Tafuta

Dominika ya II ya Majilio. Dominika ya II ya Majilio. 

Dominika II ya Majilio:Vueni nguo za huzuni,vaeni za utukufu

Popote pale penye ugomvi,hasira,huzuni,au malalamiko,kuna dhambi.Basi tunaalikwa kusawazisha hali hizi,tukiendee kiti cha kitubio na kuvua dhambi ili tuvae neema ya utakaso ndipo tutakapofurahi na kuimba;“Nitafurahi sana katika Bwana,maana amenivika mavazi ya Wokovu,amenifunika Vazi la Haki”(Isa 61:10).Kwa njia hiyo “tunakuomba Bwana kwa unyenyekevu sisi tulioshiriki fumbo hili,utufundishe kuyapima kwa hekima mambo ya dunia na kuyazingatia ya mbinguni.”

Na Padre Paschal Ighondo – Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu Domenika ya pili ya majilio mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa. Masomo ya domenika hii yamebeba ujumbe wa matumaini unaotualika tuvue nguo za huzuni na kuvaa nguo za utukufu kwa sababu Bwana anakuja kutukomboa, maana wokovu ni zawadi kutoka kwake anayotujalia bure kabisa, kwa upendo mkuu pasipo mastahili yetu. Ni Yeye tu awezaye kutuokoa. Hivyo kwa Neno lake anatualika tuitengeze njia yake katika mioyo yetu, kuyanyoosha mapito yake, tukiyaondoa yote yanayotuletea huzuni na tuweke juhudi kuyadumisha yale yote yatuleteayo furaha na Amani. Ujumbe huu unaashiriwa na maneno ya wimbo wa mwanzo yanayosema; “Enyi watu wa Sayuni, tazameni Bwana atakuja kuwaokoa mataifa; naye atawasikizisha sauti yake ya utukufu katika furaha ya mioyo yenu” (Isa. 30:19, 30). Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya mwanzo anatuombea sisi wanae akisali hivi; “Ee Mungu Mwenyenzi Rahimu, tunakuomba mambo ya dunia yasitupinge sisi tunaomkimbilia Mwanao tupate kumlaki, bali hekima yako itufanye tumshiriki yeye”.

Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Baruku (5:1-9). Katika somo hili Nabii Baruku, ambaye alikuwa katibu wa Nabii Yeremia aliyeishi miaka 600 kabla ya Kristo, anawatuliza waisraeli wakiwa utumwani Babeli akiwaambia kuwa mda si mrefu Mungu atawarudisha Yerusalemu. Hivyo anawapa matumaini akiwaonyesha furaha na heri watakayopata wakirudi nyumbani. Katika lugha ya kibibilia, kawaida Manabii wanailinganisha Yerusalemu na mwanamke au mama, na watoto wake wakiwa ni watu wake. Lakini Baruku anailinganisha Yerusalemu na mama mjane anayewalilia watoto wake waliochukuliwa mateka na kupelekwa uhamishoni. Kwa mjane huyu, kibinadamu, watoto wake walionekana kama wamekufa. Ndiyo maana mjane huyu – Yerusalemu, amevaa mavazi meusi akisikitika na kuomboleza juu ya wanawe, kana kwamba wameshakufa. Nabii Baruku anamfariji akimwambia: “Ee Yerusalemu, vua nguo za matanga na huzuni, uvae uzuri wa utukufu utokao kwa Mungu wa milele.” Baruku anaialika Yerusalemu kufurahi kwa sababu, siku yaja ambapo Mungu atawarudisha tena wanawe kwake kutoka uhamishoni.

Masimulizi yanasema kuwa walipochukuliwa mateka na kupelekwa uhamishoni, walifungwa minyororo na kuteswa sana. Lakini sasa wanaambiwa, siku inakuja ambapo badala ya kuteseka watarudi wakiwa na wingi wa furaha, wakishangiliwa kama wana wa Mfalme Mkuu. Mungu atahakikisha kwamba safari yao ya kurudi nyumbani ni safari ya furaha na mafanikio kwani watatembea kwa furaha kama watu huru. Na watakaporudi nyumbani, wataanza kuishi maisha na matakatifu wakiwa na mahusiano mazuri na Mungu. Kwa maana Mwenyezi Mungu atawatakasa na dhambi zao, naye atakuwa Mungu wao tena. Unabii huu wa Baruku ulitimia wakati Ciro, Mfalme wa Persia, alipoivamia Babeli, akaiteka, ikawa chini ya himaya yake na akawatangazia uhuru kuwa, yeyote anayetaka kurudi Yerusalemu na aende. Ndiyo maana mzaburi katika wimbo wa katikati anasema hivi; “Bwana alipowarejeza mateka wa Sayuni, tulikuwa kama waotao ndoto. Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko, na ulimi wetu kelele za furaha. Ndipo waliposema katika mataifa, Bwana amewatendea mambo makuu. Bwana alitutendea mambo makuu, tulikuwa tukifurahi. Ee Bwana, uwarejeze watu wetu waliofungwa, kama vijito vya Kusini, wapandao kwa machozi, watavuna kwa kelele za furaha. Ingawa mtu anakwenda zake akilia, azichukuapo mbegu za kupanda. Hakika atarudi kwa kelele za furaha aichukuapo miganda yake” (Zab. 126:1-6).

Lakini licha ya kutimia kwa utabiri wa Nabii Baruku, waliorudi ni wale waliokuwa katika hali ya umaskini. Ijapo walifurahia kurudi nyumbani Yerusalemu, maisha bado yalikuwa magumu kwa kukosa uhuru wa kisiasa na kiuchumi. Ni wazi walifanikiwa kulijenga upya Hekalu na kuta za mji wao zilizobomolewa na baada ya muda mageuzi ya kiroho yalianza kujionesha kati yao. Lakini haikuchukua muda maskini walianza kugandamizwa tena na ndugu zao, waliokuwa matajiri. Viongozi wa serikali na dini waliochukua madaraka, hawakuwa watetezi wa watu wao, bali watesi kinyume kabisa na kile alichowaambia Nabii Baruku. Furaha aliyowatangazia Baruku ikawa ndoto. Hii ni kwa sababu tangazo la kurudi kwao nyumbani ni utabiri tu wa kitakachotokea siku ya mwisho wakati wa hukumu ya mwisho huko mbinguni iliko Yerusalemu Mpya.

Somo la pili ni la waraka wa Mtume Paulo kwa wafilipi (1:3-6, 8-11). Katika somo hili Mtume Paulo anawasifu Wafilipi kwa uhodari katika maisha yao ya kiimani, ambayo yamewasukuma wengi kuiamini Injili. Lakini mafanikio hayo sio kazi yake yeye Paulo bali ni kwa sababu Kristo mwenyewe kwa njia ya Roho Mtakatifu, ameisukuma mioyo ya Wafilipi kuipokea Injili, na Kristo peke yake ndiye mwenye uwezo wa kuhitimisha wokovu wao kwa furaha. Hivyo anawasihi upendo wao kwa Kristo na kati yao uzidi kuongezeke siku baada ya siku. Zaidi sana waendelee kuishi maisha yasiyo na lawama, ili Kristo aje kukamilisha wokovu wao wakati wa ujio wake wa pili. Nasi tunaalikwa katika kipindi hiki cha majilio, tuishi kwa kupendana, tusilaumiane, na tusiishi kwa chuki miongoni mwetu.

Injili ni ilivyoandikwa na Luka (3:1-6). Sehemu hii ya Injili imegawanyika katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza inatueleza ni lini katika historia ya dunia na ya wokovu wetu, Yohane alianza kazi yake ya kuhubiri juu ya matayarisho ya kumpokea mwokozi. Ni mwaka wa kumi na tano wa kutawala kwake Kaisari Tiberia, Pontio Pilato alipokuwa liwali wa Uyahudi, na Herode (mtoto wa Herodi aliyewaua watoto wa Bathlehemu akijaribu kumwangamizi mtoto Yesu bila mafanikio) akiwa mfalme wa Galilaya, na Filipo ndugu yake akiwa mfalme wa Iturea na nchi ya Trakoniti, na Lisania mfalme wa Abilene, wakati wa ukuhani mkuu wa Anasi, na Kayafa aliteuliwa na mamlaka ya Kirumi kuwa Kuhani Mkuu huko Yerusalemu, akichukua nafasi ya Anasi Baba mkwe wake, baada ya kuondolewa ukuhani na mamlaka hiyohiyo ya kirumi. Lakini pamoja na kuondolewa ukuhani mkuu, Anasi alikuwa bado na ushawishi mkubwa, kwani hakuna lililofanyika bila kupata ushauri wake. Ni wakati huu neno la Mungu lilipomfikia Yohane, mwana wa Zakaria, jangwani.

Kutajwa kwa viongozi hawa ni kutudhihirishia kuwa mambo haya ni ya kweli na sio ya kutunga. Lakini kwa upande mwingine tunaona kuwa Mungu hakuwachagua hata mmoja wa hawa watawala wanaotajwa. Hii ni kutuonyesha kuwa wokovu wa mwanadamu ni mpango wa Mungu na upo mikononi mwa Mungu na sio katika uwezo wa mwanadamu. Hakuna mtu aliye na mamlaka yakujikomboa mwenyewe au kuwaokoa wengine. Ndiyo maana hata Yohane Mbatizaji, kwa unyofu anang’amua na kudhihirisha udhaifu na unyonge wake, na kwamba hata yeye anamhitaji Yesu kwa ajili ya wokovu wake akisema: “Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu?” (Mt 3:14). Kumbe tunaona kuwa Hekima na mamlaka ya kibinadamu pasipo Mungu hayawezi kutuokoa kutoka utumwa wa dhambi. Mama Kanisa akilitambua hili katika sala ya kuombea dhabihu anatuombea sisi wanae akisali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba sala na sadaka zetu sisi wanyonge zikutulize; na kwa kuwa sala zetu hazitoshi kutupatia mastahili, utujalie shime kwa rehema yako”.

Sehemu ya pili ya Injili hii imebeba ujumbe wa Yohane Mbatizaji juu ya ubatizo wa toba.  Tunaalikwa kuitengeneza njia ya Bwana, kuyanyoosha mapito yake, palipo na mabonde tupainue, palipo na mlima na kilima tupashushe, palipopotoka tupanyooshe na palipoparuza tupasawazishe (Isa 40:3-4). Matengenezo na matayarisho haya yanahusu mioyo yetu nayo yanawakilisha hali ya dhambi iliyo ndani ya mioyo yetu. Tukumbuke daima kuwa dhambi inatutenga na Mungu na hivyo tunapoteza furaha na kuwa na huzuni. Adamu anasema; “Niliposikia sauti yako niliogopa nikajificha” (Mwa 3:10). Hofu inaleta huzuni. Dhambi pia inatutenga na wenzetu na kuharibu mahusiano yetu na kutuletea chuki na huzuni. Adamu akasema; “Huyu mwanamke uliyemweka hapa pamoja nami alinipa nami nikala” (Mwa 3:12). Dhambi inaharibu urafiki wetu na ulimwengu na viumbe wengine. Mwanamke akasema; Nyoka alinidanganya nami nikala. Ndipo sasa Mungu akatoa adhabu akisema; “Ardhi itakuzalia miiba na utakula kwa jasho” (Mwa 3:18), kwa sababu umefanya haya utazaa kwa uchungu, utamponda nyoka kichwa chake, naye atakuponda kisigino” (Mwa 3:15). Dhambi hutufanya kuwa watumwa wa shetani. “Maana kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi” (Yn 8:34). Hivi ndivyo dhambi inavyoleta mtafaruku katika maisha yetu na kutuvisha mavazi ya huzuni. Popote pale penye ugomvi, hasira, huzuni, au malalamiko, kuna dhambi.

Basi tunaalikwa kusawazisha hali hizi, tukiendee kiti cha kitubio na kuvua dhambi ili tuvae neema ya utakaso ndipo tutakapofurahi na kuimba; “Nitafurahi sana katika Bwana, maana amenivika mavazi ya Wokovu, amenifunika Vazi la Haki” (Isa 61:10).  Nayo antifona ya wimbo wa Komunio inatualika ikisema; “Ondoka, ee Yerusalemu, usimame juu; tazama uione furaha inayokujia kutoka kwa Mungu (Bar.  5:5; 4:36). Ni katika tumaini hili mama Kanisa anapohitimisha maadhimisho ya dominika hii katika sala baada ya komunyo anasali hivi; “Ee Bwana, baada ya kutushibisha chakula cha roho, tunakuomba kwa unyenyekevu sisi tulioshiriki fumbo hili, utufundishe kuyapima kwa hekima mambo ya dunia na kuyazingatia ya mbinguni”. Na hili ndilo tumaini letu kwa kipindi hiki cha majilio.  

 

Tafakari Neno.Dominika II Majilio
06 December 2024, 13:21