Dominika II ya Majilio:Huruma ya Mungu ni kuu kwao wamtegemeao!
Na Padre Joseph Herman Luwela - Vatican.
Karibu tena mpendwa msikilizaji, na msomaji hama hakika wahenga walinena, siku hazigandi, baada ya Dominikaya Kwanza ya Majilio yaani Dominika iliyopita kuweka mikakati ya namna ya kukitumia kipindi cha Majilio tumefikia wapi katika maandalizi ya kumpokea Kristo? kuna maendeleo yoyote? tumepiga hatua kuandaa nyumba (roho/moyo) ili Mkombozi apate pa kufikia? Tuamke tulio bado usingizini, huruma ya Mungu ni kuu kwao wamtegemeao. Leo tunatafakari huruma ya Mungu, wazo hili linajitokeza katika masomo yote (Bar 5:1-9, Filp 1:3-6, 8-11, Lk 3:1-6). Nabii Baruch (katibu wa Yeremiha) anauonesha Gerusaleme kama mjane aliyevaa nguo za matanga, ameketi kwenye majivu. Ilikuwa desturi kwa mjane kuvaa nguo mbaya, kufunika kichwa, kuketi majivuni na kuomboleza, hapiki, hafui wala hatumii namna yoyote ya mafuta wala manukato kama tulivyo sisi leo. Wazo linaloongoza tafakari hii ni “Huruma ya Mungu ni kuu kwao wamtegemeao!”
UFAFANUZI
Baada ya Gerusaleme kutekwa wayahudi walipelekwa utumwani kwa aibu, minyororo na ukatili, mji ukabaki kama mjane aombolezaye. Ndipo Baruch analeta ujumbe wa matumaini akiitangaza huruma ya Mungu ya kukoma kwa siku za maombolezo. Mungu ataondosha vikwazo kwa kushusha vilima na kujaza mabonde na Israeli ataongozwa kwa furaha. Nasi tunahitaji kuondoa matanga na misiba ya nafsi zetu na kuvaa utukufu wa Mungu. Kama Baruch anavyotabiri juu ya Gerusaleme mpya ndivyo nasi tunavyosubiri maisha mapya kwa majilio ya Kristo. Mara si haba tumefanana na Gerusaleme: wajane, wagumba na tasa tusio na wana au binti, tumekaa matanga kwa kukosa amani ya maisha sababu ya dhambi, ubinafsi na kutosikiliza na kulishika neno la Mungu. Hatujasamehe kutosha, tunatamani visasi... Ee Jua la mashariki, uje utukomboe.
Mwinjili Luka leo anaorodhesha viongozi wakuu wa dini na serikali wakati wa kuzaliwa Kristo. Hana nia ya kutuburudisha bali kuwathibitishia wenye mashaka kuwa Kristo alizaliwa kweli na kipindi alichoishi kinafahamika... halafu anatuonesha huruma ya Mungu kwa njia ya Yohane Mb anayehubiri maneno ya nabii Isaya ‘sauti ya mtu aliaye nyikani…’ (Mt 3:4) anaeleza Yohane Mbatizaji ni mtu wa namna gani na alivaaje, singa za ngamia na mshipi wa ngozi, chakula chake na maisha ya jangwani... ni vigumu kumuona akipumzika, kula na kunywa, daima yu wima akihubiri. Japo hakufanya muujiza wowote Kristo alimsifu kuwa ni mkuu kati ya wazao wa wanawake (Yh 10:41)... Yesu na Yohane Mbatizaji walifanana kuzaliwa (Malaika Gabrieli alitangaza ujio wao japo Yohane alitungwa mimba kwa wazazi wanadamu), wote ni manabii, wote walikuwa wakweli, wote waliuawa. Mmoja aliitwa nabii wa Mungu aliye juu mwingine akaitwa Mwana wa aliye juu. Mmoja alibatiza kwa maji mwingine akabatiza kwa Roho Mtakatifu, mmoja wa kabila la Lawi mwingine wa kabila la Yuda. Mmoja anazaliwa na wazazi wazee mwingine na Bikira. Mmoja baba yake anaadhibiwa kwa kutoamini mwingine mama yake anasifiwa kwa kuamini na kukubali (Ndimi mtumishi wa Bwana...)
Hata hivyo Yesu na Yohane walitofautiana kitabia na kimwenendo. Yohane alihubiri hukumu na hasira ya Mungu, akawaita watu vizazi vya nyoka akisema shoka lipo tayari wote wasiosikia watakatwa na kutupwa motoni hivi ni muhimu kuzaa matunda yapasayo toba. Tunashukuru Kristo alikuwa tofauti akila, kunywa, kuongea na kuchangamana na wenye dhambi na kuwahurumia. Yohane Mb ni mkali asiyeogopa linapokuja suala la ukweli, mafundisho yake ni mafupi lakini yana ujumbe mzito na wa moja kwa moja. Katika miaka tuliyojaliwa kuishi hadi sasa (10, 20, 30, 40, 60, 70...) tumesikia mahubiri ya watu wangapi, maonyo ya watu wangapi? tumesomewa na kukumbushwa amri za Mungu mara ngapi? nasi tumefanya nini? tumepiga hatua polepole mno. Mara mojamoja tunawahitaji akina Yohane Mb na lugha za moto, mashoka na kauli ngumu (vizazi vya nyoka), huenda tutazinduka na kuharakisha.
Mwito wetu ni kuitengeneza njia ya Bwana na kuyanyoosha mapito yake tukiiga tabia ya Yohane na kusema ukweli, kuonyana na kurekebishana kindugu ili jamii iwe na amani na upendo na kwa namna hii huruma ya Mungu itaonekana kwetu. Tuitengeneze njia ya Bwana tukifukia mabonde ya upotovu wa imani, uchovu katika kusali, kuelemewa na majukumu, migogoro ya afya, usasa na mahusiano magumu. Milima na mabonde vinavyotakiwa kusawazishwa ni vilema: kiburi, kujikweza na dharau na maringo, uvivu, wivu, majungu, uwongo na uzushi. Milima ya kuhisi vibaya, fujo na malumbano, milima ya kero mbalimbali...
Mtakatifu Paulo katika somo II anasisitiza pia juu ya kufukia mabonde na kuyanyoosha mapito ya Bwana atakapokuja yaani kujiweka sawa na kuzidi sana katika pendo la Kristo kwa hekima na ufahamu wote, kuyakubali mema na kuwa na mioyo safi, bila kosa mpaka siku ya Kristo, Noeli… Heri yetu tukitenda haya, tutauona wokovu wa Mungu na kufurahi milele. Wokovu huo ndilo zao la huruma yake kwetu, wokovu ni kwa wote na si kwa wateule wachache na huo ndio mpango wa Mungu wa tangu milele ya kwamba sisi tuokolewe katika Mwanaye Mpenzi atakayezaliwa kati yetu, amina.