuwa Elizabeti alitamka maneno yanayomtambulisha Bikira Maria kuwa ni Chombo kiteule cha Mungu cha kumleta Mkombozi ulimwenguni akisema; “Umebrikiwa wewe kuliko wanawake wote, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa”. Haya ni maneno tunayosali katika sala ya Salamu Maria ambayo Elizabeti kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu aliyatamka na hivyo kukiri hadhi hii kubwa aliyopewa Bikira Maria ya kuupokea na kuufunua kwetu mpango wa Mungu wa ukombozi wa mwanadamu.
Elizabeti aliendelea kusema; “Limenitokeaje neno hili, hata Mama wa Bwana wangu anijie mimi?” Kwa maneno haya Elizabeti anatutangazia kuwa Bikira Maria ni Mama wa Mungu-Theotokos kwani kwake nafsi yake ya pili – Mungu-Mwana, Mwokozi Yesu Kristo ambaye kwa fumbo la umwilisho alizaliwa na Bikira Maria na hivyo akawa mama ya Kristo-Christokos. Kisha Elizabethi akaendelea kusema: “Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kiliruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu”. Mtoto huyu ni Yohane Mbatizaji, mtangulizi wa Yesu Kristo, ambaye angali bado tumboni mwa mamaye alimtambua Maria kuwa ni Mama wa Mungu na akamshangilia kwa furaha yeye na Masiya aliyemchukua. Mababa wa Kanisa wanasema kuwa kwa nafasi hii ya Yohane Mbatizaji kumtambua na kumtambulisha Kristo kwa watu angali bado tumboni, alipata bahati ya kuondolewa dhambi ya asili kabla ya kuzaliwa kwake.
Tukio hili la Bikira Maria kumtembelea Elizabeti linaweka wazi kuwa Bikira Maria ni Mama wa furaha na amani, ni mama aliyejaa fadhila ya unyenyekevu na uvumilivu, aliyeshiriki fumbo la ukombozi wetu na hivyo kustahili kupalizwa Mbinguni mwili na roho. Huko mbinguni anaendelea kutuombea nasi tufike aliko yeye. Kwa unyenyekevu na upendo kwa mwanadamu, Mungu nafsi ya pili, Yesu Kristo alijishusha na kutwaa ubinadamu wetu katika fumbo la Umwilisho ili apata kutukomboa kutoka utumwa wa dhambi na mauti. Basi nasi tumafanye Bikira Maria kimbilio letu, kiongozi wetu, na mwombezi wetu kwa mwanae ili tupate neema na baraka za kuufikia uzima wa milele. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala baada ya Komunio anahitimisha maadhimisho ya dominika hii akisali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi, tumekwisha pokea amana ya ukombozi wa milele. Tunaomba jinsi tunavyoikaribia hiyo sikukuu takatifu, tuzidishe ibada yetu, tupate kuliadhimisha vema fumbo la kuzaliwa kwake Mwanao”.