Domenika ya III ya Majilio mwaka C:Furahini Bwana yu-Karibu!
Na Padre Paschal Ighondo- Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya tatu ya majilio mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa. Dominika hii huitwa kwa kilatini Dominica Gaudete yaani Dominika ya furaha. Tunaalikwa kufurahi kwa sababu tumekaribia mwishoni mwa kipindi cha majilio. Hivyo sherehe ya Noeli i karibu, inabisha hodi katika malango ya mioyo yetu. Ndivyo wimbo wa mwanzo unaofungua maadhimisho ya dominika hii unavyosema; “Furahini katika Bwana siku zote; tena nasema furahini. Bwana yu karibu” (Flp. 4:4, 5). Na katika sala ya mwanzo mama Kanisa kwa matumaini haya anasali hivi; “Ee Mungu, unatuona sisi taifa lako tukingojea kwa imani sikukuu ya kuzaliwa kwake Bwana. Tunakuomba utujalie kuifikia hiyo sherehe kubwa ya wokovu wetu, na kuiadhimisha daima kwa ibada kuu na furaha”.
Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Zefania (Zef 3:14-18). Katika somo hili Nabii Zefania anawaalika Waisraeli wafurahi na kushangilia kwa sababu Mungu mfalme wao karibu atawaondoa na kuwaangamiza maadui wao. Historia inasimulia kuwa katika kipindi cha utawala wa mfalme Manase (689-642 KK) na Amoni (642-640 KK), waisraeli walimuasi Mungu wa kweli kwa kuabudu miungu mingine. Masimulizi yanasema kuwa Mfalme Manase alijenga madhabahu ndani ya hekalu la Yerusalemu kwa heshima ya Baali, miungu ya kipagani na kumtoa mwanae sadaka kwa miungu hiyo na kufanya mabaya mengi machoni pa Bwana, sawasawa na machukizo ya mataifa aliowafukuza Bwana mbele ya wana wa Israeli (2Fal. 21:2-18). Naye mfalme Amoni aliendeleza utovu wa baba yake, wala hakushika njia ya Bwana (2Fal. 21:19-26). Kutokana na dhambi zao, Mwenyezi Mungu aliwaadhibu kwa kuyaruhusu mataifa mengine kuwafanya watumwa wao kwa kazi nyingi.
Ni katika mukadha huu wa kuteseka utumwani na wao kujuta dhambi zao, Mungu aliwaonea huruma, akamtuma nabii Zefania kuwapa ujumbe wa furaha, kuwa wokovu wao upo karibu, wazidi kumtumainia Mungu pekee awezaye kuwaokoa. Hivyo wanaalikwa kuimba, kupiga kelele za shangwe, kufurahi na kushangilia kwa moyo wote. Sababu ya shangwera hizi ni kuwa Bwana Mungu ameziondoa hukumu zake juu yao, naye Yu katikati yao, hawapaswi kuogopa wala kuwa na wasiwasi. Zefania anasema; “Usiogope, Ee Sayuni; mikono yako isilegee. Bwana, Mungu wako, yu katikati yako, Shujaa awezaye kuokoa; shangilia kwa furaha kuu, tulia katika upendo wake, furahia kwa kuimba” (Zef. 3:14-18).
Ujumbe huu mzaburi katika wimbo wa katikati anausisitiza akisema; “Tazama, Mungu ndiye wokovu wangu, nitatumaini wala sitaogopa. Maana Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu; Naye amekuwa wokovu wangu. Basi, kwa furaha mtateka maji, katika visima vya wokovu. Maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako. Mshukuruni Bwana, liiteni jina lake; yatangazeni matendo yake kati ya mataifa. Litajeni jina lake kuwa limetukuka. Mwimbieni Bwana, kwa kuwa ametenda makuu; Na yajulikane haya katika dunia yote. Paza sauti, piga kelele, mwenyeji wa Sayuni; Maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako (Isa. 12:2-6). Mwaliko huu ni wetu sisi nyakati zetu kwamba tukimtumaiia Mungu kwa moyo wetu wote, hatupaswi kuwa na huzuni wala wasiwasi, maana hakuna baya lolote litakalotupa. Hivyo tuwe na furaha kwani ujio wa Kristo u-karibu.
Somo la pili ni la waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi (4:4-7). Katika somo hili mtume Paulo naye anawaalika wakristo wafilipi wawe na furaha daima, huku wakiendelea kumsubiri Bwana aliye utimilifu wa furaha yao. Wafilipi wanapaswa kuwa wavumilivu, wapole, wema, watulivu na wenye kudumu katika imani. Tena, wasijisumbue na mambo ambayo hayatawafikisha mbinguni, bali wadumu katika kusali, kuomba na kumshukuru Mungu kwa yote anayowajalia. Mahitaji yao yote wayafikishwe kwa Mungu. Naye kwa kuwa anawapenda, atawasaidia wakimbilia kwa moyo mnyoofu, nayo amani yake, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yao na nia zao katika Kristo Yesu.
Ujumbe huu wa Mtume Paulo kwa wafilipi ni ujumbe wa nyakati zote. Nasi hatuna budi kufurahi, kwa kuwa Bwana yu-karibu. Krismasi i-karibu. Tena furaha yetu inapaswa kuwa kubwa zaidi ya ile ya waisraeli waliyoalikwa na Zefania. Hii ni kwasababu sisi tumekwisha samehewa dhambi zetu na Mungu. Nabii Zefania aliwaambia Wayahudi kwamba dhambi zao zitasamehewa. Sisi tumekwisha samehewa. Mtu anayedaiwa na asiye na uwezo wa kulipa fidia, anakuwa na furaha kubwa anapoambiwa kwamba deni lako litafutwa na kusamehewa. Lakini atakuwa na furaha kubwa zaidi akiambia nenda na amani deni lako limefutwa na umesamehewa. Ndivyo tunavyopaswa kufurahi sisi, lakini kama tumefanya maandalizi mema rohoni mwetu kwa toba na kuungama dhambi zetu.
Injili ni kama ilivyoandikwa na Luka (3:10-18). Katika sehemu hii ya Injili, Yohane Mbatizaji anawafundisha watu wawe na mwenendo mwema. Kwa maana Kristo atakuja kuwahukumu watu wote kadiri ya matendo yao. Matendo mema ndiyo njia ya uadilifu. Ujumbe huu umejikita katika kutenda matendo ya huruma ya kimwili; mwenye kanzu mbili anapaswa kumpa asiye na kanzu; na mwenye chakula na afanye vivyo hivyo. Ujumbe huu unamhusu kila mtu, tajiri na maskini. Kwa maana hakuna mtu asiyemhitaji mwingine, hata maskini anacho cha kumsaidia jirani yake naye tajiri kipo anachokihitaji kutoka kwa maskini.
Yohane pia anayakemea na kuyaonya makundi mbalimbali ya uongozi katika jamii; watoza ushuru, askari, na wanasheria. Makundi haya yanaonywa yasiwe kikwazo cha amani kwa watu. Kwa watoza ushuru wasitoze kitu zaidi kuliko walivyoamriwa na askari wasidhulumu mtu, wala kushitaki kwa uongo; tena watoshewe na mishahara yao. Kuhusu hukumu ya mwisho, Yohane mbatizaji ansema kuwa matendo ya mwanadamu yatafananishwa na ngano bora na makapi. Wote wenye kuziandaa roho zao vizuri kwa matendo mema wataingia katika uzima wa milele, bali wasiojiandaa vyema yaani wenye dhambi, ndiyo makapi ambayo yatateketezwa kwa moto usiozimika, na kutokumuon Mungu milele yote. Ujumbe mahususi hapa ni huu, mtu yeyote, haijalishi wingi wa dhambi zake, akitubu, akaiacha njia yake mbaya, atasamehewa na kuokolewa.
Tukumbuke kuwa mwaliko wa furaha unaotolewa ni furaha katika Bwana. Tusiitafute furaha katika vitu kwani matokeo yake ni kuitafuta furaha katika dhambi, jambo ambalo halimfikishi mtu katika furaha kamili ya kuonana na Mungu, bali huleta mahangaiko moyoni. Kumbe kadiri tunavyozidi kujiandaa kusherehekea kuzaliwa kwake Kristo, tuzisafishe roho zetu, tufanye upatanisho na kutoa msamaha kwa waliotukosea. Mwokozi tunayemngojea ndiye asili na utimilifu wa furaha. Sisi wabatizwa na wafuasi wake tuwe chanzo cha furaha kwa wengine. Ndivyo antifona ya Komunio inavyotusisitiza ikisema; “Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wetu atakuja na kutuokoa” (Taz. Isa. 35:4). Ni wazi kuwa kwa nguvu zetu hatuwe kuufikia wokovu. Daima tuombe neema na baraka za Mungu. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anatuombea akisali hivi; “Ee Bwana, tunaomba tukutolee daima sadaka ya ibada yetu. Sadaka hii itimize mipango ya fumbo takatifu na kutuletea kweli wokovu wako”. Na katika sala baada ya komunyo anahitimisha maadhimisho haya akituombea hivi; “Ee Bwana, utujalie huruma yako; utuondolee dhambi zetu; na neema zako hizi zituweke tayari kuadhimisha sikukuu zijazo”.